- Kilichoharibika katika mwaka wa 2019: Tani milioni 931 ya chakula kinachouzwa kwa familia, kwa wauzaji, mikahawani na huduma nyinginezo za chakula
- Utafiti unaonyesha kuwa uharibifu wa chakula hutokea kote ulimwenguni, siyo tu katika nchi zinazoendelea
- Ripoti ya Kiwango cha Chakula Kinachoharibiwa husaidia nchi kufuatilia Lengo la Maendeleo Endelevu la 12.3 la UN la kupunguza uharibifu wa chakula kwa nusu kufikia mwaka wa 2030
Nairobi/Paris, Machi 4 2021 – Makadirio ya tani milioni 931 ya chakula, au asilimia 17 ya chakula kilichofikia watumizi katika mwaka wa 2019 kiliharibika, kilitupwa kwenye majaa ya taka majumbani, na wauzaji, mikahawani na watoa huduma nyinginezo za chakula, kwa mjibu wa utafiti mpya wa UN uliofanywa ili kuimarisha juhudi za kimataifa za kupunguza uharibifu wa chakula kwa nusu kufikia mwaka wa 2030
Kiasi hicho ni sawa na malori milioni 23 yaliyojaa pomoni yanayobeba tani 40 — yakijumuishwa, yanaweza kulisha dunia nzima mara saba.
Ripoti ya Kiwango cha Chakula Kinachoharibiwa 2021, kutoka kwa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na washirika wenza WRAP, inaangazia chakula kinachoharibika katika maeneo ya uuzaji, mikahawani na majumbani – ikijumuisha chakula na sehemu zisizolika kama vile mifupa na maganda. Ripoti hiyo inajumuisha ukusanyaji, uchanganuzi wa kina wa data kuhusiana na uhuribifu wa chakula, matumizi ya kisasa na kutoa methodolia ya kupima uharibifu wa chakula kwa nchi. Maeneo 152 ambapo chakula uharibika yalianishwa katika nchi 54.
Ripoti hiyo inagundua kuwa karibu katika kila nchi iliyokadiria uharibifu wa chakula, ilishuhudia kiwango kikubwa cha uharibifu, bila kutegemeakiwango cha mapato. Inaonyesha kuwa kiwango kikubwa cha uharibifu huo hutokea majumbani, ambacho ni asilimia 11 ya chakula chote kinachopatikana kwa matumizi katika mchakato mzima wa usambasaji. Uharibifu kwa huduma za chakula na maeneo ya uuzaji ni asilimia 5 na asilimia 2 mtawalia. Kwa kuzingatia kila mtu, kilo 121 ya chakula katika ngazi ya matumizi huharibika kila mwaka, huku jumla ya kilo 74 ya kiasi hiki ikitokea majumbani. Ripoti hii pia inajumuisha makadirio ya kila mtu binafsi katika ngazi ya eneo na ya kitaifa.
Uharibifu wa chakula una athari kubwa kwa mazingira, kwa jamii, na kwa uchumi. Kwa mfano, wakati ambapo mazingira hayajashughulikiwa kikamilifu, asilimia 8 hadi 10 ya jumla ya uzalishaji wa gesi chafu duniani huhusishwa na chakula ambacho huwa hakitumiki iwapo hasara kabla ya kutumika itazingatiwa.
"Kupunguza uharibifu wa chakula kunaweza kupunguza uzalishaji wa gesi chafu, kupunguza uharibifu wa mazingira kupitia mabadiliko ya matumizi ya ardhi na uchafuzi, kuwezesha utoshelezaji wa chakula na kupunguza baa la njaa na kuokoa fedha wakati wa mdororo wa uchumi ulimwenguni," alisema Inger Andersen, Katibu Mtendaji wa UNEP. "Iwapo tunataka kujikakamua kushughulikia mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira na uharibifu wa bayoanuai, na uchafuzi na taka, mashirika ya biashara, serikali na wananchi kote ulimwenguni ni sharti watekeleze wajibu wao wa kupunguza uharibifu wa chakula. Mkutano Mkuu wa Mifumo ya Chakula wa Umoja wa Mataifa mwaka huu utatoa fursa wa kuchukua hatua mpya dhabiti za kukabiliana na uharibifu wa chakula duniani."
Huku watu milioni 690 wakiwa wameathiriwa na baa la njaa katika mwaka wa 2019, idadi inayotarajiwa kuongozeka mno kutokata COVID-19, na watu bilioni tatuwakishindwa kupata lishe bora, watumizi wa chakula wanahitaji kupunguza uharibifu wa chakula.
Nchi zinaweza kuimarisha ahadi zake za kushughulikia mazingira kwa kujumuisha uharibifu wa chakula kwenye Ahadi Zinazotolewa na Taifa kutokana na Mkataba wa Paris, huku zikiimarisha utoshelezaji wa chakula na kupunguza gharama majumbani. Hii hufanya kuzuia uharibifu wa chakula kuwa nguzo muhimu wakati wa kuweka mikakati ya kujiimarisha baada ya COVID-19.
Changamoto ya Kimataifa
"Kwa kipindi cha mda mrefu, ilichukuliwa kuwa Uharibifu wa chakula nyumbani lilikuwa tatizo kuu tu katika nchi zilizoendelea," alisema Marcus Gover, CEO wa WRAP. "Kutokana na uchapishaji wa Ripoti ya Kiwango cha Chakula Kinachoharibiwa, tunaona kuwa mambo hayako wazi zaidi.
"Tukisalia tu na miaka 9, hatutafikia Lengo la 3 la SDG ya 12 iwapo hatutaimarisha zaidi uwekezaji wa kukabiliana na uharibifu wa chakula majumbani kote ulimwenguni. Kipao mbele kinapaswa kutolewa na serikali, mashirika ya kimataifa, mashirika ya biashara na wakfu za kutoa misaada.
Lengo 12.3 la Malengo ya Maendeleo Endelevu linalenga kupunguza chakula kinachoharibiwa na mtu binafsi duniani kwa nusu katika viwango vya uuzaji na matumizi na kupunguza chakula kinachopotea wakati wa uzalishaji na usambasaji. Mojawapo ya viashiria viwili vinavyolengwa ni Kiwango cha Uharibifu wa Chakula.
Idadi ya nchi zilizokadiria uharibifu wa chakula katika miaka ya hivi karibini inaendelea kuongezeka. Ripoti hii inaonyesha kuwa nchi 14 tayari zimekusanya data ya uharibifu wa chakula majumbani kwa kuzingatia Viwango vya Uharibifu wa Chakula. Kwa kuongezea nchi 38 zina data ya uharibifu wa chakula majumbani ambazo mabadiliko madogo yakifanywa kwenye methodolojia, maeneo ya kijiografia au kwenye kiwango cha sampuli zitaweza kutoa makadirio yanaingiliana na SDG 12.3. Kwa jumla, nchi 54 zilikuwa na data kwa angalau sekta moja kati ya sekta tatu zilizojumuisha katika ripoti hii.
Makadirio mapya ya kiwango cha uharibifu wa chakula yalitokana na data zilizopo na makadirio kwa kuzingatia yalishuhudiwa katika nchi nyinginezo. Huku asilimia 75 ya watu wakiishi katika nchi zilizoshuhudia moja kwa moja uharibifu wa chakula majumbani, uwezekano wa kuamini makadirio hayo katika sekta hii uko juu. Na kiwango kidogo zaidi cha moja kwa moja katika maeneo ya uuzaji yanayotoa huduma za chakula.
Data ya kuonyesha uharibifu wa chakula na sehemu zisizolika inapatikana tu katika nchi zenye kipato cha juu, na na inaaminika kutokea katika kiwango kinacholingana katika ngazi ya majumbani. Sehemu zisizolika ni maarifa muhimu yanayokosekana na inaweza kuwa juu katika nchi zilizo na mapato ya chini.
Kuimarisha kazi ya ripoti hii, UNEP itazindua makundi ya kufanyia kazi kwenye kanda ili kuweza nchi kuimarisha uwezo wake wa kupima uharibifu wa chakula kabla ya kuripoti tena kuhusu SDG 12.3 mwishoni mwa mwaka wa 2022, na kuwasaidia kuweka vigezo vya kimataifa vya kukadiria maendeleo kuelekea maelekeo ya 2030, na kubuni mikakati ya kitaifa ya kuzuia uharibifu wa chakula. Juma hili, WRAP imezindua kwa mara ya kwanza kama taifa Wiki la Kushukhulikia Uharibifu wa Chakula (Machi 1 hadi 7), kupitisha ujumbe kuwa kuharibu kwa chakula kunachangia mabadiliko ya tabianchi.
MAKALA KWA WAHARIRI
Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)
UNEP ni mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira ulimwenguni. UNEP hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.
Kuhusu WRAP
WRAP ni NGO ya kimataifa yenye makao yake makuu nchini Uingereza. Ni mojawapo ya mashirika matano makuu nchini Uingereza yanayotoa msaada wa kushughulikia mazingira yanayoshirikiana na serikali, mashirika ya biashara na watu binafsi kuhakikisha kuwa malighafi duniani inatumika kwa njia endelevu. Shirika lililoanzishwa katika mwaka wa 2000 nchini Uingereza, WRAP sasa hufanya kazi kote ulimwenguni na ni Mshirika wa Global Alliance, washindi wa Tuzo la Royal Foundation’s Earthshot Prize.
Kwa taarifa zaidi tafadhali wasiliana na:
Sophie Loran, Afisa wa Mawasiliano, UNEP, + 33 601377917