Nairobi, Septemba 16, 2021 - Wakikutana wiki hii mtandaoni kwenye kikao cha 18 cha Kongamano la Mawaziri wa Afrika kuhusu Mazingira (AMCEN), Mawaziri 54 wa Mazingira kutoka Afrika walikubaliana kuimarisha juhudi za bara za kujiimarisha kwa njia endelevu bila kuchafua mazingira ili kukabiliana na changamoto za aina tatu za mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa bayoanuai, na uchafuzi.
Katika Taarifa ya Mawaziri iliyotolewa leo wakati wa kufunga awamu ya kwanza ya kikao cha 18 cha AMCEN, wawakilishi wa serikali za Afrika walithibitisha tena kujitolea kwao na juhudi za kukabiliana na athari za janga la COVID-19 kwa kutoa kipaumbele kwa hatua za kujiimarisha kwa njia endelevu bila kuchafua mazingira zinazoweza kupelekea jamii, uchumi, na mazingira kuwa imara.
Akizungumza wakati wa mkutano huo wa mawaziri, Rais anayechukua usukani wa AMCEN na Waziri wa Mazingira wa Senegal, Mheshimiwa Abdou Karim Sall, alisema, "Ni kwa maslahi ya Afrika na kwa maslahi ya watu wetu kutoa kipaumbele kwa masuala ya mazingira inavyostahili, haswa kwa kuzingatia athari za COVID-19."
"Sio fursa tu bali ni wajibu, kwamba sisi Mawaziri wa Mazingira wa Afrika tunawajibika kuhakikisha kuwa kinachohitajika kinatolewa kuhakikisha malengo ya AMCEN yanafikiwa kupitia hatua za dharura," akaongezea.
Mawaziri wamejitolea kuhakikisha kuna mbinu bora za kimataifa za kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kupitia Mkataba wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC), Protokali ya Kyoto na Mkataba wa Paris. Pia walisisitiza kujitolea kwao kuhakikisha utekelezaji wake kulingana na kanuni za Mkataba, wakisisitiza kuwa upatikanaji sawa wa maendeleo endelevu, kutokomeza umaskini na kutambua mahitaji maalum ya nchi za Afrika.
Katika mkutano huo wa ngazi ya juu, uliofanyika kupitia mtandao chini ya kaulimbiu “Kuwezesha ustawi wa watu na uendelevu barani Afrika”, Mawaziri hao walitoa wito wa kujiimarisha kwa kuzingatia watu kwa kubuni nafasi za kazi na kuboresha maisha ya watu.
Bara limeathiriwa vibaya kutokana na athari za janga la COVID-19 kwa jamii na kwa uchumi . Hii imeathiri masoko ambayo tayari yamekuwa tete sana, na kupunguza Pato la Taifa barani kwa asilimia 3.4 na kupelekea hasara inayokadiriwa kuwa kati ya dola bilioni 173.1 na dola bilioni 236.7 bilioni kwa miaka ya 2020 hadi 2021.
Mawaziri walisema kuwa janga hilo lilikuwa limezuia uwezo wa nchi za Afrika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa bayoanuai, na uchafuzi, mambo ambayo tayari pia yana athari kubwa katika maeneo mengi barani.
Ili kujiimarisha kwa njia endelevu bila kuchafua mazingira barani Afrika, jukwaa la mtandaoni la Mpango wa Kuchochea Kutochafua Mazingira Barani Afrika (AGSP) ulizinduliwa rasmi. Jukwaa linatoa fursa kuu kwa serikali, wabia wa maendeleo, jamii, na wadau kupata habari na maarifa kuhusu AGSP iliyopitishwa hivi karibuni.
“ Mpango wa Kuchochea Kutochafua Mazingira Barani Afrika ni hatua muhimu ya kutumia fursa hii kikamilifu. Programu hiyo inahusu mambo yote muhimu: kushughulikia mazingira, kuboresha hewa, uboreshaji wa ardhi, bayoanuai, uchumi wa bahari, miji ya kijani na kadhalika," Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la umoja wa Mataifa (UNEP). “Itakamilishana na Mpango wa Umoja wa Afrika wa Hatua za Kujiimarisha Bila Kuchafua Mazingira kwa kuwezesha nchi na kanda kuchukua hatua zaidi kupitia ujumuishaji wa mazingira katika mipango na programu zao. Na itakuwa na msingi wake hatua za kujiimarisha zilizopo."
Mawaziri waliunga mkono msimamo wa pamoja wa kikanda kwamikutano ijayo ya Kongamano la Wanachama wa Mkataba wa Bayoanuai ya Kibayolojia (COP 15) na Kongamano la Wanachama wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa kuhudu Mabadiliko ya Tabianchi (COP26). Pia walizitaka Nchi Wanachama kutoka barani Afrika kushiriki kikamilifu na kuwakilisha kanda hilo kwenye kikao cha tano cha Baraza la Mazingira la umoja wa Mataifa (UNEA 5.2) kitakachofanyika Nairobi kuanzia tarehe 28 Februari hadi tarehe 2 Machi mwaka wa 2022.
Katika maadhimisho ya miaka 50 ya UNEP (UNEP@50) katika mwaka wa 2022, Mawaziri hao walikubaliana kushiriki katika shughuli katika ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa ili kuhamasisha kuhusu hatua kabambe za baadaye za kutunza mazingira, kukabiliana na uchafuzi, uharibifu wa ardhi na mabadiliko ya tabianchi. Mawaziri hao wa Mazingira pia walikubaliana kuunga mkono UNEP@50 kwa kutoa jukwaa pana la uhamasishaji na kuchukua hatua za kimfumo barani Afrika.
Kabla ya Kongamano la Mawaziri, mkutano wa Makundi Makuu na Wadau Barani Afrika ulifanyika tarehe 10 Septemba na kuhudhuriwa na mashirika yaliyoidhinishwa na UNEP. Ujumbe wao uliwasilishwa kwa mawaziri na mwakilishi wa maeneo wa makundi hayo.
Akiongea kwa niaba ya Makundi Makuu na Wadau Barani Afrika, Ayman Cherkaoui kutoka Moroko alisema, "Tunapongeza AMCEN kwa kazi yake ya kutoa mwongozo wa kimkakati na kisera kwa uundaji wa Mpango wa Kuchochea Kutochafua Mazingira Barani Afrika. Tunaomba kushirikishwa kwa Makundi Makuu na Wadau Barani Afrika katika Kamati ya Uratibu ya Mpango wa Kuchochea Kutochafua Mazingira Barani Afrika."
Matokeo ya kikao cha 18 cha AMCEN yatapatikana mtandaoni kupitia: https://www.unep.org/events/conference/eighteenth-session-african-ministerial-conference-environment
MAKALA KWA WAHARIRI
Kuhusu AMCEN
Kongomano la Mawaziri wa Afrika kuhusu Mazingira (AMCEN) lilianzishwa katika mwaka wa 1985, kufuatia kongomano la Mawaziri wa Mazingira wa Afrika uliofanyika Cairo, Misri. Kazi yake ni kuhamasisha kuhusu utunzaji wa mazingira barani Afrika; kuhakikisha kuwa mahitaji ya kimsingi ya binadamu yanapatikana ipasavyo na kwa njia endelevu; kuhakikisha kuwa maendeleo kwa jamii na kwa uchumi yanatekelezwa katika ngazi zote; na kuhakikisha kuwa shughuli na mazoea ya kilimo yanakidhi mahitaji ya utoshelezaji wa chakula ukandani.
Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP):
UNEP in mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira ulimwenguni. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.
Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:
Mohamed Atani, Mkuu wa Mawasilaino na Uhamasishaji, Ofisi ya Afrika ya UNEP