- Kaulimbiu ya Siku ya Mazingira Duniani katika mwaka wa 2022, ‘Dunia Moja Tu’, inaangazia kuishi kwa njia endelevu na mazingira.
- Mwaka wa 2022 unaashiria miaka 50 tangu kutokea kwa Kongamano la Stockholm lililopelekea tarehe 5 Juni kuchaguliwa kama Siku ya Mazingira Duniani.
Nairobi, Novemba 18, 2021 – Serikali ya Uswidi itakuwa mwenyeji wa Siku ya Mazingira Duniani katika Mwaka wa 2022 kwa ushirikiano na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP). Mwaka wa 2022 ni maadhimisho ya miaka 50 tangu kutokea kwa Kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira ya Binadamu - Kongamano la 1972 mjini Stockholm ambalo lilipelekea kuanzishwa kwa UNEP na kuchagua Juni 5 kila mwaka kama Siku ya Mazingira Duniani.
Siku ya Mazingira Duniani katika Mwaka wa2022 itaadhimishwa chini ya kaulimbiu Dunia Moja Tu, ikiangazia umuhimu wa kuishi kwa njia endelevu na mazingira kwa kuleta mabadiliko - kupitia kwa sera na maamuzi yetu - ili kudumisha usafi na kutochafua mazingira. Dunia Moja Tu ilikuwa kaulimbiu ya Kongamano la Stockholm la mwaka wa 1972; Miaka 50 baadaye, kaulimbiu hii bado ina mashiko - sayari hii ndiyo makaazi yetu tu, ambayo rasilimali zake zinazoweza kuisha zinapaswa kulindwa na binadamu.
Waziri wa Mazingira na Hali ya Hewa aliye pia Naibu Waziri Mkuu wa Uswidi Per Bolund alisema: "Kwa kujivunia kuwa mwenyeji wa Siku ya Mazingira Duniani katika Mwaka 2022, Uswidi itaangazia maswala nyeti zaidi ya mazingira, kuonyesha miradi ya nchi yetu na juhudi za kimataifa za kushughulikia changamoto za hali ya hewa na za mazingira. Tunatoa wito kwa jamii ya kimataifa kote ulimwenguni kushiriki kwenye mijadala muhimu na kwenye maadhimisho.”
Kulingana na ripoti ya UNEP ya Kufanya Amani na Mazingira iliyotolewa mapema mwaka huu, kubadilisha mifumo ya kijamii na kiuchumi ni sawa na kuboresha uhusiano wetu na mazingira, kuelewa thamani yake na kuzingatia thamani yake kama msingi wa kufanya maamuzi yetu.
"Katika mwaka wa 2022, tunatazamia kuona ulimwengu ukijiimarisha kutokana na madhara mabaya zaidi ya janga la COVID-19. Ila, tunafanya hivyo tukijua kwamba tunaendelea kukabiliwa na changamoto za aina tatu duniani za mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira na uchafuzi.,” alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP. "Tangazo la Uswidi - na kaulimbiu ya Siku ya Mazingira Duniani linaloweka mazingira na watu kama nguzo ya kushughulikia mazingira -ni ukumbusho tosha wa chanzo cha umuhimu wa kutunza mazingira yetu na ni kipengee muhimu kwa juhudi za kimataifa za kujiimarisha bila kuchafua mazingira.”
“Tangu kuwa mwenyeji wa Kongamano hilo mjini Stockholm miongo mitano iliyopita, Uswidi imepiga hatua kuu na uwekezaji mkuu kwenye utunzaji wa mazingira, ikiwa ni pamoja na lengo la mazingira la kudumu ka kuacha kuzalisha gesi ya ukaa kufikia mwaka wa 2045 na kutoizalisha kabisa baada ya hapo," aliongezea. “Inakubalika kama mwenyeji wa Siku ya Mazingira Duniani katika mwaka wa 2022 kutafakari kuhusu ahadi za jadi na uongozi na kutoa ahadi kabambe kwa siku zijazo.”
Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 5 mwezi wa Juni. Ni siku kuu ya Umoja wa Mataifa ya kuhamasisha na kuchukua hatua za kushughulikia mazingira duniani. Kwa miaka mingi, imekuwa jukwaa kubwa zaidi la kimataifa la kuhamasisha umma kuhusu mazingira na huadhimishwa na mamilioni ya watu kote ulimwenguni.
Kwa kuongezea, katika mwaka wa 2022, Serikali ya Uswidi itakuwa mwenyeji wa Stockholm+50, mkutano wa kimataifa wa kuadhimisha miaka 50 ya Kongamano la Stockholm la mwaka wa 1972 na kuimarisha utekelezaji wa Ajenda ya 2030 na kujikwamua na janga la COVID-19 kwa njia endelevu.
Stockholm+50 itatoa fursa kwa jamii ya kimataifa kuimarisha ushirikiano na kuonyesha uongozi unaoleta mabadiliko kuelekea jamii endelevu zaidi, sambamba na azimio lililopitishwa hivi karibuni wakati wa kuadhimishwakwa miaka 75 ya kuwepo kwa Umoja wa Mataifa.
Kongamano la Stockholm la mwaka wa 1972 lilipelekea Azimio la Stockholm kuhusu Mazingira ya Binadamu, ikijumuisha kanuni kadhaa elekezi kuhusu usimamizi wa mazingira duniani. Matokeo mengine ya mkutano huo ni kuanzishwa kwa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na Siku ya Mazingira Duniani.
MAKALA KWA WAHARIRI
Kuhusu Siku ya Mazingira Duniani
Siku ya Mazingira Duniani ni chombo kikuu cha Umoja wa Mataifa cha kuhimiza uhamasishaji kote duniani na kuchukua hatua za kushughulikia mazingira. Siku inayoadhimishwa kila mwaka tangu mwaka wa 1974, pia imekuwa jukwaa muhimu la kukuza maendeleo ya vipengele vya mazingira vya Malengo ya Maendeleo Endelevu. Zikiongozwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), zaidi ya nchi 150 hushiriki kila mwaka. Mashirika makubwa, mashirika yasiyokuwa ya serikali, jamii, serikali na watu mashuhuri kutoka pembe zote za dunia huhamasisha kuhusu mazingira wakati wa Siku ya Mazingira Duniani
Kuhusu Wizara ya Mazingira ya Uswidi
Wizara ya Mazingira ya Uswidi huwajibikia sera ya Serikali ya mazingira na hali ya hewa. Wizara hii hushughulikia masuala ya hali ya hewa, bayoanuai, kemikali, mifumo ya ekolojia, uhifadhi wa mazingira na misitu, mazingira ya bahari na ya majini, usalama dhidi ya mionzi na ushirikiano wa mazingira wa kimataifa.
Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)
UNEP ni mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira ulimwenguni. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.
UNEP@50: Wakati wa kutafakari kuhusu yaliyopita na kupanga kuhusu siku zijazo
Kongamano la Umoja wa Mataifa la mwaka wa 1972 kuhusu Mazingira ya Kibinadamu mjini Stockholm, Uswidi, lilikuwa kongamano la kwanza kabisa la Umoja wa Mataifakutumia neno “mazingira” kwenye anwani yake. Kuundwa kwa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) ni mojawapo ya matokeo makuu ya kongamano hili lilianzisha mambo mengi. UNEP iliundwa kwa urahisi kama kitengo cha Umoja wa Mataifa cha kushughulikia mazingira duniani. Shughuli zitakazoendelezwa katika mwaka wote wa 2022 zitaangazia hatua kuu zilizopigwa na yatakayojiri katikamiongo ijayo.
Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:
Keishamaza Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, UNEP
Josefin Sasse, Katibu wa Vyombo vya Habari wa Per Bolund, Waziri wa Mazingira na Hali ya Hewa, na Naibu Waziri Mkuu, Simu +46 73 0779469