Pixabay
25 Jun 2021 Toleo la habari Ocean & Coasts

Uganda yajiunga ma Kampeni ya Bahari Safi kuzuia uchafu wa plastiki kwenye maziwa na mito yake

 

Nairobi/Kampala, Juni 25, 2021 - Uganda imejiunga na Kampeni ya Bahari Safi leo, na kuonyesha kujitolea kwa nchi hiyo kukubaliana na uchafuzi wa bahari na kuzuia uchafuzi wa plastiki kuingia kwenye maziwa, mito na bahari.

Kampeni ya Bahari Safi, iliyozinduliwa na Shiririka la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) katika mwaka wa 2017, imekuwa chanzo cha mabadiliko, ikibadilisha mienendo, mazoea, kanuni na sera kote duniani.

Kwa sasa ikiwa na nchi washirika 63, Kampeni ya Bahari Safi ni vuguvugu la kimataifa linalojitolea kukomesha uchafuzi wa bahari kutoka kwenye vyanzo hadi kwa bahari. Ahadi za nchi zilizotia sahihi zinashughulia zaidi ya asilimia 60 ya fukwe duniani, na ongezeko ya wanachama kutoka katika nchi kama vile Uganda zinazofanya kazi kutunza mifumo yetu muhimu ya maji inayounganika. Ahadi zilizotolewa na watu binafsi ni zaidi ya milioni moja.

Nchi ya Afrika Mashariki isiyokuwa na bandari ni sehemu ya eneo la Maziwa Makuu (Great Lakes region) mfumo wake mkuu wa ekolojia ya maji safi ukiwa Ziwa Victoria. Maji yanayotumiwa pia na Kenya na Tanzania, ni chanzo cha mto maarufu wa Nile unaopitia eneo la kilomita 6,695 kabla ya kukamilikia kwenye Bahari ya Mediterania.

Hata hivyo, Ziwa victoria na mifumo ya ekolojia inayohusiana huhatarishwa na madhara mabaya ya changamoto za aina tatu kwa sayari – uharibifu wa bayoanuai, udharura wa hali ya hewa, na uchafuzi uliokithiri – kutokana miongo ya uzalishaji usioendelevu, matumizi mabaya ya bidhaa, na utupaji mbaya wa taka.

Kwa nchi ya uganda, uchafuzi huu unajumuisha taka, kama vile plastiki na vifaa vya uvuvi, na madini yanayotokana na kilimo, yanayoharibu huduma za mifumo ya ekolojia na kuhatarisha afya mapato ya jamii. Takribani moja kati ya samaki tano katika Ziwa Victoria ilikuwa imemeza plastiki, unaonyesha utafitiwa hivi majuzi, wakati ambapo utafiti mwingine unaonesha kuwepo na chembechembe za plastiki chini ya maji katika maeneo mbalimbali maziwani.

Juliette Biao Koudenoukpo, Mkurugenzi wa UNEP na Mwakilishi wa Eneo la Afrika: "Tukizingatia uchafuzi wa plastiki, ni muhimu kutilia mkazo umuhimu wa vyanzo vya maji – maziwa, mito, maeneo oevu, bila kusahau, bahari – ambayo huathiriwa na madhara mabaya ya plastiki na uchafuzi mwingineo. Hii inajumuisha bidhaa za uvuvi na madini mengi kutokana na kilimo."

"Tunakaribisha nchi ya Uganda - nchi ya pili isiyo na bandari, na ya kwanza barani Afrika - inapojiunga na Kampeni ya Bahari Safi. Hii haihusiani tu na bahari lakini inahusu vyanzo vyetu vyote vya maji na jinsi vinavyotoa huduma muhimu ambazo zinasaidia kuishi. Kama sehemu ya ushirikiano, UNEP pia inafurahia kuunga mkono nchi ya Uganda kuhusiana na mikakati yake ya kitaifa ya kukabiliana na taka na uchafuzi wa plastiki. "

Dkt. Tom Okurut, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira ya Uganda (NEMA), alisisitiza kuhusu gharama ya kuendelea kutumia plastiki kwa maisha ya viumbe wa majini na kwa afya ya binadamu.

"Plastiki zimeziba mabomba ya maji hali inayopelekea matumizi ya mabilioni ya pesa kuyafungua kila mwaka; kiwango ambacho kingewekeza katika huduma zingine muhimu kwenye jamii.

Ikichochewa na hitaji la kushughulikia hatari kama vile kufikiwa na visabaishi vya saratani kutokana na kumeza chembechembe za plastiki , Uganda imeshawishika kushughulikia plastiki kupitia sheria na inatafuta ubia wa kitaifa na kimataifa.

 "Sababu nyingi zimechelewesha utekelezaji wa marufuku ya plastiki nchini Uganda, lakini nina imani kwamba kujiunga na Kampeni ya Bahari Safi kutasaidia sana kukuza imani kati ya Waganda na raia wengine ulimwenguni kutumia njia mbadala zilizo endelevu zaidi," Okurut aliongezea.

Uganda tayari ni moja ya nchi 30 zilizowakilishwa katika shindano Tide Turners Plastic Challenge, mpango wa Kampeni ya Bahari Safi ambayo huelimisha vijana kote ulimwenguni kuhusu taka baharini na uchafuzi wa plastiki, kwa kuwapa maarifa ya kubadilisha mienendo yao binafsi, kuhamasisha jamii zao, na kuunda mustakabali bora kwa sayari.

Katika mwezi wa Machi mwaka wa 2021, Flipflopi, mashua ya kwanza ulimwenguni iliyotengenezwa kwa asilimia 100 kutoka kwa plastiki iliyowahi kutumika, ilijiunga na Kampeni ya Bahari Safi kupitia safari kwa kuzunguka Ziwa Victoria na kusimama nchini Kenya, Uganda na Tanzania. Usafiri huo uliangazia changamoto za ziwa na hitaji la Jumuiya ya Afrika Mashariki kukomesha janga lisilohitajika la kutumia plastiki mara linalotishia eneo hilo.

Kampeni ya Bahari Safi inachangia kufikia malengo ya Ubia wa Kimataifa wa Taka ya Baharini, ushirikiano wa wadau wengi ambao unaleta pamoja wahusika wote wanaofanya kazi kuzuia na kupunguza uchafuzi wa plastiki na wa baharini.

Bahari huwezesha maisha duniani, husaidia kudhibiti hali ya hewa, ni chanzo kikuu cha protini kwa zaidi ya watu bilioni moja na hutoa oksijeni nyingi tunayopumua. Takataka za baharini na uchafuzi wa plastiki ni tishio kwa hali nzuri ya bahari; ni wakati wa kufanya mabadiliko.

 

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu Kampeni ya Bahari Safi

Kampeni ya Bahari Safi, sehemu ya kazi pana ya UNEP ya kukabiliana na takataka za baharini na uchafuzi wa plastiki, inaonyesha kuwa asilimia 80 ya plastiki ambayo hujikuta baharini hutoka kwenye maeneo ya ardhi.  Angalau tani milioni 11 za plastiki hutupwa baharini kila mwaka - kiasi ambacho kinakadiriwa kitaongezeka mara tatu zaidi kufikia mwaka wa 2040 iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa kwa kiwango kikubwa.

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)

UNEP in mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira ulimwenguni.  Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.

Kuhusu Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira ya Uganda

NEMA ni taasisi kuu nchini Uganda, iliyo na madaraka ya kikatiba kuratibu, kufuatilia, kudhibiti na kusimamia maswala yanayohusiana na ushughulikiaji wa mazingira nchini humo. Taasisi hii husimamia ukuzaji wa sera, sheria, kanuni, viwango na miongozo ya mazingira; na vilevile kusaidia Serikali kutekeleza ahadi za kikanda na za kimataifa ikijumuisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), na kadhalika.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:

Keishamaza Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, UNEP, +254-722 677747

Heidi Savelli-Soderberg, Afisa wa Programu,Taka ya Baharini, UNEP