Waheshimiwa Mawaziri, Wajumbe, wafanyakazi wenzangu na marafiki,
Itifaki zote zimezingatiwa. Pokeeni salamu zangu!
Kwa takribani miaka 40, Kongamano la Mawaziri wa Afrika kuhusu Mazingira limetumika kama kurunzi ya kuelekeza wakati wa nyakati hatari kwa mazingira.
Limesaidia bara lenye uanuai kufikia maafikiano kuhusu vitisho vikuu zaidi kwa sayari yetu - na kuwezesha Afrika kusikika zaidi katika jukwaa la kimataifa.
Suala hili halijawahi kuwa na umuhimu zaidi kuliko ilivyo sasa.
Watu bilioni 1.4 barani Afrika wana uwezekano wa kukabiliwa maafa ya mazingira kupitia majanga ya aina tatu kwa sayari ya mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira na wa bayoanuai, na uchafuzi na taka.
Marafiki zangu, ili kukabiliana na majanga haya hatuhitaji chochote isipokuwa mbinu mpya wa kiuchumi barani Afrika...
… mbinu ambayo itasaidia ukuaji huku ikitunza bayoanuai…
…. mbinu ambayo itakomesha uchafuzi wa mazingira huku ikiwaheshimu walio hatarini zaidi…
… mbinu ambayo itabuni nafasi za kazi huku ikizuia uzalishaji wa gesi ya ukaa na kusaidia watu wa bara la Afrika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Swali kuu tunalojiuliza ni hili: katika wakati wa uhaba wa chakula, wa mfumuko wa bei, wa madhila kwa uchumi, tunawezaje kukuza mustakabali endelevu zaidi?
Nitajaribu kujibu swali hili.
Hebu tushughulikie kwanza kile ambacho bila shaka ni tishio kubwa kwa bara hili: mabadiliko ya tabianchi.
Afrika iko hatarini zaidi kuathiriwa na janga la mabadiliko ya tabianchi.
Kiwango cha joto hapa kinapanda kwa kasi zaidi kuliko wastani wa kimataifa.
Viwango vya bahari vinaongezeka kwa kasi zaidi.
Na bara hili limekumbwa na majanga, kuanzia kwa ukame wa miaka mitatu katika Pembe ya Afrika, hadi kwa Kimbunga Freddy, mojawapo ya dhoruba zenye nguvu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kusini mwa ikweta.
Licha ya hayo yote, Afrika ina sehemu ndogo tu ya fedha inazohitaji kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Na katika miaka ijayo, mabadiliko ya tabianchi yataendelea tu kuongezeka. Kufikia mwaka wa 2030, Afrika itahitaji takribani dola za Marekani trilioni 3 za kufadhili mazingira.
Ili kupata mitaji ya aina hii, nchi zitahitaji kuvutia ufadhili zaidi kutoka kwa sekta ya kibinafsi ndani ya nchi kufadhili miradi inayohusiana na mazingira.
Kwa sasa, ni asilimia 14 tu ya ufadhili wa miradi ya mazingira barani Afrika hutoka kwa mashirika binafsi ya biashara. Zaidi ya asilimia 80 hutoka kwa vyanzo vya umma vya kimataifa.
Ili kuvutia mitaji zaidi kutoka sekta binafsi, nchi zitahitaji kuboresha mifumo yake ya uwekezaji, na kurahisisha kuzunguka kwa pesa ndani ya uchumi wao.
Pia zitahitaji kuunganisha malengo yake ya mazingira kwenye mipango ya kitaifa ya uwekezaji na kuelezea wawekezaji fursa nyingi zitakazokuwepo kutokana na mabadiliko ya kutochafua mazingira.
Hatimaye, nchi ni sharti zitafute njia za kuzuia hatari za mradi na kukuza ushirikiano na sekta ya kibinafsi, ambayo mara nyingi huwa na mtaji na wataalamu wa kufanikisha miundomsingi ya miradi.
Wakati uo huo, msamaha wa deni la kimataifa ni muhimu.
Si vyema kabisa kwa Afrika, ambayo imechangia kidogo mno kwa mabadiliko tabianchi, kuteseka zaidi.
Jamii ya kimataifa ina wajibu wa kupunguzia Afrika mzigo wa deni, ambao ni muhimu kuwezesha bara hili kufadhili mabadiliko yatakayopelekea mustakabali unaostahimili mabadiliko ya tabianchi.
Wajumbe mashuhuri, huku Afrika inapokabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hatuwezi kusahau kuhusu umuhimu wa kutunza bayoanuai.
Utajiri wa asili katika bara hili, ambao unasaidia moja kwa moja zaidi ya asilimia 60 ya watu wa Afrika, inatishiwa na mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa mazingira, ujangili, utumiaji kupindukia na ubadilishaji wa makazi.
Nilifurahi kuona nchi za Kiafrika zilipotangaza mwaka jana, wakati wa CBD COP15 mjini Montreal, kwamba bayoanuai ni msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Ulikuwa ujumbe ambao sisi, katika Umoja wa Mataifa, tuliusikia kwa sauti kubwa na kwa uwazi.
Katika Mkutano wa Kilele wa Malengo ya Maendeleo Endelevu mwezi ujao, UNEP na mashirika mengine manane ya Umoja wa Mataifa yataonyesha jinsi ambavyo asili inaweza kuwa kichocheo cha mabadiliko ya kiuchumi na ustawi.
Pia tuko tayari kutoa usaidizi kutegemea nchi ili kusaidia nchi za Kiafrika zinazotaka kukuza uchumi unaojali bayoanuai.
Wizara zenu nyingi zimeanza mchakato wa upitiaji mpya ulio muhimu sana ili kufikia malengo ya Mfumo wa Bayoanuai wa Kimataifa wa Montreal-Kunming.
Mnaposonga mbele, naomba muwasiliane na wenzenu katika wizara nyinginezo na kuona jinsi ambavyo bayoanuai inaweza kuingizwa katika programu na sera za kitaifa.
Ili kuweza kufanikisha ulindaji wa urithi wa kiasili wa Afrika, ni sharti tutumie mbinu inayojumuisha serikali nzima.
Ni lazima pia tufanye kazi ya kuboresha mandhari yaliyoharibiwa, hasa yale ambayo yamekumbwa na jangwa. Sisi sote tunafuhamu kuwa, uchumi wa Afrika unategemea malighafi zake, hasa, kilimo, mifugo na madini. Kwa maneno mengine, utajiri wa Afrika uko kwenye ardhi, maji na mifumo thabiti ya ekolojia.
Katika kipindi cha miaka 70 iliopita, Afrika imepoteza theluthi mbili ya aridhi yake yenye rutuba huku wakazi wake wakiongezeka mara sita zaidi.
Ukame na uharibifu wa ardhi tayari unagharimu maisha, kuharibu uchumi na kuyumbisha amani na usalama wa nchi.
Habari njema ni kwamba bado kuna wakati wa kupunguza majangwa na kurudi kutumia ardhi kwa njia nzuri.
Msiangalie mbali ila kwa Ukuta Mkuu wa Kijani, ambao unaendelea kupata umaarufu kwa kasi katika bara zima.
Tunahitaji masimulizi zaidi kuhusu mafanikio kama haya kwa sababu uboreshaji husaidia kutunza bayoanuai, kuhifadhi maji, kupambana na umaskini na kupunguza mabadiliko ya tabianchi.
Tunapoboresha ardhi, lazima pia tufanye kazi kupunguza uharibifu unaofanywa na uchimbaji wa madini muhimu na kuanza kutumia nishati isiyochafua mazingira.
Mara nyingi sana kuchimba madini haya - ambayo ni pamoja na lithiamu, nikeli na cobalt - inamaanisha kuondoa misitu na kuharibu mandhari nyeti.
Vitendo hivi hatimaye ni vya kutuangamiza.
Waheshimiwa wajumbe, ningependa kuzungumza kwa ufupi sasa kuhusu tatizo linaloongezeka ambalo ni uchafuzi wa plastiki.
Binadamu hutengeneza zaidi ya tani milioni 430 za plastiki kila mwaka, theluthi mbili ni vitu visivyodumu ambavyo hufanywa taka baada ya muda mchache.
Ukweli ni kwamba Afrika lazima itafute njia ya kuanza kujikomboa dhidi ya plastiki.
Inaziba mito barani.
Inachafua hewa barani.
Na inajikuta kwenye mifumo ya chakula cha binadamu.
Katika mwezi wa Novemba, mataifa yatakusanyika mjini Nairobi kwa kikao cha tatu cha Kamati ya Majadiliano ya Kimataifa, ambayo inaunda chombo cha kisheria cha kimataifa kuhusu uchafuzi wa plastiki.
Ninawahimiza viongozi wa Afrika kujieleza wakati wa mazungumzo hayo. Toeni maoni yenu - na muhimu zaidi shiriki ubunifu wenu.
Kwa sababu katika sehemu nyingi za bara hili, serikali na mashirika ya biashara wanaanzisha njia mpya za kupunguza athari za plastiki kwa mazingira huku wakibuni nafasi za kazi na kukuza uendelevu.
Wajumbe waheshimiwa, tutakuwa na kalenda ya mazingira iliyojaa shughuli mbele yetu katika miezi michache ijayo.
Kwenye agenda ni Mkutano wa Kilele wa Tabianchi wa Afrika, Kongamano la Kimataifa kuhusu Ushughulikiaji wa Kemikali, Kamati ya Majadiliano ya Serikali Mbalimbali na Kongamano la Umoja wa Mataifa la Mabadiliko ya Tabianchi.
Ninaomba serikali za Afrika kushiriki kikamilifu kwenye mikusanyiko hii. Ni sauti yenu ambayo ulimwengu unahitaji kusikia. Na kwa Mkutano ujao wa Kilele wa Tabianchi wa Afrika utakaoandaliwa na kuongozwa na Afrika ni fursa ya kuwa na ujasiri na kuidhinisha matokeo yake ili kushawishi na kuingia katika mazungumzo ya kimataifa yatakayofuata mwakani.
Huo ni uhalisia wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa - UNEA - litakalofanyika mjini Nairobi mwishoni mwa Februari mwaka ujao.
Ni mwezi jana tu ambapo ofisi za pamoja za UNEA na Kamati ya Wawakilishi wa Kudumu ziliidhinisha ajenda ya UNEA na kuanza kuzingatia stakabadhi ya matokeo, inayojulikana kama, azimio la mawaziri.
Ili kufaulu kikamilifu katika maandalizi ya UNEA ambayo ni hatua muhimu kwa mazingira, ni muhimu kutambua tarehe 18 Desemba imetengwa kama tarehe ya mwisho ya kuwasilisha rasimu ya maazimio. Uwasilishaji wake wa mapema utawapa wajumbe wote muda wa kutosha kujiandaa kabla ya kuwasilishwa na kuwa tayari kwa majadiliano.
Hatimaye, kabla sijahitimisha, ningependa kusisitiza kujitolea kwa UNEP kusaidia bara la Afrika kukabiliana na changamoto za aina tatu duniani.
Tuko hapa kuunga mkono maono yenu ya mutakabali endelevu zaidi, wenye ustawi zaidi ambapo uwezo wa Afrika utatumika wote.
Asante na kila la kheri na mafanikio katika mijadala yenu.