Pixabay
14 Sep 2021 Toleo la habari Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ripoti ya UN inatoa wito wa kutafakari upya kuhusu msaada wa dola bilioni 470 za Marekani unaoathiri bei na kufanya kutozingatia malengo ya…

  • Asilimia 87 ya kati ya dola bilioni 540 ya msaada wa serikali wa kila mwaka kwa wakulima hujumuisha mikakati inayoathiri bei ile inayoweza kudhuru mazingira na afya.
  •  Kilimo ni moja wapo ya chanzo kikuu cha mabadiliko ya tabianchi kupitia uzalishaji wa gesi ya ukaa kutoka kwa vyanzo mbalimbali
  • Kuimarisha msaada kwa sekta ya kilimo kwa kutumia njia ya uwazi, iliyoboreshwa na iliyodhibitishwa, kutanufaisha sayari yetu

Nairobi/Roma/New York, Septemba 14 2021 – Msaada wa kimataifa kwa wazalishaji katika sekta ya kilimo hufikia dola za Marekani bilioni 540 kwa mwaka, ikiwa ni asilimia 15 ya jumla ya thamani ya uzalishaji wa kilimo. Kufikia mwaka wa 2030, kiwango hiki kinatarajiwa kuongezeka zaidi ya mara tatu na kufikia dola za Marekani trilioni 1.759.  Lakini asilimia 87 ya msaada huu, takriban dola za Marekani bilioni 470, huathiri bei na ni hatari kwa mazingira na afya.  Haya ni matokeo ya ripoti mpya ya UN inayotoa wito wa kutafakari upya kuhusu marupurupu hatari ili kufikia mengi ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ya mwaka wa 2030 na kufanikisha Muongo wa UN wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia.

Ripoti hiyo, Fursa ya mabilioni ya dola: Kutafakari upya kuhusu msaada wa kilimo ili kubadilisha mifumo ya chakula, iliyozinduliwa na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) inaonesha kuwa msaada ulioko kwa wakulima sanasana ni pamoja na marupurupu ya bei, kama vile ruzuku  kwa ushuru wa kuagiza nchini na ruzuku ya kuuza nje ya nchi, pamoja na ruzuku ya bajeti inayofungamanishwa na uzalishaji wa bidhaa maalum au pembejeo.  Ruzuku hizi haizitoshi, huathiri bei ya chakula, hudhuru afya za watu, huharibu mazingira, na mara nyingi hubagua, na kufanya mashirika makubwamakubwa ya kilimo kujiimarisha kuliko wakulima wadogowadogo, ambao wengi wao ni wanawake.

Katika mwaka wa 2020, watu milioni 811 ulimwenguni walikumbwa na baa la njaa na angalau mtu mmoja kati ya watatu ulimwenguni (watu bilioni 2.37) hawakuwa na uwezo wa kupata chakula cha kutosha kwa mwaka mzima. Katika mwaka wa 2019, karibu watu bilioni tatu, katika kila eneo ulimwenguni, hawakuweza kumudu kupata lishe bora.

Ijapokuwa sehemu kubwa ya msaada wa kilimo una madhara kwa sasa, takribani dola za Marekani bilioni 110 hukuza miundomsingi, utafiti na maendeleo, na inafaidi sekta ya chakula na kilimo kwa jumla. Kuangalia upya msaada kwa wazalishaji wa kilimo, badala ya kuuondoa, kutasaidia kukomesha umaskini, kutokomeza baa la njaa, kuwa na utoshelezaji wa chakula, kuboresha lishe, kukuza kilimo endelevu, kukuza matumizi na uzalishaji endelevu, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha mazingira, kupunguza uchafuzi wa mazingira, na kupunguza ubaguzi.

Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Qu Dongyu, alisema: "Ripoti hii, iliyotolewa usiku wa kuamkia Mkutano Mkuu wa UN wa Mifumo ya Chakula, ni wito wa serikali kote ulimwenguni kuwa macho na kutafakari upya kuhusu mipango ya misaada ya kilimo ili kuzifanya imara kwa lengo la kubadilisha mifumo yetu ya chakula kutokana na kilimo na kuchangia kwa njia Nne kuwa na:  Lishe bora, uzalishaji bora, mazingira bora na maisha bora."

Kilimo ni moja wapo ya chanzo kikuu cha mabadiliko ya tabianchi kupitia uzalishaji wa gesi ya ukaa kutoka kwa vyanzo mbalimbali, ikijumuisha mbolea kwenye ardhi ya malisho ya mifugo, mbolea za kemikali, kilimo cha mpunga, uchomaji wa taka ya mimea, na mabadiliko ya matumizi ya ardhi.  Wakati uo huo, wakulima wamo hatarini zaidi kuathariwa na mabadiliko ya tabianchi, kama vile joto kali, kuongezeka kwa viwango vya bahari, ukame, mafuriko, na uvamizi wa nzige.

Kuendelea na msaada kama kawaida kutazidisha makali ya changamoto tatu kwa mazingira na hatimaye kudhuru maisha ya binadamu. Kufikia malengo ya Mkataba wa Paris kunahitaji kubadilisha msaada hasa katika nchi zenye kipato cha juu unaotolewa kwa sekta kuu za nyama na maziwa, ambayo huchangia asilimia 14.5 ya uzalishaji wa gesi ya ukaa duniani. Katika nchi zenye kipato cha chini, serikali zinapaswa kuchunguza upya msaada zinazotoa kwa dawa za kuua wadudu zilizo na sumu na mbolea za kemikali au ukuzaji wa kilimo cha aina moja ya mmea.

"Serikali zina fursa sasa ya kubadilisha kilimo illi kijali maisha ya binadamu, na kukifanya kuwa suluhisho kwa vitisho vilivyopo vya mabadiliko yatabianchi, uharibifu wa mazingira, na uchafuzi wa mazingira," alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP. "Kwa kuanza kuwa na msaada wa kilimo unaojali mazingira, usiobagua na ulio na ufanisi, tunaweza kuboresha maisha, na wakati uo huo kupunguza uzalishaji wa gesi chafu, kutunza na kuboresha mifumo ya ekolojia, na kupunguza matumizi ya kemikali za kilimo."

Ripoti hiyo inaangazia visa ambapo mchakato kama huu ulianza kutumiwa: jimbo nchini India la Andhra Pradesh ambalo lilipitisha sera ya Kilimo cha Kiasili Bila Bajeti Yoyote; mabadiliko ya sera ya kilimo ya mwaka wa 2006 nchini China ambayo inaunga mkono kupunguza kwa matumizi ya mbolea za madini na dawa za kuua wadudu za kemikali; Mpango wa Malipo ya Mara Moja nchini Uingereza ulioondoa ruzuku kutokana na makubaliano na Muungano wa wa Kitaifa wa Wakulima; Muungano wa Ulaya, ambapo kuna marupurupu kwa kilimo mseto kupitia marekebisho ya Sera ya Jumla ya Kilimo (CAP) na mpango wa Senegali wa PRACAS unaotoa marupurupu kwa wakulima kulima mazao anuwai.

Ingawa hakuna mkakati maalum utakaotosheleza wakulima wote wakati wa kutafakari upya, ripoti hii inapendekeza hatua sita pana kwa serikali:  

  • kutathmini msaada uliotolewa;  
  • kuelewa athari zake chanya na ghasi;  
  • kutambulishaa kinachopaswa kurekebishwa;  
  • kukadiria athari zake;  
  • kuboresha mkakati uliopendekezwa na kuelezea kwa kina utakavyotekelezwa;   
  • hatimaye, kufuatilia mkakati uliotekelezwa.

"Kutafakari upya kuhusu msaada wa kilimo ili kubadilisha mifumo yetu ya chakula isichafue mazingira, iwe endelevu zaidi - ikiwa ni pamoja na kutuza mazoea mazuri kama vile kilimo endelevu na njia nzuri zinazojali mazingira - kunaweza kuboresha uzalishaji na matokeo kwa mazingira," alisema Msimamizi wa UNDP, Achim Steiner.  "Pia itaimarisha maisha ya wakulima wadogowadogo milioni 500 kote ulimwenguni - wengi wao wakiwa wanawake - kwa kuhakikisha kuna usawa zaidi nyanjani."

Kwa kutumia msaada kwa sekta ya kilimo kwa kwa njia ya uwazi, iliyoboreshwa na iliyofanyiwa utafiti, sayari yetu itafaidika kutokana na mfumo wa chakula duniani ulio na virutubishi, endelevu zaidi, usiobagua na ulio na ufanisi.  Ripoti hiyo imezinduliwa kabla ya Mkutano Mkuu wa Mifumo ya Chakula wa mwaka wa 2021 (Septemba), COP15 kuhusu bayoanuai (Octoba) na COP26 kuhusu mabadiliko ya tabianchi (Novemba). Hafla hizi zitawezesha serikali kutoa ahadi za kimataifa za kutafakari upya kuhusu ruzuku za kilimo zilizopitwa na wakati, kujiimarisha vyema baada ya COVID-19, kujitolea kwa mkakati kama huu na kuratibu na kufuatilia utekelezaji wake. 

 

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu Mkutano Mkuu wa Mifumo ya Chakula

Tarehe 23, Septemba mwaka wa 2021, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ataitisha Mkutano Mkuu wa Mifumo ya Chakulakama sehemu ya juhudi za Muongo wa kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kufikia mwaka wa 2030. Mkutano huo utazindua hatua dhabiti za kupiga hatua za kufikia SDG zote 17, ambazo kila mojawapo kwa kiwango fulani hutegemea mifumo bora ya chakula, endelevu zaidi na isiyobagua.

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)

UNEP ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira duniani. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.

Kuhusu Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa  

FAO ni shirika maalum la Umoja wa Mataifa linaloongoza juhudi za kimataifa za kutokomeza baa la njaa. Lengo la FAO ni kuwa na utoshelezaji wa chakula kwa watu wote na kuhakikisha kuwa watu wanapata chakula cha hali ya juu cha kutosha mara kwa mara ili kuwa na maisha mazuri, na watu wenye afya.   Na zaidi ya nchi wanachama 194, FAO hufanya kazi kwa nchi zaidi 130 kote ulimwenguni.

Kuhusu Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa

UNDP hufanya kazi katika maeneo na nchi 170 kusaidia kutokomeza umaskini, kupunguza ubaguzi na kutengwa, na kujiimarisha ili nchi ziweze kuwa na maendeleo. Kama shirika la maendeleo la UN, UNDP hutekeleza jukumu muhimu la kusaidia nchi kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Keisha Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa,