Kisa cha SEKEM kinaanzia jangwani nchini Misri na hema, trekta na piano.
Katika mwaka wa 1977, mwanzilishi wa shirika hili la maendeleo, Ibrahim Abouleish, alirudi nchini Misri baada ya miaka 20 ya kufanya kazi nje ya nchi katika kemia na famakolojia.
Wakati huo, Misri ilikuwa inakabiliwa na mtanziko. Ilihitaji kulisha idadi ya watu inayoongezeka kwa kasi, lakini sekta yake ya kilimo ilikuwa duni, mashamba yalikuwa yakigeuka na kuwa majangwa, na matumizi ya kupita kiasi ya dawa za kuua wadudu na mbolea za kemikali yalikuwa yakidhuru udongo.
Kwa hivyo, kwenye eneo ambalo halikuwa limewahi kuguswa la jangwa la kaskazini-mashariki mwa Cairo, Abouleish alisimamisha hema na kuanzisha SEKEM. Shirika lililopewa jina la hieroglifu ya "uhai wa jua ”, shirika hili baadaye likawa kitovu cha kilimo cha bayodinamiki, aina ya kilimo hai kinachosisitiza amani kati ya mazingira, maendeleo ya binadamu na imani ya kidini.
Vitega uchumi viwili vya kwanza vya Abouleish vilikuwa trekta na - kifaa kilichowashangaza wakulima wadogo wa eneo hilo - piano.
Mwanawe, Helmy, afisa mkuu mtendaji wa SEKEM kwa sasa, anasema piano iliashiria umuhimu wa "mihimuko na hisia" kwa kuunganisha binadamu na mazingira. Wawili hao waliongoza SEKEM pamoja hadi kifo cha Ibrahim katika mwaka wa 2017.
"Kwa baba yangu, kila mara ilikuwa ni kukuza uhusiano na jangwa ambapo, bila ya chochote, unakuza viumbe," Helmy Abouleish anasema huku akitabasamu wakati wa mahojiano na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP).
Sasa, miaka 47 baada ya kuanzishwa kwake, SEKEM imekua na kuwa shirika la maendeleo lililo na nyanja nyingi ambalo linasaidia kukabiliana na kuenea kwa majangwa, kukuza mifumo thabiti ya chakula, kukabiliana na umaskini na kushughulikia janga la mabadiliko ya tabianchi. Mwishoni mwa mwaka, SEKEM inasema kuwa itakuwa imesaidia wakulima 15,000 kukumbatia kilimo cha bayodinamiki tangu mwaka wa 2022, na kuendeleza shughuli hiyo katika angalau hekta 19,000 za mashamba.
Uboreshaji wa SEKEM wa ardhi iliyoharibika na majangwa na kuyafanya kuwa mifumo inayofanya kazi na inayoweza kuzalisha hutoa ahueni inayohitajika kwa mifumo ya ekolojia iliyo hatarini, wataalam wanasema. Kote duniani, hekta milioni 12 za ardhi zilizo na uwezo wa kuzalisha tani milioni 20 za nafaka hupotea kutokana na ukame na kuenea kwa majangwa kila mwaka.
Kutokana na juhudi zake za kukabiliana na uharibifu wa ardhi na kuenea kwa majangwa huku ikihimiza maendeleo endelevu, SEKEM imetajwa kuwa Bingwa wa Dunia wa mwaka wa 2024– tuzo la Umoja wa Mataifa ya ngazi ya juu zaidi - katika kitengo cha Maono ya Ujasiriamali. SEKEM ni mojawapo wa washindi sita katika kundi la mwaka wa 2024 .
"Mara nyingi, njia ambayo wanadamu hutumia kuzalisha chakula sio endelevu. Hili ni tishio kwa dunia asilia na uwezo wetu wa muda mrefu wa kujilisha wenyewe,” anasema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP. "SEKEM inaonyesha kuwa inawezekana kufanya mifumo ya chakula kufanyia kazi watu na sayari, ambayo ni muhimu ili kushinda majanga kwa mazingira kama vile majangwa na kurejesha amani kati ya wanadamu na mazingira."
Kupanda mbegu
Kwa milenia kadhaa, kilimo kimekuwa nguzo ya uchumi wa Misri. Hutoa riziki kwa asilimia 55 ya jumla ya dadi ya watu nchini, lakini miongo kadhaa ya kuenea kwa majangwa, uharibifu wa ardhi na kuongezeka kwa idadi ya watu vimefanya kuhakikisha utoshelezaji wa chakula kuwa changamoto, kulingana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).
Katika juhudi za kukidhi ongezeko la mahitaji ya chakula na kusaidia idadi ya watu ambapo zaidi ya robo ya watu wanaishi katika umaskini, Misri kwa muda mrefu imekuwa ikitegemea matumizi ya mbolea za kemikali na dawa za kuulia wadudu. Hizi mara nyingi huzingatiwa kama njia za bei nafuu zaidi ya kuimarisha mavuno. Lakini zikitumiwa kupita kiasi, zinaweza kuingia kwenye maji ya ardhini na kudhoofisha muundo wa udongo, kumomonyoa ardhi na hatimaye kutoa nafasi kwa majangwa.
SEKEM inaepuka mbolea za kemikali. Inafanya kazi na wakulima kote nchini ili kuhakikisha aina mbalimbali za mimea na wanyama - kuanzia kwa nyuki hadi kwa bundi - wamo mashambani, kimsingi kuunda mifumo ndogo ya ekolojia. SEKEM hunufaika kutumia mabaki ya mimea na samadi ya wanyama ili kuongeza mavuno ya mazao. Mzunguko huu hudumisha afya ya udongo na husaidia kufanya mashamba kustahilili kuenea kwa majangwa.
Kilimo cha bayodinamiki pia kinaweza kutoa msaada unaohitajika katika vita dhidi ya janga la mabadiliko ya tabianchi, wataalam wanasema. Udongo wenye afya ni miongoni mwa njia bora zaidi za kuhifadhi hewa ya ukaa inayoongeza joto kwenye sayari. Udongo pia ni makazi kwa zaidi ya asilimia 25 ya bayoanuai ya kimataifa na husaidia viumbe wengi juu ya ardhi, kulingana na FAO .
Matumaini ya mavuno
SEKEM inasema inalenga kusaidia wakulima 40,000 kuanza kufanya kilimo cha bayodinamiki kufikia mwishoni mwa mwaka wa 2025 kwa ushirikiano na Chama cha Bayodinamiki cha Misri. Kufikia mwaka wa 2028, lengo ni kufikia wakulima 250,000 wenye mashamba ya ukubwa wa ekari milioni 1.6.
Hali hii ni tofauti na siku za awali za SEKEM, wakati kilimo cha bayodinamiki kilikuwa dhana ambayo haijafanyiwa majaribio barani Afrika, anasema Abouleish.
"Baba yangu alitaka kuthibitisha kuwa unaweza kutafakari upya kuhusu uchumi, kutafakari upya kuhusu kilimo," anasema. "Aliyaita maono yake 'Uchumi wa upendo'."
Miongoni mwa jitihada nyingine za SEKEM ni jitihada za kuboresha hekta 1,000 za jangwa na kuanzisha jamii inayojitosheleza. Huku asilimia 96 ya ardhi nchini Misri ikiwa jangwa, mpango uliopewa jina la "Kufanya Jangwa kuwa Kijani" unalenga kulisha maelfu ya watu huku ukiondoa hewa ya ukaa.
Kutoka kwa hema katika jangwa ambalo halijaguswa, SEKEM imekua hadi kuwa shirika ku la maendeleo. Inaendesha shule, vituo vya kutoa mafunzo na chuo kikuu, kutayarisha wakulima na vijana kukabiliana na uharibifu wa ardhi na kuenea kwa majangwa.
SEKEM huuza bidhaa za kilimo hai ndani na nje ya nchi, na ushirikiano wake na benki za Ulaya na miungano ya kimataifa huwezesha uwekezaji unaoendelea katika mbinu za kilimo cha bayodinamiki nchini Misri. Vipengele mbalimbali vya mpango huo ni pamoja na kampuni maalum zinazojumuisha kampuni za kutengeneza dawa za kiasili, mavazi, na kadhalika.
Baada ya Ibrahim Abouleish kuadhimisha katika mwaka wa 2017 - maadhimisho ya miaka 40 ya SEKEM - Helmy Abouleish na shirika walianzisha mpango utakawaongoza hadi mwaka wa 2057. Mpango huo unajumuisha kupanua kilimo cha baodinamiki kwa wakulima milioni 7 nchini Misri.
"Tusipofikia haya, hatutakuwa tumefikia maono yetu ya awali," Abouleish anasema. "Watu wengi walituambia haya hayawezekani. Lakini sisi ni wataalamu katika mambo yasiowezekana. Tunapenda mambo yasiowezekana."