Seoul, Oktoba 28, 2024 - Wizara ya Mazingira ya Jamhuri ya Korea na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) walitangaza leo kwamba Mkoa Maalum wa Jeju Unaojitawala utakuwa mahali pa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani tarehe 5 Juni mwaka wa 2025.
Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 5 mwezi wa Juni tangu mwaka wa 1973. Tangu wakati huo, Siku hii imekua na kuwa jukwaa kubwa zaidi la kimataifa la kuhamasisha kuhusu masuala ya mazingira.
Siku ya Mazingira Duniani mwaka wa 2025 itaangazia umuhimu wa kukomesha uchafuzi wa plastiki, na kuendana na mazungumzo yanayoendelea ili kuunda chombo cha kisheria cha kimataifa kuhusu uchafuzi wa plastiki, ikiwa ni pamoja na mazingira ya baharini, ambayo kikao chake cha tano kitafanyika katika Jamhuri ya Korea Novemba hii.
Jeju, kisiwa kinachojulikana kutokana na maajabu yake ya kiasili, kinaongoza juhudi za sera za Jamhuri ya Korea za kukabiliana na uchafuzi wa plastiki. Ni mkoa wa kwanza kuanzisha mfumo wa kurejesha vikombe vinavyoweza kutupwa baada ya kutumiwa katika Jamhuri ya Korea - Jeju ilitangaza katika mwaka wa 2022 maono yake ya kutokuwa na uchafuzi wa plastiki kufikia mwaka wa 2040.
"Kujitolea kwa Kisiwa cha Jeju kuwa na mustakabali usio na uchafuzi wa plastiki kunarandana kikamilifu na malengo ya Siku ya Mazingira Duniani ya mwaka wa 2025," alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP. "Kwa kuonyesha uzuri wake wa kiasili na mipango bunifu ya mazingira, Jeju itawahimiza wengine kuchukua hatua na kulinda sayari yetu."
Kim Wan-sup, Waziri wa Mazingira wa Jamhuri ya Korea, alisema, "Siku ya Mazingira Duniani mwaka wa 2025 itakuwa wakati muhimu kwa juhudi za kimataifa za kukomesha uchafuzi wa plastiki. Tutafanya kazi pamoja na Kisiwa cha Jeju ili kuhakikisha mafanikio ya hafla hiyo na kujiweka kama nchi inayoongoza katika kukabiliana na uchafuzi wa plastiki.
MAKALA KWA WAHARIRI
Kuhusu Wizara ya Mazingira, Jamhuri ya Korea
Dhamira ya Wizara ya Mazingira ya Jamhuri ya Korea ni kuhifadhi mazingira asilia na maeneo ya makazi, kuzuia uchafuzi wa mazingira, na kuhifadhi, kutumia na kukuza rasilimali za maji kwa njia endelevu.
Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)
UNEP ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira ulimwenguni. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano wa utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.
Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:
Kitengo cha Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa