Picha na Unsplash/Ma Ti
11 Jan 2022 Hotuba Youth, education & environment

Vijana wafafanua mustakabali

Mheshimiwa Abdel Fattah Al-Sisi, Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri  

Mheshimiwa Mostafa Kamal Madbouly, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri 

Mheshimiwa Sameh Shoukry, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, 

Mawaziri, mabalozi, mabibi na mabwana

Natoa shukrani zangu za dhati kwa kualikwa kuzungumza nanyi kwenye Jukwaa la Vijana Duniani.

Tunaanza mwaka, kama tufanyavyo mara nyingi wakati kalenda inapobadilika, kwa kuangalia yajayo. Kuangalia jinsi tunavyoweza kujiboresha zaidi. Jinsi tunavyoweza kujiimarisha. Kukuza mustakabali bora kwa manufaa yetu na kwa manufaa ya wale tunaowapenda. Mwaka huu, ni muhimu zaidi kwamba tuendelee kuwa na maono chanya na kutafuta masuluhisho mapya kwa changamoto zinazokabili sayari yetu na watu. 

Tulikuwa na matarajio mengi kwa mkutano wa Mazingira wa COP26 mjini Glasgow. Tulipata sehemu ya tulichokuwa tukitafuta. Ahadi zilitolewa kuhusu kupunguza matumizi ya makaa ya mawe na kukomesha ruzuku kwa mafuta ya visukuku. Fedha zaidi za kukukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Msaada kwa nchi zilizo hatarini ambazo zimeathiriwa na mabadiliko ya tabianchi. Kukomesha ukataji miti. Kupunguza uzalishaji wa methani.

Lakini tukizingatia ahadi zote, bado dunia inatarajiwa kushuhudia ongezeko la joto la zaidi ya nyuzijoto 2. Hii itamaanisha madhara zaidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi kuliko tunayoshuhudia. Dhoruba. Mafuriko. Mioto misituni. Kupoteza makao. Madhara kwa afya ya binadamu, kwa uchumi na kwa mashirika ya biashara. Itamaanisha kuwa maonyo yaliyotolewa kwenye ripoti ya hivi karibuni ya Jopo la Kimataifa kuhusu Mabadiliko ta Yabianchi yatatimia.

Ili kuepuka mustakabali huu mbaya, ni sharti dunia ipunguze karibu nusu ya uzalishaji wa gesi chafu katika kipindi cha miaka minane ijayo. Haya ndiyo tunahitaji ili kuwewesha kudhibiti ongezeko la joto lisizidi nyuzijoto 1.5. Na hatupaswi kusahau kwamba janga la mabadiliko ya tabianchi ni sehemu moja tu ya majanga matatu duniani yanayoingiliana yayojumuisha uharibifu wa mazingira, uharibifu wa bayoanuai, na uchafuzi na taka. Tunapaswa kubadilisha mifumo yetu yote iwe isiyochafua mazingira, endelevu na inayojali sayari. 

Wandani wangu, bado tunaweza kubadilika.

Bado tunaweza - kwa kujitolea, kuhamasisha, kutumia nguvu zetu kama vijana walio mstari mbele - kujenga mustakabali usiochafua mazingira ulio na mafanikio zaidi. Sasa, nasema vijana walio mstari mbele wasiruhusu vizazi vingine kutowajibika. Ninasema vijana wahimize vijana wanaoendelea kuzungumza kwa ujasiri kote duniani, waendelee kufanya hivyo kwenye nyanja za kijamii, kiuchumi, kisiasa na kimazingira.

Uongozi wa vijana utaweza kuleta mafanikio au kufeli kuhusiana na majanga matatu duniani yanayoingiliana ya mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira na uharibifu wa bayoanuai, na uchafuzi na taka. Uongozi wa vijana pia utakuwa muhimu kuwezesha hatua kuchukuliwa kuhusiana na uamuzi wa hivi karibuni wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa wa kutambua haki ya kuwa na mazingira safi, dhabiti na endelevu.

Kazi hii ndipo inaanza. UNEP inaingia kwenye awamu ya kushughulikia mambo kwa dharura - ikiwa ni pamoja na kupitia hafla zinazolenga kubuni hatua mpya na kuleta watu pamoja kwenye vita hivi. Tuna kikao cha tano cha Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa mwaka huu. Hii ni taasisi ya ngazi ya juu inayofanya uamuzi kuhusu mazingira duniani. Maazimio muhimu yanawekwa ili kutunza dunia yetu asilia.

Tuna UNEP@50 mwezi wa Machi, kisha Stockholm+50 na Siku ya Mazingira Duniani mwezi wa Juni, hafla zitakotumika kuadhimisha miaka hamsini tangu vuguvugu la mazingira duniani lilipoanzishwa. Dunia Moja Tu ndiyo kaulimbiu ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu. Ilikuwa pia kaulimbiu ya Kongamano la Stockholm la Mwaka wa 1972. Miaka hamsini baadaye, kauli hii bado ina mashiko - sayari Dunia ndio makaazi yetu pekee. Wanadamu ni lazima washirikiane ili kutunza rasilimali zinazoweza kuisha Duniani na kutunza na kuboresha dunia asili inayotegemewa na jamii na uchumi.   

Hatuna miaka mingine 50 ya kutatua changamoto zetu za mazingira. Hatuna hata miaka tano. Tunahitaji ushirikiano wa kimataifa, na hasa ushirikishwaji wa vijana kote duniani, katika hafla hizi na baadaye - kama vile kupitia Kikosi Kazi cha Vijana cha Stockholm+50, kilichozinduliwa kwenye mkutano wa kilele wa hali ya hewa mjini Glasgow katika mwezi wa Novemba.

Wandani wangu,

Tumeona uwezo na hasira halali ya vijana hivi karibuni barabarani mjini Glasgow. Mna haki ya kukasirika. Vizazi vilivyotutangulia vimetufeli. Sasa mnaweza kutumia nguvu hizo kuonyesha ulimwengu jinsi inavyopaswa kuwa. Sasa unaweza kujiunga na waleta mabadiliko. 

Kuna njia nyingi ambazo mnaweza kutumia nguvu hizo. Njia nyingi za kuwa waleta mabadiliko. Kuweni na ujasiri ndani ya mashirika ili kuyalazimisha kuacha kuongea tu na kuchukua hatua endelevu. Tumieni kura yenu kuchagua viongozi watakaojali sayari na hatima yenu. Shinikizeni shule zenu, vikundi vya kidini na mashirika kutumia fedha zao na mifuko ya pensheni kuweka miradi inayowezesha masuluhisho na uendelevu wa mazingira.  Anzisheni biashara yenu isiyochafua mazingira ili kuondoa kampuni za zamani ambazo hazitabadilika. Hamasisheni na muweke utaratibu kwenye jamii zenu, majiji yenu au maeneo mnamoishi. Toeni mawazo yenu na ubunifu wenu - kwa sababu tunahitaji teknolojia mpya na njia mpya za kuishi ili kuachana na mazoea yetu yaliyopitwa na wakati na yalio hatari.

Lakini pia fikiria kukusu utakachofanya mwenyewe. Na tafakari upya kuhusu aina ya uamuzi unaofanya kila siku. Uamuzi wa mtu binafsi ni muhimu. Ni muhimu kuchagua mbinu ya usafiri isiyochafua mazingira, tumia protini mbadala katika mlo wako, na urekebishe, utumie tena na kuunda bidhaa kutoka kwa vitu viyivyotumiwa. Lakini tukianza na juhudi za mtu binafsi na kuchukua hatua pamoja, ndipo tutakapopiga hatua kubwa.

Wandani wangu,

Ni wazi kuwa tuna kazi ya kufanya. Ni lazima sote tutimize wajibu wetu. Misri imeonyesha uongozi wake kwa kushikilia urais wa Kikao cha 14 wa Kongamano la Washirika wa Mkataba wa Ubayoanwai wa Kibayolojia. Taifa hilo pia litasimamia Kongamano lijalo la Wanachama kuhusu mabadiliko ya tabianchi, litakalofanyika mjini Sharm El-Sheikh baadaye mwaka huu. Tunahitaji zaidi uongozi wa namna hii. Pamoja, tukifanya kazi kwa ushirikano na vizazi mbalimbali, tukichochewa na nguvu za vijana, tunaweza kuubadilisha ulimwengu. Vijana hawako tayari kutulia kwenye lindi lilelile ambalo limesababishia sayari yetu majeraha makubwa. Hamko tayari kuwa sehemu ya siku zijazo tu. Mna uwezo, na ni sharti, mufafanue mustakabali.  Kwa maana ni wenu. 

Niruhusu nimalizie kwa maneno ya Askofu Mkuu Desmond Tutu ambaye tunaomboleza kifo chake kilichotekea mwezi huu.  “Fanya wema wako mdogo hapo ulipo; ni huo mewa mdogomdogo unapojumuishwa, huishangaza dunia.”

Asanteni.