Bogotá/Nairobi, Juni 5, 2020 – Wakati ambapo mataifa ulimwenguni yanapong'ang'ana kusitisha janga la COVID-19, mwaka huu, Siku ya Mazingira Duniani suala la jinsi ya kubadilisha mienendo yetu kwa mazingira ili kuhifadhi jamii zetu na kuzuia majanga yanayoweza kutokea siku zijazo linaangaziwa.
Siku ambayo huadhimishwa tarehe 5 mwezi wa Juni kila mwaka, ni maadhimisho makuu ya umoja wa Mataifa yanayotoa wito wa kuchukua hatua kwa manufaa ya mazingira na haja ya kutunza sayari yetu. Tangu yalipozinduliwa mwaka wa 1974, maadhimisho hayo yamepanuka na kuwa jukwaa la kimataifa la kuhamasisha kuhusu masuala ya mazingira.
Mwaka huu – licha ya janga linaloendelea kuangaisha jamii ya kimataifa – Kolombia na Ujerumani walishirikiana kuwa wenyeji wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, yaliyoadhimishwa moja kwa moja mtandaoni kutoka Bogotá. Rais wa Kolombia Iván Duque Márquez na Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira Duniani (UNEP), walikuwa mstari mbele kutoa wito wa kimataifa wa kuuita"Ni Wakati wa #KutunzaMazingira,” wito unaolenga kuchukuliwa kwa hatua za kukomesha hali inayoendelea ya uangamiaji wa spishi na uharibifu wa dunia asilia.
"Kujali binadamu ni kujali mazingira. Tunapofanya kazi ili kujiimarisha, tushughulikie mazingira jinsi inavyotakikana - kwa kuyafanya kitovu cha uamuzi wetu," alisema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres. "Wakati wa Siku ya Mazingira Duniani, na kila siku, ni wakati wa kutunza mazingira."
"Sasa ni wakati wa kutafakari kuhusu mazingira, kuhusu mabadiliko ya tabianchi, kuhusu mienendo tunayopaswa kuwa nayo, kuhusu kinachopaswa kuwa maadili katika jamii zetu, ili tuweze kutunza spishi na kutunza mifumo ya ekolojia," alisema Rais Duque. Kolombia, mojawapo ya mataifa sita yaliyotunukiwa na uanuai mkuu katika eneo la Amerika ya Latini, linalenga kupanda miti milioni 180 kufikia mwezi wa Agosti mwaka wa 2020.
Huku mahitaji yetu yanavyoendelea kuongezeka, binadamu wametumia mazingira kiwango ambacho hayawezi kustahimili. Kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita, idadi ya watu imeongezeka mara dufu; uchumi wa kimataifa na biashara duniani imeimarika takribani mara nne na mara kumi, mtawalia. Kuzuka kwa COVID-19 kumeonyesha kuwa, tunapoharibu bayoanuai, tunaharibu mifumo ambayo hutuwezesha kuishi. Kwa kudhuru uwezo dhaifu wa mazingira, tunawezesha vijidudu vya magonjwa-ikiwa ni pamoja na virusi vya korona-kuenea.
“Leo, Siku ya Mazingira Duniani, ninatoa wito kwa kila mmoja kushirikiana ili kutunza mazingira yanatuwezesha sote kuwepo. Tukiimarisha mifumo inayowezesha sayari kuwepo, tutakuwa na maisha mazuri na mali ya kutosha," alisema Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP.
Takribani nusu ya GDP duniani hutegemea mazingira. Bahari zetu na misitu yetu huhudumia mabilioni ya watu na kutoa ajira isiyochafua mazingira - nafasi za kazi milioni 86 hutokana tu na misitu. Watu bilioni nne hutegemea madawa ya kienyeji pekee. Masuluhisho yanayotokana na mazingira - kama vile upandaji wa miti na kurembesha miji kutumia kijani na kupunguza joto kwenye majengo -yanaweza kutusaidia kupunguza uzalishaji wa gesi chafu ili tuweze kufikia malengo ya Mkataba wa Paris.
Licha ya changamoto za mikakati kutokana na janga liliopo, serikali, sekta ya binafsi, mashirika ya uraia na watu binafsi kote duniani walioshiriki katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika leo, walitoa wito wa kushughulikia mazingira na kuonyesha umuhimu wake kwa afya zetu, kwa chumi zetu na kwa jamii zetu.
Nchini Kanada, Waziri wa Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi Siku ya Mazingira Duniani alitangaza kuhusu zaidi ya miradi 60 inayoendelezwa. Na ufadhili kutoka kwa Mradi wa 'Canada Nature Fund’s Target 1 Challenge', miradi hii inalenga kukuza bayoanuai, kutunza spishi zilizo hatarini kuangamia, na kukuza uwajibikaji wa kiekolojia, na kuongeza maeneo yaliyohifadhiwa nchini Kanada. Miradi hii inaimarisha juhudi za Kanada za kufikia malengo ya kuhifadhi asilimia 25 ya ardhi yake kuhifadhi na asilimia 25 ya bahari zake kufikia mwaka wa 2025.
Nchini Perú, Rais Martin Vizcarra alisafiri hadi Mbuga ya Kitaifa ya Tambopata inayopatikana Amazon, ili kusimamia uzalishaji wa miche 741,238 ya kukuza misitu na kusaidia jamii za kiasili zilizokumbwa na janga la COVID-19.
Nchini Chile, serikali ilizindua mradi wa kitaifa wa kuwezesha kutumia bidhaa zaidi ya mara moja, kuboresha ushughulikiaji na utupaji wa taka, ikijumuisha taka kutokana na huduma za matibabu kutokana na janga lililopo.
Nchini Kenya, marufuku ya matumizi ya plastiki inayotumiwa tu mara moja katika mbuga za kitaifa, fukweni, misituni na maeneo mengine yaliyohifadhiwa ilianza kutekelezwa leo. Waziri Mkuu wa Ethiopia, Dkt. Abiy Ahmed, alizindua mradi unaonuia kupanda miti bilioni 5 kama sehemu ya mradi wa nchi hiyo wa 'Green Legacy'.
Katika eneo la Asia ya Kusini Mashariki, Waziri Mkuu wa Thailand Prawit Wongsuwon na Waziri wa Mali Ghafi na Mazingira, Varawut Silpa-archa, walizindua kampeni ya kitaifa ya kutumia plastiki zaidi ya mara moja. Wizara ya Mali Ghafi na Mazingira, ya Vietnam ilizindua "Wakati wa Kutunza Mazingira" na kutenga Mwezi wa Kushughulikia Mazingira huku kampeni ya Wild For Life ikizinduliwa Bahasa Indonesia.
Pia, nchi zinazopatikana eneo la Asia Kusini ziliweka hatua madhubuti wakati wa kusherehekea Siku ya Mazingira Duniani. Bhutan, nchi pekee isiyozalisha gezi chafu, ilionyesha kujitolea kwake kushughulikia mazingira kwa kuzindua Mkatati wa Kitaifa wa Mazingira uliofanyiwa marekebisho. Nchini Nepal, Mamlaka ya Kitaifa ya Umeme, ilianza kutumia awamu ya kwanza ya mfumo wake wa kawi inayotokana na jua wa megawati 25.
Nchini India, Wizara ya Mazingira, Misitu na Mabadiliko ya Tabianchi na Ofisi ya UNEP nchini India zilianzisha mradi wa kupanda misiti mjini katika miji 200, huku UNEP na TED-Ed’s “Earth School” ikishirikishwa katika Wizara ya Rasilimali Watu ili kutumika kama jukwaa la kidijitali kwa walimu, DIKSHA.
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson leo alitangaza kuwa pauni milioni 10.9 zitatumika kutunza wanyamapori wasiopatikana kwa urahisi na makaazi yake, ikijumuisha kobe wanaopatikana katika visiwa vya British Virgin Islands, ndege wa 'penguin' wanaopatikana katika eneo la Georgia Kusini na Visiwa vya South Sandwich, matumbawe yanayopatikana Comoros, na sokwe wanaopatikana nchini Uganda.
Viongozi kadhaa wa dunia, kama sehemu ya kile kinachojulikana kama 'Ambition Coalition for Nature and People', waliidhinisha kauli iliyotolewa ikitoa wito "kwa serikali zote duniani kutunza mifumo iliyosalia ya ekolojia na mapori, kutunza na kushughulikia ipasavyo takribani asilimia 30 ya ardhi na bahari zinazopatikana kwenye sayari yetu kufikia mwaka wa 2030, na kuboresha na kutunza bayoanuai, kama hatua muhimu za kusaidia kuzuia majanga kutokea baadaye na kupunguza athari za dharura kwa afya ya umma, na kuweka msingi wa kukuza uchumi imara duniani kwa kubuni nafasi za kazi na kuboresha maisha ya binadamu.
Vijana - ambao wamekuwa mstari mbele kuhamasisha kuhusu masuala ya mazingira - wameimarisha juhudi za kurekebisha mienendo yetu mibofu dhidi ya mazingira. Leo, Vuguvugu la Maskauti Duniani lilizindua mpango mpya wa'Earth Tribe' jukwaa litakalotumiwa kutoa beji za mazingira kwa wanachama wake milioni 50. Kwa kuongezea, taasisi za elimu zaidi ya 500, zilizo na wanafunzi milioni 4.5, watazungumzia leo jinsi watakavyotoa mchango wao kwa "Race to Zero" kwa kujitolea kutozalisha gesi ya ukaa na kushirikisha masuala ya mazingira kwenye mitaala yao kufikia nwaka wa 2050.
Wakionyesha mshikamano wao na nchi zinazofanya kazi ili kukomesha janga lililopo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP alisema kuwa kuhifadhi mazingira ni muhimu kutuwezesha kujiimarisha baada ya janga hili. Pia, aliongezea kuwa dunia innahitaji masuluhisho anuai kwa changamoto za mazingira ambazo huvuka mipaka ya jamii na kuvuka mipaka ya mataifa.
"Dunia ni kubwa mno na inategemeana mno, na hivyo mtu mmoja hawezi kukabiliana na changamoto kwa mazingira zinazokumba spishi zetu," alisema.
MAKALA KWA WAHARIRI
Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)
UNEP in mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.
Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:
Keishamaza Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, UNEP
Moses Osani, Habari na Vyombo vya Habari, UNEP,