Shelton Nyakundi, mwanafunzi wa umri wa miaka 18 katika shule ya bweni ya Menengai mjini Nakuru, Kenya, anaamini jambo moja rahisi linaweza kupelekea kufaulu na kutofaulu shuleni kwa wanafunzi wengi: mwangaza.
Nyakundi anasema ili kuokoa pesa, shule yake huzima taa zake zisizo za kutegemewa saa nne usiku na kuwanyima wanafunzi muda muhimu wa kusoma. "Kwa sasa, ukosefu wa mwanga ni kizingiti, nyakati za jioni na asubuhi," anasema Nyakundi, ambaye anataka kufanya kazi kama mhudumu wa afya atakapohitimu.
Kituo cha Tabianchi cha Copenhagen cha Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) kinafadhili mradi wa majaribio unaolenga kumulikia Nyakundi na wanafunzi wenzake mustakabali wao. Jitihada hizi zinaweka kwa shule 100 za bweni nchini Kenya taa za bei nafuu, zinazotumia nishati vizuri au taa za LED, hali itakayowezesha wasimamizi wa shule kuhifadhi pesa na kuwasha taa kwa muda mrefu.
Mradi huu unafanywa kwa ushirikiano na Nishati Endelevu kwa Wote, mpango unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa, na Wizara ya Elimu nchini Kenya. Ni sehemu ya juhudi kubwa zaidi za Kenya za kuboresha matumizi ya nishati, ambayo ni sehemu muhimu ya mipango ya nchi hii ya kupanua upatikanaji wa nishati jadidifu kwa bei nafuu.
"Kutumia nishati vizuri ni mojawapo ya njia za haraka zaidi na za gharama nafuu za kuboresha viwango vya maisha na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kote duniani na haihitaji mabadiliko makuu kwa mifumo iliyopo ya nishati," anasema John Christensen, Mkurugenzi wa Kituo cha Tabianchi cha Copenhagen cha UNEP.
Data kutoka kwa Shirika la Kimataifa la Nishati zinaonyesha kuwa matumizi mazuri ya nishati kote duniani yanaweza kupelekea asilimia 40 ya upunguzaji wa uzalishaji wa hewa chafu unaohitajika ili kufikia malengo ya Mkataba wa Paris kuhusiana na mabadiliko ya tabianchi, ambayo yanalenga kudhibiti ongezeko la joto duniani lisizidi nyuzijoto 2 kuliko viwango vya kabla ya viwanda. Katika COP28 Dubai mwaka jana, serikali ziliahidi kuongeza maradufu kiwango cha wastani cha kimataifa cha kila mwaka cha uboreshaji wa matumizi ya nishati kila mwaka hadi mwaka wa 2030. Ripoti ya Pengo la Uzalishaji wa hewa chafu ya mwaka wa 2024 ya UNEP pia iliangazia umuhimu wa nchi kuelezea katika Michango yao Inayoamuliwa na Taifa jinsi zinavyopanga kufikia matumizi haya mazuri ya nishati.
Kukumbatia matumizi mazuri ya nishati – na hasa taa za LED – kunaweza kunufaisha zaidi nchi zinazotatizika kuweka umeme kwa shule zao. Kote duniani, asilimia 25 ya shule za msingi na takriban asilimia 15 ya shule za sekondari hazina umeme, hali inayoathiri watoto milioni 186, unasema Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto (UNICEF). Hata katika shule zilizo na umeme, mwanga usioweza kutegemewa unamaanisha wengi wanatatizika kumudu kulipia umeme, na hivyo kusababisha kukatwa.
Kuwasha taa kunawajibikia takriban nusu ya matumizi ya umeme shuleni nchini Kenya, kwa mjibu wa uchanganuzi uliofanywa na Kituo cha Tabianchi cha Copenhagen cha UNEP. Sanasana inatokana na utegemezi wa balbu za inkandesenti, ambazo zina filament ambazo zinapopashwa moto huwaka, na taa za fluoresenti, ambazo hutoa gesi kutokana na migongano ya atomiki. Michakato yote miwili ina mapungufu ikilinganishwa na taa za LED, ambazo hupitisha umeme kupitia mikrochipu, inayowasha vyanzo vidogo vya mwanga.
Shuleni nchini Kenya, LEDs zinaokoa rasilimali ambazo zinaweza kuwekezwa tena katika mahitaji mengine, kama vile vitabu vya shule, vifaa vya michezo na kutoa mafunzo kwa walimu.
Mkuu wa Shule ya Upili ya Menegai, John Ngunyi, alisema kuwa kuanza kutumia LEDs, iliyoanza Septemba, kutanufaisha zaidi ya wanafunzi 2500.
"Mfumo wa LED utaongeza muda ambao wanafunzi wanakuwa nao wa kusoma na muda ambao wanaweza kuwasha taa," anasema.
Balbu hizi za LED hutolewa na Wakfu wa Signify, kitengo cha hisani cha shirika la Signify, mtengenezaji wa taa duniani. Eric Otenio, Meneja wa Programu wa Signify wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, anaeleza kuwa balbu za LED ni bora zaidi kwa macho ya wanafunzi. "Hazizimizimi zikijiwashawasha sana na kwa hivyo kupunguza kuumwa na macho na maumivu ya kichwa," anasema. Pia anaonyesha kuwa balbu za LED zinahitaji kubadilishwa kwa nadra kuliko balbu za fluoresenti, na hivyo kupunguza uharibifu.
Kama mkuu wa shule Ngunyi anavyosema, si wanafunzi pekee watakaounufaika na mfumo mpya wa taa: “[Zamani] tulidhibiti matumizi ya taa kwa wapishi na walinzi, tukiwaamuru wasiwashe taa hadi muda fulani.” Mara tu taa mpya za LED zitakapowekwa, Ngunyi anasema hatakuwa na wasiwasi kuhusu bili ya umeme wa shule ya mwisho wa mwezi.
Mradi wa majaribio ya taa za LED utakamilika mwishoni mwa mwaka wa 2024 na utapelekea taa zaidi ya 10,000 za fluoresenti ya jadi kubadilishwa. Hiyo inatarajiwa kusababisha akiba ya dola za Marekani ya zaidi ya 213,000 kwa mwaka katika shule zote 100, punguzo la asilimia 27 ya bili zao za sasa za umeme. Itaokoa nishati sawa na kutolewa kwa kilogram 460,000 za kaboni dioksidi kila mwaka.
"Huu ni ushindi mkuu kwa shule," anasema Christensen. "Na inaonyesha athari kubwa ambayo kitu rahisi kutekelezeka kinaweza kuwa nayo katika maisha ya wanafunzi."
UNEP iko mstari mbele kuunga mkono lengo la Mkataba wa Paris la kudhibiti kiwango cha joto duniani kisizidi nyuzijoto 2, na kulenga nyuzijoto 1.5, ikilinganishwa na viwango vya kabla ya viwanda. Ili kufikia lengo hili, UNEP imeunda Masuluhisho ya Kisekta, mwongozo wa kupunguza uzalishaji wa hewa chafu katika sekta mbalimbalikwa kuzingatia ahadi katika Mkataba wa Paris ili kuwezesha kuwa na mazingira thabiti. Sekta sita zilizoainishwa ni: nishati; viwanda; kilimo na chakula; misitu na matumizi ya ardhi; uchukuzi; na ujenzi na miji.
Msururu wa Juhudi za UNEP za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi
Kote ulimwenguni, jamii, watu binafsi na wajasiriamali wanaimarisha hatua bunifu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Pitia awamu mpya ya Msururu wa Juhudi za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi za UNEP, inayoangazia visa vya viongozi wanaoendeleza masuluhisho makubwa, jumuishi na endelevu kwa mabadiliko ya tabianchi yanayopelekea maendeleo endelevu.