- Makadirio ya uzalishaji wa hewa chafu kufikia mwaka wa 2030 yanapaswa kupungua kwa asilimia kati ya 28 na 42 ili kuwezesha kufikia nyuzijoto 2 na 1.5
- Upunguzaji usiokoma na mabadiliko ya kupunguza hewa ya ukaa ni muhimu ili kupunguza pengo la uzalishaji wa hewa chafu
- COP28 na Tathmini ya Kimataifa ni fursa ya kuwa na matarajio makubwa zaidi kwa awamu inayofuata ya ahadi za kushughulikia mazingira
Nairobi, Novemba 20, 2023 – Huku hali ya joto duniani na uzalishaji wa gesi ya ukaa vinapovunja rekodi, Ripoti ya hivi punde ya Pengo la Uzalishaji wa Hewa Chafu kutoka kwa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) inaonyesha kuwa ahadi zilizopo chini ya Mkataba wa Paris zitafanya ulimwengu kushuhudia joto la nyuzijoto kati 2.5 na 2.9 zaidi ya viwango vya kabla ya viwanda katika karne hii, hali inayoashiria umuhimu wa kushughulikia mazingira kwa dharura.
Ripoti inayotolewa kabla ya mkutano wa kilele wa mazingira wa COP28 mjini Dubai, Miliki za Falme za nchi za Kiarabu, Ripoti ya Pengo la Uzalishaji Wa Gesi Chafu mwaka wa 2023: Rekodi iliyovunjwa –Ongezeko la joto lilizidi zaidi, ila dunia imeshindwa kupunguza uzalishaji wa hewa chafu (tena), inaonyesha kuwa mabadiliko ya kupunguza hewa ya ukaa duniani yanahitajika ili kuwezesha kufikia makadirio ya kupunguza hewa ya ukaa kwa asilimia 28 ili kufikia nyuzijoto 2 na asilimia 42 ili kufikia nyuzijoto 1.5 kufikia mwaka wa 2030.
“Tunafahamu kuwa bado kuna uwezekano wa kuweza kudhibiti ongozeko la joto lisizidi nyujijoto 1.5. Inahitaji kukabiliana na chanzo kikuu cha janga la mabadiliko ya tabianchi: nishati ya mafuta. Na inahitaji mabadiliko yalio na haki na usawa ya nishati jadidifu,” alisema Antònio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Kudumisha uwezekano wa kufikia malengo ya Mkataba wa Paris inategemea kuimarisha kwa kiwango kikubwa ukabilianaji wa hali katika muongo huu ili kupunguza pengo ya uzalishaji wa hewa chafu. Hii itawezesha malengo kabambe zaidi kufikia mwaka wa 2035 katika awamu inayofuata ya Ahadi Zinazotelewa na Taifa (NDCs) na kuimarisha uwezo wa kutimiza ahadi za kutozalisha hewa chafu, ambazo kwa sasa zinashughulikia angalau asilimia 80 ya uzalishaji wa hewa chafu duniani.
"Hakuna mtu au uchumi duniani usioathiriwa na mabadiliko ya tabianchi, na kwa hivyo tunahitaji kuacha kuweka rekodi zisizohitajika za uzalishaji wa gesi ya ukaa, kuongeza kiwango cha joto duniani na hali mbaya ya hewa," alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP. "Ni sharti tukome kuendelea na mambo kama kawaida kwa kutotoa ahadi za kutosha na kutochukua hatua za kutosha, na kuanza kuweka rekodi mpya: kuhusu kupunguza uzalishaji wa hewa chafu, kuhusu mabadiliko ya haki ya kutochafua mazingira na kuhusu ufadhili wa kushughulikia mazingira."
Rekodi zilizovunjwa
Kuanzia Januari hadi mwanzoni mwa Oktoba mwaka huu, siku 86 zilishuhudia kiwango cha joto cha zaidi ya nyuzijoto 1.5 kuliko viwango vya kabla ya viwanda. Septemba ndio mwezi ulishuhudia kiwango cha juu zaidi cha joto kuwahi kurekodiwa, huku wastani ya joto duniani ikiwa zaidi kwa nyuzijoto 1.8 kuliko viwango vya kabla ya viwanda.
Ripoti hii inaonyesha kuwa uzalishaji wa gesi ya ukaa (GHG) uliongezeka kwa asilimia 1.2 kutoka mwaka wa 2021 hadi mwaka wa 2022 hadi kufikia viwango vipya sawa na Gigatani 57.4 za Kaboni dioksidi (GtCO2e). Uzalishaji wa GHG katika nchi zote za G20 uliongezeka kwa asilimia 1.2 katika mwaka wa 2022. Mitindo ya uzalishaji wa hewa chafu ina ukosefu wa usawa. Kutokana na mienendo hii inayotia wasiwasi na juhudi zisizotosha za kukabiliana na hali hii, dunia inaenda kushuhudia ongezeko la joto zaidi ya malengo ya kimataifa ya mazingira katika karne hii.
Iwapo jitihada za kukabiliana na hali kwa kuzingatia sera zilizopo zitaendelea zilivyo, ongezeko la joto duniani litadhibitiwa tu hadi nyuzijoto 3 kuliko viwango vya kabla ya viwanda katika karne hii. Utekelezaji kikamilifu wa juhudi zilizoainishwa kwa Ahadi Zinazowekwa na Taifa (NDCs) zitawezesha ulimwengu kudhibiti ongezeko la joto hadi nyuzijoto 2.9. NDC zilizo na masharti zikitekelezwa kikamilifu zitasababisha joto kutozidi nyuzijoto 2.5 kuliko viwango vya kabla ya viwanda. Yote haya yana fursa ya asilimia 66.
Makadirio haya ya joto ni ya juu kidogo kuliko katika Ripoti ya Pengo la Uzalishaji wa Hewa Chafu ya mwaka wa 2022, kwani ripoti ya mwaka wa 2023 inajumuisha idadi kubwa ya mifumo katika makadirio ya ongezeko la joto duniani.
NDCs zilizopo sisizo na masharti zinaonyesha kuwa upunguzaji wa ziada wa uzalishaji wa GtCO2e 14 unahitajika kufikia mwaka wa 2030 kuliko viwango vilivyotabiriwa ili kufikia nyuzijoto 2. Upunguzaji wa GtCO2e 22 unahitajika ili kuweza kufikia nyuzijoto 1.5. Utekelezaji wa NDC zilizo na masharti hupunguza makadirio haya yote kwa GtCO2e 3.
Kwa kuzingatia asilimia, dunia inahitaji kupunguza uzalishaji wa hewa chafu kufikia mwaka wa 2030 kwa asilimia 28 ili kuweza kufikia lengo la Mkataba wa Paris la nyuzijoto 2 ikiwa na fursa ya asilimia 66, na asilimia 42 kufikia lengo la nyuzijoto 1.5.
Ikiwa NDC zote zilizo na masharti na ahadi za muda mrefu za kutozalisha hewa chafu zitatimizwa, kudhibiti ongezeko la joto lisizidi nyuzijoto 2 kunawezekana. Hata hivyo, ahadi za kutozalisha hewa chafu hazizingatiwi kwa sasa: hakuna nchi yoyote kati ya nchi za G20 inapunguza uzalishaji wa hewa chafu kwa kasi inayorandana na malengo yao ya kutozalisha hewa chafu. Hata tukiwa na matumaini zaidi, uwezekano wa kudhibiti ongezeko la joto lisizidi nyuzijoto 1.5 ni asilimia 14.
Kuna hatua zimepigwa, lakini hazitoshi
Hatua za kisera tangu Mkataba wa Paris ulipotiwa saini mwaka wa 2015 zimepunguza pengo la utekelezaji, linalofafanuliwa kama tofauti kati ya makadirio ya uzalishaji wa hewa chafu chini ya sera zilizopo na utekelezaji wa NDC kikamilifu. Uzalishaji wa GHG katika mwaka wa 2030 kwa kuzingatia sera zilizopo ulitarajiwa kuongezeka kwa asilimia 16 wakati wa kupitishwa kwa Mkataba wa Paris. Leo, makadirio ya ongezeko ni asilimia 3.
Kufikia tarehe 25 Septemba, nchi tisa zilikuwa zimewasilisha NDC mpya au zilizosasishwa tangu COP27 mwaka 2022, na hivyo kufanya jumla ya idadi ya NDC zilizosasishwa kuwa 149. Ikiwa NDC zote mpya na zilizosasishwa zisizo na masharti zitatekelezwa kikamilifu, kuna uwezekano wa kupunguza uzalishaji wa GHG kwa takriban GtCO2e 5.0, takriban asilimia 9 ya uzalishaji wa hewa chafu wa mwaka wa 2022, kila mwaka kufikia mwaka wa 2030, ikilinganishwa na NDC za awali.
Hata hivyo, bila viwango vya uzalishaji wa hewa chafu kupunguzwa zaidi kufikia mwaka wa 2030, haitawezekana kupata njia za gharama nafuu za kudhibiti ongezeko la joto duniani lisizidi 1.5 na wala visiongezeke au kuongezeka kidogo tu katika karne hii. Kuimarisha utekekezaji kwa kiwango kikubwa katika muongo huu ni njia ya pekee ya kuepuka kuongezeka kwa kiwango zaidi ya nyuzijoto 1.5.
Mabadiliko ya kufanya maendeleo kwa kupunguza hewa ya ukaa
Ripoti hii inatoa wito kwa mataifa yote kuchukua hatua za kuleta mabadiliko ya kupunguza hewa ya ukaa mara moja na kwa uthabiti kwa uchumi wote. Makaa ya mawe, mafuta na gesi inayochimbwa katika kipindi chote cha uzalishaji na mipango ya kuchimba migodi na maeneo ya uchumbaji vinaweza kuzalisha zaidi ya mara 3.5 ya bajeti iliopo ya hewa ya ukaa ya kudhibiti ongezeko la joto lisizidi nyuzijoto 1.5, na karibu bajeti yote iliopo ya kufikia nyuzijoto 2.
Nchi zilizo na uwezo mkubwa na huchangia zaidi kwa uzalishaji wa hewa chafu – hasa nchi za kipato cha juu na nchi zinazozalisha hewa chafu nyingi kati ya nchi za G20 – zitahitaji kuchukua hatua kabambe kwa dharura na kutoa msaada wa kifedha na kiufundi kwa mataifa yanayoendelea. Kwa vile nchi za kipato cha chini na cha kati tayari zinachangia zaidi ya theluthi mbili ya uzalishaji wa GHG duniani, kukidhi mahitaji ya maendeleo na uzalishaji mdogo wa gesi ya ukaa vipewe kipaumbele katika mataifa kama haya – kama vile kushughulikia ruwaza ya mahitaji ya nishati na kutoa kipaumbele kwa nishati isiyochafua mazingira wakati wa mifumo yao ya usambazaji.
Mabadiliko ya kufanya maendeleo kwa kupunguza hewa ya ukaa yana changamoto za kiuchumi na kitaasisi kwa nchi za kipato cha chini na cha kati, lakini pia hutoa fursa muhimu. Mabadiliko katika nchi kama hizo yanaweza kusaidia kuwezesha ufikiaji wa nishati kwa wote, na kuondoa mamilioni ya watu kutoka lindi la umaskini na kupanua viwanda vilivyo na mikakati. Maendeleo yanayohusishwa na nishati yanaweza kutekelezwa kikamilifu na kwa usawa huku nishati inayozalisha kiwango kidogo cha hewa ya ukaa kama nishati jadidifu ikiwa nafuu, na kuhakikisha kuna ajira isiyochafua mazingira na hewa safi.
Ili kufikia hili, msaada wa ufadhili wa kimataifa utalazimika kuongezwa kwa kiwango kikubwa, huku vyanzo vipya vya mtaji vya umma na vya kibinafsi vikifanyiwa marekebisho kupitia mifumo ya ufadhili –ikiwa ni pamoja na ufadhili wa madeni, ufadhili ulio na masharti nafuu wa muda mrefu, dhamana na fedha za kuimarisha hali – ambazo zinapunguza gharama za mtaji.
COP28 na Tathmini ya Kimataifa
Tathmini ya kwanza ya Kimataifa (GST), inayohitimishwa katika COP28, itakuwa nguzo kwa awamu inayofuata ya NDCs ambazo nchi zinapaswa kuwasilisha katika mwaka wa 2025, na malengo ya mwaka wa 2035. Ahadi za kimataifa katika awamu inayofuata ya NDCs ni sharti zifanye uzalishaji wa GHG kufikia mwaka wa 2035 kurandana na viwango vya chini ya nyuzijoto 2 na nyuzijoto 1.5, huku zikifidia uzalishaji wa ziada hadi viwango vinavyowiana na hali hii kufikiwa.
Maandalizi ya awamu inayofuata ya NDCs yanatoa fursa kwa nchi za kipato cha chini na cha kati kuweka mikakati ya kitaifa iliyo na sera kabambe na hatua za kushughulikia mazingira, na shabaha ambazo mahitaji ya fedha na teknolojia vinabainishwa wazi. COP28 inapaswa kuhakikisha kwamba msaada wa kimataifa unatolewa ili kukuza mikakati hii.
Kuondolewa kwa kaboni dioksidi
Ripoti hii inaonyesha kuwa kuchelewesha upunguzaji wa uzalishaji wa GHG kutaongeza utegemezi wa siku zijazo wa kuondolewa kwa kaboni dioksidi kutoka angani. Uondoaji wa kaboni dioksidi tayari unatekelezwa, hasa kupitia upandaji miti, kurejesha misitu na usimamizi wa misitu. Uondoaji wa sasa wa moja kwa moja kupitia mbinu za juu ya ardhi unakadiriwa kuwa GtCO2e 2 kila mwaka. Hata hivyo, njia za gharama ya chini zaidi zinakisiwa kuongeza zaidi uondoaji wa kaboni dioksidi kwa njia ya kawaida na njia mpya – kama vile kunasa na kuhifadhi hewa ya ukaa.
Kufikia viwango vya juu vya uondoaji wa kaboni dioksidi bado hakuko dhahiri na huhusishwa na madhara: kuhusu ushindani wa ardhi, ulinzi wa umiliki na haki ya kumiliki na mambo mengine. Kuimarisha mbinu mpya za uondoaji wa kaboni dioksidi huhusishwa na aina mbalimbali ya madhara, ikiwa ni pamoja na mahitaji ya kiufundi, kiuchumi na kisiasa, hivyo utekelezaji kwa kiasi kikubwa huenda usitokee kwa wakati.
MAKALA KWA WAHARIRI
Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)
UNEP ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira duniani. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.
Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:
Kitengo cha Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa