Oktoba 20, 2021 - Ripoti ya Pengo la Uzalishaji ya mwaka wa 2021, ya taasisi kuu za utafiti na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), inaonyesha kuwa licha ya kuongezeka kwa ahadi kabambe za kushughulikia mazingira na kutozalisha gesi chafu, serikali bado zina mpango wa kuzalisha zaidi ya maradufu kiwango cha mafuta ya visukuku katika mwaka wa 2030, kiwango zaidi kuliko kile kinachohitajika kudhibiti kiwango cha joto duniani lisizidi nyuzijoto 1.5.
Ripoti hiyo, iliyozinduliwa kwa mara ya kwanza katika mwaka wa 2019, inapima pengo kati ya mipango ya serikali ya uzalishaji wa makaa ya mawe, mafuta, na gesi na viwango vya uzalishaji wa kimataifa vitakavyowezesha kufikia viwango vya joto vya Mkataba wa Paris. Miaka miwili baadaye, ripoti ya mwaka wa 2021 inaonyesha kuwa pengo la uzalishaji halijabadilika mno.
Kwa kipindi cha miongo miwili ijayo, serikali kwa jumla zinakadiria ongezeko kwa uzalishaji wa mafuta na gesi ulimwenguni, na kupungua kwa kiasi tu kwa uzalishaji wa makaa ya mawe. Kwa ujumla, mipango na makadirio yao kote ulimwenguni yatapelekea uzalishaji wa jumla wa mafuta ya visukuku kuongezeka hadi angalau kufikia mwaka wa 2040, na kufanya pengo la uzalishaji kuzidi kuongezeka kila mara.
"Madhara mabaya ya mabadiliko ya tabianchi yapo na sote tunayashuhudia. Bado kuna mda wa kupunguza ongezeko la joto kwa kipindi kirefu hadi nyuzijoto 1.5, lakini fursa hii inadidimia haraka, " anasema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP. “Kwenye COP26 na baadaye, serikali ulimwenguni zinapaswa kuchukua hatua zaidi, kuchukua hatua za haraka sasa ili kuziba pengo la uzalishaji wa mafuta ya visukuku na kuhakikisha mabadiliko ya haki yasiyobagua. Hivi ndivyo ahadi za mazingira zinapaswa kuwa.
Ripoti ya mwaka wa 2021 ya Pengo la Uzalishaji inatoa maelezo mafupi kuhusu nchi 15 za wazalishaji wakuu: Australia, Brazil, Kanada, China, Ujerumani, India, Indonesia, Meksiko, Norwe, Urusi, Saudia, Afrika Kusini, Milki za Kiarabu, Uingereza, na Marekani. Maelezo mafupi kuhusu nchi yanaonyesha kuwa nyingi ya serikali hizi zinaendelea kutoa msaada mkubwa wa kisera kwa uzalishaji wa mafuta ya visukuku.
"Utafiti huu unaeleweka kwa urahisi: uzalishaji kote ulimwenguni wa makaa ya mawe, mafuta, na gesi lazima uanze kupungua sasa kwa kasi ili kuweza kupunguza ongezeko la joto kwa kipindi kirefu hadi nyuzijoto 1.5,” anasema Ploy Achakulwisut, mwandishi mkuu wa ripoti na mwanasayansi wa SEI. “Hata hivyo serikali inaendelea kuweka mikakati na kuunga mkono uzalishaji wa mafuta ya visukuku kwa kiwango kikubwa na hatari.”
Matokeo makuu ya ripoti hii ni pamoja na:
- Serikali ulimwenguni zinapanga kuzalisha takribani asilimia 110 zaidi ya mafuta ya visukuku katika mwaka wa 2030 kinyume na kinachohitajika ili kudhibiti kiwango cha joto kisizidi nyuzijoto 1.5, na asilimia 45 zaidi ya kiwango kinachohitajika cha nyuzijoto 2. Kiwango cha pengo la uzalishaji kimesalia pakubwa bila mabadiliko ikilinganishwa na tathmini zetu za awali.
- Mipango na makadirio ya serikali ya uzalishaji utapelekea ongezeko la takribani asilimia 240 zaidi ya makaa ya mawe, asilimia 57 zaidi ya mafuta, na asilimia 71 zaidi ya gesi katika mwaka wa 2030 kuliko kiwango kinachohitajika kudhibiti kiwango cha joto duniani lisizidi nyuzijoto 1.5.
- Uzalishaji wa gesi kote ulimwenguni unatarajiwa kuongezeka zaidi kati ya mwaka wa wa 2020 na mwaka wa 2040 kuzingatia mipango ya serikali. Hali ikiendelea hivi, ongezeko la mda mrefu la uzalishaji wa gesi kote ulimwenguni ni kinyume cha Mkataba wa Paris wa kudhibiti ongezeko la joto.
- Nchi zimeelekeza zaidi ya Dola za Marekani bilioni 300 kama ufadhili mpya kuelekea shughuli za mafuta ya visukuku tangu janga la COVID-19 lilipoanza — zaidi ilivyo na nishati isiyochafua mazingira.
- Kwa upande mwingine, ufadhali wa kimataifa kwa umma wa uzalishaji wa mafuta ya visukuku kutoka nchi za G20 na benki kuu za maendeleo za kimataifa (MDBs) umepungua sana katika miaka ya hivi karibuni; theluthi moja ya MDBs na taasisi za ufadhili wa maendeleo za G20 (DFIs) kutegemea mali yake zimepitisha sera ambazo zinaondoa shughuli za uzalishaji wa mafuta ya visukuku kwenye ufadhili katika siku zijazo.
- Habari inayoweza kuthibitishwa na kulinganishwa kuhusu uzalishaji na msaada kwa mafuta ya visukuku - kutoka kwa serikali na kampuni — ni muhimu ili kushughulikia pengo la uzalishaji.
"Juhudi za mapema kutoka kwa taasisi za kufadhali maendeleo za kupunguza msaada wa kimataifa kwa uzalishaji wa mafuta ya visukuku ni za kutia moyo, lakini mabadiliko haya yanahitaji kufuatwa na sera kabambe madhubuti za kuondoa mafuta ya visukuku ili kudhibiti kiwango cha joto duniani lisizidi nyuzijoto 1.5", anasema Lucile Dufour, Mshauri Mwandamizi wa Sera, Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo Endelevu (IISD).
“Mataifa yanayozalisha mafuta ya visukuku lazima yatambue jukumu na wajibu wao katika kuziba pengo la uzalishaji na kutuelekeza kwa mazingira salama katika siku zijazo,” anasema Måns Nilsson, mkurugenzi mtendaji wa SEI. ”Wakati nchi zinapozidi kutoa ahadi za kutozalisha hewa chafu kufikia katikati ya karne, pia zinahitaji kutambua kupunguza kwa kasi kwa uzalishaji wa mafuta ya visukuku kutahitajika ili kufikia malengo ya mazingira.”
Ripoti hiyo imetolewa na Taasisi ya Mazingira ya Stockholm (SEI), Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo Endelevu (IISD), Taasisi ya Maendeleo ya Nje ya Nchi (ODI), E3G, na UNEP. Watafiti zaidi ya 40 walichangia uchanganuzi na uhakiki, kutoka kwa vyuo vikuu kadhaa, taasisi kuu za utafiti mashirika mengine ya utafiti.
MAKALA KWA WAHARIRI
Maoni Kuhusu Ripoti ya Pengo la Uzalishaji
“Matangazo yaliyotolewa hivi karibuni na chumi kubwa zaidi duniani ya kukomesha ufadhili wa kimataifa wa makaa ya mawe ni hatua zinazohitajika ili kukomesha matumizi ya mafuta ya visukuku. Ila, inavyojitokeza kwenye hii ripoti bado kuna mengi ya kufanywa ili kutumia nishati isiyochafua mazingira katika siku zijazo. Ni suala la dharura kwa wafadhili wa umma waliosalia na wafadhili wa sekta ya kibinafsi ikijumuisha benki za biashara na wasimamizi wa mali wagome kufadhili makaa ya mawe na kuanza kufadhili nishati jadidifu ili kuwezesha kutozalisha gesi ya ukaa kwa sekta ya nishati na kuwezesha matumizi ya nishati isiyochafua mazingira kwa wote.”
- António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
“Ripoti hii inaonyesha, kwa mara nyingine tena, masuala yanayoelewa kwa urahisi ila ni nyeti: tunahitaji kuacha kutoa mafuta na gesi ardhini iwapo tunataka kufikia malengo ya Mkataba wa Paris. Ni lazima tutumie mbinu zote, huku tukishughulikia mahitaji na usambazaji wa mafuta ya visukuku kwa wakati mmoja. Hii ndiyo sababu, kwa ushirikiano na Denmark, tunasimamia kuundwa kwa Muungano wa Baada ya Matumizi ya Mafuta na Gesi (Beyond Oil and Gas Alliance ili kukomesha ukuzaji na uchimbaji wa mafuta ya visukuku, kupanga mabadiliko yatakayofanywa na wafanyakazi kwa njia ya haki kwa wafanyakazi na kuanza kuhitimisha uzalishaji uliopo kwa njia bora.”
- Andrea Meza, Waziri wa Mazingira na Nishati wa Costa Rica
“Ripoti ya Pengo la Uzalishaji ya mwaka wa 2021 kwa mara nyingine tena inaonyesha bila shaka kwamba tunahitaji kupunguza uzalishaji wa mafuta ya visukuku ikiwa tunataka kufikia malengo ya Mkataba wa Paris. Kushughulikia hali hii, Denmark imechukua uamuzi wa kutupilia mbali leseni za uchimbaji mafuta na gesi, na kukomesha kabisa uzalishaji wetu kufikia mwaka wa 2050. Kwa ushirikiano na Costa Rica tunahimiza serikali zote kuchukua hatua kama hizi na kujiunga na Baada ya Matumizi ya Mafuta na Gesi ili kukuza ukomeshaji wa uzalishaji wa mafuta ya visukuku chini ya usimamizi bora kwa njia ya haki.”
- Dan Jørgensen, Waziri wa Mazingira, Nishati na na Huduma wa Denmark
Kuhusu Ripoti ya Pengo la Uzalishaji
Ripoti iliyoandikwa kwa kutumia kielelezo cha matoleo ya Ripoti ya Emissions Gap — na kuchukuliwa kama uchanganuzi wa kukamilishana — ripoti hii inaonyesha pengo kubwa liliopo kati ya mipango ya nchi ya uzalishaji wa mafuta ya visukuku na viwango vya kimataifa vya uzalishaji vinavyohitajika ili kudhibiti ongezeko la joto lisizidi nyuzijoto 1.5.
Kuhusu Taasisi ya Mazingira ya Stockholm
Taasisi ya Mazingira ya Stockholm ni taasisi ya kimataifa ya utafiti inayojitegemea inayojishughulisha na masuala ya mazingira na maendeleo katika ngazi ya eneo, ya kitaifa na ya kanda na sera ya kimataifa kwa zaidi ya robo ya karne. SEI huunga mkono maamuzi ya kuleta maendeleo endelevu kwa kutumia sayansi na sera.
Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)
UNEP ni mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano wa utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.
Kuhusu Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo Endelevu
Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo Endelevu (IISD) ni taasisi ya kujitegemea ya utafiti ambayo imewahi kushinda tuzo, inayopigania masuluhisho yanayotokana na utafiti kwa changamoto kuu za mazingira duniani. Dira yetu ni kuwa na dunia isiyobagua ambapo watu na mazingira wananawiri; dhima yetu ni kuharakisha mabadaliko duniani yatakayosababisha matumizi ya maji safi, chumi bora na mazingira dhabiti. Na ofisi mijini Winnipeg, Geneva, Ottawa na Toronto, kazi yetu huathiri maisha ya watu kwenye angalau nchi 100.
Kuhusu Taasisi ya Maendeleo ya Nje ya Nchi (ODI)
Taasisi ya Maendeleo ya Nje ya Nchi ni taasisi ya kimataifa ya utafiti inayojitegemea inayofanya kazi ili kuchochea watu kukabiliana na ukosefu wa haki na ukosefu wa usawa. Kupitia utafiti, kutoa matokeo na kuchochea ODI huzalisha mawazo muhimu kwa watu na sayari.
Kuhusu E3G
E3G ni taasisi ya kimataifa ya utafiti inayojitegemea ya kushughulikia mabadiliko ya tabianchi Ulaya inayohakikisha hali ya hewa inaboreshwa duniani. E3G inajumuisha waundamikakati wakuu kuhusiana na siasa na uchumi kuhusiana na mabadiliko ya tabianchi, inayojitolea kuhakikisha kuwa kuna mazingira salama kwa wote. E3G huunda miungano ya sekta mbalimbali ili kuwa matokeo mazuri, inayochaguliwa kutokana na uwezo wa kuleta mabadiliko. E3G inafanya kazi kwa ushirikiano na wabia wenye nia kama yao kutoka katika serikali, siasa, mashirika ya biashara, makundi ya uraia, sayansi, vyombo vya habari, wakfu za masilahi ya umma na kutoka kwengineko. E3G inawezesha mambo muhimu kutokea.
Kwa taarifa zaiditafadhali waliliana na:
Annika Flensburg, Afisa Mkuu wa Habari, Taasisi ya Mazingira ya Stockholm.
Keisha Rukikaire, Mkuu wa Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa.
Angela Picciariello, Afisa Mwandamizi wa Utafiti, Taasisi ya Maendeleo ya Nje ya Nchi.
Paulina Resich, Afisa Mwandamizi wa Mawasiliano, Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo Endelevu.
Mawasiliano kwa vyombo vya habari kutoka E3G.