Photo credit: UNEP
10 Dec 2024 Toleo la habari Kutumia mazingira kushughulikia tabianchi

Tuzo la UNEP la Mabingwa wa Dunia wa mwaka wa 2024 linatolewa kwa viongozi sita waliojitolea kushughulikia mazingira kwa dhati

Photo credit: UNEP

Nairobi, Disemba 10, 2024 – Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) leo lilitangaza wapokeaji wa mwaka wa 2024 wa Tuzo la Mabingwa wa Dunia, wanaotunukiwa kwa uongozi wao bora, hatua thabiti na masuluhisho endelevu ya kukabiliana na uharibifu wa ardhi, ukame na kuenea kwa majangwa. Washindi wa tuzo mwaka huu ni pamoja na waziri wa Watu wa Kiasili, mtetezi wa mazingira, mpango wa kilimo endelevu, mtetezi wa haki za Watu wa Kiasili, mwanasayansi anayezingatia upandaji miti na mwanaekolojia mwanzilishi. 

Tuzo lilalotolewa kila mwaka la Mabingwa wa Dunia, tuzo la ngazi la Umoja wa Mataifa linalotolewa kwa heshima ya mazingira, linatolewa kwa watu walio msitari mbele kuanzisha juhudi za kulinda watu na sayari. Tangu mwaka wa 2005, tuzo hili limetolewa kwa washindi 122 kwa uongozi bora na wa kutia moyo wa kushughulikia mazingira.

“Angalau asilimia 40 ya ardhi ulimwenguni tayari imeharibiwa, kuenea kwa majangwa kunaongezeka na ukame mbaya unazidi kushuhudiwa mara kwa mara. Habari njema ni kwamba masuluhisho tayari yapo kwa sasa, na kote duniani, watu na mashirika ya kipekee yanadhihirisha kwamba inawezekana kupigania na kuiponya sayari yetu,” alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP.

"Juhudi za Mabingwa wa Dunia wa mwaka wa 2024 zimesimama kidede kama ukumbusho kwamba vita vya kulinda ardhi yetu, mito yetu na bahari zetu ni vita tunavyoweza kushinda. Kukiwa na sera mwafaka, mafanikio ya kisayansi, mageuzi ya mifumo, uanaharakati, pamja na uongozi muhimu na hekima ya Watu wa Kiasili, tunaweza kuboresha mifumo yetu ya ekolojia.

Washindi wa tuzo la UNEP la Mabingwa wa Dunia wa mwaka wa 2024  ni::

  • Sonia GuajajaraWaziri wa Watu wa Kiasili nchini Brazili anayetuzwa katika kitengo cha Uongozi Unaozingatia Sera, amekuwa akitetea haki za Watu wa Kiasili kwa zaidi ya miongo miwili. Guajajara alikua Waziri wa kwanza wa Watu wa Kiasili nchini Brazili na waziri wa kwanza mwanamke wa Kiasili katika mwaka wa 2023. Chini ya uongozi wake, maeneo 13 yametambuliwa kuwa ardhi ya Watu wa Kiasili ili kuzuia ukataji miti, ukataji miti kinyume cha sheria na walanguzi wa madawa ya kulevya. 
     
  • Amy Bowers Cordalismtetezi wa haki za Watu wa Kiasili anayetuzwa katika kitengo cha Motisha na Kuchukua Hatua, anatumia ujuzi wake wa kisheria na kujitolea kwake kuboresha mifumo ya ekolojia kukuza mustakabali bora wa kabila la Yurok na Mto Klamath nchini Marekani. Kazi ya Cordalis ya kuboresha mfumo wa ekolojia wa mto na kuhimiza matumizi ya mazoea endelevu ya uvuvi yanaonyesha jinsi hatua thabiti za kushughulikia mazingira zinavyoweza kuleta mabadiliko chanya, huku zikipelekea haki na kipato kwa watu wa kiasili.
     
  • Gabriel Paunmtetezi wa mazingira kutoka Romania anayetuzwa katika kitengo cha Motisha na Kuchukua Hatua, ni mwanzilishi wa NGO Agent Green, shirika ambalo limekuwa likisaidia kuokoa maelfu ya hekta za bayoanuai inayothaminiwa katika Carpathians tangu mwaka wa 2009 kwa kufichua uharibifu na ukataji miti kinyume cha sheria wa msitu wa jadi wa mwisho barani Ulaya. Paun amepokea vitisho vya kuuawa na ameshambuliwa mwili kutokana na kazi yake ya kuandika kuhusu uharibifu wa misitu katika eneo ambalo ni muhimu kwa mfumo wa ekolojia na lililo na bayoanuai ya kipekee kama vile linksi (paka mwitu) na mbwa mwitu.  
     
  • Lu Qi, mwanasayansi wa China anayetuzwa katika kitengo cha Sayansi na Ubunifu, amefanya kazi katika sekta za sayansi na sera kwa miongo mitatu huku akiisaidia China kukabiliana na uharibifu na kupunguza majangwa yake.  Akiwa Mwanasayansi Mkuu wa Chuo cha Misitu cha China na Rais mwanzilishi wa Taasisi ya Ukuta Mkuu wa Kijani, Lu ametekeleza wajibu muhimu katika utekelezaji wa mradi mkubwa zaidi wa upandaji miti duniani, na kuanzisha mitandao ya wataalam watafiti na ushirikiano, na kuhimiza ushirikiano wa mashirika mbalimbali ili kuzuia kuenea kwa majangwa, uharibifu wa ardhi na ukame. 
     
  • Madhav Gadgil, mwanaekolojia wa Kihindi anayetuzwa katika kitengo cha Mafanikio ya Kudumu, ametumia miongo kadhaa kulinda watu na sayari kupitia utafiti na kushirikisha jamii. Kuanzia na tathmini muhimu za athari kwa mazingira za sera za serikali na za kitaifa hadi kwa ushirikishwaji wa mazingira ya mashinani, kazi ya Gadgil imeathiri sana maoni ya umma na sera rasmi kuhusu ulinzi wa malighafi. Anasifika kwa utafiti wake wa kipekee katika eneo dhaifu kiekolojia la Western Ghats nchini India, ambalo ni kitovu cha bayoanuai ya kipekee duniani.  
     
  • SEKEM, mpango wa kilimo endelevu unaotuzwa katika kitengo cha Maono ya Ujasiriamali unasaidia wakulima nchini Misri kuhamia kwa kilimo endelevu zaidi. Uendelezaji wake wa kilimo cha bayodinamiki pamoja na kazi ya upandaji miti na upandaji miti kwa maeneo iliokatwa vimekuwa vikibadilisha maeneo makubwa ya jangwa kuwa biashara ya kilimo inayostawi, na kuendeleza maendeleo endelevu kote nchini.  

Takriban watu bilioni 3.2 kote duniani wameathiriwa na kuenea kwa majangwa. Kufikia mwaka wa 2050, zaidi ya robo tatu ya jumla ya idadi ya watu ulimwenguni wanatarajiwa kuathiriwa na ukame.   

Mwezi Machi mwaka wa 2019, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kutangaza mwaka wa 2021 hadi 2030 kuwa Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia. Kampeni ya UNEP ya #GenerationRestoration inalenga kuunga mkono hatua zinapopigwa kwa kasi kuhusu ahadi hizi kwa kutafuta uungwaji mkono kwa Ajenda ya 2030 ya kufanya kazi muhimu ya uboreshaji wa mifumo ya ekolojia ili kulinda asilimia 30 ya asili kwenye ardhi na baharini na kuboresha asilimia 30 ya sayari iliyoharibiwa. Kote ulimwenguni, nchi zimeahidi kuboresha hekta bilioni 1 za ardhi kufikia mwaka wa 2030, wakati mwelekeo wa sasa unaonyesha hekta bilioni 1.5 zitahitaji kuboreshwa ili kufikia malengo ya mwaka wa 2030 ya kutokuwa na uharibifu wowote wa ardhi.    

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu Mabingwa wa Dunia 

Tuzo la UNEP la  Mabingwa wa Dunia hutuza watu binafsi, makundi na mashirika ambayo huchukua hatua za kusababisha mabadiliko chanya kwa mazingira.  Tuzo hili ni la Umoja wa Mataifa la ngazi ya juu zaidi linalotolewa kwa heshima ya mazingira. #MabingwaWaDunia 

Kuhusu Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia 

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limetangaza mwaka wa 2021 hadi wa 2030 kama Muongo wa UN wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia. Unaongozwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa kwa ushirikiano na wabia. Ulizinduliwa ili kuzuia, kusitisha na kukabiliana na udidimiaji na uharibifu wa mifumo ya ekolojia kote ulimwenguni.  Unalenga kuboresha mabililioni ya hekta za aridhi ya nchi kavu pamoja na mifumo ya ekolojia ya majini. Wito wa kimataifa wa kuchukua hatua, Muongo wa Umoja wa Mataifa unaungwa mkono na wanasiasa, utafiti wa kisayansi, na ufadhili ili kuimarisha uboreshaji wa mifumo ya ekolojia. #GenerationRestoration

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Kitengo cha Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa