22 Nov 2022

Tuzo la Umoja wa Mataifa la Ngazi ya Juu zaidi Linawatuza Waboreshaji wa Mifumo ya EkolojiaShirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) leo lilitangaza washindi wake wa mwaka wa 2022 wa Tuzo la Mabingwa wa Dunia. Linawatuza mhifadhi wa Mazingira, shiri

Nairobi, Novemba22, 2022 – Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) leo lilitangaza washindi wake wa mwaka wa 2022 wa Tuzo la Mabingwa wa Dunia. Linawatuza mhifadhi wa Mazingira, shirika, mwanauchumi, mwanaharakati wa haki za wanawake, na mwanabiolojia wa wanyamapori kwa hatua zao za kuleta mabadiliko chanya ya kuzuia, kusitisha na kukabiliana na uharibifu wa mifumo ya ekolojia.   

Tangu kuzinduliwa kwake katika mwaka wa 2005,  tuzo la Mabingwa wa Dunia linalotolewa kila mwaka, limetolewa kwa watu walio msitari mbele kufanya juhudi za kuhifadhi ulimwengu asilia. Ni tuzo la Umoja wa Mataifa la ngazi ya juu zaidi linalotolewa kwa heshima ya mazingira. Kufikia sasa,  limewatuza washindi 111: viongozi wa dunia 26, watu binafsi 69 na mashirika 16. Mwaka huu, idadi ya watu 2,200 walipendekezwa kushiriki kutoka pembe zote za dunia.

"Mifumo dhabiti ya ekolojia, inayofanya kazi ni muhimu ili kuzuia dharura ya tabianchi na kuzuia uharibifu wa bayoanuai kusababisha uharibifu usioweza kurekebika kwa sayari yetu. Mabingwa wa Dunia wa mwaka huu wanatupa matumaini kwamba uhusiano wetu na mazingira unaweza kuboreshwa,” alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP. "Mabingwa wa mwaka huu wanaonyesha jinsi kuboresha mifumo ya ekolojia na kuimarisha uwezo wa kipekee wa mazingira wa kujiimarisha ni wajibu wa kila mtu: serikali, sekta ya kibinafsi, wanasayansi, jamii, NGOs na watu binafsi."

Mabingwa wa Dunia wa Mwaka wa 2022 ni:

  • Arcenciel (Lebanon), kampuni inayotuzwa katika kitengo cha Motisha na Kuchukua Hatua, ni shirika linalokuza mazingira safi na bora na kuchangia msingi wa kuwekwa kwa mkakati wa kitaifa wa kushughulikia taka nchini Lebanon. Kwa sasa, arcenciel huchakata zaidi ya asilimia 80 ya taka za hospitali zinazoweza kuambukiza magonjwa nchini Lebanon kila mwaka.
  • Constantino (Tino) Aucca Chutas (Peru), ambaye pia ametuzwa katika kitengo cha Motisha na Kuchukua Hatua, ameanzisha mfumo wa upandaji miti katika jamii unaoendeshwa na wenyeji na jamii za kiasili. Hali ambayo imepelekea miti milioni tatu kupandwa nchini Peru.  Pia anaongoza juhudi kabambe za upandaji miti katika nchi zingine za eneo la Andes.
  • Hababi (Sir) Partha Dasgupta (Uingereza), anayetuzwa katika kitengo cha Sayansi na Ubunifu, ni mwanauchumi mashuhuri ambaye ukaguzi wake wa kipekee kuhusu uchumi wa bayoanuai unatoa wito kutafakari upya mno kuhusu uhusiano wa binadamu na mazingira asilia ili kuzuia mifumo muhimu ya ekolojia kuporomoka.
  • Dkt Purnima Devi Barman (India), anayetuzwa katika kitengo cha Maono ya Ujasiriamali, ni mwanabiolojia wa wanyamapori anayeongoza "Jeshi la Hargila", vuguvugu la wanawake pekee la uhifadhi mashinani linalojitolea kulinda Korongo aina ya Greater Adjutant Stork dhidi ya kuangamia.  Wanawake hawa hutengeneza na kuuza nguo zilizo na michoro ya ndege hao, na kusaidia kuhamasisha kuhusu spishi hii huku wakiweza kujitegemea kifedha.
  • Cécile Bibiane Ndjebet (Kameruni), anayetuzwa katika kitengo cha Motisha na Kuchukua Hatua, ni mtetezi asiyechoka wa haki za wanawake za kumiliki ardhi barani Afrika, hali inayohitajika kuwawezesha kutekeleza wajibu muhimu wa koboresha mifumo ya ekolojia, kupambana na umaskini na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.  Pia anaongoza juhudi za kushawishi kuwepo na sera kuhusu usawa wa kijinsia katika usimamizi wa misitu katika nchi 20 barani Afrika.

Kufuatia uzinduzi wa Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia (2021-2030), matuzo ya mwaka huu yanaangazia juhudi za kuzuia, kusitisha na kukabiliana na uharibifu wa mifumo ya ekolojia kote duniani.

Mifumo ya ekolojia katika kila bara na katika kila bahari inakabiliwa na vitisho vikuu. Kila mwaka sayari hupoteza maeneo ya misitu kiasi sawa na taifa la Ureno. Samaki huvuliwa baharini kupita kiasi na bahari kuchafuliwa, huku tani milioni 11 za plastiki pekee zikielekea katika mazingira ya baharini kila mwaka. Spishi milioni moja ziko katika hatari ya kutoweka kwani makazi yao yanapotea au kuchafuliwa.

Uboreshaji wa mifumo ya ekolojia ni muhimu ili kudhibiti ongezeko la joto duniani lisizidi nyuzijoto 2 na kuweza kusaidia jamii na uchumi kukabiliana na mabadiliko yatabianchi. Pia ni muhimu ili kukabiliana na baa la njaa: uboreshaji kupitia kilimo cha misitu pekee una uwezo wa kuongeza utoshelezaji wa chakula kwa watu bilioni 1.3. Kurejesha tu asilimia 15 ya ardhi ambayo matumizi yamebadilishwa kunaweza kupunguza hatari ya kutoweka kwa spishi kwa asilimia 60. Uboreshaji wa mifumo ya ekolojia utafaulu tu ikiwa kila mtu atajiunga na vuguvugu la #GenerationRestoration.

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)

UNEP ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira duniani. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.

Kuhusu  Tuzo la UNEP la Mabingwa wa Dunia

Tuzo la Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa la Mabingwa wa Dunia hutuza watu binafsi, makundi na mashirika ambayo huchukua hatua za kusababisha mabadiliko chanya kwa mazingira. Tuzo linalotolewa mara moja kwa mwaka la Mabingwa wa Dunia ni tuzo la umoja wa mataifa la ngazi ya juu linalotolewa kwa heshima ya mazingira. Hutuzwa kwa viongozi wa kipekee kutoka kwa serikali, mashirika ya uraia na sekta binafsi.      

Kuhusu Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia 

Baraza la Umoja wa Mataifa lilitangaza kuanzia mwaka wa 2021 hadi mwaka wa 2030 kuwa  Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia. Muongo unaongozwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, pamoja na msaada kutoka kwa wabia lilibuniwa kuzuia, kukomesha na kukabiliana na uharibifu wa mifumo ya ekolojia kote ulimwenguni. Unalenga kuboresha mabililioni ya hekta za aridhi ya nchi kavu pamoja na mifumo ya ekolojia ya majini. Mwito kwa jamii ya kimatifa, Muongo wa UN huungwa mkono na wanasiasa, utafiti wa kisayansi, na ufadhili ili kuimarisha uboreshaji.  

 Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Keishamaza Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa

 

Дополнительная информация