Picha: UNEP /Florian Fussstetter
02 Feb 2023 Toleo la habari Kushughulikia kemikali na uchafuzi

Siku ya Mazingira Duniani mwaka wa 2023 itaandaliwa na Côte d'Ivoire na itaangazia masuluhisho kwa uchafuzi wa plastiki

Picha: UNEP /Florian Fussstetter

 

Nairobi/Abidjan, Februari 2, 2023 Côte d’Ivoire itakuwa mwenyeji wa Siku ya Mazingira Duniani tarehe 5 Juni mwaka wa 2023 chini ya kaulimbiu ya masuluhisho kwa uchafuzi wa plastiki. Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na Côte d’Ivoire walitangaza hayo leo.

Mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 50 ya Siku ya Mazingira Duniani, baada ya kuanzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika mwaka wa 1972. Katika kipindi cha miongo mitano iliyopita, siku hiyo imekua na kuwa mojawapo ya majukwaa makubwa zaidi ya kimataifa ya kuhamasisha kuhusu mazingira. Mamilioni ya watu hushiriki kupitia mtandaoni na kupitia shughuli za ana kwa ana, kupitia hafla na kuchukuliwa kwa kote ulimwenguni.

“Janga la uchafuzi wa plastiki ni tishio linalodhihirika wazi linaloathiri kila jamii kote ulimwenguni," amesema Jean-Luc Assi, Waziri wa Mazingira na Maendeleo Endelevu wa Côte d'Ivoire. “Kama nchi mwenyeji ya Siku ya Mazingira Duniani, tunatoa wito kwa sekta zote, ikijumuisha serikali, makampuni ya biashara, na mashirika kuungana kutafuta na kupigania masuhulisho.”

Nchi ya Côte d'Ivoire ilipiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki tangu mwaka wa 2014, na kuwezesha matumizi ya mifuko inayoweza kutumiwa tena. Mji mkubwa zaidi nchini humo, Abidjan, pia umekuwa kitovu cha mashirika anzilishi yanayojizatiti kukomesha uchafuzi wa plastiki. 

Zaidi ya tani milioni 400 za plastiki huzalishwa kila mwaka kote duniani, nusu ikiwa ya kutumika tu mara moja. Kati ya hiyo, chini ya asilimia 10 huchakatwa. Takriban tani kati milioni 19 na milioni 23 hujipata kwenye maziwa, mito na bahari kila mwaka.

Chembechembe za plastiki – ndogo zinazoweza kuwa milimita 5 – hujikuta kwenye chakula, maji na kwenye hewa. Inakadiriwa kuwa, kila mtu kwenye sayari huvuta zaidi ya chembechembe 50,000 za plastiki kwa mwaka –na kiwango kikubwa zaidi tukizingatia uvutaji wa hewa.  Plastiki inayotupwa au kuteketezwa baada ya kutumiwa mara moja tu hudhuru afya ya binadamu na bayoanuai na kuchafua kila mfumo wa ekolojia kuanzia kwa vilele vya milima hadi chini ya bahari.

Kukiwepo na sayansi na masuluhisho ya kukabiliana na tatizo hili, serikali, makampuni na washikadau wengine lazima waimarishe na kuharakisha hatua za kutatua janga hili. Hii inasisitiza umuhimu wa Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu kuhamasisha kuchukuliwa kwa hatua za kuleta mabadiliko chanya kutoka kila pembe ya dunia.

Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu itawezeshwa na Serikali ya Uholanzi, ambayo ni mojawapo ya nchi zinazochukua hatua kabambe kuhakikisha pplastiki inatumika tena. Nchi hii imetia sahihi Makubaliano Mapya ya Kimataifa ya Uchumi wa Plastiki Duniani na ni mwanachama wa Ushirikiano wa Kimataifa kuhusu Uchafuzi wa Plastiki na Takataka za Baharini. Pia ni mwanachama wa Muungano wa Juhudi Kabambe unaotoa wito wa kuwepo kwa chombo chenye nguvu na kabambe cha kisheria cha kimataifa ili kukabiliana na uchafuzi wa plastiki.

"Uchafuzi wa plastiki na athari zake mbaya kwa afya, kwa uchumi na kwa mazingira ni mambo yasiyoweza kupuuzwa. Hatua ya dharura zinahitajika. Wakati uo huo, tunahitaji masuluhisho ya kweli, madhubuti na kabambe,” alisema Vivianne Heijnen, Waziri wa Mazingira wa Uholanzi. "Kama sehemu ya sera kadhaa za kushughulikia plastiki, Uholanzi na jumuiya ya Ulaya kwa ujumla wamejitolea kikamilifu kupunguza uzalishaji na matumizi ya plastiki inayotumika mara moja, ambayo inaweza na sharti ibadilishwe na njia mbadala za kudumu na endelevu." 

Tangazo la hivi leo linafuatia azimio lililopitishwa mwaka wa 2022 katika Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa ili kuunda chombo cha kisheria kuhusu uchafuzi wa plastiki, ikiwa ni pamoja na mazingira ya baharini, kwa nia ya kukamilisha majadiliano kufikia mwishoni mwa mwaka wa 2024. Mkutano wa kwanza wa Kamati ya Majadiliano kati ya Serikali (INC-1) ulifanyika nchini Uruguay mwezi wa Desemba na mkutano wa pili unatarajiwa kufanywa mjini Paris mwaka wa 2023. Chombo hicho kitazingatia mbinu ya kina ambayo inashughulikia hali halisi ya maisha ya plastiki.

“Ni sharti tutumie kila fursa na kushauriana na kila mshikadau ili kukabiliana na tatizo la plastiki kabisa," Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP alisema.  “Côte d'Ivoire na Uholanzi ni miongoni mwa nchi kadhaa zinazokabiliana na changamoto hii na kukumbatia manufaa ya uchumi ambao plastiki hutumika zaidi ya mara moja. Maadhimisho ya 50 ya ya Siku ya Mazingira Duniani ni wakati kwa serikali zote, mashirika ya biashara, makundi katika jamii na watu binafsi kujiunga na vuguvugu.   

Kampeni ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka wa 2023 itatumia hashtagi na kaulimbiu #KomeshaUchafuziWaPlastiki.

 

MAKALA KWA WAHARIRI   

Kuhusu Siku ya Mazingira Duniani

Siku ya Mazingira Duniani ni chombo kikuu cha Umoja wa Mataifa cha kuhimiza uhamasishaji kote duniani na kuchukua hatua za kushughulikia mazingira. Siku inayoadhimishwa kila mwaka tangu mwaka wa 1973, pia imekuwa jukwaa muhimu la kukuza maendeleo ya vipengele vya mazingira vya Malengo ya Maendeleo Endelevu. Ikiongozwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), zaidi ya nchi 150 hushiriki kila mwaka. Mashirika makubwa, mashirika yasiyokuwa ya serikali, jamii, serikali na watu mashuhuri kutoka pembe zote za dunia hutumia Siku ya Mazingira kuangazia masuala ya mazingira.

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)

UNEP ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira duniani. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano wa kutunza mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:  

Kitengo cha Habari na Vyombo vya Habari cha Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa