Dunia inarejelea hali yake ya awali: Umoja wa Mataifa unatambua Miradi Saba Mikuu ya Kuboresha Mifumo ya Ekolojia
Juhudi zinazofanyika Afrika, Amerika ya Kusini, Mashariki ya Kati na Asia Kusini zinazotajwa kuwa mbinu bora za kukabiliana na uharibifu wa mifumo ya ekolojia.
Nairobi, Februari 13, 2024 – Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) wametaja mipango saba kutoka Afrika, Amerika ya Kusini, Mediterania na Kusini-mashariki mwa Asia kuwa Miradi Mikuu ya Umoja wa Mataifa ya Kuboresha Mifumo ya Ekolojia. Mipango hii ni pamoja na mifumo ya ekolojia iliyo karibu kuharibiwa kabisa kutokana na mioto misituni, ukame, ukataji miti, na uchafuzi wa mazingira. Sasa inastahiki kupata usaidizi wa kiufundi na kifedha kutoka kwa Umoja wa Mataifa.
Tuzo za Miradi Mikuu ya Kurejesha Dunia katika Hali ya Awali ni sehemu ya Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Uboreshaji wa Mifumo ya Ekolojia – unaoongozwa na UNEP na FAO - ambao unalenga kuzuia, kusitisha, na kukabiliana na uharibifu wa mifumo ya ekolojia katika kila bara na katika kila bahari. Tuzo hizo hufuatilia mipango inayotambulika inayounga mkono ahadi za kimataifa za kurejesha katika hali ya awali hekta bilioni moja - eneo lililo kubwa kuliko Uchina.
Miradi iliyoshinda inatangazwa kabla ya kikao cha 6 cha Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa. (UNEA-6), chombo cha ngazi ya juu zaidi duniani kinachofanya maamuzi kuhusu masuala yanayohusiana na mazingira, kitakachofanyika kuanzia Februari 26 hadi Machi 1 katika makao makuu ya UNEP jijini Nairobi, Kenya. Kwa pamoja, miradi mikuu hiyo saba inatarajiwa kurejesha katika hali ya awali karibu hekta milioni 40 - eneo ambalo ni karibu mara 600 ya ukubwa wa Nairobi - na ibuni nafasi za kazi takribani 500,000.
"Kwa muda mrefu sana, maendeleo ya kiuchumi yalitokea kwa kugharama mazingira. Ingawa leo tunaona juhudi za kimataifa za kurudisha mazingira katika hali yake ya asili,” Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, alisema. "Juhudi hizi zinaonyesha jinsi tunavyoweza kuishi kwa amani na mazingira, kufanya jamii za eneo husika kuwa kitovu cha juhudi za kurejesha hali ya awali na bado tubuni ajira mpya. Tunapoendelea kukabiliwa na na majanga ya aina tatu duniani ya mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira na bayoanuai, na uchafuzi wa mazingira na taka, sasa ndio wakati ambao lazima tuzidishe maradufu na kuimarisha miradi ya kuboresha mifumo ya ekolojia.”
Miradi Mikuu ya Kurejesha Dunia katika Hali ya Awali huchaguliwa kama mifano bora ya urejeshaji mkubwa na wa muda mrefu wa mifumo ya ekolojia unaoendelea na unaofanywa na Majopo Kazi ya Sayansi na Mbinu Bora za Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia na kuidhinishwa na Halmashauri Kuu yake. Uteuzi hufuata mchakato wa ukaguzi wa kina wenye zaidi ya viashiria na vigezo 60, vinavyojumuisha Kanuni 10 za Kurejesha katika Hali ya Awali za Muongo wa Umoja wa Mataifa.
Mkurugenzi Mkuu wa FAO QU Dongyu alisema: "FAO inafuraha kutambua mabingwa hawa saba wanaostahili kutuzwa, na kuthibitisha kwamba tunaweza kutoa mifano bora ya kuigwa ya kukabiliana na uharibifu wa mifumo ya ekolojia kwa kiwango kikubwa, huku pia tukishughulikia athari za janga la mabadiliko ya tabianchi na uharibifuu wa bayoanuai. Kurejesha mifumo ya ekolojia ya maeneo ya nchi kavu na majini ni hatua muhimu katika kuleta mabadiliko ya mifumo ya kimataifa ya kuboresha kilimo chakula, na kukifanya kuwa bora, shirikishi, stahimilivu na endelevu. Uboreshaji wa mifumo ya ekolojia ni suluhisho la kudumu katika mapambano ya kutokomeza umaskini, njaa na utapiamlo, huku tukikabiliwa na ongezeko la idadi ya watu na kuongezeka kwa hitaji la vyakula na bidhaa na huduma za mifumo ya ekolojia.
Katika mwaka wa 2022, Miradi Mikuu Kumi ya Urejeshaji wa Dunia katika Hali ya Awali ilitambuliwa kama sehemu ya Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia, na inapaswa kufuatiwa na juhudi kama hizo kila baada ya miaka miwili hadi mwaka wa 2030. Miradi Mikuu ya Kurejesha Dunia katika Hali ya Awali ya mwaka huu ni sehemu ya uwekezaji ulioimarishwa katika mazingira kutoka kwa serikali na wafadhili wa kibinafsi, hasa inavyodhihrika katika Dola za Marekani billion 1.4 zilizotolewa mwaka jana na Mfuko wa Ufadhili wa Mazingira Duniani (GEF).
Jason Momoa mwigizaji na Mtetezi wa UNEP wa Maisha Chini ya Maji: "Uhifadhi wa mazingira, ingawa ni muhimu, hautoshi kwa sasa. Tumepoteza sehemu kubwa ya sayari yetu kwa sasa na lazima tujenge upya kile tulichoharibu, tukarabati kile tulichovunja, turejeshe katika hali ya awali kile kilichoharibika. Miradi hii ya uborejeshaji wa mifumo ya ekolojia ni kama majibu ya kusisimua kwa maswali makuu yanayoibuliwa kutokana na uhusiano wetu na ulimwengu asilia - kama vile filamu bora zaidi zinavyofanya."
Kila mojawapo ya Miradi Mikuu Saba ya Kurejesha Dunia katika Hali ya Awali inatangazwa kupitia jumbe za video zinazotolewa kwenye chaneli za mitandao ya kijamii za Umoja wa Mataifa na Balozi au Mtetezi wa UN au UNEP, wakiwemo waigizaji Dia Mirza, Jason Momoa, na Edward Norton, mpishi mkuu Leyla Fathallah, na mwanamitindo mkuu na mwandishi anayeuza zaidi Gisele Bündchen.
Kutoka kwa Mioto hadi kwa Misitu - Ustahimilivu katika Mediterania
Bonde la Mediterania ni eneo la pili kwa ukubwa kwa kuzingatia bayoanuai duniani, lakini asilimia 16 ya spishi zake za misitu ziko hatarini kutoweka, kwa kiasi fulani kutokana na vipindi virefu vya ukame vinavyosababishwa na tabianchi, mawimbi ya joto kali na mioto misituni. Katika muongo uliopita, eneo hilo limekumbwa na misimu mibaya zaidi ya mioto kuwahi kurekodiwa.
Mpango wa Kuirejesha katika Hali ya Awali Misitu ya Mediterania unaohusisha Lebanon, Morocco, Tunisia na Türkiye una mbinu mpya ya kulinda na kurejesha katika hali ya awali makazi haya ya asili na mifumo ya ekolojia iliyo hatarini na imesababisha zaidi ya hekta milioni mbili za misitu kurejeshwa katika ukanda huu twote tangu mwaka 2017, huku zaidi ya hekta milioni nane zikipangwa kurejeshwa kufikia mwaka wa 2030.
Mpango huu unafadhiliwa na Kamati ya FAO ya Maswali ya Misitu ya Mediterania - Silva Mediterranea, serikali za Lebanon, Morocco, Tunisia, na Türkiye, na Chama cha Misitu, Maendeleo na Uhifadhi cha Lebanon (AFDC).
Living Indus – Kurejesha katika Hali ya Awali Chimbuko la Ustaarabu
Mto Indus, wenye urefu wa kilomita 3,180, umetumika kama kiini cha maisha ya kijamii, kitamaduni, na kiuchumi ya kile ambacho leo kinajulikana kama Pakistan kwa zaidi ya miaka 5,000. Asilimia 90 ya watu wa Pakistani na zaidi ya robo tatu ya uchumi wake wanaishi katika Bonde la Indus, na linatumiwa kumwagilia maji zaidi ya asilimia 80 ya ardhi yake ya kilimo. Ukosefu wa utunzaji, uharibifu wa mazingira, na mabadiliko ya tabianchi vimetishia mfumo wa ekolojia wa mto huo, pamoja na samaki wake wengi na ardhi yenye rutuba.
Mpango wa Living Indus uliidhinishwa na bunge la Pakistan baada ya mafuriko mabaya ya 2022 yaliyosababishwa na mabadiliko ya tabianchi na ulizinduliwa rasmi katika Kongamano la Umoja wa Mataifa la Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) mjini Sharm el-Sheikh. Unalenga kurejesha katika hali ya awali hekta milioni 25 za bonde la mto kuafika mwaka 2030, ikijumuisha asilimia 30 ya eneo la Pakistani kupitia utekelezaji wa mambo 25 yenye athari kubwa kwa watunga sera, weledi na mashirika ya uraia. Mpango huo unabainisha Mto Indus kama kitu hai kilicho na haki - hatua iliyochukuliwa ili kuilinda mito kwingineko, ikiwa ni pamoja na Australia, Bangladesh, Bolivia, Brazil, Canada, Ecuador, India, New Zealand, Peru, na Sri Lanka.
Wabia katika mpango huu ni pamoja na Serikali ya Pakistan, FAO na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa.
Acción Andina – Kuokoa Kitovu cha Maji na Tabianchi Duniani
Vuguvugu la kijamii la Acción Andina linaongozwa na shirika lisilo la biashara la uhifadhi wa Peru, ECOAN (Asociacion Ecosistemas Andinos). Linapanua modeli ya upandaji miti katika jamii, ambayo imejidhihirisha katika miongo miwili iliyopita kama suluhisho la gharama nafuu kwa mipango ya kudhibiti na kuhimili mabadiliko ya tabianchi ili kurejesha na kukuza miti milioni 30 kufikia mwaka wa 2030 katika ukanda wa mimea wenye upana wa karibu hekta 800,000 nchini Argentina, Bolivia, Chile, Colombia, Ecuador, Peru, na Venezuela.
Mpango huo hatimaye unalenga kulinda na kurejesha eneo la msitu la hekta milioni moja. Tayari watu 25,000 kutoka jamii za Andean zilizotengwa wanahusika katika kurejesha katika hali ya awali hekta 5,000 na kulinda zaidi ya hekta 11,000 za misitu ya Andean. Wanatarajiwa kunufaika na mpango huo kufikia mwaka wa 2030 kwa njia mbalimbali, kutoka kwa upatikanaji wa dawa, paneli za jua, na majiko ya udongo yasiyochafua mazingira, hadi kwa usimamizi bora wa malisho, kilimo endelevu, biashara ndogondogo, na usimamizi wa utalii wa ekolojia wa tamaduni za kiasili. Pia unafanya kazi kupata hati miliki za ardhi kwa jamii za wenyeji, kulinda msitu dhidi ya uchimbaji madini siku zijazo, ukataji wa miti kutengeneza mbao na vichochezi vingine vya uharibifu.
Wabia katika mpango huu ni pamoja na Asociación Ecosistemas Andinos (ECOAN) na Uzalishaji wa Misitu Duniani (GFG).
Sri Lanka Iliacha Kupanda Mikoko – na Kuanza Kuikuza
Nchini Sri Lanka, misitu ya mikoko ni mifumo ya ekolojia ya pwani yenye thamani kubwa ambayo hustawi kwenye mpaka kati ya ardhi na bahari na hutumika kama daraja muhimu kati ya viumbe hai vya baharini na nchi kavu. Riziki ya jamii za pwani nchini Sri Lanka hutegemea sana mifumo ya ikolojia ya baharini na pwani. Hata hivyo, mabadiliko ya tabianchi na shughuli za binadamu zinatishia mfumo huu wa ekolojia wa kipekee.
Mpango wa Kukuza Upya Mikoko wa Sri Lanka unaendeshwa na sayansi, ukiongozwa kwa pamoja na jamii za wenyeji, na unalenga kurejesha usawa wa asili katika mfumo wa ekolojia. Tangu mpango huo uzinduliwe mwaka 2015, tayari juhudi zimezalisha hekta 500 za mikoko iliyorejeshwa, ba kunufaisha familia 150. Hekta 10,000 zingine zimepangwa kurejeshwa katika hali ya awali kufikia mwaka wa 2030, na familia5,000 zitanufaika na zaidi ya nafasi 4,000 mpya za ajira zitapatikana.
Wabia katika mpango huu ni pamoja na Wizara ya Mazingira ya Sri Lanka na serikali za Australia, Uingereza na Marekani.
Mandhari ya Terai Arc - kuimarisha fauna kuu ya Asia
Zaidi ya watu milioni saba hutegemea Mandhari ya Terai Arc, yaliyotanda katika hekta milioni 2.47 na kupatikana India na Nepal. Pia ni mojawapo ya makazi muhimu zaidi ulimwenguni kwa simbamarara ambao idadi yao imepungua sana, pamoja na ile ya spishi zingine kama vile vifaru na tembo, kutokana na uwindaji haramu, kupoteza makazi, uharibifu wa mazingira, na migogoro kati ya wanadamu na wanyamapori.
Mpango wa Mandhari ya Terai Arc umelenga kurejesha katika hali ya awali misitu ya korido muhimu za Mandhari ya Terai Arc na inashirikiana na jamii za wenyeji zinazofanya kazi kama wanasayansi raia, vitengo vya jamii vya kupambana na uwindaji haramu, walinzi wa misitu na wahamasishaji wa kijamii. Urejeshaji katika hali ya awali wa hekta 66,800, pamoja na hatua zingine, umesaidia idadi ya simbamarara katika eneo hilo, ambayo imeongezeka leo hii hadi 1,170 - ikiwa mara tatu ya idadi yake ya chini wakati programu ilipozinduliwa katika mwaka wa 2001. Mpango wa uborejeshaji wa mifumo ya ekolojia umeboresha riziki ya familia zipatazo 500,000 na kuunda nafasi mpya za kazi 40,000. Maendeleo yanatarajiwa kuendelea kwani karibu hekta 350,000 zitarejeshwa kufikia mwaka wa 2030.
Mfuko wa Wanyamapori Ulimwenguni wa Kulinda Uasili (WWF) Nepal ndio mbia mkuu katika mpango huu, ukisaidia serikali ya Nepal.
Kurejesha Kijani katika Kilimo cha Afrika
Mpango wa Kurejesha Kijani Afrika umekuwa ukitumia mbinu zilizothibitishwa za kilimo mseto, zilizotumiwa kukidhi mahitaji ya wakulima katika mazingira tofauti ya kijamii na kiikolojia katika miongo miwili iliyopita, iki kurejesha katika hali ya awali zaidi ya hekta 350,000 nchini Ethiopia, Ghana, Kenya, Mali, Niger, Rwanda, Senegal, na Somalia. Kufikia mwaka wa 2030, hekta milioni tano zaidi zimepangwa kurejeshwa.
Mpango huo unatarajiwa kunufaisha zaidi ya familia 600,000. Pia unaongeza uhifadhi wa hewa ya ukaa, kukuimarisha mazao ya mimea na nyasi, kufanya udongo kustahimili zaidi (na hili huzuia mafuriko) na kuuongezea nitrojeni isiyobadilika ambayo hufanya kazi kama mbolea ya kiasili.
Wabia katika mpango huu ni pamoja na CARE Nederland, Huduma za Msaada wa Katoliki, CIFOR-ICRAF, Oxfam, Regreening Africa, Sahel Eco, na World Vision ya Australia.
Kukuza misitu katika maeneo kame barani Afrika
Mpango wa Bustani ya Misitu, uliozinduliwa mwaka wa 2015, unajumuisha miradi mingi ya Bustani ya Misitu nchini Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Gambia, Kenya, Mali, Senegal, Uganda, na Tanzania. Kupitia mbinu za utafiti wa kilimo mseto, mbinu za kilimo zisizo endelevu hubadilishwa na mazingira hujiimarisha, huku wakulima wakipokea mafunzo muhimu, mahitaji na vifaa kwa ili wafanikiwe.
Kwa kupanda mamilioni ya miti kila mwaka, unalenga kupanuka kutoka hekta 41,000 zilizorejeshwa kwa sasa hadi hekta 229,000 kufikia mwaka wa 2030, na kusaidia watu wengi zaidi kupitia kwa nafasi za kazi 230,000 zilizopatikana.
Wabia katika mpango huu ni pamoja na Tume ya Umoja wa Afrika na Trees for the Future.
MAELEZO KWA WAHARIRI
Kuhusu Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza mwaka 2021–2030 kuwa Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia. Ukiongozwa na shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, pamoja na usaidizi wa wabia, umeundwa kuzuia, kusitisha, na kukabiliana na kushughulikia uharibifu wa mifumo ya ekolojia kote duniani. Unalenga kuboresha mabilioni ya hekta, yaliyotanda katika mifumo ya ikolojia ya nchi kavu na ya majini. Ukiwa wito wa kimataifa wa kuchukua hatua, Muongo wa Umoja wa Mataifa unajumuisha uungwaji mkono wa kisiasa, utafiti wa kisayansi, na uwezo wa kifedha wa kuuwezesha kuongeza kwa kiasi kikubwa urejeshaji wa hali ya awali.
Kuhusu Miradi Mikuu ya Umoja wa Mataifa ya Kurejesha Dunia katika Hali yake ya Awali
Tayari nchi zimeahidi kurejesha katika hali yake ya awali hekta bilioni moja – eneo kubwa kuliko Uchina – kama sehemu ya ahadi zao kwa makubaliano ya tabianchi ya Paris, Malengo ya Aichi ya bayoanuai, malengo ya Usitishaji wa Uharibifu wa Ardhi na Bonn Challenge. Hata hivyo, si mengi yanayojulikana kuhusu maendeleo au ubora wa urejeshaji huu. Kwa kutekeleza Miradi Mikuu ya Kurejesha Dunia katika Hali ya Awali, Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia unatambua mifano bora ya urejeshaji wa mifumo ya ekolojia kwa kiwango kikubwa na wa muda mrefu katika nchi au eneo lolote, inayojumuisha Kanuni 10 za Urejeshaji za Muongo wa Umoja wa Mataifa. Maendeleo ya Miradi Mikuu yote za Kurejesha Dunia katika Hali ya Awali yatafuatiliwa kwa uwazi kupitia Mfumo wa Ufuatiliaji wa Uborejeshaji wa Mifumo ya Ekolojia, jukwaa la Muongo wa Umoja wa Mataifa la kufuatilia juhudi za uboreshaji wa mifumo ya ekolojia duniani.
Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)
UNEP ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira duniani. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.
Kuhusu Shirika la Chakula na Kilimo (FAO)
FAO ni shirika maalum la Umoja wa Mataifa linaloongoza juhudi za kimataifa za kukomesha baa la njaa. Lengo lake ni kufikia utoshelezaji wa chakula kwa wote na kuhakikisha kuwa watu kwa kawaida wanapata chakula cha kutosha cha hali ya juu ili kuishi maisha yenye afya. Ikiwa na zaidi ya Mataifa Wanachama 194, FAO inafanya kazi katika zaidi ya nchi 130 kote duniani.
Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:
Ofisi ya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa: unep-newsdesk@un.org
Chumba cha Habari cha FAO: +39 06 570 53625, FAO-Newsroom@fao.org