- Tuzo la Mabingwa wa Dunia hutuza watu binafsi, makundi na mashirika ambayo huchukua hatua za kusababisha mabadiliko chanya kwa mazingira.
- Mwaka huuupendekezaji wa watu binafsi na mashirika ambayo yamesaidia kuzuia, kukomesha na kukabiliana na uharibifu wa mifumo ya ekolojia haswa wanahimizwa kushiriki.
- Upendekezaji utaanza tarehe 15 Machi hadi tarehe 11 Aprili mwaka wa 2022.
Nairobi, Machi 15 2022 – Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) leo limezindua wito wa kupendekeza watakaowania tuzo lake la Mabingwa wa Dunia linalotolewa kila mwaka – tuzo la Umoja wa Mataifa la ngazi ya juu linalotolewa kwa heshima ya mazingira ili kujivunia viongozi wa kipekee kutoka kwa serikali, mashirika ya uraia na sekta binafsi kwa mchango wao chanya kwa mazingira.
Ili kuonyesha umuhimu wa kuboresha mifumo ya ekolojia, wito wa mwaka wa 2022 unahimiza upendekezaji wawatu na mashirika ambayo yamechangia kuzuia, kukomesha na kukabiliana na uharibifu wa mifumo ya ekolojia kote duniani. Takribani mwaka mmoja tangu kuzinduliwa kwa Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia, hakujawahi kuwa na hitaji la kukabiliana na uharibifu wa mifumo ya ekolojia kuliko sasa. Mifumo yetu ya ekolojia ikiwa dhabiti, watu na sayari vitanawiri.
Tangu kuzinduliwa kwake katika mwaka wa 2005, tuzo hili limemulika viongozi ambao wamejitolea kufanya kazi kuhakikisha kuna sayari endelevu isiyobagua. Jumla ya washindi 106, kuanzia kwa wakuu wa nchi na wanaharakati katika jamii hadi kwa vinara wa viwanda na wanasayansi waanzilishi, wametuzwa kama Mabingwa wa Dunia
Katika mwaka wa 2021, Tuzo la Mabingwa wa Dunia lilishuhudia tena kiwango kikubwa cha watu waliopendekezwa kutoka pembe zote za dunia. Kuongezeka kwa wanaowania kwa kipindi cha miaka iliyopita kunaonyesha kuongezeka kwa idadi ya watu wanajitolea kupigania mazingira na kutambua mno umuhimu wa kazi yao.
Washindi wa UNEP wa mwaka wa 2021 wa Tuzo la Mabingwa wa Dunia walikuwa:
- The Sea Women of Melanesia (Papua na Visiwa vya Solomoni), wanaotuzwa katika kitengo cha Uongozi Unaozingatia Sera, hutoa mafunzo kwa wanawake kutoka eneo hilo kufuatilia na kutathmini athari za uchujukaji wa matumbawe kwenye baadhi ya miamba ya matumbawe iliyo hatarini kuangamia kwa kutumia sayansi na teknolojia ya baharini.
- Maria Kolesnikova (Jamhuri ya Kyrgyz), aliyetuzwa katika kitengo cha Maono ya Ujasiriamali, ni mwanaharakati wa mazingira, mtetezi wa vijana na msimamizi wa MoveGreen, shirika linalofanya kazi kufuatilia na kuboresha hewa katika eneo la Asia ya kati.
- Dkt. Gladys Kalema-Zikusoka (Uganda), aliyetuzwa katika kitengo cha Sayansi na Ubunifu, alikuwa daktari wa mifugo wa kwanza kabisa wa Mamlaka ya Wanyamapori nchini Uganda, na ni mamlaka inayotambulika duniani inayoshughulikia wanyama wa familia ya nyani na magonjwa kutoka kwa wanyama.
Watu binafsi, mashirika ya serikali, makundi na mashirika yanaweza kuteuliwa chini ya vitengo vya Uongozi Unaozingatia Sera, Kujitolea na Kuchukua Hatua, Maono ya Ujasiriamali na Sayansi na Ubunifu. Yeyote anaweza kutoa mapendekezo. Tarehe ya mwisho ya kutuma mapendekezo ni Aprili 11, 2022.
MAKALA KWA WAHARIRI
Kuhusu Tuzo la UNEP la Mabingwa wa Dunia
Tuzo la UNEP la Mabingwa wa Dunia hutuza watu binafsi, makundi na mashirika ambayo huchukua hatua za kusababisha mabadiliko chanya kwa mazingira. Tuzo linalotolewa mara moja kwa mwaka la Mabingwa wa Dunia ni tuzo la umoja wa mataifa la ngazi ya juu linalotolewa kwa heshima ya mazingira. Hutuzwa kwa viongozi wa kipekee kutoka kwa serikali, mashirika ya uraia na sekta binafsi.
Kuhusu Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia
Baraza la Umoja wa Mataifa limetangaza kuanzia mwaka wa 2021 hadi mwaka wa 2030 kuwa Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia. Muongo unaongozwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) la Umoja wa Mataifa na msaada kutoka kwa wabia ulibuniwa kuzuia, kukomesha na kukabiliana na uharibifu wa mifumo ya ekolojia kote ulimwenguni. Unalenga kuboresha mabililioni ya hekta za aridhi ya nchi kavu pamoja na mifumo ya ekolojia ya majini. Mwito kwa jamii ya kimatifa, Muongo wa UN huleta pamoja wanasiasa, watafiti wa kisayansi, na wabia ili kuimarisha uboreshaji.
Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)
UNEP ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira duniani. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.
UNEP@50: Ni wakati wa kutafakari kuhusu yaliyopita na kutazamia yajayo
Kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira ya Binadamu mjini Stockholm, Uswidi katika mwaka wa 1972, lilikuwa kongamano la kwanza la Umoja wa Mataifa kutumia neno "mazingira" kwenye anwani yake kwa mara ya kwanza. Kuanzishwa kwa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) ni mojawapo wa matokeo makuu ya kongamano hili lililoanzisha mambo mengi. UNEP ilianzishwa kuwa kitengo cha kushughulikia mazingira cha Umoja wa mataifa kote ulimwenguni. Shughuli zinazoendelea katika mwaka wa 2022 zitaangazia hatua kubwa zilizopigwa na yanayojiri katika miongo ijayo.
Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:
Keishamaza Rukikaire, Mkuu wa Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa MataifaMoses Osani, Afisa wa Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa