Pixabay
08 Nov 2023 Toleo la habari Kushughulikia Mazingira

Serikali zinapanga kuzalisha mafuta ya visukuku maradufu mwaka wa 2030 kuliko kiwango kinachoruhusiwa kudhibiti ongezeko la joto lisizidi…

Stockholm, Novemba 8 2023 – Ripoti mpya kuu iliyochapishwa leo ina onyesha kuwa serikali zinapanga kuzalisha takriban asilimia 110 zaidi ya mafuta ya visukuku katika mwaka wa 2030 kuliko inavyotakiwa kudhibiti ongezeko la joto lisizidi nyuzijoto 1.5, na asilimia 69 zaidi ya inavyohitajikakudhibiti ongezeko la joto lisizidi nyuzijoto 2.

Haya yanajiri licha ya serikali 151 za kitaifa kuahidi kutozalisha hewa chafu kabisa na utabiri wa hivi punde ambao unapendekeza mahitaji ya kimataifa ya makaa ya mawe, mafuta na gesi yatafikia kilele katika muongo huu, hata bila sera mpya.  Ikiunganishwa, mipango ya serikali itapelekea ongezeko la uzalishaji wa makaa ya mawe duniani hadi mwaka wa 2030, na katika uzalishaji wa mafuta na gesi duniani hadi angalau mwaka wa 2050, na hivyo kuongeza pengo linaloendelea kuongezeka la uzalishaji wa mafuta ya visukuku.

Matokeo kuu ya ripoti ni pamoja na:

  • Kwa kuzingatia hatari na kutokuwa na uhakika wa kufyonza na kuhifadhi gesi ya ukaa na kuondoa kaboni dioksidi, nchi zinapaswa kulenga kukomesha kabisa uzalishaji na matumizi ya makaa ya mawe kufikia mwaka wa 2040, na kupunguza kwa pamoja uzalishaji na matumizi ya mafuta na gesi kwa robo tatu kufikia mwaka wa 2050 kutoka kwa viwango vyake vya mwaka wa 2020, kama kiwango cha chini zaidi.
  • Ingawa nchi 17 kati ya 20 zilizoangaziwa zimeahidi kutozalisha gesi chafu kabisa — na nyingi ya nchi hizo zimeanzisha miradi ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafu kutoka kwa shughuli za kuzalisha mafuta ya visukuku— hakuna nchi iliyojitolea kupunguza uzalishaji wa makaa ya mawe, mafuta na gesi ili kuwezesha kupunguza ongezeko la joto lisizidi nyuzijota 1.5.
  • Serikali zilizo na uwezo mkubwa wa kuachana na nishati ya visukuku zinapaswa kujitolea zaidi kupunguza zaidi na kusaidia michakato ya kuleta mabadiliko katika nchi zilizo na rasilimali chache.

 Ripoti ya Pengo la Uzalishaji wa Gesi ya Ukaa mwaka wa 2023: "Kupunguza au kuongeza? Wazalishaji wakuu wa mafuta ya visukuku wanapanga uchimbaji zaidi licha ya ahadi za kushughulikia mazingira” imetolewa na Taasisi ya Mazingira ya Stockholm (SEI), Climate Analytics, E3G, Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo Endelevu (IISD) na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP). Inatathmini uzalishaji wa makaa ya mawe, mafuta na gesi uliopangwa na unaokadiriwa na serikali kinyume cha viwango vya kimataifa kulingana na Mkataba wa Paris’s vya malengo la joto.

"Serikali kihalisia zinaongeza uzalishaji wa nishati ya visukuku; hali itakayodhuru watu na sayari maradufu," alisema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres. “Hatuwezi kukabiliana na janga la mabadiliko ya tabianchi bila kushughulikia chanzo chake: kutegemea nishati ya visukuku. COP28 ni sharti ipitishe ujumbe unaoeleweka wazi kwamba hatuwezi kuendelea kutumia nishati ya visukuku — na kwamba mwisho wake umetimia. Tunahitaji ahadi za kuaminika ili kuimarisha matumizi ya nishati jadidifu, kukoma kutumia nishati ya visukuku, na kuimarisha ufanisi wa nishati, huku tukihakikisha mabadiliko ya haki na ya usawa."   

Julai mwaka wa 2023 ulikuwa mwezi ulioshuhudia kiwango cha juu zaidi cha joto kuwahi kushuhudiwa, na kuna uwezekano mkubwa ulikuwa mwezi mwezi ulioshuhudia kiwango cha juu zaidi cha joto kwa kipindi cha miaka 120,000 iliyopita, kulingana na wanasayansi. Kote duniani,  mawimbi mabaya ya joto, ukame, mioto misituni, dhoruba, na mafuriko vinagharimu maisha na njia za kujipatia riziki, na kuonyesha wazi kwamba mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na binadamu yatadumu. Uzalishaji wa kabonidioksidi duniani— ambao angalau asilimia 90 hutoka kwa nishati ya visukuku — uliongezeka hadi viwango vya juu kati ya mwaka wa 2021 na mwaka wa 2022. 

"Mipango ya serikali ya kuongeza uzalishaji wa mafuta ya visukuku ni kizingiti kwa mabadiliko yanayohitajika ili kutozalisha hewa chafu kabisa, na kutilia mashaka mustakabali wa binadamu," Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP alisema.  "Kuimarisha uchumi kupitia nishati bora isiochafua mazingira ndiyo njia pekee ya kumaliza umaskini wa nishati na kupunguza uzalishaji wa gesi chafu kwa wakati mmoja."

"Kuanzia kwa COP28, mataifa ni sharti yaungane kuchukua hatua za usawa za kukoma kutumia makaa ya mawe, mafuta na gesi — ili kupunguza janga lijalo kwa manufaa ya kila mtu kwenye sayari hii," aliongezea.

Ripoti ya Pengo la Uzalishaji wa gesi ya Ukaa ya mwaka wa 2023 inatoa taarifa mpya kwa mapana kuhusu nchi 20 ambazo ni wazalishaji wakuu wa nishati ya visukuku: Australia, Brazil, Kanada, Uchina, Colombia, Ujerumani, India, Indonesia, Kazakhstan, Kuwait, Meksiko, Nigeria, Norway, Qatar, Urusi, Saudi Arabia, Afrika Kusini, Miliki za Falme za nchi za Kiarabu, Uingereza ikijumuisha Uingereza na Ireland Kaskazini, na Marekani. Maelezo haya yanaonyesha kuwa nyingi ya serikali hizi zinaendelea kutoa msaada muhimu wa kisera na kifedha kwa uzalishaji wa mafuta ya visukuku.

"Tunaona kwamba serikali nyingi zinakuza gesi ya visukuku kama nishati muhimu 'kipindi cha mpito' lakini hatuoni mipango dhahiri ya kukoma kuitumia baadaye," anasema Ploy Achakulwisut, mwandishi mkuu wa ripoti hii na mwanasayansi wa SEI. “Ila sayansi inasema lazima tuanze kupunguza uzalishaji wa makaa ya mawe, mafuta na kuanza kutumia — mbali na kuimarisha matumizi ya nishati isiyochafua mazingira, kupunguza uzalishaji wa methani kutoka kwa  vyanzo vyote, pamoja na juhudi zingine za kushughulikia mazingira — ili kuweza kutimiza lengo la joto kutozidi nyuzijoto 1.5.”

 Licha ya kuwa chanzo kikuu cha janga la mabadiliko ya tabianchi, nishati ya visukuku ni suala lililokuwa linapuuzwa zaidi katika majadiliano ya kimataifa kuhusu mazingira hadi miaka ya hivi majuzi. Wakati wa COP26 mwishoni mwa mwaka wa 2021, serikali ziliahidi kuimarisha juhudi za "kupunguza matumizi ya nishati ya makaa ya mawe na kuondoa ruzuku isiyofaa kwa nishati ya visukuku", ingawa hazikukubaliana kushughulikia uzalishaji wa aina zote za nishati ya visukuku.

“COP28 inaweza kuwa wakati muhimu ambapo serikali hatimaye zitajitolea kuacha kutumia nishati zote za visukuku na kutambua wajibu unaostahili kutekelezwa na kuwezesha mabadiliko yanayosimamiwa kwa njia sawa,"  anasema Michael Lazarus, mwandishi mkuu wa ripoti na Mkurugenzi wa Kituo cha SEI US. "Serikali zilizo na uwezo mkubwa wa kuachana na uzalishaji wa nishati ya visukuku ziwajibike zaidi huku zikitoa fedha na usaidizi ili kusaidia nchi zingine kufuata nyayo."   

 Zaidi ya watafiti 80, kutoka kwa nchi zaidi ya 30, walichangia katika uchanganuzi na mapitio, kutoka kwa vyuo vikuu mbalimbali, makundi ya wataalamu watafiti na mashirika mengine ya utafiti. 

 

Maoni kuhusu Ripoti ya Pengo la Uzalishaji wa Gesi ya Ukaa mwaka wa 2023

"Madhara ya nishati ya visukuku yanaonekena wazi. Kufikia katikati ya karne hii, tunahitaji kuwa tumeweka makaa ya mawe katika kaburi la sahau, na kupunguza uzalishaji wa mafuta na gesi kwa angalau robo tatu — ili kuweza kukoma kabisa kutumia nishati ya visukuku. Bado, licha ya ahadi zao za kushughulikia mazingira, serikali zinapanga kuwekeza pesa nyingi zaidi katika tasnia chafuzi inayokufa, wakati ambapo kuna fursa nyingi katika kukuza sekta ya nishati isiochafua mazingira. Mbali na kuwa kero kwa uchumi, ni janga la mtabianchi tuliloejitengenezea sisi wenyewe."

– Neil Grant, Mchanganuzi Wa Masuala Ya Mazingira na Nishati, Climate Analytics

 

"Licha ya serikali kote ulimwenguni kutia saini malengo kabambe ya kutozalisha gesi chafu, uzalishaji wa makaa ya mawe, mafuta na gesi kote duniani bado unaongezeka huku upunguzaji uliopangwa hautoshi kuepusha athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi. Upanuzi huu wa tofauti kati ya matamshi ya serikali na juhudi wanazofanya mbali na kuwa kizingti kwa mamlaka yao huongeza hatari kwetu sote. Tayari kwa muongo huu tunaelekea kuzalisha makaa ya mawe zaidi kwa asilimia 460, gesi zaidi kwa asilimia 82, na mafuta kwa asilimia 29 zaidi kuliko inavyohitajika kudhibiti joto lizizidi nyuzijota 1.5. Kabla ya COP28, serikali ni sharti zijikakamue kuimarisha uwazi kwa kiasi kikubwa kuhusu jinsi zitakavyofikia malengo ya kutozalisha hewa chafu na kuweka hatua za kisheria ili kuunga mkono malengo haya."

– Angela Picciariello, Mtafiti Mkuu, IISD

 

“Huku mahitaji ya makaa ya mawe, mafuta na gesi vikifikia kilele muongo huu hata bila sera za ziada, ni wazi kwamba mahitaji ya  kiuchumi kwa sasa yatategemea matumizi ya nishati isiochafua mazingira na kupunguza matumizi ya nishati ya visukuku — ilihali serikali zinashindwa kuweka mikakati ya kuleta mabadiliko. Kuendelea kuwekeza katika uzalishaji mpya wa mafuta ya visukuku huku mahitaji ya kimataifa ya makaa ya mawe, mafuta na gesi yakipungua ina umuhimu wa kiuchumi kwa muda mfupi kwa wote isipokuwa kwa wazalishaji wa bei nafuu zaidi. Na uharibifu kutokana na majanga ya tabianchi utaongezeka zaidi tusipositisha upanuzi wa mafuta ya visukuku sasa. Wakati ni sasa kwa serikali kuchukua udhibiti wa kuleta mabadiliko ya nishati isiyochafua mazingira na kuoanisha sera zao na ukweli wa kile kinachohitajika kuwa dunia inayojali mazingira." 

– Katrine Petersen, Mshauri Mkuu wa Masuala ya Sera wa E3G

 

Makala kwa Wahariri

Kuhusu Ripoti ya Pengo la Uzalishaji wa Gesi ya Ukaa:

Ripoti inayoiga msururu wa Ripoti ya UNEP ya Pengo la Juhudi za Kukabiliana na Gesi Chafu — ripoti hii inaonyesha tofauti kubwa kati ya uzalishaji wa mafuta ya visukuku uliopangwa wa nchi na viwango vya kimataifa  vya uzalishaji vinavyolenga  kupunguza ongezeko la joto lisizidi nyuzijoto 1.5 na nyuzijoto 2°C.

Kuhusu Taasisi ya Mazingira ya Stockholm

Taasisi ya Mazingira ya Stockholm ni taasisi ya kimataifa ya utafiti inayojitemea ambayo hushughulikia masuala ya mazingira na maendeleo katika ngazi za sera za eneo, za kitaifa, za kikanda na za kimataifa kwa zaidi ya robo ya karne. SEI huwezesha kufanya maamuzi ya maendeleo endelevu kwa kuonyesha uhusiani kati ya sayansi na sera.

Kuhusu Climate Analytics

Climate Analytics ni taasisi ya kimataifa ya sayansi na sera ya mazingira inayojishughulisha kote ulimwenguni kuendesha na kuunga mkono hatua za kushughulikia mazingira kwa kuzingatia kudhibiti kiwango cha joto kisizidi nyuzijoto 1.5. uwa tunaonyesha uhusiano kati ya sayansi na sera ili kujengea uwezo nchi zilizo hatarini kuweza kushiriki katika mazungumzo ya kimataifa kuhusu mazingira na kuwezesha mikakati ya kitaifa kupitia utafiti, uchambuzi na msaada unaohitajika.

Kuhusu E3G 

E3G ni shirika la Ulaya linalojitegema linaloshughulikia mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha juhudi za kukuza mazingira salama. E3G inaundwa na wataalamu wakuu wa mikakati duniani kuhusu uchumi wa kisiasa wa mabadiliko ya tabianchi, na kujitolea kuwezesha kuwepo na mazingira salama kwa wote. E3G huunda miungano ya sekta mbalimbali ili kuwa na matokeo yaliyofafanuliwa kwa uangalifu, yaliyochaguliwa kwa uwezo wake wa kuleta mabadiliko. E3G inafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na washirika walio na nia sawa katika serikali, siasa, mashirika biashara, mashirika ya uraia, sayansi, vyombo vya habari, taasisi zinazojali maslahi ya umma na kadhalika. E3G inawezesha yawezekanayo.

Kuhusu Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo Endelevu

Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo Endelevu (IISD), mshindi wa tuzo, ni taasisi ya watafiti wanaojitegemea wanaopigania masuluhisho kutokana na utafiti kwa changamoto kuu za mazingira duniani. Maono yetu ni kuwa na ulimwengu ambapo watu na sayari watastawi; dhamira yetu ni kuharakisha dunia kuwa na maji safi, uchumi wa haki na mazingira thabiti. Tukiwa na ofisi zetu mijini Winnipeg, Geneva, Ottawa na Toronto, kazi yetu huathiri maisha katika takriban nchi 100.

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) 

UNEP ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira duniani. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano wa kutunza mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.  

 

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Ulrika Lamberth, Afisa Mkuu wa Vyombo vya Habari (Stockholm, Sweden), na Lynsi Burton, Afisa wa Mawasiliano (Seattle, Marekani), Taasisi ya Mazingira ya Stockholm

Keisha Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, (Nairobi, Kenya)

Paul May, Mkuu wa Mawasiliano, na Neil Grant, Mchanganuzi Wa Masuala Ya Mazingira na Nishati, Climate Analytics (Berlin, Ujerumani)

Aia Brnic, Afisa Mwandamizi wa Mawasiliano, na Angela Picciariello, Mtafiti Mwandamizi, Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo Endelevu (Geneva, Uswisi)

Riya Amin, Afisa Mawasiliano wa Ngazi ya Chini, E3G (London, Uingereza)