Photo by Evans Dims on Unsplash
26 Oct 2023 Toleo la habari Kushughulikia Mazingira

Tanzania inakuza ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi katika juhudi kuu za kuboresha mazingira yalio makazi kwa waliopoteza makazi…

Tbilisi, Oktoba 25, 2023 – Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na Mfuko wa Mazingira ya Kijani (GCF) leo wametangaza mradi unaogharimu dola za Marekani milioni 19 unaolenga ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sehemu ya ushirikiano wa kihistoria na UNHCR, Shirika Linalowahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa.

Mradi huu unalenga mkoa wa Kigoma nchini Tanzania – katika mwambao wa kaskazini mashariki mwa Ziwa Tanganyika - ulio na  wakazi takriban milioni 2.3 mbali na wakimbizi 250,000 kutoka nchi jirani, ambao wengi wao wanaishi katika kambi za wakimbizi za Nduta na Nyarugusu. Makazi haya, ambayo yalianzishwa kwa haraka ili kushughulikia mahitaji muhimu ya kibinadamu, yameongeza shinikizo la idadi ya watu kwa mifumo ya ekolojia iliyoharibika katika eneo hili.

Mabadiliko ya tabianchi, kwa sasa na inayokadiriwa, yaongeza zaidi shinikizo kwa mazingira haya na uwezekano wa kuathiriwa na tabianchi kwa jamii za wenyeji na za walizopoteza makao. 

Mradi huu wa miaka mitano wa Kukuza ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi katika mazingira ya Mkoa wa Kigoma nchini Tanzania, uliidhinishwa na Bodi ya GCF katika mkutano wake wa 37 uliofanyika mjini Tblisi, Georgia.

Mpango huu unatarajiwa kuwa mbinu bora kwa juhudi za kutumia masuluhisho ya kiasili na uboreshaji wa mifumo ya ekolojia kama mkakati kamili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi - yanayojulikana kitaalamu kama ukabilianaji wa hali kutegemea mfumo wa ekolojia - haswa katika mazingira yalio makazi kwa waliopoteza makao yao.

Unalenga kushughulikia mahitaji changamano na yanayoingiliana ya ustahimilifu kwa jamii zinazowakaribisha watu waliopoteza makao na watu waliopoteza makao katika mazingira ambapo tabianchi, misaada ya kibinadamu na maendeleo huingiliana na kuwa na athari changamano.

Mradi huu utanufaisha moja kwa moja hadi watu 570,000, huku ukiboresha na kuhifadhi hekta 261,000 za misitu na mazingira ya ekolojia ya kilimo ili kusaidia kutoa riziki kwa wenyeji katika wilaya za Kasulu, Kakonko na Kibondo. Mipango ya matumizi ya ardhi kwa kustahimili mabadiliko ya tabianchi, ukuzaji misitu, kilimo, utoshelezaji wa maji, udhibiti wa mafuriko na ukuzaji wa sera vitatekelezwa kwa mbinu inayojali mazingira.

Katika hafla ya utiaji sahihi Mkataba wa Kisheria kati ya GCF na UNEP, Jessica Troni, Meneja wa Ofisi ya Kukabiliana na Hali wa UNEP, alisema:  “Mradi huu unatoa fedha zinazohitajika kwa ajili ya mahitaji ya kukabiliana na hali ya zaidi ya watu nusu milioni katika eneo la mazingira magumu zaidi nchini Tanzania. Inaashiria hatua muhimu na ya msingi katika kushughulikia uhusiano kati ya chakula, misitu na nishati na hatari ya hali ya hewa ya jamii za wenyeji na watu waliopoteza makao wanaotegemea mifumo muhimu, nyeti ya ekolojia na huduma zao.

"UNHCR imekuwa ikiongoza juhudi za kushughulikia masuala ya uharibifu wa mazingira na utoaji wa nishati endelevu katika maeneo yanayohifadhi wakimbizi nchini Tanzania, na tunashukuru sana kwa mradi huu wa GCF - wa kwanza wa aina yake - ambao utasaidia wakimbizi na jamii karimu ambazo zimekuwa zikiwakaribisha kukabiliana na changamoto zinazowakabili kutokana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema Bi. Mahoua Parums, Mwakilishi wa UNHCR nchini Tanzania. 

Katika miongo ya hivi karibuni, mkoa wa Kigoma umekabiliwa na uharibifu mbaya zaidi wa mazingira kutokana na ongezeko la watu, kilimo kisicho endelevu na ukataji miti. Udhaifu uliojitokeza umedhihirika katika kupungua kwa mavuno ya chakula kikuu ambacho ni mahindi na matukio ya mafuriko yaliyoongezeka.

Kupitia mkabala wake unaojumuisha mambo mengi, mradi huu unalenga kushughulikia changamoto hizi kwa kuzingatia manufaa mengi ya mienendo ya kukabiliana na hali kutegemea mfumo wa ikolojia. UNEP na Serikali ya Tanzania sasa tayari wameshirikiana kufanya kazi kwa miradi ya kukabiliana na hali kutegemea mfumo wa ekolojia nchini katika maeneo ya pwanimijinimaeneo ya vijijini, na katika mwambao wa Ziwa Victoria.

Mfumo wa Kimataifa Warszawa (WIM) wa UNFCCC wa Hasara na Uharibifu na Kundi la Uhamiaji Ulimwenguni, ambao wote hushirikiana na UNEP, unaangazia umuhimu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa ili kushughulikia athari za mabadiliko ya tabianchi kwa uhamaji wa binadamu na kupoteza makao. 

Akiangazia maono hayo mapana, Bw. Fredrick Ibrahim Kibuta, Balozi wa Tanzania nchini Urusi, alisema: “Mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuwa miongoni mwa changamoto kuu zinazokabili binadamu kwa sasa. Mikakati ya kitaifa na kimataifa inaendelea, ikijumuisha uundaji wetu wa Mpango wa Kitaifa wa Kukabiliana na Hali. Lakini mipango hii ya sera inahitaji kufanywa miradi inayoweza kutekelezeka. Hapo ndipo mradi mpya wa Kigoma unapoingilia.” 

"Tunapongeza na kushukuru ushirikiano wa dhati na GCF wakati wote wa kuendesha mradi.  Tanzania inatarajia kuendelea kufanya kazi na UNEP na GCF kwa kupendekeza zaidi miradi ya kukabiliana na hali,” Balozi aliendelea.

Verónica Gálmez, Naibu Mkurugenzi wa Kitengo cha Kushughulikia na Kukabiliana na Hali cha Mfuko wa Mazingira ya Kijani, alisema:  “Nimefurahishwa sana kuona mradi huu ukipitishwa leo, mradi ambao utanufaisha watu walio katika mazingira magumu zaidi nchini Tanzania. Kwa ushirikiano na UNEP, UNHCR, na Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mradi huu wa kukabiliana na hali kutegemea mfumo wa ekolojia utaimarisha ustahimilivu wa mazingira ya Kigoma na wa wakazi wake, ikiwa ni pamoja na jamii za wenyeji na watu waliopoteza makazi yao”. 

Kwa sasa Tanzania inatoa makazi kwa takriban wakimbizi 250,000, hasa kutoka Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

 

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa

UNEP in mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano wa utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.    

Kuhusu Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR)

UNHCR, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, ni shirika la kimataifa linalojitolea kuokoa maisha, kulinda haki na kukuza mustakabali bora kwa watu wanaolazimika kugura makwao kutokana na mizozo na mateso. Tunaongoza hatua za kimataifa za kulinda wakimbizi, jamii zilizolazimishwa kupoteza makwao na watu wasio na utaifa.  Maono yetu ni ulimwengu ambapo kila mtu anayelazimishwa kugura kwao anaweza kukuza mustakabali bora. 

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:

Kitengo cha Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa

Faith Kasina, UNHCR, Nairobi, +254 113 427 094

Bahia Egeh, UNHCR, Dar Es Salaam, +255 765 168 179