Kupitia njia nyingi, 2022 ulikuwa mwaka wa juhudi mpya za kushughulikia mazingira. Kuelekea mwanzoni mwa mwaka, katika Kikao cha Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa, Nchi Wanachama zilipitisha maazimio ya kihistoria ya kuimarisha juhudi za kukabiliana na uchafuzi, kupunguza na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kutunza na kuboresha mazingira kote ulimwenguni. Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka wa 2022 ulichangia historia kupitia kuanzishwa kwa mfuko wa hasara na uharibifu. Majadiliano ya kimataifa ya kukomesha uchafuzi wa plastiki yalianza nchini Uruguay. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitambua haki ya watu wote kuwa na mazingira safi, bora na endelevu. Na mwaka ulipoisha, Kongamano la Umoja wa Mataifa la Bayoanuai mjini Montreal lilipelekea kupitishwa kwa mfumo kabambe wa kutunza na kuboresha bayoanuai kufikia mwaka wa 2030. Mwaka huu pia ulishuhudua maadhimisho ya miaka 50 ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na kongamano la Stockholm+50.
Hata hivyo ulikuwa pia mwaka wa changamoto nyingi. Madhara makubwa ya changamoto za aina tatu duniani za mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira na bayoanuai, na uchafuzi na taka vilichangiwa na kuongezeka kutokana na ukosefu wa usawa, vita nchini Ukraine na kupanda kwa bei ya chakula na ya nishati. Kama kawaida, maskini na walio hatarini zaidi waliathiriwa zaidi na ukame, mafuriko, mioto misituni, kupungua kwa bayoanuai na kuongezeka kwa viwango vya uchafuzi.
Kama ripoti hii inavyoonyesha, shirika lilianza kutekeleza mkakati wake mpya, mkatati wa 2022-2025. Lilipata ushindi kwa kukabiliana na changamoto za aina tatu kwa sayari na kusaidia dunia kuanza kutekeleza ahadi zake za kuboresha mifumo ya ekolojia, kupunguza shinikizo la uchafuzi wa hewa na kulinda mamilioni ya watu katika mataifa yanayoendelea walio hatarini kuathiriwa na hali ya hewa.
Basi, haishangazi kwamba mahitaji ya kuchukuliwa kwa hatua badala ya kutoa ahadi tu yanazidi kuongezeka. UNEP iliimarisha juhudi za kukabiliana na majanga haya na kuanza kutekeleza mkakati wake, mkakati wa 2022-2025. Kwa kuzingatia uwezo wa wabia wake, UNEP ilifanya kazi na Nchi Wanachama kutimiza ahadi za kupunguza na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kutunza na kuboresha mifumo ya ekolojia, na kupunguza shinikizo la uchafuzi. Kupitia haya yote, UNEP inaendelea kuunga mkono nchi kutekeleza azimio la 4/17 la Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa kwa kujumuisha usawa wa kijinsia na haki za binadamu katika sera, mikakati, programu na miradi ya mazingira, hata inapoendelea kufanyia marekebisho mfumo wake wa kijinsia ili kutimiza kazi yake vyema.
Kama shirika, UNEP imejitolea kuwa shirika sikivu na linalojali. UNEP ilibadilisha mfumo wake wa kushirikiana na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa kupitia Vikosi vya Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa ili kushughulikia vyema vipaumbele vya Nchi Wanachama na Malengo ya Maendeleo Endelevu, na kuunda mifuko mipya tatu ya fedha inayotoa ufadhili unaoweza kubadilika ili kuwa na mazingira thabiti, kuishi kwa amani na mazingira na kutochafua sayari. UNEP pia ilifikia usawa wa kijinsia katika viwango vyote vya kitaaluma na ngazi za juu na kuboresha uanuai ya kijiografia wa wafanyikazi wake.
Lakini kazi kubwa iliyo mbele yetu ni kupunguza changamoto za aina tatu duniani. Kama mamlaka kuu ya kimataifa ya mazingira, UNEP itatoa shinikizo zaidi na kushirikiana kwa karibu zaidi na nchi, mfumo wa Umoja wa Mataifa, mashirika ya uraia na sekta binafsi ili kutoa masuluhisho na kufanya kazi ili kuwa na ulimwengu ambapo watu wote, popote walipo, wanaweza kufurahia haki yao kuwa na mazingira bora.