Nairobi, Mei 12, 2020 – Shirika la Mazingira Duniani (UNEP) linaimarisha juhudi zake za kukabiliana na magonjwa yanayotokana na wanyama na kutunza mazingira ili kupunguza uwezekano wa maradhi yanayoenea kutokea katika siku zijazo. Maradhi hayo ni kama vile janga la virusi vya COVID-19 vinavyoendelea kuenea kote ulimwenguni.
Kupitia toleo la leo ‘Kushirikiana na Mazingira ili Kulinda Binadamu’ UNEP inaonyesha jinsi ambavyo inafanyia marekebisho utendakazi wake ili kukabiliana na virusi vya COVID-19 kwa kusaidia mataifa na wabia "kujiimarisha" - kupitia sayansi iliyoimarika, utungaji wa sera zinazosaidia kutunza sayari na kuwekeza kwa makampuni yasiyochafua mazingira.
Kwa sasa UNEP inajishughulisha na vitu vinne kukabiliana na hali iliopo: kusaidia mataifa kukabiliana na taka inayotokana na janga la COVID-19, kuleta mageuzi yatakayonufaisha mazingira na watu, kufanya juhudi za kuimarisha uchumi ili uweze kustahimili iwapo majanga yatatokea, na kushughulikia mazingira kwa njia za kisasa kote ulimwenguni.
"Kupitia COVID-19, dunia imefaulu kutupa onyo kuu kuwa ni sharti mienendo ya binadamu ibadilike,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP Inger Andersen. "Kusitisha shughuli za kibiashara ili kushughulikia onyo hili ni kwa kupindi kifupi tu. Hali hii haiwezi kudumu. Wafanyabiashara wanaojali mazingira ni muhimu katika ukuzaji wa uchumi wa mataifa."
Ili kusaidia mataifa katika juhudi zao za kushughulikia athari zinazotokana na COVID-19 kwa jamii, kwa uchumi na kwa mazingira, UNEP itafanya kazi kwa ushirikiano na taasisi nyingine za Umoja wa Mataifa. Mifano ya baadhi ya mambo yatakayofanywa ni:
- Kusaidia watunza sera kukabiliana na taka hatari - kama vile vifaa vya kujilinda, vifaa vya elektroniki na vifaa kutoka kwa makampuni ya dawa - bila kusababisha madhara zaidi kwa binadamu au kwa mazingira.
- Programu ya kukabiliana na magonjwa yanayotokana na wanyamapori inalenga kuboresha uwezo wa nchi kukabiliana na majanga bila kudhuru mazingira. Hii ni pamoja na juhudi mpya za kimataifa za kupunguza madhara yanayotokana na kutokuwepo na sheria dhidi ya bidhaa zinazotokana na wanyamapori, unyakuzi wa maeneo ya makazi na uharibifu wa bayoanuai.
- Kuimarisha uwezo wa kuwekeza kwa mazingira na maendeleo ya kudumu kama njia mojawapo ya kukabiliana janga la COVID-19 - ikijumuisha kupitia kwa Mifuko iliopo inayosimamiwa na UNEP na miradi ya kukuza na kuimarisha uchumi inayoandaliwa na nchi.
- Kufikia watu wanaohusika na ujenzi wa uchumi ili kukuza na kuimarisha uzalishaji na matumizi ya bidhaa kwa njia endelevu na kubuni nafasi mpya za ajira isiyochafua mazingira. Hii ni pamoja na kuyafikia mashirika ya biashara kupitia ubia na Taasisi za Umoja wa Mataifa, Mashirika ya Fedha, serikali na Taasisi za Sekta ya binafsi na kuimarisha masoko na mifumo ya usambasaji ili kuzalisha bila kuchafua mazingira na kuunda bidhaa za kudumu.
- Kutafakari kuhusu athari za kuamishia ushughulikiaji wa mazingira na shughuli za mashirika ya kimataifa mtandaoni na hivyo, kupunguza athari kwa mazingira na kubuni majukwaa ya kufanyia mikutano.
“Ukweli kuwa dunia asilia iliyo dhabiti ni muhimu kwa afya ya binadamu, kwa jamii na kwa uchumi ndiyo nguzo ya kazi ya UNEP," alisema Andersen. " Lakini sasa, UNEP ni sharti itoe usaidizi zaidi kwa nchi zinapopunguza uwezekano wa majanga zaidi kutokea baadaye kwa kumairisha mifumo ya ekolojia na bayoanuai iliyoharibika, kwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kupunguza uchafuzi.”
MAKALA KWA WAHARIRI
Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)
UNEP ni mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.
Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:
Keishamaza Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, UNEP, +254722677747