Maoni haya yalionekana kwa mara ya kwanza katika gazeti la The Nation Africa
Kote ulimwenguni, miji, bahari mandhari imejazwa na taka za plastiki, na kuhatarisha afya ya binadamu, kutishia bayoanuai na kudhuru hali ya hewa. Hii ndiyo sababu, wakati wa Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa linatoa wito kwa kila mtu kufanya awezalo kukomesha uchafuzi wa plastiki.
Dunia huzalisha takriban tani za mfumo wa mita milioni 430 za plastiki kwa mwaka na kiwango kinaendelea kuongezeka. Mifumo ya kuchakata haiwezi kukabiliana na kiasi hiki; viwango vya uchakataji ni chini ya asilimia 10. Hatuwezi kuwa na matumaini ya uwezekano wa kuchakata hadi kujinasua na janga hili. Tunahitaji kubuni upya kikamilifu jinsi tunavyotumia, kuzalisha, kuchakata na kutupa plastiki - ubunifu mpya unaoanza na kuondoa plastiki nyingi iwezekanavyo, na kemikali hatari zinazohusiana nazo, kutoka kwa bidhaa na mifuko ya kufungia.
Ubunifu huu ulianza mwaka jana katika Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa mjini Nairobi, wakati ambapo mataifa yalikubali kuanza mazungumzo kuhusu makubaliano ya kisheria yankukomesha uchafuzi wa plastiki. Awamu ya pili ya mazungumzo kuhusu mkataba huu ndiyo imekamilika, na kutoa fursa ya rasimu ya makubaliano ya kutozalisha gesi chafu kujadiliwa katika makao makuu ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa mjini Nairobi baadaye mwakani.
Kenya, na bara zima la Afrika, watakuwa na wajibu muhimu wa kutekeleza katika maafikiano haya - zaidi kwa sababu makubaliano haya yalizaliwa nchini Kenya. Zaidi kwa sababu ni katika mataifa ya Afrika, na nchi nyingine zinazoendelea, kwamba changamoto za kutotendea haki uchafuzi wa plastiki hujitokeza. Hii inaonekana kwa maeneo kama Dandora barani, ambapo wafanyakazi wa kushughulikia taka kwa njia zisizo rasmi huhatarisha afya zao ili kujikimu kimaisha.
Uwepo mkubwa wa Kundi la Wazungumzaji wa Kiafrika katika mchakato wa mazungumzo umeashiria kujitolea kwa Afrika kukomesha uchafuzi wa plastiki. Mataifa ya Kiafrika yanaweza kuendesha mkondo wa makubaliano, kumaanisha kuelekeza mawazo ya kila mtu katika ubunifu mpya. Kuunda upya bidhaa ili kutumia plastiki kidogo - hasa plastiki isiyohitajika na inayodhuru. Kubuni upya jinsi ya kufunga bidhaa ili kutumia plastiki kidogo. Kuunda upya mifumo na bidhaa ili ziweze kutumika tena, kujazwa tena na kuchakatwa - ili, kwa mfano, polima iliyochakatwa iwe ithamaniwe zaidi kuliko polima ambayo haijawahi kutumika. Kuunda upya mfumo mpana wa haki - ili vikundi kama vile wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi ya kushughulikia taka wapate kazi za heshima na mazingira safi.
Lengo ni kuboresha viwango vya chini vya ukusanyaji wa taka barani Afrika. Inamaanisha kuwekeza katika uchakataji na miundomsingi ya kushughulikia taka ili kushughulikia plastiki ambazo haziwezi kuonddolew wala kutumika tena. Lengo ni kushughulikia mazoea ya uchafuzi wa plastiki katika bahari zetu unaoendelea kutua kwenye fukwe za nchi za Afrika. Lengo linapaswa pia kumaanisha ushirikiano, ili nchi zinazoendelea ziwe na rasilimali muhimu za kifedha.
Mataifa ya Kiafrika pia yanaweza kuendeleza lengo lake kwa kubadilishana ujuzi wao. Mamilioni ya Waafrika tayari wanafanya mambo mengi wanayopaswa kufanya katika maisha yao ya kila siku. Watu kutumia tena and kukarabati bidhaa – mtindo wa maisha na utamaduni ambao ni muhimu kwengineko, ambapo mfumo wa “kuchukua-kutengeneza-kutumia-kutupa” hudhihirika zaidi. Kote barani Afrika, tunashuhudia miradi ya ubunifu: kama vile nchini Rwanda, ambapo serikali imesaidia viwanda vya ndani ya nchi kuanza kuzalisha bidhaa kutoka kwa mianzi na makaratasi baada ya kupiga marufuku mifuko ya plastiki inayotumika mara moja
Hizi ni aina za miradi ambayo itaruhusu mataifa ya Kiafrika kugeukia mustakabali usio na plastiki - kuanzisha ubunifu wa masuluhisho ya kuzalisha na kufunga bidhaa kama vile Kenya ilivyoanzisha kutuma na kupokea pesa kupitia simu. Serikali za Kiafrika zinaweza kuleta mabadiliko yanayohitajika, ndani ya nchi na katika ngazi ya kimataifa, kwa kuzungumzia hali hii - na kuhakikisha kuwa sheria zinakuza miundo mipya ya biashara badala ya kurudi nyuma kwa kuzalisha plastiki inayotumika mara moja. Utekelezaji pia ni muhimu, na ni vyema kuona Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira ya Kenya ikichukua hatua dhidi ya plastiki inayotumika mara moja.
Siku ya Mazingira Duniani ya mwaka huu ni wakati kwa Kenya, Afrika na dunia nzima kujianda na kujitolea kuchukua hatua thabiti zaidi. Serikali lazima zifanye maafikiano thabiti ya kukomesha uchafuzi wa plastiki. Viwanda na sekta ya kibinafsi lazima zibuni ili kuepukana na mifumo ya biashara iliyo na plastiki. Wateja wanaweza kupunguza mahitaji ya plastiki kwa kukataa plastiki inapowezekana. Juhudi zaiazoongozwa na jamii ziinaweza kuweka shinikizo kwa kutumia sauti zao kupiga kelele inayostahili.
Kuchukua hatua za kukomesha uchafuzi wa plastiki ni fursa kubwa. Tukichukua hatua kwa ushirikiano, tunaweza kukomesha uchafuzi wa plastiki kufikia mwaka wa 2040; kupunguza gharama kwa jamii, mazingira na afya ya binadamu; kubuni maelfu ya nafasi mpya za ajira, hasa katika nchi zinazoendelea; na kufungua masoko mapya na fursa za biashara.
Kila mtu atashinda, mradi tutahakikisha mabadiliko ya haki kwa nchi zinazoendelea na mavikundi kama vile wafanyikazi katika sekta isiyo rasmi ya taka. Wakati wa Siku ya Mazingira Duniani, natoa wito kwa kila mtu kujiunga na vuguvugu la kimataifa na kukomesha uchafuzi wa plastiki mara moja.
Inger Andersen ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)