Nayim Ahmed/ UNEP
16 May 2023 Toleo la habari Kushughulikia kemikali na uchafuzi

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inatoa masuluhisho ya kupunguza uchafuzi wa plastiki duniani

Nairobi, Mei 16, 2023 – Uchafuzi wa plastiki unaweza kupunguzwa kwa asilimia 80 kufikia mwaka wa 2040 iwapo nchi na kampuni zinaweza kuweka sera thabiti na mabadiliko ya masoko kwa kutumia teknojia iliopo, kwa mjibu wa ripoti mpya ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP). Ripoti hii imetolewa tunapoelekea awamu ya pili ya mazungumzo mjini Paris kuhusiana na makubaliano ya kimataifa ya kukomesha uchafuzi wa plastiki, na inaelezea kiwango na hali ya mabadiliko yanayohitajika kukomesha uchafuzi wa plastiki na kukuza uchumi unaotumia bidhaa tena na tena.

Kukomesha Mtiririko: Jinsi dunia inavyoweza kukomesha uchafuzi wa plastiki na kukuza uchumi unaotumia bidhaa tena na tena ni ripoti inayozingatia uchanganuzi wa mienendo thabiti, mabadiliko ya masoko na ya sera zinazoweza kusaidia serikali kutafakari kuhusu hatua viwandani.

“Jinsi tunavyotengeneza, kutumia na kutupa plastiki kunachafua mifumo ya ekolojia, kuhatarisha afya ya binadamu na kudhuru mazingira,” alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP. "Ripoti hii ya UNEP inatoa mwongozo wa njia ya kupunguza hatari hizi kwa kutumia mbinu ya kutumia tena na tena itakayozuia plastiki kwenye mifumo ya ekolojia, kwenye miili yetu na katika uchumi. Ikiwa tutafuata mwongozo huu, ikijumuisha katika mazungumzo kuhusu mpango wa uchafuzi wa plastiki, tunaweza kupata mafanikio makubwa ya kiuchumi, kijamii na kimazingira.

Mabadiliko ya soko yanahitajika ili kuwa na mabadiliko yatakayopelekea kuwepo na soko zinazotumia bidhaa tena na tena

Kupunguza uchafuzi wa plastiki kwa asilimia 80 kote duniani kufikia mwaka wa 2040, ripoti hii inapendekeza kuanza kwa kuondoa plastiki inayosababisha matatizo isiyohitajika ili kupunguza ukubwa wa tatizo. Kisha, ripoti hii inatoa wito wa mabadiliko matatu katika masoko – kutumia tena, kuchakata, matumizi mapya na matumizi mbalimbali ya bidhaa:

  1. Kutumia tena: Kukuza utumiaji tena, ikijumuisha chupa zinazoweza kujazwa, dispensa kubwa, kurejeshewa pesa ukirudisha, mipango ya kurejesha mifuko na kadhalika, inaweza kupunguza asilimia 30 ya uchafuzi wa plastiki kufikia mwaka wa 2040. Kufikia lengo hili, serikali zinapaswa kusaidia kukuza biashara thabiti inayowezesha bidhaa kutumiwa tena.
  1. Kuchakata: Kupunguza uchafuzi wa plastiki kwa asilimia 20 ya ziada kufikia mwaka wa 2040 inawezekana iwapo uchakataji utaimarishwa na kuwa na manufaa. Kuondoa ruzuku kwa mafuta ya visukuku, kutekeleza yaliyomo kwenye mwongozo wa kukuza uchakataji, na hatua nyinginezo vinaweza kuongeza kiwango cha plastiki inayoweza kuchakatwa kutoka asilimia 21 hadi asilimia 50.
  1. Matumizi mapya na matumizi mbalimbali: Kubadilisha kwa uangalifu bidhaa kama vile mifuko ya plastiki, vikopa vya plastiki na vitu vya plastiki vya kupakia chakula na bidhaa zilizotengenezwa kutoka kwa nyenzo mbadala (kama vile makaratasi au vitu vinavyoweza kuoza, plastiki iliyochakatwa, n.k.) inaweza kupunguza asilimia 17 ya ziada ya uchafuzi wa plastiki. 

Hata na hatua zilizopo hapo juu, tani milioni 100 za plastiki kutoka kwa bidhaa zinazotumika mara moja na zile zisizodumu zinapaswa kushughulikiwa kwa njia salama kufikia mwaka wa 2040 – pamoja na urathi mkuu wa uchafuzi wa plastiki uliopo. Hii inaweza kushughulikiwa kwa kuweka na kutekeleza mfumo na viwango vya usalama vya jinsi ya kutupa plastiki isiyoweza kuchakatwa, na kwa kuwajibisha watengenezaji wa bidhaa kuondoa maikroplastiki, na kadhalika.

Kwa ujumla, mabadiliko yatakayowezesha uchumi unaotumia bidhaa tena na tena yanaweza kuokoa dola za Marekani trilioni 1.27 kwa kuzingatia gharama na mapato ya kuchakata. Dola za Marekani trilioni 3.25 zaidi zitaokolewa kutokana na mambo ya nje yatakayoepukwa kama vile afya, mazingira, uchafuzi wa hewa, uharibifu wa mifumo ya ekolojia ya maeneo ya bahari, na gharama zinazohusiana na kuchukuliwa hatua. Mabadiliko haya pia yanaweza kupelekea ongezeko la nafasi za kazi 700 000 kufikia mwaka wa 2040, hasa katika nchi za kipato cha chini, na kwa kiasi kikubwa kuboresha maisha ya mamilioni ya wafanyikazi katika sekta zisizo rasmi.

Gharama za uwekezaji kwa mabadiliko ya kimfumo yaliyopendekezwa ni muhimu, ila ni kidogo bila kujumuisha mabadiliko ya kimfumo: Dola za Marekani bilioni 65 kwa mwaka ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni 113 kwa mwaka. Kiasi kikubwa cha mambo haya yanaweza fikiwa iwapo uwekezaji uliopangiwa vifaa vipya vya uzalishaji wa plastiki – isiyohitajiki tena kwa kupunguza nyenzo zinazohitajika – au kutoza ushuru uzalishaji wa plastiki ambayo haijawahi kutumika hadi kwa miundomsingi inayohitajika ya kutumia bidhaa tena na tena. Bado wakati ni muhimu: kuchelewa kwa kipindi cha miaka mitano kunaweza kupelekea ongezeko la  tani milioni 80 za uchafuzi wa plastiki kufikia mwaka wa 2040.

Gharama za juu zaidi katika uchumi wa kutupa na uchumi wa kutumia bidhaa tena na tena ni za kuendesha shughuli. Kukiwa na sheria zitakapohakikisha kwamba plastiki zinazotengenezwa zinaweza kutumika tena na tena, mipango ya Uwajibikaji Mpana wa Mzalishaji wa Bidhaa (EPR) inaweza kugharamia uendeshaji wa shughuli kwa kuhakikisha kuwa mifumo inatumia bidhaa tena na tena kwa kuwataka wazalishaji kufadhili ukusanyaji, uchakataji na kuwajibikia utupaji wa plastiki baada ya kumaliza kutumia. 

Katika ngazi ya kimataifa sera zilizokubaliwa zinaweza kusaidia kukabiliana na vizingiti kwa mikakati ya kitaifa na shughuli za biashara, kudumisha uchumi unaotumia bidhaa tena na tena duniani, kutoa fursa za biashara na kubuni nafasi za kazi. Hii inaweza kujumuisha vigezo vinavyokubalika kwa bidhaa za plastiki zinazoweza kupigwa marufuku, maarifa ya kuvuka mipaka, sheria kuhusu  viwango vya chini zaidi vinavyohitajika kufanya kazi kutokana na mipango ya EPR na viwango vingine.

Ripoti hii inapendekeza kwamba mfumo wa fedha wa kimataifa unaweza kuwa sehemu ya sera za kimataifa za kuwezesha vitu vinavyochakatwa kushindana katika mizani sawa na vile ambavyo havijawahi kutumika, kunufaisha uchumi wakati wa kutoa masuluhisho, na kuanzisha mifumo ya ufuatiliaji na utaratibu wa ufadhili.

Kimsingi, watungasera kukumbatia mbinu inayojumuisha vyombo vya kisheria na sera zinazoshughulikia hatua katika mzunguko mzima, masuluhisho katika mfumo mzima kwa sababu huimarishana kuwezesha kufikia lengo la kufanyia mabadiliko uchumi. Kwa mfano, kubuni sheria za kufanya bidhaa ziweze kutumika tena kwa uchumi pamoja na malengo ya uchakataji na ruzuku za kifedha kwa kwa kampuni za uchakataji.

Ripoti hii pia inaangazia sera mahususi, ikijumuisha viwango vya muundo, usalama, na plastiki zinazoweza kuoza na kuharibika; malengo ya kiwango cha chini cha kuchakata; Mipango ya EPR; ushuru; marufuku; mikakati ya mawasiliano; manunuzi ya umma, na kuweka lebo. 

 

MAKALA KWA WAHARIRI   

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)

UNEP ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira duniani. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano wa kutunza mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.

 

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:    

Kitengo cha Habari na Vyombo vya Habari cha Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa