Nairobi, Novemba 9, 2020 – Wawakilishi zaidi ya 500 wa wataalamu, serikali, mashirika ya uraia, wanazuoni na sekta binafsi kutoka barani Afrika na katika maeneo mengine duniani walikubaliana kuwa watashirikiana na kuimarisha matumizi ya nishati ya mvuke barani Afrika wakati wa kuhitimisha kikao cha nane cha Kongamano la Nishati ya Mvuke Bondeni Afrika (ARGEO C8) tarehe 6 mwezi wa Novemba.
Washiriki walitambua kuna umuhimu wa kujengea uwezo wataalamu wa masuala ya matumizi ya mvuke wanaoshughulikia miradi hii ya maendeleo kupitia jukwaa jipya lililoanzishwa la Kituo Kikuu cha Matumizi ya Mvuke Barani Afrika. Kuwezesha utafiti na maendeleo kufaulu, walikubaliana kuwa rasilimali za nishati ya mvuke zielekezwe kwa utafiti unaoongeza maarifa ili kusaidia wafanya maamuzi kubuni sera mwafaka na sheria zinazohitajika.
Kongamano lililoendesha mtandaoni kwa siku tano chini ya kaulimbiu “Energy and sustainability, seizing the moment to invest in geothermal resources for sustainable development”, liliendeshwa na Serikali ya Kenya kwa Ushirikiano na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), tawi la Afrika la Muungano wa Kimataifa wa Nishati ya Mvuke, Kampuni ya Kuzalisha Umeme nchini Kenya, Kampuni ya Kuzalisha Nishati ya Mvuke pamoja na Muungano wa Nishati ya Mvuke Nchini Kenya.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Waziri wa Nishati nchini Kenya, Charles Keter, alilisisitiza kuna umuhimu wa uvumbuzi na kujengea uwezo wahusika ili kuimarisha matumizi ya nishati ya mvuke ili kukuza uchumi na kuleta maendeleo kwa jamii barani Afrika.
"Kongamano hili linatoa jukwaa la kushirikiana na nchi zingine barani Afrika zilizo katika awamu mbalimbali za kukuza matumizi ya nishati ya mvuke, na kuimarisha maarifa ya kushirikiana, kujengea uwezo na kukuza teknolojia," Keter alisema.
Washiriki waligundua iwapo rasilimali za nishati ya mvuke zitatumika moja kwa moja kutakuwa na mabadiliko makubwa kwa uchumi na kwa maisha ya watu waoishi vijijini kote barani Afrika kupitia kushirikisha jamii kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya nishati ya mvuke.
Juliette Biao Koudenoukpo, Mkurugenzi na Mwakililishi wa Ofisi ya UNEP barani Afrika, alieleza kuwa kongamano hilo na matokeo yake yatachangia kufikia lengo la saba la maendeleo endelevu kuhusu nishati isiyochafua mazingira inayopatikana kwa bei nafuu.
"Nishati jadidifu isiyochafua mazingira italeta mabadiliko kwa changamoto zinazokumba nishati barani Afrika. Data ya matumizi ya nishati barani Afrika inaonyesha kuwa tunapaswa kuwa na wasiwasi; Afrika ina asilimia 13 ya idadi ya watu duniani; ila matumizi yake ya umeme duniani hayafikii asilimia 3, na ni asilimia 25 tu ya Waafrika wana umeme. Zaidi ya asilimia 70 ya Waafrika hutegemea fueli ya bayomasi," alisema.
Washiriki walikubaliana kuongeza rasilimali kwa nishati ya mvuke na kuimarisha uwezo wake wa kuzalisha umeme kwa megawati 2,500 kufikia mwaka wa 2030. Wadau wa nishati ya mvuke wataendelea kushirikiana na UNEP kupitia mradi wa ARGeo kuunda jukwaa la ushirikiano wa kikanda ili kuhamasisha watu kuhusu uwezo wa rasilimali ya nishati ya mvuke barani Afrika.
Ólafur Ragnar Grímsson, Rais mstaafu wa Iceland, pia alihutubia wakati wa kongamano hilo, na kueleza kuwa maendeleo ya viwanda kwa kasi katika nchi yake yalichangiwa na uwekezaji kwenye nishati jadidifu.
"Tunatoa wito kuwa uzalizaji wa chakula ujumuishwe kwenye kipengele cha kukuza nishati ya mvuke. Nishati ya jua, nishati ta upepo na nishati ya mvuke ni muhimu katika kukabiliana na uchafuzi unatokana na nishati ya visukuku na nishati inayochafua mazingira, inayopelekea vifo vya takribani watu milioni 7 kote duniani. Tunanuia kuendelea kushirikiana kukuza nishati ya mvuke barani Afrika," alisema.
Kwenye hotuba yake wakati wa kuhutubia mkutano huo mtandaoni, Amani Abu-Zeid, Kamishna wa Nishati na Muundo Msingi wa Afrika Mashariki (AU) alisema kuwa AU inatambua umuhimu wa ushirikiano wa kanda, na umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi na mashirika ya kimataifa kwenye uwekezaji ili kuimarisha maendeleo kutokana na rasilimali za nishati ya mvuke katika eneo hili. Alielezea kuwa kuna haja ya kukuza maarifa ya wataalamu kutoka eneo la Afrika kupitia taasisi zinazopatikana kwenye ukanda wa Afrika, na akasisitiza kuwa kuna umuhimu wa wanawake kushirikishwa kwenye mchakato mzima wa ukuzaji wa nishati ya mvuke.
Washiriki pia walikubaliana kufanya kazi kupitia mradi mpya uliozinduliwa wa Wanawake waokuza Nishati ya Mvuke kwa ushirikiano na Muungano wa Nishati ya Mvuke barani Afrika ili kuimarisha ushirikiano na kubadilishana maarifa kwenye ukanda huu.
MAKALA KWA WAHARIRI
Kuhusu ARGeo
Mradi wa Kiwanda cha Kukuza Nishati ya Mvuke Bondeni Afrika (ARGeo) umefadhiliwa na GEF na unatekelezwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP).
Mradi wa ARGeo ulizinduliwa mwezi wa Novemba mwaka wa 2010 wakati wa kikao cha kufungua Kongamano la Tatu la Kiwanda cha Kukuza Nishati ya Mvuke Bondeni Afrika (ARGeo-C3) nchini Djibouti. Mradi huo unalenga kukuza rasilimili zilizopo za nishati ya mvuke Afrika Mashariki na lengo kuu la kupunguza madhara yanayotokana na utafiti wa rasilimali. Pia, unalenga kupunguza uzalishaji wa gesi ya ukaa (GHG) kwa kutumia nishati ya mvuke katika eneo hili.
Mradi huu uliofadhiliwa na GEF ulikamilika mwaka wa 2019. Mradi wa baada ya GEF UNEP ARGeo uliidhinishwa kupitia mikakati yake ya miaka miwili (2021-22) wakati wa mkutano wa Kamati ya Maandalizi ya mkutano uliofanyika tarehe 2 Novemba mwaka wa 2020.
Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)
UNEP in mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.
Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:
Mohamed Atani, Mkuu wa Mawasiliano na Uhamasishaji kwenye Ofisi ya UNEP barani Afrika.
Benard Namunane, Afisa wa Mawasiliano, Wizara ya Nishati Kenya