- Awamu ya 16 ya shindano la kitengo cha mazingira la International Poster Biennial ambalo hutokea kila baada ya miaka miwili nchini Meksiko kwa miongo mitatu sasa, itaangazia bayoanuai
- Wasanii kote ulimwenguni wanaombwa kutuma mabango yao hadi tarehe 15 Mei mwaka wa 2020
- Bayoanuai ni kauli mbiu ya Siku ya Mazingira Duniani katika mwaka wa 2020
Mji wa Meksiko, January 22, 2020 – IIi kunufaika kutokana na sanaa kuhamasisha watu kuhusu mazingira na kuwafanya kuchukua hatua mwafaka, awamu ya 16 ya International Poster Biennial, imetoa wito, unaowataka wasanii kutuma mabango katika vitengo sita, mojawapo ikiegemea masuala ya mazingira.
Wito wa kushiriki utaendelea hadi tarehe 15 Mei mwaka wa 2020.
Kwa miaka 30 sasa, takribani mabango 70,000 kutoka katika mabara tano yamewahi kutumwa katika haya maonyesho ambayo hutokea mjini Mexico. Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) hushirikiana na Biennial tangu mwaka wa 1990 ili kudhamimi kitengo kinachoshughulikia masuala ya mazingira.
Awamu ya mwaka huu itaangazia bayoanuai, ambacho ndicho kiini cha Siku ya Mazingira Duniani, jukwa kubwa mno linalotumiwa na Umoja wa Mataifa kuhamasisha umma kuhusu masuala ya mazingira, na hutokea kila mwaka tarehe 5 mwezi wa sita. Kolombia itakuwa mwenyeji wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani.
Wasanii wa kisasa kutoka pembe zote za dunia wamewahi kushiriki katika mashindano ya International Poster Biennial, huku wakitumia ubunifu wao na vifaa vyao kuelezea changamoto za mazingira kwa njia mwafaka na ya dharura, suala ambalo mara nyingi ni vigumu kulipuuza.
Kwa mfano, Maja Zurawiecka, msanii kutoka Uholanzi, alitumia bango lililokuwa na mchoro wa ajabu wa mkono ulioumia sana kuashiria tishio lililopo kwa msitu mkuu wa Bialowieza, eneo ambalo ni Turathi ya Dunia kwenye mpaka kati ya Belarus na nchi yake.
"Ujumbekwenye bango langu ulikuwa rahisi: bila mazingira, sisi si chochote. Unapokata mti, kuna uwezekano ni mkono wako unaoukata. Unapunguza maisha yetu duniani," alisema Zurawiecka, aliyechukua nambari moja kwenye awamu ya 14 ya mashindano haya.
Baadhi ya masuala nyeti yanayohusiana na mazingira ambayo yameshughulikiwa na wasanii waliowahi kushiriki mashindano haya ni pamoja na: uchafu wa plastiki; ongezeko la joto duniani; uchumi usiyochafua mazingira; ukabilianaji wa hewa ya ukaa kutokana na chakula na kadhalika. Kwenye awamu ya mwisho kutokea ya mashindano haya, kitengo cha mazingira kilipokea mabango 1,645. Msanii mchoraji kutoka Uchina Yongkang Fu alichukua nambari moja kutokana na kazi yake ya "Eneo la Makazi" ambayo ilionyesha kwa njia ya kushawishi mno madhara mabaya ya uchafu wa plastiki kwa viumbe vinavyoishi baharini.
Mwaka wa 2020 umeitwa ‘mwaka mkuu’ kwa mazingira, mwaka ambao unatarajia kushuhudia mikutano mikuu ya kimataifa na nia ya kuweka agenda ya mazingira na hatua zitakazochuchukuliwa kwa kipindi cha muongo mmoja ujao, ikijumuisha Mkutano wa 15 wa Kongamano la Nchi Wanachama wa Bayoanuai ya Kibayolojia (COP 15), mjini Kunming, nchini China, na Kongamano la Umoja wa Mataifa la Mabadiliko ya Tabianchi litakalotokea Glasgow. COP15 itajadili mapendekezo makuu ya kutunza asilimia 30 ya maeneo yote ya ardhi na bahari.
Aina milioni moja ya viumbe viko hatarini kuangamia kutokana na mabadiliko katika matumizi ya ardhi na matumizi ya bahari, kutokana na uchafuzi, kutokana na mabadiliko ya tabianchi na kutokana na matumizi mabaya ya rasilimali, kwa mjibu wa ripoti ya Jukwaa la Kuunda Sera za Sayansi kati ya Mataifa kuhusu Bayoanuai na Huduma za Mifumo ya Ikolojia (IPBES) .
Maslahi ya mifumo ya ekolojia ambayo sisi na viumbe vingine vyote hutegemea yanaendelea kudidimia kwa kasi mno kuliko katika kipindi kingine chochote, kwa mjibu wa Sir Robert Watson, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa IPBES. Pia, alisema kuwa binadamu wanaharibu msingi wa uchumi wetu, wa maisha yetu ya kila siku, wa kuwepo kwa chakula cha kutosha wa afya na wa kiwango cha ubora wa aina ya maisha.
"Mwaka huu, kauli mbiu ya mashindano ambayo hutokea kila baada ya miaka miwili ni mwafaka zaidi, kwa sababu tunashuhudia uharibifu mbaya mno wa bayoanuai unaotokea kwa kiwango cha kuhofisha," alisema Leo Heileman, Mkurugenzi wa UNEP wa ukanda wa Amerika ya Latini na Karibean. "Tuna furaha kuendelea kushirikiana na International Poster Biennial, mashindano ambayo huyotokea mjini Meksiko, Mji ulio na utamaduni wa kila aina kule Amerika.
"Ubongo wetu unahitaji sekunde tatu tu kuhifadhi kwenye kumbukumbu bango zuri," alisema Xavier Bermúdez, Mkurugenzi wa Biennial tangu ilipoanzishwa. "International Poster Biennial wakishirikiana na UNEP, huhamasisha watu na kuwashawishi kuchukua hatua kwa kubadili mienendo yao maishani. Haitoshi tu kutushawishi kutotulia – bango zuri pia hutia watu motisha ya kufanya maamuzi chanya."
Kiwango cha uharibifu wa bayoanuai kwa sasa ni cha kusikitisha; ripoti ya IPBES inaonya kuwa zaidi ya theluthi moja ya wanyama wanyonyeshao wanaoishi baharini, zaidi ya asilimia 40 ya wanyama wanaoweza kuishi ardhini na majini kwa wakati mmoja na asilimia 10 ya wadudu wamo hatarini.
"Mabadiliko huanza ya kuelewa. Kuelewa kuwa hatuko pekee yetu kwenye sayari hii ya dunia. Kuelewa kuwa maamuzi yetu yote na matendo yetu yote yanaathiri maisha yetu, yanaathiri wanyama na mimea," alisema Fatoumata Dravé, msani mchoraji kutoka Kanada aliyeshikilia nambari ya pili wakati wa mashindano ya Biennial ya mwaka wa 2016. Kazi yake kwa anwani ya “Toxicité”, iliangazia madhara mabaya mno ya uzalishaji wa alumini kwa maisha ya viumbe wa baharini.
"Kila mara, nimekuwa nikiwaza jinsi ambavyo wasani wachoraji wanavyoweza kuchangia katika masuala ya jamii," aliongezea "Nilichukua fursa wakati wa Biennial kutengeza bango kuhusu bayoanuai kutokana na utafiti huku likiwa na ujumbe wenye uwezo wa kuathiri."
MAKALA KWA WAHARIRI
Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa
UNEP ni msemaji mkubwa wa masuala ya mazingira kote duniani. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika kutunza mazingira kupitia kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.