Pixabay
17 Feb 2022 Toleo la habari Uchunguzi wa mazingira

Mioto mibaya zaidi, uchafuzi wa kelele na usumbufu usikofaa kwa majira maishani: Ripoti ya Umoja wa Mataifa yaainisha hatari zitakazokabili…

Nairobi, Februari 17 2022 - Mioto misituni inatokea mara kwa mara na inaendelea kuwa mikali zaidi, uchafuzi wa kelele mijini unaendelea kuwa kero na kuathiri afya ya umma, na kusababisha kutoingiliana kifenelojia – kuathiriwa kwa misimu mbalimbali ya maisha kwenye mifumo asilia – vinasababisha madhara ya kiekolojia. Masuala haya nyeti ya mazingira, yanayohitaji kushughulikiwa mno, yameangaziwa katika Ripoti mpya ya Masuala Ibuka iliyochapishwa leo na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP).

Hili ni toleo la nne la Ripoti ya Masuala Ibuka, ambayo ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika mwaka wa 2016 kwa kutoa onyo dhidi ya uwezekano wa kuongezeka kwa magonjwa kutoka kwa wanyama, miaka minne kabla ya kuzuka kwa janga la COVID-19..

“Ripoti ya Masuala Ibuka inabainisha na kutoa masuluhisho kwa masuala matatu ya mazingira yanayopaswa kushughulikiwa na serikali na umma kwa jumla," Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP alisema.  "Uchafuzi wa kelele mijini, mioto misituni na mabadiliko ya kifenolojia - mada tatu kwenye ripoti hii ya Masuala Ibuka - ni maswala ambayo yanaonyesha umuhimu wa kushughulikia kwa dharura changamoto tatu duniani za mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi na uharibifu wa bayoanuai.”

Toleo mpya la ripoti ya Masuala Ibuka, Kelele, Mioto na Kutoingiliana: Masuala Ibuka Yanayoathiri Mazingira, imetolewa siku chache kabla ya kuanza kwa kikao cha tano cha Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA):

Uchafuzi wa kelele katika miji ni hatari inayoongezeka dhidi ya afya ya umma

  • Sauti zisizofaa, kwa muda mrefu na zilizo juu sana kutoka kwa trafiki barabarani, reli au shughuli za burudani huathiri afya na ustawi wa binadamu. Hii ni pamoja na kukerwa mno na kukosa usingizi, hali inayopelekea magonjwa ya moyo mabaya zaidi na matatizo ya kimetaboliki kama vile kisukari, kutoweza kusikia vizuri, na kudorora kwa afya ya akili.
  • Uchafuzi wa kelele tayari husababisha vifo vya mapema 12,000 kila mwaka kwa EU na huathiri mmoja kati raia watano wa EU. Viwango vya kelele vinavyokubalika hupitwa katika miji mingi kote duniani, ikijumuisha Algiers, Bangkok, Damascus, Dhaka, Ho Chi Minh City, Ibadan, Islamabad na New York.
  • Wanaoathiriwa zaidi ni watoto, wazee na jamii zilizotengwa karibu na barabara kuu za trafiki, na maeneo ya viwanda na mbali na maeneo yalio na miti.
  • Pia ni tishio kwa wanyama, huathiri mawasiliano na tabia ya viumbe mbalimbali, ikijumuisha ndege, dudu, na  amfibia.
  • Wakati uo huo, sauti asilia zinaweza kuwa na manufaa mbalimbali ya kiafya. Wapangaji wa miji wanapaswa kutoa kipaumbele kwa upunguzaji wa kelele kwenye vyanzo vyake; kuwekeza kwenye njia mbadala za usafiri; na miundomsingi ya mijini inayounda mandhari chanya kwa sauti kama vile kupanda miti, kuta zisizochafua mazingira, mimea paani na maeneo mengi yaliyo na mimea mijini.
  • Mifano chanya ni pamoja na Eneo la Uzalishaji wa Chini Zaidi wa Gesi Chafu mjini London, njia mpya za baisikeli kwenye barabara pana mjini Berlin, na mpango wa kitaifa kukabiliana na kelele nchini Misiri.
  • Kuzuia kwa watu kujumuika wakati wa COVID-19 kulipelekea kuona umuhimu maeneo yaliyo na mimea na kupunguza kelele za trafiki mijini. Programu zinazolenga ‘kujiimarisha vyema’ ni fursa ambayo bado haijatumiwa na watunga sera, wapangaji miji na jamii kuunda maeneo ya ziada yaliyo na mimea kwa watu wote.

Hali ya mioto hatari misituni inakadiriwa kuwa mbaya zaidi  

  • Kila mwaka, kati ya mwaka wa 2002 na mwaka wa 2016, takriban hekta milioni 423 au kilomita mraba milioni 4.23 za eneo la nchi kavu duniani - eneo lenye ukubwa wa eneo la Muungano wa Ulaya mzima - ziliteketea, hali iyiyotokea mara kwa mara katika misitu iliyo na miti mbalimbali na mifumo ya ekolojia ya maeneo ya savana.  Takriban asilimia 67 ya eneo jumla linaloteketezwa ulimwenguni kila mwaka kutokana na aina zote za mioto, ikijumuisha mioto misituni, ilitokea barani Afrika.
  • Hali ya mioto hatari misituni inakadiriwa kutokea mara kwa mara, kuwa mikali zaidi na kudumu kwa muda mrefu, ikijumuisha maeneo yaliyoathiriwa hapo awali na mioto. Mioto mikali zaidi misituni inaweza kusababisha ngurumo za radi kutokana na moshi na upepo mkali kwa kasi isiyo ya kawaida na kusababisha miale inayowasha mioto mingine mbali zaidi na sehemu hiyo, na kuzalisha matokeo hatari mno.
  • Hii inatokana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na joto kali na hali ya kiangazi na ukame wa mara kwa mara. Mabadiliko ya matumizi ya ardhi ni tatizo lingine, ikijumuisha ukataji miti ili kupata mbao na shamba la kilimo, kuunda eneo la kulishia migufo na kupanua miji. Chanzo kingine cha kuenea kwa mioto misituni ni uzuiaji mkali wa mioto ya kiasili, ambao ni muhimu katika baadhi ya mifumo asilia ili kupunguza kiasi cha nyenzo zinazoweza kuwaka, na sera zisizofaa za usimamizi wa mioto ambazo hazijumuishi mbinu za kijadi na maarifa ya kiasili ya kusimamia mioto.
  • Athari za muda mrefu kwa afya ya binadamu ni zaidi ya kukabiliana na mioto misituni, kuhamishwa, au kupata hasara. Moshi na chembechembe kutoka kwa mioto misituni huwa na madhara makubwa kwa afya katika makazi ya maeneo upepo huelekea, wakati mwingine maelfu ya kilomita kutoka chanzo, na athari mara nyingi huwa mbaya zaidi kwa walio na magonjwa mengineyo, wanawake, watoto, wazee na maskini. Mabadiliko katika mifumo ya mioto pia yanatarajiwa kusababisha uharibifu mkubwa wa bayoanuai, na kuhatarisha maisha ya zaidi ya spishi 4,400 za nchi kavu na maji yasio na chumvi.
  • Mioto misituni huzalisha kaboni nyeusi na vichafuzi vingine vinavyoweza kuchafua vyanzo vya maji, kuongeza uyeyukaji wa barafu, kusababisha maporomoko ya ardhi na maua makubwa ya mwani katika bahari, na kugeuza viteka kaboni kama vile misitu ya mvua kuwa vyanzo vya kaboni.
  • Ripoti inatoa wito wa uwekezaji mkubwa zaidi wa kupunguza uwezekano wa kutokea kwa mioto misituni; uundaji wa mbinu za kuzuia na kuishughulikia zinazohusisha jamii zilizo hatarini kuathiriwa, za vijijini, za wenyeji na za kiasili; na uboreshaji zaidi wa uwezo wa kutambua mioto kwa umbali, kama vile setilaiti, rada na vitambua miale.   

Mabadiliko ya tabianchi huvuruga ruwaza asilia ya mimea na wanyama

  • Fenolojia ni majira ya hatua za maisha zinazojirudiarudia, zinazoongozwa na hali ya mazingira, na jinsi, ndani ya mfumo wa ekolojia, spishi zinazoingiliana huathiriwa na hali ya mabadiliko. Mimea na wanyama katika mifumo ikolojia ya nchi kavu, majini na baharini hutumia joto, urefu wa siku au kipindi cha mvua kuonyesha wakati wa kuweka matawi, kuweka maua, kuzaa matunda, kuongezeka, kujikunyata, kuchavusha, kuhama au kujibadilisha.  
  • Mabadiliko ya kifenolojia hutokea wakati spishi hubadilisha majira ya hatua fulani maishani kutokana na mabadiliko ya hali ya mazingira kutokana na mabadiliko ya tabianchi.  Tatizo ni kwamba spishi zinazoingiliana katika mfumo wa ekolojia hazishuhudii mababiliko wakati mmoja au kwa kiwango sawa.
  • Mabadiliko haya ya kifenolojia yanazidi kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi, na kufanya  mimea na wanyama kutoingiliana na ruwaza asilia na kusababisha kutoingiliana, kama mimea inapobadilisha hatua za maisha kwa kasi kuliko wanyama walao majani.
  • Wahamiaji wa masafa marefu huathirika zaidi na mabadiliko ya kifenolojia.  Hali ya hewa kwenye eneo ambalo kwa kawaida huchochea uhamaji huenda isiwezekane kubashiri bila kukosea hali ya wanapokwenda na maeneo ya kupumzika njiani. 
  • Mabadiliko ya kifenolojia kwa mimea kukabiliana na kubadilika kwa misimu yatapelekea changamoto kwa uzalishaji wa chakula wakati wa mabadiliko ya tabianchi. Mabadiliko kwa fenolojia ya spishi muhimu baharini kwa biashara na mawindo yao yana athari kubwa kwa uzalishaji na usambazaji wa samaki. 
  • Athari kamili za kutoingiliana kifenolojia zinahitaji utafiti zaidi. Kudumisha makazi mwafaka na kuingiliana kwa ekolojia, kuimarisha uadilifu wa uanuai wa kibayolojia, kuratibu juhudi za kimataifa kwenye njia za wahamaji, kuwezesha ustahimilivu na kudumisha spishi zilizo na jenetiki mbalimbali ni malengo muhimu ya uhifadhi. Zaidi ya yote, kupunguza kiwango cha ongezeko la joto kwa kupunguza uzalishaji wa CO2 ni muhimu.

 

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA)

UNEA ni taasisi kuu duniani inayofanya maamuzi kuhusiana na mazingira, na inayoshughulikia baadha ya masuala nyeti kabisa kwetu. Mwaka huu, mamia ya wafanya maamuzi, mashirika ya biashara, wawakilishi wa mashirika ya serikali na mashirika ya uraia, watakusanyika kwa awamu ya pili ya UNEA-5, kwa makao makuu ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa mjini Nairobi.

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)

UNEP ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira duniani.  Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano wa utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.  

UNEP@50: Wakati wa kutafakari kuhusu yaliyopita na kutazamia yajayo

Kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira ya Binadamu mjini Stockholm, Uswidi katika mwaka wa 1972, ulikuwa mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa kutumia neno "mazingira" kwenye anwani yake kwa mara ya kwanza.  Kuanzishwa kwa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) ni mojawapo wa matokeo makuu ya kongamano hili lilianzisha mambo mengi.  UNEP ilianzishwa kuwa kitengo cha kushughulikia mazingira cha Umoja wa mataifa kote ulimwenguni. Shughuli zitakazoendelea katika mwaka wa 2022 zitaangazia hatua zilizopigwa na yatakayojiri katika miongo ijayo.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:

Keisha Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, UNEP

Moses Osani, Afisa wa Mawasiliano, UNEP