- Costa Rica yashinda tuzo muhimu la mazingira linalotolewa na Umoja wa Mataifa katika kitengo cha sera na uongozi
- Nchi kotoka Amerika ya Kati imetuzwa kwa kuwa mstari mbele kuhakikisha kutokuwepo kwa hewa ya ukaa siku zijazo
Septemba 20, 2019 -- Costa Rica imekabidhiwa tuzo la Mabingwa wa Dunia, tuzo kuu la mazingira linatolewa na Umoja wa Mataifa kutokana na juhudi zake za kutunza mazingira na sera zake za kipekee zinazowezesha kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa lilituza Costa Rica katika kitengo cha sera na uongozi.
Kiongozi anayedumisha uendelevu duniani, kutoka Amerika ya Kati, ni taifa lililoweka mpango maalum wa kukomesha uzalishaji wa hewa ya ukaa katika uchumi wake ifikiapo mwaka wa 2050 kwa mjibu wa Mkataba wa Paris kuhusu Tabianchi na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa. Lina matumaini ya kuweka mfano utakaoigwa na mataifa mengine ili kukabiliana na uzalishaji wa hewa chafu unaopelekea mabadiliko sugu ya tabianchi kutokea kwa kasi.
Costa Rica imefaulu kufanya maamuzi ya kisera na kisiasa ya kushughulikia changamoto za mazingira na ni wazi kuwa kuna uwezekano wa kuwa na uendelevu kwa manufaa ya uchumi.
"Costa Rica imekuwa mstari wa mbele katika utunzaji wa mazingira na kudumisha amani na ni mfano wa kuigwa kwenye kanda na kote ulimwenguni;" alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa.
"Ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, sisi sote tunapaswa kufanya maamuzi ya dharura yanayoleta mabadiliko. Na mpango wake kabambe wa kukomesha hewa ya ukaa katika uchumi wake, Costa Rica ina uwezo wa kufaulu", aliongezea. "Uzalishaji wa hewa chafu ulimwenguni unaongezeka kwa kasi. Wakati wa kufanya maamuzi ya kuwa na uchumi dhabiti usiochafua mazingira ni sasa.”
Suala la haja ya kuchukua hatua kali kote ulimwenguni ili kukabiliana ya mabadiliko ya tabianchi litaangaziwa wakati wa Mkutano Mkuu wa Kushughulikia Mazingira ulioitishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres’ utakaofanyika tarehe 23 Septemba mjini New York. Katibu Mkuu ametoa wito kwa viongozi duniani, wamiliki wa biashara na mashirika ya uraia kuhudhuria mkutano wakiwa na suluhisho tosha la jinsi watakavyopunguza uchafuzi wa hewa kwa asilimia 45 kufikia karne ijayo na kuepukana na hewa chafu kabisa kufikia mwaka wa 2050. Hii ni sambamba na Mkataba wa Paris na Malengo ya Maendeleo Endelevu.
Mpango wa Kitaifa wa Kukomesha Hewa ya Ukaa ulizinduliwa Feburuari na una malengo ya kipindi kifupi na malengo ya kipindi kirefu ya kuleta mabadiliko kwenye sekta za usafiri, nishati, taka na matumizi ya ardhi. Lengo lake ni kutozalisha kabisa hewa ya ukaa kufikia mwaka wa 2050. Hii inamaanisha kuwa nchi hii haitazalisha tena hewa chafu kwa kuchukua hatua kama vile za kutunza misitu na kupanua eneo la misitu.
Tayari, zaidi ya asilimia 98 ya nishati inayotumiwa na Costa Rica ni jadidifu na zaidi ya asili mia 53 ni eneo lililo na misitu baada ya juhudi kubwa za kukabiliana na hali ya ukataji miti iliyoshudiwa kwa karne nzima. Katika mwaka wa 2017, nchi hiyo ilitumia tu nishati jadidifu kwa siku 300. Lengo likiwa kutumia asilimia 100 ya umeme unaotokana na nishati jadidifu ifikapo mwaka wa 2030. Asilimia sabini ya mabasi na teksi zote zinatarajiwa kutumia umeme kufikia mwaka wa 2030, na inatarajiwa kuwa ifikiapo mwaka wa 2050, magari yote yatakuwa yanatumia umeme.
Kujitolea kwa Costa Rica kuwa taifa anzilishi la kukuza teknolojia ya kudumu isiyochafua mazingira ni suala la kupigiwa upatu kutokana na ukweli kuwa taifa hili lililo na idadi ya takribani watu milioni 5 huzalisha tu 0.4 ya hewa chafu duniani.
"Ninapopokea tuzo la Bingwa wa Dunia kwa niaba ya Costa Rica, wananchi wake wote, vizazi vilivyopita vilivyotunza mazingira, na kwa niaba ya vizazi vijavyo, ni jambo ninalonifanya kujivuna kutokana na mafanikio ya Costa Rica na yale ambayo tunaweza kuendelea kufanya ili kupata mafanikio zaidi. Ninajivunia kuwa mwananchi wa Costa Rica," alisema Rais Carlos Alvarado Quesada.
"Takribani miaka 50 iliyopita, nchi hii ilianzisha kubuni sera kadhaa za mazingira kwa sababu mageuzi ya kuleta maendeleo endelevu ni sehemu ya maisha ya kila mwananchi wa Costa Rica. Mpango wa kutozalisha kabisa hewa ya ukaa unalenga kuongeza nafasi za kazi ili kuimarisha uchumi, kwa wakati uo huo ukipunguza matumizi ya nishati ya visukuku ili kupunguza uchafuzi wa hewa. Tutatimiza lengo hili vipi? Kupitia vyombo vya usafiri wa umma visivyochafua mazingira; miji imara ya kisasa; ushughulikiaji mzuri wa taka; kilimo endelevu na sera zilizoboreshwa," aliongezea.
Tuzo la Mabingwa wa Dunia linatambua uwezo wa Costa Rica wa kuwa endelevu na kuonyesha umuhimu wa udharura wa kupata masuluhisho ya changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Mwaka jana, Jopo la Kimataifa ya Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi liligundua kuwa ili kudhibiti joto duniani kuwa nyusi joto 1.5 mabadiliko ya dharura yanahitajika ili kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kwa asilimia 45 kufikia mwaka wa 2030 ikilinganishwa na kiwango kilichoshuhudiwa mwaka wa 2010, na kuepukana na hewa chafu kabisa kufikia mwaka wa 2050.
Mabingwa wa Dunia, ni tuzo la kimataifa linalotolewa na Umoja wa Mataifa kwa heshima ya mazingira. Lilianzishwa na UNEP mwaka wa 2005 kuwatuza watu wa kipekee ambao matendo yao yamekuwa na athari chanya zinazoleta mabadiliko kwa mazingira. Kutoka kwa viongozi duniani hadi kwa watetezi wa mazingira na hadi kwa wanaobuni teknolojia, waanzilishi hawa wanaoleta mabadiliko ili kutunza sayari yetu kwa ajili ya vizazi vijavyo hutuzwa.
Costa Rica ni mojawapo wa washindi tano wa mwaka huu. Vitengo vingine ni pamoja na maono ya ujasiriamali; motisha na kuchukua hatua; na sayansi na ubunifu. Washindi wa mwaka wa 2019 watatuzwa wakati wa sherehe ya gala mjini New York tarehe 26 Septemba wakati wa kikao cha 74 cha Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Wengine watakaotuzwa pia wakati wa hafla hii ni wanamazingira wa kipekee saba wa umri wa kati ya miaka 18 hadi miaka 30. Watatuzwa tuzo la Vijana Bingwa Duniani.
Washindi wa awali kutoka eneo hili ni pamoja na Michelle Bachelet, aliyekuwa Rais wa Chile, kutokana na uongozi wake wa kipekee wa kuunda maeneo ya bahari yaliyohifadhiwa na kukuza nishati jadidifu (mwaka wa 2017); aliyekuwa waziri wa mazingira wa Brazil Izabella Teixeira kutokana na sera zake za uongozi na kazi aliyoifanya ya kupunguza ukataji wa miti katika misitu ya Amazon (mwaka wa 2013); na mwanaekolojia kutoka Meksiko José Sarukhán Kermez kwa uongozi wake wa kudumu na ubunifu wake wa kutunza bayoanuai nchini Meksiko na kote ulimwenguni (mwaka wa 2016).
MAKALA KWA WAHARIRI
Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa
Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa ni msemaji mkubwa wa kimataifa kuhusu mazingira. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika kutunza mazingira kupitia kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.
Kuhusu Weibo
Mabingwa wa Dunia huandaliwa kwa msaada wa ufadhili kutoka kwaWeibo – Mtandao mkuu wa kijamii nchini China unaowezesha watu kuunda, kushiriki na kupata makala mtandaoni. . Weibo ina zaidi ya watumizi milioni 486 kila mwezi.
Kuhusu Mabingwa wa Dunia
Tuzo linalotelewa kila mwaka la Mabingwa wa Dunia hutuza viongozi vya kipekee kutoka kwa serikali, mashirika ya uraia na sekta ya kibinafsi ambao matendo yao yamesababisha mabadiliko chanya kwa mazingira. Tangu mwaka wa 2005, tuzo la Mabingwa wa Dunia limewatuza washindi 88, kuanzia kwa wakuu wa nchi hadi kwa wanaobuni teknolojia.
Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:
Keisha Rukikaire, UNEP Habari na Vyombo vya Habari, rukikaire@un.org, +254 722 677747