Amy Bowers Cordalis - Inspiration and Action

Wakili na mwanachama wa Kabila la Kiasili la Yurok mjini California

Wakili na mwanachama wa Kabila la Asili ya Yurok la California, Amy Bowers Cordalis ametumia miongo kadhaa kujitahidi kurejesha mtiririko wa kiasili wa Mto Klamath nchini Marekani.

Mto Klamath, unaopitia katika majimbo ya Oregon na California, hapo awali ulikuwa mkondo wa tatu kwa ukubwa uliozalisha samoni katika Marekani Magharibi. Lakini mabwawa manne ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji - yaliyojengwa kati ya mwaka wa 1911 na mwaka wa 1962 - yalizuia mtiririko wa mto, na kupunguza idadi ya samoni katika eneo hili. Samaki ni spishi muhimu na ni muhimu kwa njia ya maisha ya watu wa Yurok.

Katika mwezi wa Oktoba, hata hivyo, Cordalis na Yurok walisherehekea wakati wafanyakazi walipobomoa bwawa la mwisho kati ya mabwawa manne ya mto Klamath. Ubomoaji huo ulitokana na matokeo ya tetemeko la ardhi ya mwaka wa 2022 ambapo taasisi za serikali za utungaji na utekelezaji wa sheria ziliangazia uondoaji wa mabwawa na uboreshaji wa mto.

Uamuzi huo uliashiria kilele cha miongo kadhaa ya kupigania Yurok, maandamano na hatua za kisheria. Cordalis alitekeleza wajibu muhimu katika juhudi hizi. Aliongoza rufaa kwa watungasheria na kusaidia kufikia makubaliano baada ya mazungumzo na California, Oregon na mmiliki wa mabwawa ambayo yalisababisha kuondolewa kwake.

"Nilidhani tulikuwa tunaenda kuwa kizazi ambacho kilishuhudia kuangamia na kukauka kabisa kwa mto huu," anasema. "Lakini sasa tutakuwa kizazi kinachoshuhudia kuzaliwa upya na kuboreshwa kwa mfumo wetu wa ekolojia, utamaduni wetu na uhai wetu."

Kutokana na kujitolea kwake kushughulikia haki za Watu wa Kiasili na utunzaji wa mazingira, Cordalis ametajwa kuwa Bingwa wa Dunia wa mwaka wa 2024– tuzo la Umoja wa Mataifa la ngazi ya juu zaidi - katika kitengo cha Motisha na Kuchukua Hatua. Ni mojawapo wa washindi sita katika kundi la mwaka wa 2024.

“Watu wa Kiasili wako mstari wa mbele katika uhifadhi wa mazingira wa kimataifa. Kuwajengea uwezo kunaweza kusaidia kukuza mifumo ya ekolojia yenye afya kwa manufaa ya wote,” anasema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)

"Uanaharakati wa Amy Bowers Cordalis na uhamasishaji wake wa jamii umesababisha ushindi madhubuti wa kuwa na mfumo wa ekolojia wenye afya na utunzaji wa mazingira. Hii inaweza kuwatia moyo wanaharakati na watetezi wa haki za Watu wa Kiasili kila mahali.”

Mito iliyo hatarini

Mito ni mishipa ya maisha ya binadamu, wanyamapori na mifumo ya ekolojia. Zaidi ya spishi 140,000 hutegemea makazi ya maji safi, mito na maziwa, kuwepo.

Bado mito michache ulimwenguni imesalia katika hali yake ya kiasili, inayotiririka vizuri, na inazidi kutishiwa na mambo mengi, ikiwa ni pamoja na uchafuzi, ubadilishaji wa matumizi ya ardhi na mabadiliko ya tabianchi. Mtiririko wa mito umepungua katika mabonde 402 duniani, ongezeko la mara tano zaidi tangu mwaka wa 2000, kulingana na data ya UNEP.

Watu wachache wanaelewa hili vyema zaidi kuliko Cordalis na mwenzake Yurok, ambao ni kabila kubwa zaidi la Watu wa Kiasili nchini Marekani mjini California, walio na zaidi ya watu 5,000, kulingana na kabila hilo.

Wanaojulikana kama "watu wa samoni", Yurok kihistoria walikuwa wanategemea samaki kama chanzo cha riziki na nguzo ya utamaduni wao. Lakini mabwawa kwenye Mto Klamath yamesababisha kuzuka kwa msimu wa maua ya mwani yalio na sumu, ambayo hubadilisha hali ya joto na kupelekea magonjwa, na kupunguza ubora wa maji, wanasema maafisa wa California. Ongezeko la idadi ya watu na makazi yao yameongeza shinikizo kwa mto huu.

Katika mwaka wa 2002, serikali ya shirikisho ilidadilisha mkondo wa maji kutoka Mto Klamath kwa ajili ya kilimo, na kusababisha mtiririko mdogo wa mto. Hii ilihatarisha angalau maisha ya samoni 34,000 wazima.

"Ilikuwa kama kushuhudia familia yako yote ikiuawa mbele ya macho yako," Cordalis anakumbuka. "Ilikuwa aina ya uharibifu wa mazingira kimakusudi."

Kuchanganya utamaduni, sayansi na sheria

Kifo cha samaki kiliwatia kiwewe lakini pia kiliwatia nguvu watu wa Yurok, ambao waliimarisha harakati zao za kuondoa mabwawa, wakishirikiana na jamii nyingine, wanasayansi, wavuvi wa samaki za biashara na makundi ya mazingira.

Kwa Cordalis, ilikuwa wakati mahususi ambao ulimtia moyo kujiunga na shule ya sheria na baadaye kuwa mwanasheria mkuu wa Kabila la Yurok.

Alipochukua wajibu huo katika mwaka wa 2016, Mto Klamath ulikuwa na mojawapo ya samoni wachache kuwahi kurekodiwa, na kulazimisha Yurok kufunga uvuvi wake wa samaki wa biashara. Kwa kuchochewa na urithi wa mjomba wake - ushindi wake wa Mahakama ya Juu katika mwaka wa 1973 ulithibitisha haki ya ardhi na uhuru wa Kabila la Yurok - Cordalis alizindua mfululizo wa hatua za kisheria ambazo zimesaidia kuendeleza idadi ya samoni.

Katika mwaka wa 2020, aliunda shirika lisilo la biashara la Ridges to Riffles ili kutoa utetezi na usaidizi wa sera kwa jamii za Kiasili kulinda na kuboresha malighafi zao.

"Tunatumia maarifa yetu ya jadi na kuyaunga mkono na sayansi na sheria ili kuzungumza lugha ya uboreshaji wa kisasa wa ardhi," Cordalis anaelezea.

Kuirejesha na Kuiboresha

Ushindi wa kisheria wa Yurok mwaka wa 2022 ulisababisha kile kinachojulikana kama mradi mkubwa zaidi wa kuondoa bwawa na kurejesha mito nchini Marekani.

Wakati mapambano ya miongo kadhaa ya kuondoa mabwawa yamekamilika, kazi ya Cordalis bado haijakamilika. Mpango wa Yurok wa kurejesha na kupanda mimea kwa angalau hekta 900 za ardhi iliyozama hapo awali, kurudisha eneo hili chini ya umiliki wa kabila, kuboresha makazi ya majini na nchi kavu kwa manufaa ya samaki na wanyamapori, kuboresha mtiririko wa maji, na kuongeza idadi ya samoni.

Samoni wamerejea kwa zaidi ya kilomita 640 za mto uliofunguliwa tena karibu na mpaka wa California na Oregon, unavyoripoti Utawala wa Kitaifa wa Bahari ni Masuala ya Anga. Wahifadhi wa mazingira wameshuhudia samoni wa Chinook wakihamia kwa makazi ambayo hayakuweza kufikiwa juu ya eneo la mojawapo ya mabwawa manne yaliyobomolewa, kulingana na ripoti za vyombo vya habari. Ndani ya miongo minne, idadi yao katika Mto Klamath inaweza kuongezeka kwa wastani wa takriban asilimia 81, kulingana na serikali ya shirikisho ya Marekani.

Kuondolewa kwa mabwawa ya Klamath ni sehemu ya vuguvugu la kimataifa la kuboresha mito na kuboresha ustahimilivu kwa tabianchi. Nchi kadhaa, kwa mfano, ziliahidi mwaka jana kuuisha kilomita 300,000 za mito iliyoharibiwa chini ya Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia. Inatosha kuzunguka Dunia mara saba.

"Ikiwa tunaweza kufanya hivyo kwa Mto Klamath, tunaweza kufanya hivyo kote ulimwenguni," Cordalis anasema. "Maono yangu ni kwamba maji yatakuwa safi na mengi, na kwamba kutakuwa na samaki wakubwa, wenye afya na wanaong'aa mtoni."

Ikiwa tunaweza kufanya hivyo kwa Mto Klamath, tunaweza kufanya hivyo kote ulimwenguni. Maono yangu ni kwamba maji yatakuwa safi na mengi, na kwamba kutakuwa na samaki wakubwa, wenye afya na wanaong'aa mtoni.

Habari na Matukio