Jua linapotua eneo la kati nchini Zambia, miale ya rangi ya machungwa inaakisi kwenye Kinamasi cha Lukanga, eneo kubwa la ardhi oevu lililo na upana wa kilomita mraba 2,600.
Njia yenye maji mengi hupita kwenye mianzi ya kinamasi na yungiyungi za maji ya zambarau, ambayo hutumiwa na mitumbwi kila siku, huku ikivusha wavuvi kwenda na kurudi kwenye kambi zao zinazoelea. Miongoni mwao ni John Chisela, mmoja wa zaidi ya watu milioni 6 wanaotegemea maeneo oevu - na misitu inayoyazunguka - kupata chakula, kuni na mapato.
Lakini kwa wengi hapa, maisha yanaendelea kuwa hatari zaidi
"Samaki wanaovuliwa wanaendelea kupungua," anasema Chisela, ambaye anapata dola 60 za Marekani kutokana na kuvua kilo 50 ya samaki, fedha zinazotosha tu kukidhi mahitaji ya familia yake. "Ila hakuna kazi zingine katika eneo hili."
Kinamasi cha Lukanga kinashambuliwa. Katika maeneo oevu, ambayo ni makazi ya viumbe wengi walio hatarini kuangamia, mabadiliko ya tabianchi yanapelekea mawimbi ya joto na hali mbaya ya hewa, kama vile mafuriko na ukame. Baadhi ya sehemu za kinamasi kinachosalia na unyevunyevu mwaka mzima zinazidi kukumbwa na mafuriko, huku maeneo kame yakizidi kukauka.
Katika Shule ya Msingi ya Mukubwe, Mwalimu Mkuu Mwamba Achilleus Bwalya anaeleza kuwa kwa kuwa na pampu moja tu katika mji mzima ya kusambazia maji kwa wanafunzi 800 na nyumba 300, ukame huathiri uendaji shuleni huku familia zikihangaika kulisha watoto wao.
"Moyo wangu husononeka ninapoona watoto wakizunguka tu na hawaji shuleni," anasema Bwalya.
Wakati uo huo, uvuvi wa kupita kiasi katika maeneo oevu na ukataji miti katika misitu inayozunguka maeneo hayo ni hali inayoendelea kupunguza kwa kasi malighafi ya eneo hilo na kusababisha uharibifu wa udongo. Kote ulimwenguni, maeneo oevu ndio mfumo wa ekolojia unaokabiliwa na vitisho zaidi, unaotoweka kote ulimwenguni kwa viwango vinavyotisha – mara tatu zaidi kuliko misitu. Kufikia mwaka wa 2000, baadhi ya asilimia 85 ya maeneo oevu yaliyokuwepo katika mwaka 1700 yalikuwa yamepotea, huku kuanzisha shughuli za kilimo ikiwa miongoni mwa vitishio vikuu vinavyoendelea kukabili mfumo huu wa ekolojia.
"Licha ya umuhimu wake, mifumo ya ekolojia ya maeneo oevu na misitu nchini Zambia kwa sasa inakabiliwa na ukataji miti kwa kiasi kikubwa na uharibifu," alisema Jean Kapata, Waziri wa Ardhi na Maliasili, katika hafla iliyoandaliwa na serikali Aprili 2021.
Kurejesha Ustahimilifu
Ili kusaidia kubadilisha hali hiyo, serikali ya Zambia inatekeleza mradi mpya wa miaka minne ili kusaidia jamii karibu na maeneo oevu ya Lukanga na Bangweulu kwenye mkoa wa Kati na Luapula nchini humo.
Kwa kuzingatia mkabala unaozidi kuthaminiwa wa kujenga ustahimilifu dhidi ya tabianchi, unaojulikana kama uboreshaji kutegemea mfumo wa ekolojia, mradi huo unarejesha mifumo ya ekolojia ya maeneo oevu na ya misitu ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwa jamii.
Maeneo oevu na misitu hupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kunyonya maji ya mvua kupita kiasi ardhini wakati wa mafuriko na kuwa vyanzo vya maji wakati wa ukame. Kadiri mfumo wa ekolojia unavyotoweka, vivyo hivyo vidhibiti hivi muhimu vya hali ya hewa hutoweka, na hivyo jamii hukumbwa mara kwa mara na vipindi vya mafuriko na ukame.
Mradi wa Zambia unafadhiliwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na kupokea ufadhili wa dola milioni 6 za Marekani kutoka kwa Global Environment Facility, mfadhili mkuu wa miradi ya mabadiliko ya tabianchi.
Uboreshaji wa mifumo ya ekolojia utajumuisha mbinu inayojulikana kama 'kusaidiwa kujiboresha kiasili', njia ya gharama ya chini ambayo inalenga kukabiliana na vitendo vinavyoharibu maliasili, kama vile mioto misituni, kulisha mifugo kupindukia na kukata miti ili kupata mbao, na kujumuisha shughuli za kuzalisha mapato zisizoharibu maliasili. kama vile ufugaji wa samaki kutokana na maji yanayokusanywa wakati wa mafuriko.
Mradi huu pia utabainisha mikakati ya kuondoa magugu ya Kariba, spishi vamizi ambayo huziba njia za maji na kudhuru spishi za samaki. Kwa kuzingatia ari ya masuluhisho yanayotokana na mazingira, mradi huu unafikiria kujumuisha mbinu iliyofanyiwa majaribio ya kutumia wadudu walao nafaka, wanyama wanaokula magugu ya Kariba.
“Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia ulizinduliwa mwaka jana kwa kutambua manufaa mengi ambayo kuboresha mazingira huletea jamii," alisema Jessica Troni, Mkuu wa Kitengo cha Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi cha UNEP. "Hii ni pamoja na uwezo wa mazingira kututunza na kutukinga dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, na maeneo oevu nchini Zambia ni mfano mzuri wa hali hii kupitia vitendo."
Kupitia mtaji wa kuanzia na msaada wa kiufundi, mradi huu utafanya kazi na jamii, kama zile zilizo karibu na Shule ya Msingi ya Mukubwe, kupanda mazao yanayostahimili hali ya hewa ili kustahimili ukame vyema, lakini pia kuweka mifumo ya kukusanya maji ya mvua wakati wa misimu ya mvua.
Kukabiliana na Hali Mbaya Inayojirudiarudia
Mwanafunzi Clement Katemba anasema kuwa jamii yake inaendelea kutafuta njia mbadala za kujikimu zisizodhuru maeneo oevu na misitu - jambo ambalo mradi huu utalishughulikia moja kwa moja. Lakini uzalishaji wa makaa, unaohusisha ukataji wa miti inayozunguka eneo oevu, unaonekana kama njia ya pekee ya kujipatia mapato siku baada ya siku.
"Tunakata miti kupata makaa kwa sababu hiyo ndiyo njia ya pekee tunayoweza kutumia kukimu mahitaji ya familia zetu. Wakati wa kiangazi, sisi hulazimika kufanya chochote ili kuwa na maisha bora, ili kuhakikisha kuwa mahitaji ya wazazi yanatimizwa. Lakini msitu ni muhimu kwetu - hatutaki kuuharibu,” anasema Katemba.
Mbewe, Msimamizi wa mradi huu, anasema wanajamii watasaidiwa na mradi huu ili kuwa na njia mbadala za kujikimu, ikijumuisha ufugaji wa nyuki, ambao unapunguza shinikizo la uvuvi.
"Hatua ya kwanza itakuwa kufanya tathmini ya madhara ya tabianchi ili kuonyesha eneo oevu na kujua ni hatua gani zinahitajika kwa haraka na ni wapi zinapohitajika," alisema Mbewe. "Kisha tunaweza kusaidia jamii kukuza mbinu endelevu zaidi za kuzalisha mapato, ili kuchoma makaa, uvuvi wa kupita kiasi na ukataji miti zisiwe njia pekee za kutegemewa.
Changamoto ya kimataifa
Licha ya uwezo wa kusaidia kukabiliana na hali ya hewa kama makazi kwa wanyamapori, kuchuja uchafuzi wa mazingira na kufanya kazi kama hifadhi muhimu za kaboni, maeneo oevu hukabiliwa na vitisho vinavyoongezeka kote ulimwenguni kutokana na kupanda kwa usawa wa bahari, uchujukaji wa matumbawe na mabadiliko ya hali ya hewa yanayotokea kwa kasi.
Chini ya Lengo la 6 la Maendeleo Endelevu, nchi zote zimejitolea kutunza na kuboresha maeneo oevu kufikia mwaka wa 2030. UNEP ina jukumu maalum la kusaidia kufuatilia na kufikia lengo hili, na kwa kuchukua hatua ya kuboresha mifumo ya ekolojia iliyoongeza kuharibiwa kwa kasi wakati wa Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia.
Ili kuunga mkono masuluhisho yanayotokana na mazingira kote ulimwenguni kukabiliana na tabianchi, UNEP na Muungano wa Kimataifa wa Kuhifadhi Mazingira (IUCN) wanasimamia kwa pamoja Mfuko wa Global EbA Fund, kwa sasa wanatoa angalau yuro milioni 30 kwa mtaji wa kuanzia kufadhili mbinu bunifu.
Kwa habari zaidi kuhusu mradi huu, kwa jina rasmi la Kujengea Ustahimilivu Jamii nchini Zambia kupitia Matumizi ya Mbinu Inayotegemea Mifumo ya Ekolojia katika Mifumo iliyopewa Kipaumbele, tafadhali wasiliana naJessica.Troni@un.org. Jiifahamishe zaidi kuhusu kazi yetu inayoungwa mkono na GEF katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hapa.