Wakili na mwanachama wa Kabila la Asili ya Yurok la California, Amy Bowers Cordalis ametumia miongo kadhaa kujitahidi kurejesha mtiririko wa kiasili wa Mto Klamath nchini Marekani.
Mto Klamath, unaopitia katika majimbo ya Oregon na California, hapo awali ulikuwa mkondo wa tatu kwa ukubwa uliozalisha samoni katika Marekani Magharibi. Lakini mabwawa manne ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji - yaliyojengwa kati ya mwaka wa 1911 na mwaka wa 1962 - yalizuia mtiririko wa mto, na kupunguza idadi ya samoni katika eneo hili. Samaki ni spishi muhimu na ni muhimu kwa njia ya maisha ya watu wa Yurok.
Katika mwezi wa Oktoba, hata hivyo, Cordalis na Yurok walisherehekea wakati wafanyakazi walipobomoa bwawa la mwisho kati ya mabwawa manne ya mto Klamath. Ubomoaji huo ulitokana na matokeo ya tetemeko la ardhi ya mwaka wa 2022 ambapo taasisi za serikali za utungaji na utekelezaji wa sheria ziliangazia uondoaji wa mabwawa na uboreshaji wa mto.
Uamuzi huo uliashiria kilele cha miongo kadhaa ya kupigania Yurok, maandamano na hatua za kisheria. Cordalis alitekeleza wajibu muhimu katika juhudi hizi. Aliongoza rufaa kwa watungasheria na kusaidia kufikia makubaliano baada ya mazungumzo na California, Oregon na mmiliki wa mabwawa ambayo yalisababisha kuondolewa kwake.
"Nilidhani tulikuwa tunaenda kuwa kizazi ambacho kilishuhudia kuangamia na kukauka kabisa kwa mto huu," anasema. "Lakini sasa tutakuwa kizazi kinachoshuhudia kuzaliwa upya na kuboreshwa kwa mfumo wetu wa ekolojia, utamaduni wetu na uhai wetu."
Kutokana na kujitolea kwake kushughulikia haki za Watu wa Kiasili na utunzaji wa mazingira, Cordalis ametajwa kuwa Bingwa wa Dunia wa mwaka wa 2024– tuzo la Umoja wa Mataifa la ngazi ya juu zaidi - katika kitengo cha Motisha na Kuchukua Hatua. Ni mojawapo wa washindi sita katika kundi la mwaka wa 2024.
“Watu wa Kiasili wako mstari wa mbele katika uhifadhi wa mazingira wa kimataifa. Kuwajengea uwezo kunaweza kusaidia kukuza mifumo ya ekolojia yenye afya kwa manufaa ya wote,” anasema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)
"Uanaharakati wa Amy Bowers Cordalis na uhamasishaji wake wa jamii umesababisha ushindi madhubuti wa kuwa na mfumo wa ekolojia wenye afya na utunzaji wa mazingira. Hii inaweza kuwatia moyo wanaharakati na watetezi wa haki za Watu wa Kiasili kila mahali.”
Mito iliyo hatarini
Mito ni mishipa ya maisha ya binadamu, wanyamapori na mifumo ya ekolojia. Zaidi ya spishi 140,000 hutegemea makazi ya maji safi, mito na maziwa, kuwepo.
Bado mito michache ulimwenguni imesalia katika hali yake ya kiasili, inayotiririka vizuri, na inazidi kutishiwa na mambo mengi, ikiwa ni pamoja na uchafuzi, ubadilishaji wa matumizi ya ardhi na mabadiliko ya tabianchi. Mtiririko wa mito umepungua katika mabonde 402 duniani, ongezeko la mara tano zaidi tangu mwaka wa 2000, kulingana na data ya UNEP.
Watu wachache wanaelewa hili vyema zaidi kuliko Cordalis na mwenzake Yurok, ambao ni kabila kubwa zaidi la Watu wa Kiasili nchini Marekani mjini California, walio na zaidi ya watu 5,000, kulingana na kabila hilo.
Wanaojulikana kama "watu wa samoni", Yurok kihistoria walikuwa wanategemea samaki kama chanzo cha riziki na nguzo ya utamaduni wao. Lakini mabwawa kwenye Mto Klamath yamesababisha kuzuka kwa msimu wa maua ya mwani yalio na sumu, ambayo hubadilisha hali ya joto na kupelekea magonjwa, na kupunguza ubora wa maji, wanasema maafisa wa California. Ongezeko la idadi ya watu na makazi yao yameongeza shinikizo kwa mto huu.
Katika mwaka wa 2002, serikali ya shirikisho ilidadilisha mkondo wa maji kutoka Mto Klamath kwa ajili ya kilimo, na kusababisha mtiririko mdogo wa mto. Hii ilihatarisha angalau maisha ya samoni 34,000 wazima.
"Ilikuwa kama kushuhudia familia yako yote ikiuawa mbele ya macho yako," Cordalis anakumbuka. "Ilikuwa aina ya uharibifu wa mazingira kimakusudi."
Kuchanganya utamaduni, sayansi na sheria
Kifo cha samaki kiliwatia kiwewe lakini pia kiliwatia nguvu watu wa Yurok, ambao waliimarisha harakati zao za kuondoa mabwawa, wakishirikiana na jamii nyingine, wanasayansi, wavuvi wa samaki za biashara na makundi ya mazingira.
Kwa Cordalis, ilikuwa wakati mahususi ambao ulimtia moyo kujiunga na shule ya sheria na baadaye kuwa mwanasheria mkuu wa Kabila la Yurok.
Alipochukua wajibu huo katika mwaka wa 2016, Mto Klamath ulikuwa na mojawapo ya samoni wachache kuwahi kurekodiwa, na kulazimisha Yurok kufunga uvuvi wake wa samaki wa biashara. Kwa kuchochewa na urithi wa mjomba wake - ushindi wake wa Mahakama ya Juu katika mwaka wa 1973 ulithibitisha haki ya ardhi na uhuru wa Kabila la Yurok - Cordalis alizindua mfululizo wa hatua za kisheria ambazo zimesaidia kuendeleza idadi ya samoni.
Katika mwaka wa 2020, aliunda shirika lisilo la biashara la Ridges to Riffles ili kutoa utetezi na usaidizi wa sera kwa jamii za Kiasili kulinda na kuboresha malighafi zao.
"Tunatumia maarifa yetu ya jadi na kuyaunga mkono na sayansi na sheria ili kuzungumza lugha ya uboreshaji wa kisasa wa ardhi," Cordalis anaelezea.
Kuirejesha na Kuiboresha
Ushindi wa kisheria wa Yurok mwaka wa 2022 ulisababisha kile kinachojulikana kama mradi mkubwa zaidi wa kuondoa bwawa na kurejesha mito nchini Marekani.
Wakati mapambano ya miongo kadhaa ya kuondoa mabwawa yamekamilika, kazi ya Cordalis bado haijakamilika. Mpango wa Yurok wa kurejesha na kupanda mimea kwa angalau hekta 900 za ardhi iliyozama hapo awali, kurudisha eneo hili chini ya umiliki wa kabila, kuboresha makazi ya majini na nchi kavu kwa manufaa ya samaki na wanyamapori, kuboresha mtiririko wa maji, na kuongeza idadi ya samoni.
Samoni wamerejea kwa zaidi ya kilomita 640 za mto uliofunguliwa tena karibu na mpaka wa California na Oregon, unavyoripoti Utawala wa Kitaifa wa Bahari ni Masuala ya Anga. Wahifadhi wa mazingira wameshuhudia samoni wa Chinook wakihamia kwa makazi ambayo hayakuweza kufikiwa juu ya eneo la mojawapo ya mabwawa manne yaliyobomolewa, kulingana na ripoti za vyombo vya habari. Ndani ya miongo minne, idadi yao katika Mto Klamath inaweza kuongezeka kwa wastani wa takriban asilimia 81, kulingana na serikali ya shirikisho ya Marekani.
Kuondolewa kwa mabwawa ya Klamath ni sehemu ya vuguvugu la kimataifa la kuboresha mito na kuboresha ustahimilivu kwa tabianchi. Nchi kadhaa, kwa mfano, ziliahidi mwaka jana kuuisha kilomita 300,000 za mito iliyoharibiwa chini ya Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia. Inatosha kuzunguka Dunia mara saba.
"Ikiwa tunaweza kufanya hivyo kwa Mto Klamath, tunaweza kufanya hivyo kote ulimwenguni," Cordalis anasema. "Maono yangu ni kwamba maji yatakuwa safi na mengi, na kwamba kutakuwa na samaki wakubwa, wenye afya na wanaong'aa mtoni."

Hababi David Attenborough alipokuwa mdogo, alitumia mwingi wa muda wake alipokuwa hafanyi kazi kupitia machimbo yaliyosahaulika maeneo ya mashambani nchini Uingereza huku akiwa na nyundo mkononi. Alichowinda: visukuku vilivyo na amonia, moluska wenye umbo la mzunguko walioishi wakati wa dinosaria.
Kwa Attenborough akiwa kijana, visukuku vilikuwa kama hazina iliyozikwa na alishangaa kuwa wa kwanza kuviona katika kipindi cha mamilioni ya miaka.
Ulimwengu asilia umeendelea kumfurahisha maisha yake yote.
Kwa sasa, Attenborough mwenye umri wa miaka 95, bila shaka ndiye mtangazaji anayejulikana zaidi katika historia kwa kutangaza kuhusu ulimwenguni asilia vizuri zaidi. Wakati wa kazi yake iliyoanza wakati televisheni zilipoziduliwa, ameandika na kuwasilisha baadhi ya filamu zenye ushawishi mkubwa kuhusu hali ya sayari, ikijumuisha mfululizo wa makala yake kwa kipindi cha muongo mmoja, yalio na sehemu tisa za Awamu za Maisha.
Kupitia kile New York Times ilichokiita "masimulizi kupitia sauti ya Mungu" na udadisi usiokoma, ametumia miaka 70 kufichua urembo wa ulimwengu asilia - na kufichua vitisho vinavyoukabili. Kwa kufanya hivyo, ametoa matumaini kwa mamilioni ya watazamaji ya kuwa na mustakabali endelevu.
“Ikiwa kwa kweli, ulimwengu ungeweza kuokolewa, basi Attenborough angefanya zaidi kuuokoa kuliko mtu mwingine yeyote aliyewahi kuishi,” aliandika mwanamazingira na mwandishi Simon Barnes.
Umoja wa Mataifa umetambua athari kubwa ya Attenborough kwa vuguvugu la kimataifa la mazingira, na kumkabidhi tuzo la Mabingwa wa Dunia la Umoja wa Mataifa kwa Mafanikio ya Kudumu. Tuzo hili ni tuzo la Umoja wa Mataifa la ngazi ya juu linalotolewa kwa heshima ya mazingira na linasherehekea wale waliojitolea maishani kukabiliana na majanga kama vile mabadiliko ya tabianchi, uangamiaji wa spishi na uchafuzi.
"Umekuwa mtu wa kuigwa na watu wengi," Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), alipokuwa akimkabidhi Attenborough tuzo hilo.
"Ulizungumza kwa niaba ya sayari kwa muda mrefu kabla ya mtu mwingine yeyote kufanya hivyo na unaendelea kutuelekeza kuliko na hatari."
Pamoja na kazi yake katika vyombo vya habari, Attenborough ni mojawapo ya wahamasishaji wakuu wa vuguvugu la mazingira duniani. Amehudhuria mikutano mikuu ya kilele kama vile Kongamano la Mabadiliko ya Tabianchi mjini Paris Mwaka wa 2015, ambapo alitoa wito wa kuwepo na ushirikiano kote ulimwenguni kwenye juhudi za kukabiliana na vitisho kwa Dunia.
Pia ameshirikiana na UNEP kwa angalau miongo minne, akitumia sauti yake kwa mfululizo wa kampeni na filamu fupi ambazo zimeangazia juhudi za shirika hili za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa bayoanuai na uchafuzi. Kazi hiyo inaendeshwa na imani kwamba hakuna nchi moja tu inayoweza kutatua matatizo ya mazingira duniani.
"Tunaishi katika enzi ambayo utaifa hautoshi," Attenborough alisema alipokuwa anapokea Tuzo la UNEP la Mabingwa wa Dunia kwa Mafanikio ya kudumu. "Lazima tuhisi kama sisi sote ni raia wa sayari hii moja. Tukishirikiana, tunaweza kutatua matatizo haya.”
Attenborough alihitimu kutoka Chuo Kikuu cha Cambridge katika mwaka wa 1947 na shahada sayansi ya asili, lakini akabaini kuwa hageweza kufanya tu utafiti maisha yake yote. Hapo, akajiunga na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) wakati televisheni ilivyokuwa ikianza kujipenyeza majumbani.
Alionekana mara ya kwanza kwenye runinga tarehe 21 Desemba, mwaka wa1954, kwenye Zoo Quest, mfululizo wa makala yaliyopelekea Waigereza kutazama viumbe mbalimbali kutoka pembe zote za dunia kama vile orangutan na Dragoni wa Komodo.
Akiwa msimamizi mwenye kipaji kama alivyokuwa mtangazaji mwenye kipaji, Attenborough alipanda vyeo kama mtangazaji wa kitaifa wa Uingereza, na hatimaye akaja kuongoza BBC Two. Huko, alizindua Monty Python’s Flying Circus, na mfulizo wa filamu nyinginezo.
Lakini kazi ya kuwa msimamizi haikumfurahisha, na katika mwaka wa 1973 Attenborough aliachana na ofisi kuu na kurudi kuunda filamu.
Matokeo yake yalikuwa mfululizo wa filamu zake kuu Life on Earth katika mwaka wa 1979, zilizoonyesha historia ya viumbe duniani, kuanzia kwa vijidudu vya kwanza hadi kwa wanadamu.
Filamu hizo zilichukua miaka tatu kutengeneza na Attenborough alisafiri maili milioni 1.5 wakati wa utengenezaji wa filamu hizo. Kwa kuzingatia upeo na matarajio yake, Life on Earth ilibadili filamu ya masimulizi kuhusu historia ya asili na kutazamwa na watu wapatao milioni 500.
Katika miongo mitatu iliyofuata, Attenborough alitunga na kuwasilisha filamu nane bora zaidi, akielekeza ulimwengu kwa kile alichokiita “spectacular marvel” ya asili.
Lakini kazi yake iliposonga mbele, Attenborough alikuja kutoa ushahidi wa kulipuliwa kwa ulimwengu asilia. Idadi ya binadamu ilipoongezeka, asili ilipungua. Shughuli za binadamu zimebadilisha robo tatu ya eneo la Dunia na kuweka spishi milioni moja hatarini kutoweka.
"Ijapokuwa tuko imara leo, ni wazi kuwa tutakuwa imara zaidi katika siku zijazo," alisema wakati wa kuhitimisha The Living Planet katika mwaka wa 1984. "Ni wazi tunaweza kuangamiza ulimwengu. [Dunia] kuendelea kuwepo sasa iko mikononi mwetu.”
Filamu za Attenborough zilionyesha ulimwengu kuwa wanyamapori wanaweza kuangamia, kwamba ni wadhaifu na wanahitaji kulindwa - na kwamba wanadamu wanaendelea kuwa hatari kwa asili.
Mwaka jana, katikati ya miaka yake 90, alihutubia viongozi wa dunia katika Kongamao la Umoja wa Mataifa la Mabadiliko ya Tabianchi mjini Glasgow, Scotland.
“Tayari tuko hatarini,” alisema. “Je hii ndiyo hatima ya hali yetu? Hali halisi ya spishi bora zaidi zimeangamizwa kutokana na tabia ya binadamu ya kushindwa kuona hali kamili wanapokimbizana na malengo ya muda mfupi.”
Lakini basi, kama kawaida, maneno ya Attenborough yalileta matumaini. Mada inayojitokeza mara kwa mara kweye filamu zake ni kuwa licha ya hali mbaya ya sayari, binadamu bado wanaweza kupunguza madhara waliofanya.
"Hatujakata tamaa," alisema katika mwaka wa 2020 wakati wa A Life on Our Planet,, akiangazia kazi yake hapo awali. "Kuna fursa ya kuboresha mambo, kukamilisha safari yetu ya maendeleo na kwa mara nyingine tena tujali asili. Tunachohitaji ni nia ya kufanya hivyo."
Katika filamu iyo hiyo, alitoa maagizo ya kufanya amani na asili. Ilijikita katika kuinua viwango vya maisha katika nchi maskini ili kupunguza ongezeko la watu, kutumia nishati isiyochafua mazingira, kama nishati ya jua na upepo, kula vyakula vingi vinavyotokana na mimea, visivyodhuru mazingira, na kuachana na nishati ya visukuku.
"Tukitunza asili, asili itatutunza," alisema. "Sasa ni wakati wa spishi zetu kuacha kukua tu, kuishi kwenye sayari yetu kwa kujali mazingira, ili kuanza kustawi."
Kazi na uanaharakati wa Attenborough ilimpelekea kufanywa hababi (mara mbili) na jina lake kuongezwa kwa aina mbalimbali ya spishi, kuanzia kwa attenborosaurus (mtambaazi wa zamani wa kuogelea) hadi kwa nepenthes attenboroughii (mmea alaye wanyama).
Katika miaka ya hivi karibuni, Attenborough ameendelea kuandaa makala ya filamu kuhusu asili, na kujishindia matuzo mawili ya Emmy ya masimulizi katika mwaka wa 2021. (Katika kazi yake, ameshinda matuzo matatu ya Emmy na BAFTA nane.)
Kwa miongo kadhaa, Attenborough amekuwa akitafutwa na viongozi duniani wanaotafuta suluhu kwa majanga yanayokabili ulimwengu asilia - na hata pegine kutaka kuhisi kujitolea kwake.
Katika mwaka wa 2015 alizuru Ikulu ya White House kwa mazungumzo na Rais wa Marekani Barack Obama. Obama alimuuliza Attenborough ni nini kilimchochea kuanza kuwa na “kuupenda mno” ulimwengu asilia.
“Sijawahi kukutana na mtoto asiyependa historia ya asili,” alijibu, labda akikumbuka siku alipowinda visukuku vijijini Uingereza. "Kwa hivyo, swali ni, mtu anawezaje kutozigatia haya?"

Mkoa wa Zhejiang ulipata jina lake kutoka kwa Mto Zhe, kwa maana ya mto "usionyooka" au "uliopinda". Mito katika mkoa wa Zhejiang ina umuhimu kwa jamii kutoka kitambo, inatiririka kupitia miji ya zamani, kati ya nyumba za jadi zilizo na kuta nyeupe na paa nyeusi, na hunufaisha mashamba ya mpunga. Licha ya hayo, Zhejiang pia ni mojawapo ya mikoa Uchina ambayo ni tajiri zaidi na imeendelea zaidi, na maendeleo ya kasi yalibadili mkondo wa maji.

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa linamutambua Waziri Mkuu wa India Narendra Modi kwa uungozi wake wa kishujaa kuhusiana na masuala ya mazingira katika ngazi ya kimataifa. Chini ya uongozi wa Narendra Modi, India iliahadi kukomesha matumizi ya plastiki zinazotumiwa tu mara moja katika nchi hiyo kufikia mwaka wa 2022. Waziri Mkuu, Modi, pia anaunga mkono na kupigania kuwepo kwa Muungano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua, ambao ni ubia wa kimataifa wa kuimarisha matumizi ya nishati ya jua.

Joan Carling amekuwa akipigania haki za ardhi na za mazingira ya watu wa kiasili kwa zaidi ya miaka 20. Alishiriki kikamilifu katika Jukwaa la Mapatano la Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi na REDD+. Amefanya kazi kama Katibu Mkuu wa Mkataba wa Watu wa Asili ya Asia mara mbili. Pia alikuwa mwenyekiti wa Muungano wa Watu wa Cordillera.

Impossible Foods na Beyond Meat walishinda kwa pamoja Tuzo la Mabingwa wa Dunia, katika kitengo cha Sayansi na Ubunifu. Wanatoa vibadala vya kudumu kwa baga za nyama ya ng'ombe ambavyo ni rafiki zaidi kwa mazingira na vinatoa ushindani kwa ladha ya nyama. Washindi hawa wanaamini kuwa haiwezekani kufikia malengo ya Mkataba wa tabia nchi wa Paris bila kupunguza kilimo cha ufugaji kwa kiwango kikubwa.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amelipa swala la utunzaji wa mazingira kipau mbele katika ajenda yake ya nchi za kigeni. Anatambuliwa kwa kupigania kuwepo kwa Muungano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua na kukuza ushirikiano wa kimataifa ili kushughulikia masuala ya mazingira, na kwa uongozi wake kuhusiana na Mkataba wa Kimataifa wa Mazingira.
