- Takribani robo tatu ya mataifa yameweka mikakati fulani ya kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kutegemea na eneo, ila ufadhili na utekelezi wake uko chini kuliko kiwango kinachotarajiwa
- Gharama ya kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kutegemea na eneo katika nchi zinazoendelea pekee hukadiriwa kuwa dola za Marekani bilioni 70 kwa mwaka. Inatarajiwa kuongezeka na kufikia kati ya dola za Marekani bilioni 140 na bilioni 300 kufikia mwaka wa 2030 na kati ya dola za Marekani bilioni 280 na bilioni 500 kufikia mwaka wa 2050.
- Masuluhisho yanayotokana na mazingira, muhimu katika kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kutegemea na eneo, yanahitaji kuimarishwa
Nairobi, Januari 14, 2021 – Kiwango cha joto kinapoendelea kuongezeka na athari za mabadiliko ya tabianchi zinapoendelea kuwa mbaya zaidi, mataifa yanastahili kuchukua hatua za dharura ili kukabiliana na hali mpya ya hewa au yakabiliane na gharama, madhara na hasara kubwa, Ripoti mpya ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) yaonyesha.
Kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kutegemea na eneo – kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwa nchi na jamii zilizo na uwezo wa kuathirika mno kwa kuboresha uwezo wa kustahimili– ni nguzo kuu kwenye Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi. Mkataba huo unawataka walioutia sahihi kuweka mikakati ya kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kutegemea na eneo kupitia mikakati ya kitaifa, mifumo ya kutoa taarifa kuhusu hali ya hewa, kutoa onyo mapema, kuweka mikakati ya kujikinga na kuwekeza ili kutochafua mazingira katika siku za usoni.
Ripoti ya UNEP Adaptation Gap Report 2020 inaonyesha kuwa ijapokuwa uwekezaji kwenye mikakati umeimarishwa na mataifa, kuna pengo kubwa la ufadhili katika nchi zinazoendelea na hivyo miradi ya kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kutegemea na eneo haijafikia kiwango cha kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kama vile ukame, mafuriko na kupanda kwa uwiano wa bahari.
Ufadhili wa kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kutegemea na eneo unapaswa kuimarishwa kwa dharura, ikifuatiwa na utekelezaji wake. Masuluhisho yanayotokana na mazingira – juhudi mwafaka zinazopatikana katika eneo husika za kukabiliana na changamoto katika jamii, kama vile mabadiliko ya tabianchi, na zinazojali maisha ya binadamu na iliyo na manufaa kwa bayoanuai kwa kuboresha na kufanyia marekebisho mifumo ya ekolojia kwa njia endelevu, iwe ya kiasili au la – ni mambo yanayopaswa pia kupewa kipaumbele.
“Ukweli mgumu ni kuwa tunakabiliwa na mabadiliko ya tabianchi,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Inger Andersen. “Madhara yake yataongezeka na kudhuru nchi na jamii zilizo na uwezo wa kuathirika zaidi – hata ikiwa tutafikia malengo ya Mkataba wa Paris ya kupunguza ongezeko la joto lifikie nyuzijoto 2 na kuendelea kupunguza hadi zifikie nyuzijoto 1.5.”
“Jinsi ambavyo Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa amesema, jamii ya kimataifa inastahili kujitolea ili kutenga nusu ya fedha duniani kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kutegemea na eneo katika mwaka ujao," aliongezea. "Hali hii itawezesha hatua kubwa za kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kutegemea na eneo – ikijumuisha mambo kama vile mifumo ya kutoa onyo mapema, rasilimali dhabiti ya maji na masuluhisho yanayotokana na mazingira.”
Mikakati ya kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kutegemea na eneo inaamarika, ila ufadhili na uwekezaji bado haujatosha
Suala la kujivunia kwenye matokeo ya ripoti hiyo ni kwamba asilima 72 ya nchi imeweka angalau mkakati wa kitaifa wa kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kutegemea na eneo. Nchi nyingi zinazoendelea zinaandaa Mikakati ya Kitaifa ya Kushughulikia Mabadiliko ya Tabianchi kutegemea na eneo. Hata hivyo, fedha zinazohitajika ili kutekeleza mikakati haiongezeki inavyopaswa.
Kiwango cha fedha za kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kutegemea na eneo kinaongezeka, ila gharama ya kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kutegemea na eneo inaendelea kuongezeka kwa kasi. Gharama ya kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kutegemea na eneo katika nchi zinazoendelea pekee hukadiriwa kuwa dola za Marekani bilioni 70 kwa mwaka. Inatarajiwa kuongezeka na kufikia kati ya dola za Marekani bilioni 140 na bilioni 300 kufikia mwaka wa 2030 na kati ya dola za Marekani bilioni 280 na bilioni 500 kufikia mwaka wa 2050.
Kuna mambo ya kufurahisha. Mfuko wa Green Climate (GCF) umetenga asilimia 40 ya jumla ya bajeti yake kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kutegemea na eneo na inaendelea kuongeza uwekezaji katika sekta ya binafsi. Kitu kingine cha muhumu ni kasi ya kuhakikisha kuwa kuna mifumo endelevu ya kutoa ufadhili. Hata uwekezaji wa kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kutegemea na eneo unapaswa kuimarishwa katika sekta za umma na sekta binafsi. Masuala mapya kama vile mbinu endelevu za uwekezaji, kanuni za kutoa taarifa kuhusiana na hali ya hewa kwa njia wazi na kujumuisha athari za mazingira wakati wa kufanya uamuzi wa uwekezaji inaweza kuchombea uwekezaji utalaowezesha mazingira kustahimili hali ya hewa.
Utekelezaji wa hatua za kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kutegemea eneo unaendelea kuimarika. Tangu mwaka wa 2006, takribani miradi 400 ya kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kutegemea na eneo imefadhiliwa na mifuko ya kimataifa inayoshughulikia Mkataba wa Paris katika nchi zinazoendelea. Ijapokuwa miradi ya hapo awali haikuzidi dola za Marekani milioni 10, miradi 21 tangu mwaka wa 2017 ilifikisha kiwango kinachozidi dola za Marekani milioni 25. Hata hivyo, kwa miradi 1,700 iliyochunguzwa, ni asilimia tatu tu ilionyesha kupungua kwa athari kwa mazingira katika jamii husika ambapo miradi hiyo ilitekelezwa.
Masuluhisho yanayotokana na mazingira yanaweza kuwa na mchango mkubwa
Ripoti hiyo inasisitiza kuwa masuluhisho yanayotokana na mazingira yana gharama ya chini inayopunguza athari kwa mazingira, kuboresha na kutunza bayoanuai huku yakiwa na manufaa kwa jamii na kwa uchumi.
Uchanganuzi wa mifuko mikuu minne ya kushughulikia mazingira na kuleta maendeleo – Mfuko wa Kushughulikia Mazingira Duniani, Mfuko wa Green Climate, Mfuko wa Adaptation na Mradi wa Kushughulikia Mazingira Duniani – ulionyesha kuwa kuunga mkono kwa miradi isiyochafua mazingira inayojumuisha vipengele fulani vya masuluhisho yanayotokana na mazingira kumeongezeka katika miongo miwili iliyopita. Jumla ya uwekezaji kwenye miradi ya kushughulikia na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kutegemea na eneo chini ya miradi hiyo minne ulifikia dola za Marekani bilioni 25. Hata hivyo, ni dola za Marekani milioni 12 tu zilitumika kwa masuluhisho yanayotokana na mazingira - kiwango kidogo cha jumla ya fedha za kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kutegemea na eneo na za kutunza mazingira.
Kuimarisha juhudi
Kwa mjibu wa ripoti hiyo, kupunguza uzalishaji wa gesi ya ukaa kutapunguza athari na gharama zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi. Kufikia lengo la nyuzijoto 2 kama inavyohitajika chini ya Mkataba wa Paris kunaweza kupunguza hasara kwa mwaka kufikia asilimia 1.6, ikilinganishwa na asilimia 2.2 itayowezesha kufikia nyuzijoto 3.
Mataifa yote yanapaswa kuchukua hatua zinazoainishwa katika Ripoti ya UNEP ya Emissions Gap ya mwaka wa 2020, iliyotoa wito wa kuimarisha uchumi bila kuchafua mazingira baada ya janga la korona na kuweka malengo mapya kwa Ahadi Zilizowekwa na Taifa zinazojumuisha kutozalisha gesi ya ukaa. Hata hivyo, ni sharti dunia ipange, ifadhili na kutekeleza hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili kusaidia mataifa yaliyo na uwezo mdogo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ila yana uwezo mkubwa wa kuathiriwa.
Ijapokuwa janga la COVID-19 linatarajiwa kuathiri uwezo wa nchi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuwekeza kwenye ushughulikiaji wa mabadiliko ya tabianchi kutegemea na eneo ni uamuzi utakakuwa na manufaa kwa uchumi.
MAKALA KWA WAHARIRI
Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa
UNEP ni mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira ulimwenguni. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.
Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:
Keisha Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, UNEP +254 722 677747