Mwaka jana ulishuhudia utimizaji wa ahadi nyingi na kuvunjwa kwa ahadi nyingi pia. Tulishuhudia viwango vipya vya juu vya uzalishaji wa gesi ya ukaa, hali ya joto ikiyumbayumba na athari za mabadiliko ya tabianchi kushuhudiwa kwa kishindo na kwa kasi zaidi. Fedha za kusaidia jamii zilizo hatarini zaidi kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hazijatolewa. Wakati uo huo, mengi ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yako mbali kufikia nusu ya Ajenda ya 2030. Kuna sababu nyingi za kuwepo kwa hali hii, lakini ni wazi kwamba ushughulikiaji hafifu wa changamoto za aina tatu duniani za mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira na uharibifu wa bayoanuai, na uchafuzi na taka ni chanzo kikuu.
Hii ndio hali hasi. Hali chanya ni kwamba juhudi za kimataifa za kushughulikia changamoto za aina tatu duniani ziliamarika. Juhudi za kukabiliana na uchafuzi wa mazingira na taka zilipigwa cheki kutokana na makubaliano ya Mfumo wa Kimataifa kuhusu Kemikali na hatua zilizopigwa kwenye chombo cha kimataifa kuhusu uchafuzi wa plastiki, ambacho kinapaswa kuwa tayari kufikia mwaka 2024. Mataifa yalipitisha mkataba wa kulinda bayoanuai katika bahari nje ya mipaka ya kitaifa, huku miongozo muhimu ya kusaidia sekta ya kibinafsi kupunguza athari zake kwa mazingira ikitolewa - kupigwa cheki kwa Mfumo wa Kimataifa wa Bayoanuai wa Kunming-Montreal, ambao utekelezaji wake ulianza kwa kasi. Hatimaye, Kongamano la Umoja wa Mataifa la Mabadiliko ya Tabianchi, COP28, lilitoa wito unaoleweka wazi kwa nchi kuacha matumizi ya nishati ya visukuku - pamoja na mfumo wa Lengo la Kimataifa la Kukabiliana na Hali, kutekeleza Mfuko wa Hasara na Uharibifu, na ahadi mpya kuhusu upunguzaji wa joto kwa njia endelevu, upunguzaji wa methani, kuzidisha uzalishaji wa nishati jadidifu mara tatu na mafanikio ya kujali mazingira.
Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) lilitekeleza wajibu muhimu katika nyingi ya michakato hii – kwa kutoa sayansi muhimu na masuluhisho kuhusiana na changamoto za aina tatu duniani, kuitisha na kuwezesha mazungumzo muhimu, kuandaa mikataba muhimu ya kimataifa ya mazingira, kufanya kazi na watu binafsi na sekta za fedha ili kuoanisha ufadhili na michakato ya kimataifa na kusaidia nchi wanachama kutekeleza ahadi zao.
Hatua zinapigwa. Kazi kubwa iliyo mbele yetu ni kuimarisha hatua hizi ili zisonge haraka kuliko kuongezeka kwa janga la changamoto za aina tatu duniani. Kama mamlaka kuu ya kimataifa ya mazingira, UNEP itafanya kazi bila kuchoka kusaidia kuwezesha hili lifanyike - kupitia kutoa teknolojia za kidijitali ili kutoa sayansi inayofaa na inayotoa mtazamo wa mambo ya mbeleni, kuimarisha utekelezaji wa makubaliano ya kimataifa ya mazingira ambayo hufanya mabadiliko yawezekane, na kuunga mkono Nchi Wanachama ili kukuza uthabiti wa tabianchi, kuishi kwa amani na mazingira na kukuza mustakabali usio na uchafuzi. Hivi ndivyo tutakavyofanikisha Ajenda ya 2030 na kuunda mazingira ya ulimwengu wenye amani na ustawi zaidi.
UNEP iko mstari wa mbele katika juhudi za kimataifa za kusaidia nchi kupunguza uzalishaji wa gesi ya ukaa na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ambayo ni mambo msingi ya SDG13 kuhusu kushughulikia mabadiliko ya tabianchi. Kazi hii pia inachangia kwa mengi ya malengo mengine ambayo yanaunga mkono afya ya binadamu na hali bora ya sayari, ustawi na usawa, ikiwa ni pamoja na kutokomeza umaskini (SDG1), kukomesha baa la njaa (SDG2), kuimarisha upatikanaji wa nishati nafuu na isiyochafua mazingira (SDG7), kupunguza ukosefu wa usawa (SDG10) na kukuza jamii endelevu (SDG11).
Uchanganuzi wa UNEP kabla ya Kongamano la Umoja wa Mataifa la Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) ulizingatia kwa kina kuenea kwa janga la mabadiliko ya tabianchi na kutoa kwa watungasera msururu wa masuluhisho.
Ripoti ya Uzalishaji wa Gesi Chafu ya Mwaka wa 2023: Rekodi iliyovunjwa – Ongezeko la joto lilizidi zaidi, ila dunia imeshindwa kupunguza uzalishaji wa hewa chafu (tena) ilionyesha kuwa ahadi zilizopo za tabianchi zitafanya ulimwengu kushuhudia joto la nyuzijoto kati 2.5 na 2.9 katika karne hii, kiwango cha juu kuliko malengo ya Mkataba wa Paris. Kufanya ongezeko la joto lisizidi nyuzijoto 1.5, uzalishaji wa gesi ya ukaa lazima upungue kwa asilimia 42 kufikia mwaka wa 2030. Ripoti ya Pengo la Juhudi za Kukabiliana na Gesi Chafu: "Kupunguza au kuongeza? Wazalishaji wakuu wa mafuta ya visukuku wanapanga kuzalisha zaidi licha ya ahadi za kushughulikia mazingira inaonyesha kuwa mipango ya serikali ya kuzalisha nishati ya visukuku itafifiisha bajeti ya kukabiliana na hewa ya ukaa isizidi nyuzijoto 1.5.
Wakati uo huo Ripoti ya Kukabiliana Na Pengo la Juhudi za Kukabiliana na Uzalishaji wa Gesi Chafu: Hakuna ufadhili wa kutosha, Wala maandalizi ya kutosha– Uwekezaji duni na mikakati duni ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni hatari kwa dunia inaonyesha kuwa pengo la kukabiliana na hali ya kifedha lilikuwa kubwa kwa asilimia 50 kuliko ilivyokadiriwa hapo awali. Nchi zinazoendelea zinahitaji kati ya dola bilioni 215 na dola bilioni 387 kwa mwaka ili kuthibiti athari zinazoongezeka za mabadiliko ya tabianchi.
Uchambuzi wa UNEP ulitajwa na wakuu wa nchi na walioshiriki mazungumzo wakati wa COP28, ilhali Ripoti ya Kukabiliana Na Pengo la Juhudi za Kukabiliana na Uzalishaji wa Gesi Chafu ilinukuliwa katika Tathmini ya Kimataifa, uamuzi wa mwisho wa COP28 ambao ulitoa wito kwa kila nchi kuhama kutoka mafuta ya visukuku. Zaidi ya nakala 3,300 kuhusu uchanganuzi huu wa “pengo” zilichapishwa katika nchi zaidi ya 75.
Katika mwaka wa 2023, UNEP ilisaidia takriban nchi 43 zinazoendelea zilipokuwa zikitayarisha ripoti zao za uwazi za kila baada ya miaka miwili - yaani hati zinazopima jinsi mataifa binafsi yanavyotekeleza ahadi zao za kushughulikia tabianchi. Ripoti hizi za kitaifa zilifadhiliwa na dola za Marekani milioni 32 katika ufadhili kutoka kwa Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF), mojawapo ya fedha za juu zaidi kuwahi kutolewa na taasisi kufadhili ripoti za tabianchi.
UNEP ilisaidia mataifa kadhaa kuimarisha utoaji wake wa taarifa kwa njia mbadala, ikiwa ni pamoja na kuendeleza mifumo ya kusimamia takwimu za tabianchi. Kupitia kwa Kituo cha Tabianchi cha UNEP-Copenhagen, UNEP ilianzisha mitandao sita ya kikanda ili kutoa mafunzo na usaidizi wa kiufundi kuhusu kutoa ripoti. Mchakato wa kuripoti kwa njia ya wazi unachukuliwa kuwa muhimu kwa Mkataba wa Paris kwa sababu unaelimisha kuhusu utungaji sera na kujenga uaminifu miongoni mwa mataifa.
Mfumo wa Tahadhari na Kushughulikia Methani wa msingi ulifuatilia uwezo mkubwa wa utoaji mkuu wa gesi ya ukaa kutoka kwa mitambo ya mafuta na gesi. Mfumo huu umetengenezwa na UNEP na washirika wake, na ni mpango wa kwanza wa aina yake unaotumia data ya setilaiti, kufunza mashine na mambo mengine ya mbinu za kisasa. Katika mwaka wa 2023, uliarifu kampuni na serikali juu ya mabomba ya methani zaidi ya 120 katika mabara manne, na kuhimiza hatua za kupunguza uzalishaji wake.
UNEP ilishauri Brazili juu ya kuboresha ukuzaji wa viwango bora vya nishati kwa matumizi ya friji za biashara, juhudi zinazolenga kupunguza utoaji wa kaboni dioksidi kwa tani milioni 11 kila mwaka - sawa na asilimia 15 ya uzalishaji wa hewa chafu kutoka kwa sekta ya umeme nchini humo. Wakati uo huo, UNEP ilisaidia miji 10 nchini Colombia, Costa Rica, India, Kenya na Türkiye kuendeleza mipango ya kuondoa hewa ya ukaa katika sekta zao za ujenzi.
Nchi tano - Angola, Kazakhstani, Kenya, Romania na Turkmenistani - zilijiunga na Ahadi ya Kimataifa ya Methani katika mwaka 2023, na kujumuisha ushiriki wa jumla ya mataifa 155. UNEP ni mtekelezaji msingi wa ahadi hiyo, ambayo ilikuwa maarufu katika COP28 na inalenga kupunguza uzalishaji wa methani duniani kwa asilimia 30 kufikia mwaka wa 2030. Hii ni muhimu ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa muda mchache na kujitayarisha kuondoa hewa ya ukaa kikamilifu.
Mpango unaosimamiwa na UNEP waTumeungana ili Kufanikiwa ulisaidia zaidi ya nchi 80 zilipokuwa zinatayarisha viwango vya ufanisi wa nishati ya kutoa mwangaza, vifaa na mitambo. Kufikia mwaka wa 2040, hatua hizi zinaweza kuokoa takriban Megawati (MW) 30,000 za nishati, kiwango sawa na mitambo mikubwa 60 ya nishati.
Katika mwaka wa 2023, washirika 11 wa ziada waliidhinisha marekebisho ya Kigali ya Mkataba wa Montreal ambao ni wito wa kupunguza haidrofluorokaboni (HFCs). Kupunguzwa kwa matumizi ya gesi hizi za ukaa kunaweza kuzuia ongezeko la joto la hadi nyuzijoto 0.5 kufikia katikati mwa karne hii. Mfuko wa Kimataifa katika mkataba huu uliwekewa fedha tena mwezi wa Oktoba mwaka wa 2023 kiasi cha dola milioni 965 kwa kipindi cha mwaka wa 2024 hadi mwaka wa 2026. Zaidi ya nchi 60 zilijiunga na Ahadi ya Kupunguza Joto, iliyoandaliwa na Muungano wa UNEP wa Cool Coalition. Makubaliano haya yanalenga kupunguza uzalishaji wa gesi za ukaa zinazohusishwa na sekta ya kupunguza joto kwa angalau asilimia 68 kote duniani kufikia mwaka wa 2050.
UNEP na washirika wake waliandaa Wiki ya Tabianchi barani Afrika iliofanyika sambamba na Mkutano wa Kilele wa Tabianchi wa Afrika wa kwanza ulioleta pamoja zaidi ya washiriki 10,000 wakiwemo wakuu 20 wa nchi, mjini Nairobi, Kenya. Mkutano huo ulisisitiza kuwa Afrika inaweza kuleta suluhisho kwa janga la mabadiliko ya tabianchi. "Tunalenga kuzungumza kwa sauti moja ya Kiafrika ambayo itazaa matunda ... hadi kwa COP28 na baadaye,” alisema Rais wa Kenya William Ruto.
UNEP iliongoza kuanzishwa kwa mifumo ya tahadhari ya mapema kwa majanga yanayohusiana na tabianchi katika
nchi sita: Visiwa vya Cook, Visiwa vya Marshall, Niue, Palau, Timor-Leste, Tuvalu. Baadhi ya mifumo hiyo imestawi na inaendelea kufanya kazi, ikiwa ni pamoja na mfumo wa utabiri wa hewa kutokana na mtandao ambao ulionya wakazi wa Visiwa vya Cook kuhusu mafuriko ya pwani wakati wa dhoruba ya mwezi Mei. UNEP inatekeleza miradi kama hiyo katika mataifa mengine 19, kama sehemu ya msukumo mpana wa Umoja wa Mataifa kuhakikisha kuwa mifumo ya tahadhari za mapema italinda kila mtu Duniani kufikia mwaka wa 2027.
UNEP pia iliimarisha juhudi za kusaidia jamii kukabiliana na mabadiliko ya muda mrefu ya tabianchi, huku ikisaidia miradi karibu 80. UNEP ilisaidia Panama na Uganda kuendeleza mipango ya kitaifa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kufanya jumla ya idadi ya nchi ambazo zimesaidika kuwa 23.
Kituo cha Teknolojia na Mtandao wa Tabianchi (CTCN), taasisi inayosimamiwa na UNEP, ilisaidia nchi zinazoendelea kutumia teknolojia kushughulikia na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Hatua hizi zinatarajiwa kunufaisha watu milioni 69 na kuzuia uzalishaji wa chafu kiasi cha tani milioni 21 za kaboni dioksidi kila mwaka - sawa na kuondoa magari milioni 4 kutoka barabarani. Kwa mfano, kituo hiki kilisaidia Botswana, Eswatini, Lesotho, Malawi, Namibia, Zambia na Zimbabwe kuendeleza viwango vya chini vya utenda kazi wa nishati kwa friji na transfoma.
Muungano wa Wamiliki wa Mali Isiyozalisha Hewa Chafu, kundi la wawekezaji wa makampuni waliojitolea kuondoa hewa ya ukaa katika kampuni zao, uliongezeka na kufikia wanachama 87 kufikia Novemba mwaka wa 2023, kutoka 77 mwaka uliopita. Malengo ya kupunguza uzalishaji wa gesi ya ukaa miongoni mwa wanachama yalipungua kwa asilimia 3 katika mwaka 2022. Wanachama wa muungano huu, ambao wana mali kiasi cha dola za Marekani trilioni (US$) 9.5, walikuwa wametoa zaidi ya dola za Marekani bilioni 380 kwa masuluhisho kwa tabianchi kufikia mwaka wa 2022, mwaka wa mwisho kwa data kupatikana.
Kufikia mwishoni mwa mwaka, zaidi ya wakopeshaji 320, wakiwakilisha nusu ya mali ya benki duniani, walikuwa wamejiunga na Kanuni za Uwajibikaji wa Benki. Mfumo huo, unaosimamiwa na Mpango wa Fedha wa UNEP (UNEP-FI), husaidia benki kuoanisha biashara zao kuu na mikataba ya mazingira ya kimataifa. Karibu asilimia 71 ya waliotia saini wamejitolea kukabiliana na hali. Wengi wao pia ni makampuni ya kifedha ambayo hutoa masuluhisho kwa mabadiliko ya tabianchi. Kwa mfano, mkopeshaji mmoja mkuu alitoa mkopo wa dola bilioni 1.2 kwa fundi anayetumia nishati jadidifu nchini India kuunda megawati 900 za nishati ya upepo na megawati 400 za nishati ya jua.
UNEP ilisaidia kulinda, kuboresha na kusimamia vyema mifumo ya ekolojia ya maji safi, ambayo ilikuwa imetishiwa kuangamia kutokana na kuongezeka kwa mabadiliko ya tabianchi. Mwezi Machi, UNEP na washirika kadhaa walizindua Mradi wa Maji Safi, ambao unalenga kulinda kilomita 300,000 za mito na hekta milioni 350 za ardhioevu kote ulimwenguni. Mataifa yapatayo 43 yalijiunga na juhudi hizo, ikijumuisha mengi katika COP28, matokeo muhimu ya Ajenda ya Maji ya COP28. UNEP pia ilianzisha mradi, unaofadhiliwa na Mpango wa Kimataifa wa Tabianchi wa Ujerumani, kusaidia kusimamia kwa njia endelevu Bonde la Mto Kongo. Ni mojawapo ya juhudi kadhaa zinazoongozwa na UNEP katika eneo hilo, makazi kwa zaidi ya watu milioni 75. Vilevile, UNEP ilitangaza itafanya kazi na miji 19 kote duniani kuboresha mifumo ya ekolojia ya mijini, mito mingi, mifereji na ardhioevu. UNEP pia iliunga mkono uzinduzi wa Kenya wa Tume ya Mito ya Nairobi, ambayo inalenga kufufua bonde la mto linalotegemewa na mji mkuu. Hatimaye, ripoti ya UNEP ya Maji Taka: Kubadilisha Shida kuwa Suluhisho iligundua kuwa kukiwa na sera mwafaka, maji taka yanaweza kutoa nishati mbadala kwa watu milioni 500, kuwezesha usambazaji mara 10 ya maji yanayotolewa na uwezo wa sasa wa kuondoa chumvi kote duniani na kupunguza kwa asilimia 10 matumizi ya mbolea duniani.
Ripoti ya UNEP inaonyesha kuwa pengo la uzalishaji wa hewa chafu ni mfano wa korongo kuu la uzalishaji wa hewa chafu. Korongo lililotapakaa ahadi zilizovunjwa, maisha yaliyokatizwa, na rekodi zilizovunjwa.
Wakati ambapo mazingira na bayoanuai vipo chini ya shinikizo kubwa, UNEP inaongoza juhudi za kulinda, kuboresha na kusimamia malighafi kwa njia endelevu. Kwa kuwa mazingira ni nguzo kwa jamii na uchumi, kazi hii inasaidia kulinda maisha chini ya maji (SDG14) na maisha juu ya ardhi (SDG15), miongoni mwa malengo mengine. Juhudi nyingi za UNEP katika mwaka wa 2023 zililenga kusaidia nchi kutekeleza Mfumo wa Kimataifa wa Bayoanuai wa Kunming-Montreal (GBF).
Kwa msaada kutoka kwa GEF, UNEP inaongoza miradi 24 katika nchi 21, kuanzia Chile hadi Sri Lanka, kulinda na kuboresha mandhari mbalimbali ya maeneo ya ardhi na bahari. Katika mwaka wa 2023, kazi hiyo ilisaidia usimamizi endelevu wa zaidi ya hekta 560,000 za mifumo ya ekolojia, eneo linalokaribia kutoshana na Trinidad na Tobago. Pia ilisababisha kuundwa kwa hekta 254,000 ya maeneo yaliyolindwa na uhifadhi au urejeshaji wa hekta 110,000 za misitu.
Kupitia kwa Mpango wa UN-REDD, UNEP ilisaidia nchi 17 kuhifadhi na kurejesha misitu, ambayo ni muhimu kwa ufyonzaji wa hewa ya ukaa. Mpango huo ulisaidia nchi kustahiki kwa jumla ya Dola za Marekani bilioni 1.5 katika ufadhili wa misitu unaozalisha matokeo. Juhudi hizo pia zinatarajiwa kupunguza uzalishaji wa gesi ya ukaa kwa zaidi ya milioni tani 100 kati ya sasa na mwaka wa 2026.
Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia, unaoongozwa na UNEP na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), ulionyesha miradi 10 kuu ya juhudi za kuboresha mifumo ya ekolojia. Miradi Mikuu ya Uboreshaji wa Mifumo ya Ekolojia iliangaziwa katika matukio ya habari 1,500 na kupata kutazamwa na watu milioni 70 kwenye mitandao ya kijamii.
Miradi hii inalenga kuboresha kufikia mwaka wa 2030 zaidi ya hekta milioni 60 za ardhi na bahari kama sehemu ya ahadi ya nchi kuboresha hekta bilioni 1, eneo kubwa kuliko Uchina, kufikia mwaka wa 2030.
UNEP iliishauri Brazili kuhusu muundo wa sheria, iliyotiwa sahihi kuwa sheria na Rais Luis Inacio Lula da Silva, ili kukuza kilimo endelevu mijini na pembezoni mwa miji. Hatua hizi kinatarajiwa kufanya chakula bora kupatikana kwa urahisi na kuhifadhi bayoanuai. Ilikuwa sehemu ya mradi wa nchi saba, ambao ulimalizika mwaka wa 2023, ili kupunguza athari kwa mazingira za uzalishaji wa chakula.
UNEP na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) zilisaidia nchi 138 zilipokuwa zinaoanisha sera zake za kitaifa za bayoanuai, malengo na mifumo ya ufuatiliaji na GBF. Hii ni hatua muhimu kwa mafanikio ya makubaliano hayo.
Katika mwezi wa Septemba, UNEP na washirika wake walizindua Mikakati ya Kitaifa ya Bayoanuai na Ushirikiano wa Kuharakisha Mipango ya Utekelezaji, ambayo hutoa usaidizi wa kiufundi ili kuharakisha utekelezaji wa GBF. UNEP pia ilitoa mafunzo kwa maafisa kutoka nchi 50 kutumia zana ya kuripotia data, ambazo husaidia kurahisisha kuripoti kuhusu mikataba inayohusiana na bayoanuai.
Mwezi Juni, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zilipitisha makubaliano ambayo yanaweka msingi wa uhifadhi na matumizi endelevu ya theluthi mbili za bahari nje ya mamlaka ya kitaifa. UNEP ilitoa ushauri wa kitaalamu wakati viongozi walipokuwa wakijadili makubaliano hayo, ambayo ni muhimu katika kutekeleza GBF, haswa lengo lake la kulinda asilimia 30 ya ardhi na bahari kufikia mwaka wa 2030.
Katika maadhimisho yake ya miaka 20, mkataba unaosimamiwa na UNEP wa Carpathian ulipitisha mfumo mpya wa kulinda bayoanuai katika mojawapo ya safu za milima mirefu zaidi barani Ulaya, dhihirisho la juhudi za kikanda za kutekeleza GBF.
Katika mwaka wa 2023, UNEP ililenga kusaidia washiriki wa sekta ya kifedha, pamoja na benki na bima, ili kujumuisha mambo yanayohusiana na bayoanuai katika shughuli zao za biashara. Hii ni muhimu kwa kukusanya mtaji unaohitajika ili kutimiza ahadi ya GBF.
Katika mwezi wa Septemba, Kikosi Kazi cha Ufichuzi wa Fedha zinazohusiana na Mazingira kilitoa mfumo unaoelezea jinsi makampuni yanavyoweza kutathmini na kufichua hatari zinazohusiana na mazingira na kuyategemea. UNEP-FI ilianzisha kikosi kazi hiki kwa pamoja na wakafanyia majaribio toleo la beta la viwango vya ubora na taasisi 50 za fedha katika nchi 25. Nchi za G7 na G20 zilizingatia rasmi mfumo huo, ambao unaunga mkono Lengo la 15 la GBF linalotoa wito kwa mashirika ya biashara kupunguza athari hasi za biashara zao kwa bayoanuai.
UNEP na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa yaliunga mkono Mwongozo wa Kiuchumi wa Kitaifa wa 2023-2045 wa Serikali ya Indonesia. Ulizinduliwa Julai na unaelezea jinsi nchi hiyo inavyoweza kutumia rasilmali zake za bahari kukuza uchumi kwa njia endelevu. Usaidizi wa UNEP ulikuwa chini ya Mpango wa Athari za Juu Unaopelekea Mabadiliko ya Kiuchumi kwa Mazingira, sehemu pana ya juhudi za Umoja wa Mataifa za kuimarisha hatua za SDGs.
Katika mwaka wote wa 2023, UNEP ilisaidia Nchi Wanachama kukabiliana na kuenea kwa majangwa na aina nyinginezo za uharibifu wa ardhi, ambavyo huathiri zaidi ya watu bilioni 3 na ni chanzo kikii cha uharibifu mkubwa wa bayoanuai. UNEP ilisaidia nchi mbalimbali kutekeleza malengo yake chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Majangwa na, kwa ushirikiano na mashirika mengine, ilisaidia nchi zingine kupata fedha za kushughulikia changamoto za aina mbili za kukabiliana na kuenea kwa majangwa na mabadiliko ya tabianchi.
Mfano mahsusi wa kazi za UNEP unapatikana barani Afrika, ambapo shirika hili linafadhili mradi wa Ukuta Mkubwa wa Kijani, unaojumuisha miti na vichaka kwa kilomita 8,000 ambavyo vinasaidia kuzuia kuenea kwa Jangwa la Sahara. Miradi inayoungwa mkono na UNEP katika nchi 11 ilisaidia kuimarisha ushirikiano kupitia ‘ukuta’ huo huku ikitathmini kuenea kwa uharibifu wa ardhi. Hiyo ilikuwa ni sehemu ya juhudi za miaka mingi za kutoa usaidizi wa kiufundi kwa nchi za Ukuta Mkubwa wa Kijani, na kubuni na kutekeleza miradi ya kupunguza ardhi inayokaliwa na majangwa.
Vilevile, UNEP ilitoa msaada kwa nchi za Asia Magharibi zinazokabiliana na dhoruba za mchanga, ambazo zinaweza kuwa chanzo cha majanga na zinatarajiwa kutokea mara kwa mara wakati ambapo mabadiliko ya tabianchi na kuenea kwa majangwa kunapongezeka.
Hatimaye, Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia, ushirikiano kati ya UNEP na FAO, unaangazia umuhimu wa kurejesha maeneo ya nyanda, kuendeleza kilimo kinachojali mazingira na kuboresha hali ya udongo, yote ambayo ni mambo muhimu wakati wa kukabiliana na kuenea kwa majangwa.
Tukiwa na miaka saba tu ya kutekeleza (Mfumo wa Kimataifa wa Bayoanuai) ni lazima sisi wote tuchukue hatua sasa. Na ni lazima tuendelee kuchukua hatua hadi pale ambapo mfumo wetu wa maisha utakapokuwa salama.
UNEP inazisaidia nchi kuachana na kemikali hatari, kudhibiti plastiki zinazotumika mara moja, kufunga mahali wazi pa kutupia takataka, kuboresha hali ya hewa na kukuza uchumi unaotumia bidhaa tena na tena. Kukabiliana na uchafuzi wa mazingira na janga la taka ni muhimu ili kuhakikisha kuna afya njema na ustawi (SDG3), kutoa maji safi na usafi wa mazingira (SDG6), kukuza miji na jamii endelevu (SDG11), kuanzisha mifumo endelevu ya uzalishaji na matumizi ya bidhaa (SDG12), na kulinda maisha chini ya maji (SDG14).
Katika mwezi wa Septemba, ulimwengu ulikubaliana kuhusu Mfumo wa Kimataifa kuhusu Kemikali, mpango wa kihistoria wa kulinda watu na mazingira dhidi ya uchafuzi wa kemikali, unaosababisha vifo takriban milioni 2 kila mwaka. Mkataba huo una malengo 28, ikiwa ni pamoja na wito wa kuchukua hatua dhidi ya matumizi ya dawa hatari za kuua wadudu na kuangamiza kemikali haramu. UNEP itasimamia hazina maalum ya kufadhili mfumo huu. Ujerumani imetoa yuro milioni 20 kwa ufadhili huo, huku Ufaransa, Uholanzi, Uhispania na Uswisi pia zikichangia hazina hiyo.
Mwanzoni mwa mwaka wa 2023, UNEP ilitoa ripoti ya Kukabiliana na vimelea sugu. Ripoti hiyo inayoangalia kwa kina jinsi gani uharibifu wa mazingira unavyochangia kwa ongezeko la vimelea sugu iliangaziwa na vyombo vya habari katika nchi 70. "Lazima lenge letu lisalie kubadilisha hali ya janga hili kupitia uhamasishaji na kwa kuweka jambo hili la umuhimu wa kimataifa katika ajenda ya mataifa duniani,” alisema Waziri Mkuu wa Barbados Mia Amor Mottley, ambaye alizindua ripoti hiyo pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP Inger Andersen.
Kamati ya Majadiliano ya Serikali Mbalimbali kuhusu Uchafuzi wa Plastiki, iliyoandaliwa na UNEP, ilitoa nakala ya rasimu ya chombo cha kimataifa kilicho na uwezo wa kisheria wa kukomesha uchafuzi wa plastiki. Rasimu hii, ambayo inashughulikia mzunguko mzima wa plastiki, ilipitiwa upya wakati wa mazungumzo mjini Nairobi, Kenya mwishoni mwa mwaka kuashiria hatua muhimu kuelekea kukamilisha makubaliano kufikia mwisho wa mwaka wa 2024.
Serikali sita mpya zilitia saini Ahadi Mpya ya Kimataifa ya Uchumi wa Plastiki, inayoongozwa na UNEP na Wakfu wa Ellen MacArthur. Zinajiunga na mataifa 55 na mamia ya mashirika ambayo kwa pamoja yalipunguza matumizi yake ya plastiki inayotumika mara ya kwanza kila mwaka kwa tani milioni 3 tangu mwaka wa 2018. Hii ni zaidi ya matumizi ya kila mwaka ya plastiki kwa ufungaji mizigo nchini Ufaransa. Serikali za Muungano wa Nia Kuu ya Kukomesha Uchafuzi wa Plastiki zimejitolea kukomesha uchafuzi wa plastiki kufikia mwaka wa 2040.
Ushirikiano wa UNEP na Tume ya Mto Mekong ulisababisha kuundwa kwa sheria za mataifa kadhaa za kwanza duniani kufuatilia uchafuzi wa plastiki wa Mto Mekong ya Chini. Inakadiriwa kuwa asilimia 80 ya karibu watu milioni 65 wanaoishi katika Bonde la Mto Mekong ya Chini wanategemea mto huo na malighafi yake kwa maisha yao ya kila siku.
Katika eneo la Karibiani, UNEP iliongoza mradi wa kikanda wa kuzuia nyavu zilizofungwa kwa plastiki na mitego inayosafirishwa wakati wa dhoruba. Juhudi hizi, ambazo ni ushirikiano kati ya Taasisi ya Uvuvi ya Ghuba na Karibiani na Mpango wa Global Ghost Gear, zilihusisha nchi tisa. Ilijumuisha kampeni za kuhamasisha wavuvi na ramani ya AI ya maeneo yenye uchafuzi mkuu wa mazingira.
UNEP ilitumia zana zake za utetezi zenye ushawishi kuangazia masuluhisho kwa uchafuzi wa plastiki. Kaulimbiu ya Siku ya Mazingira Duniani, Juni 5, ilikuwa juu ya uchafuzi wa plastiki. Hafla iliyosimamiwa rasmi na Côte d’Ivoire, Siku hiyo ilivuma sana kwenye mtandao wa X (uliojulikana awali kama Twitter). Maudhui yanayohusiana yaliangaliwa zaidi ya mara milioni 300 kwenye mitandao yote ya kijamii. Serikali kadhaa pia zilitoa ahadi siku hiyo, huku mwenyeji Côte d'Ivoire ikizindua kanuni mpya ya mazingira ya kupambana na uchafuzi wa plastiki. Mabingwa wa Dunia, tuzo la ngazi ya juu zaidi la Umoja wa Mataifa linalotolewa kwa heshima ya mazingira, liliangazia watu binafsi na vikundi vinavyobuni upya uhusiano wa binadamu na plastiki. Matuzo hayo yalikuwa karibu kuongezeka maradufu katika mitandao ya kijamii kuanzia mwaka wa 2022.
UNEP iliongeza juhudi zake za kukabiliana na uchafuzi wa hewa, ambao hupelekea vifo milioni 6.7 kila mwaka na kupandisha gharama za afya zaidi ya asilimia sita ya pato la taifa duniani.
Shirika hili lilisaidia Kazakhstan na Kyrgyzstan, ambako baadhi ya miji ni miongoni mwa miji iliyochafuliwa zaidi katika Asia ya Kati wakati wa kupasha joto msimu wa baridi, kuunda utaratibu wa kuanzisha viwango vya kisasa vya ubora wa hewa. Nchi za Asia Magharibi, kwa msaada kutoka UNEP na Shirika la Afya Duniani, zilikubali kuanzisha mtandao wa kikanda ili kuboresha hewa katika ushirikiano wa kwanza wa kipekee katika kanda hiyo.
Muungano wa Mazingira na Hewa Safi unaosimamiwa na UNEP ulisaidia nchi 50 – zikiwemo Kambodia, Kenya, Pakistani, Nigeria na Thailand - kuendeleza mipango ya kitaifa ya kupunguza uchafuzi wa muda mfupi, kama vile methani na hydrofluorokaboni, ambayo huchangia kwa mabadiliko ya tabianchi na uchafuzi wa hewa.
Hatimaye, Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi ili kuwa na anga za bluu iliyoongozwa na UNEP iliangazia jinsi nchi zinavyoweza kukabiliana na uchafuzi wa hewa. Watu kadhaa mashuhuri walijiunga na wito wa hewa safi, huku Balozi wa Nia Njema, Dia Mirza akisema: “Kupumua kusiwe hatari kamwe.”
Kipindi chote cha mwaka wa 2023, UNEP ilisaidia nchi kupunguza taka. Ripoti ya Pengo la Kutumia Bidhaa Tena na Tena iligundua kwamba nchi za Amerika Kusini na Karibea zinaweza kupunguza kwa asilimia 30 matumizi ya nyenzo na athari za hewa ya ukaa kwa kutekeleza mikakati ya uchumi unaotumia bidhaa tena na tena. Mfumo wa mwaka wa 2050 Taka za Umeme na Kielektroniki huko Asia Magharibi uligundua kuwa kuchakata elektroniki katika kanda kunaweza kurejesha tani 130 za dhahabu, tani milioni 17 za mabati na chuma, na tani 5,000 za metali adimu kufikia mwaka wa 2050. Ripoti hii ilitolewa wakati wa maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Kimataifa ya Kutozalisha Taka Kabisa, yalioongozwa na UNEP na UN-Habitat kwa msaada kutoka Türkiye.
UNEP, kwa usaidizi kutoka kwa GEF, iliongoza miradi kote ulimwenguni kusafisha taka iliyo na madhara, na kusababisha utupaji mwafaka wa tani 216 za taka za elektroniki nchini Nigeria, tani 32 za dawa ya kuulia wadudu ya dichlorodiphenyltrichloroethane (DDT) nchini Ethiopia na tani 211 ya biphenyls poliklorini (PCBs) nchini Kamerun.
UNEP ilisaidia hoteli za kifahari nchini Qatar, Saudi Arabia na Miliki za Falme za nchi za Kiarabu kupunguza taka ya chakula kwa asilimia 65 wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Juhudi hizi zilikuwa sehemu ya 'Recipe for Change' (Recipe ya mabadiliko), kampeni ya kanda nzima ya kupunguza taka ya chakula.
Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki, unaosimamiwa na UNEP, uliadhimisha miaka 10 tangu ulipopitishwa. Wajumbe kutoka nchi 147 waliweka tarehe mpya za kukomesha bidhaa zilizoongezwa zebaki, ikiwa ni pamoja na taa za fluoresenti na vipodozi, katika Kongamano la tano na Nchi Wanachama. Pia walifikia makubaliano juu ya viwango vya taka za zebaki.
Vilevile, UNEP ilisaidia nchi 33 kuandaa mipango ya kitaifa ya kupunguza uchafuzi wa zebaki kwa mazingira kutoka kwa migodi midogo ya dhahabu, chanzo kikuu cha kemikali ya sumu. Kupitia kwa juhudi zinazofadhiliwa na GEF, mataifa 26 yamewasilisha mipango kwa Mkataba wa Minamata. Mpango wa PlanetGold, unaolenga kuboresha shughuli za uzalishaji wa bidha na mazingira ya kazi katika migodi midogo midogo, uliongezeka na kufikia nchi 24, huku migodi iliyoidhinishwa ikiuza dhahabu ya thamani ya dola za Marekani milioni 42 kupitia mpango huo, unaoongozwa na UNEP kwa ufadhili wa GEF.
UNEP iliimarisha msingi wa azimio la Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa kwa kuitisha mara mbili kikundi cha kazi ambacho kinatayarisha mapendekezo ya jopo la sera ya sayansi kuhusu kuzuia kemikali, taka na uchafuzi. Jopo hilo, linalotarajiwa kuanzishwa mwaka wa 2024, litasaidia serikali kufanya maamuzi sahihi juu ya ushughulikiaji mzuri wa kemikali na taka.
Kongamano la nchi wanachama wa Mkataba wa Basel, Rotterdam na Stockholm unaosimamiwa na UNEP lilipitisha maamuzi 54 zaidi ya kupunguza taka yenye madhara, kuondoa vichafuzi vya ogani vinavyosumbua sana na kudhibiti biashara ya kemikali na taka zenye sumu. Mkataba wa Stockholm uliorodhesha vichafuzi vitatu vipya vya ogani ili viondolewe, viwili kwavyo ni vitu vinavyoongezwa kwa plastiki. Mkataba wa Basel ulipitisha miongozo ya kiufundi kuhusu ushughulikiaji wa taka za plastiki kwa kujali mazingira.
Kila mtu kwenye sayari hii anapaswa kuweza kuishi na kufanya kazi bila woga wa kuugua au kufa kutokana na kemikali hatari. Mfumo huu unaashiria maono ya dunia isiyo na madhara ya kemikali na taka, ili kuwa na mustakabali salama, bora na endelevu.
UNEP iliendelea kukuza SDG5 juu ya usawa wa kijinsia, na kuwawezesha wanawake na wasichana kuchukua nafasi za uongozi katika uhifadhi na uboreshaji wa mifumo ya ekolojia kwa kuendeleza Sera na Mikakati ya Jinsia kwa mara ya pili. Matokeo ya awali yanaonyesha kuwa takriban asilimia 90 ya miradi iliyobuniwa katika nusu ya kwanza ya mwaka wa 2023 ilijumuisha jinsia ipasavyo kulingana na kipimo cha kina kinachotumiwa na Umoja wa Mataifa. UNEP ilizindua awamu ya pili ya mradi wa EmPower (WezEsha), ambao unasaidia wanawake nchini Bangladesh, Kambodia na Viet Nam kununua vifaa vya nishati jadidifu kwa kiwango kidogo, kama pampu za maji zinazotumia nishati ya jua. Wanawake 100,000 wanatarajiwa kufaidika na mpango huu. UNEP pia ilitekeleza wajibu muhimu nchini Kenya kwa kutoa mafunzo kwa wanawake wanaojishughulisha na uvuvi endelevu, kukuza kipato chao, na kuchangia katika uhifadhi wa rasilimali za baharini zinazodidimia. Aidha, nchini Rwanda, Togo na Uganda, UNEP na washirika wake walizindua mpango wa kutoa ruzuku kwa waanzilishi wa usafiri unaotumia umeme na kuzingatia zaidi kubuni fursa za ajira kwa wanawake.
Picha: Unsplash/Ashwini Chaudhary
UNEP iliendelea kutumia uwezo wa teknolojia kutoa masuluhisho ili kuendeleza malengo ya mazingira. Kwa ushirikiano na Chuo cha Wafanyakazi cha Umoja wa Mataifa, Muungano wa Uendelevu wa Mazingira Kidijitali na GIZ, UNEP ilizindua mpango wa kujifunza kielektroniki, Digital4Sustainability. Ikihusisha moduli mpya ya tabianchi, jukwaa hili limevutia zaidi ya washiriki 12,000 kutoka serikalini, sekta binafsi, mashirika ya uraia na mashirika ya kimataifa. Mpango wa 10YFP ambao ni mpya unaoongozwa na UNEP wa Uwekaji wa Dijitali na Sekretarieti ili kuwa na uchumi unaotumia bidhaa tena na tena ulisaidia mashirika ya sekta ya umma na ya kibinafsi kutumia teknolojia ya kidijitali. Wakati uo huo, UNEP na washirika wake walitoa Kutafakari, Kupanua, Kutumia Upya: Kutumia Teknolojia za Kidijitali ili Kuwa na Uchumi Unaotumia Bidhaa Tena na Tena, ambayo inaonyesha jinsi bidhaa za pasipoti za kidijitali zinavyoweza kuchangia kushughulikia nyenzo mda wote zinapokuwepo.
Picha: Unsplash/Markus Spiske
Mizozo ilipozidi kuongezeka ulimwenguni, UNEP ilipata njia mpya za kusaidia jamii kudhibiti malighafi na kupunguza uharibifu wa mazingira. Kupitia Mfumo wa Mratibu wa Umoja wa Mataifa, UNEP ilitoa ushauri wa kisayansi katika ngazi ya nchi. Shirika hili liliunga mkono ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, ambapo mabadiliko ya tabianchi yalichochea zaidi migogoro iliokuwepo kwa muda mrefu. Katika eneo la Asia Magharibi, UNEP ilionyesha jinsi jamii zinavyoweza kukabiliana na matukio mabaya ya hali ya hewa, hasa ukame. UNEP inazidi kutumia data ya kutambua kwa mbali na setilaiti kuelewa kuhusu uharibifu wa mazingira unaohusiwhwa na mizozo na kutoa mapendekezo ya sera.
Maoni haya yalichukuliwa kwa makini katika kutathmini kwa haraka hali ya mazingira ya uvunjaji wa Bwawa la Kakhovka la Ukraine mwezi Juni. UNEP pia ilisaidia vikosi vya nchi za Umoja wa Mataifa nchini Syria na Türkiye kupima na kudhibiti kiasi kikubwa cha uchafu uliotokana na tetemeko la ardhi lenye uzito wa 7.8 mwezi wa Februari.
Picha: UNEP/Igor Riabchuk
Hali ya Kifedha ya mwaka wa 2022 na 2023 kufikia Desemba mwaka wa 2023 (Mamilioni ya Dola za Marekani)
Wachangiaji wakuu wa fedha zilizotengewa miradi maalum mwaka wa 2023 (Mamilioni ya Dola za Marekani)*
Ujerumani | 66.6 |
Taasisi za Umoja wa Mataifa | 36.0 |
Umoja wa Ulaya/Tume ya Ulaya | 28.2 |
Mpango wa Fedha wa UNEP** | 26.7 |
Wakfu/NGOs | 24.7 |
Canada | 11.4 |
Japan | 11.4 |
Uingereza ikijumuisha Uingereza Kuu na Ireland Kaskazini | 10.8 |
Marekani | 8.5 |
Uswidi | 7.7 |
Norway | 5.0 |
Ufini | 4.1 |
Ubelgiji | 3.8 |
Austria | 3.5 |
Ufaransa | 2.8 |
Wachangiaji 15 wakuu wa Mfuko wa Mazingira mwaka wa 2023 (Mamilioni ya Dola za Marekani)
Norway | 12.3 |
Uholanzi | 10.2 |
Ujerumani | 8.1 |
Marekani | 7.6 |
Ufaransa | 7.6 |
Denmark | 7.2 |
Uswidi | 5.1 |
Uingereza ikijumuisha Uingereza Kuu na Ireland Kaskazini | 4.5 |
Ubelgiji | 4.2 |
Uswisi | 4.0 |
Canada | 2.8 |
Italia | 2.6 |
Ufini | 2.3 |
Uhispania | 1.6 |
Japan | 1.5 |
- Albania
- Armenia
- Barbados
- Ubelgiji
- Bosnia na Herzegovina
- Bulgaria
- Canada
- Cyprus
- Denmark
- Jamhuri ya Dominika
- Eritrea
- Fiji
- Ufaransa
- Georgia
- Guinea
- Guyana
- Iceland
- Ireland
- Jamaica
- Jordan
- Kenya
- Latvia
- Liechtenstein
- Lithuania
- Luxembourg
- Maldives
- Malta
- Mauritius
- Micronesia (Shirikisho la Mataifa ya)
- Monaco
- Montenegro
- Moroko
- Uholanzi
- New Zealand
- Norway
- Panama
- Peru
- Saint Lucia
- Serbia
- Ushelisheli
- Slovenia
- Sri Lanka
- Uswidi
- Uswisi
- Tajikistan
- Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
- Uingereza ikijumuisha Uingereza Kuu na Ireland Kaskazini
- Uruguay
- Andorra
- Australia
- Austria
- Chile
- Uchina
- Costa Rica
- Croatia
- Ufini
- Ujerumani
- Honduras
- Hungari
- India
- Indonesia
- Iraq
- Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
- Italia
- Japan
- Kazakhstan
- Kuwait
- Malaysia
- Meksiko
- Paraguay
- Ufilipino
- Ureno
- Jamhuri ya Korea
- Singapore
- Slovakia
- Afrika Kusini
- Uhispania
- Thailand
- Trinidad na Tobago
- Marekani
UNEP ingependa kushukuru Nchi Wanachama na washirika wengine wafadhili kwa michango yao katika mwaka wa 2023. Msaada huu wa kifedha ni muhimu katika kusaidia UNEP kutekeleza wajibu wake wa kukabiliana na changamoto za aina tatu duniani na kukuza mustakabali endelevu zaidi kwa wote.