Nairobi, Septemba 19, 2022 – asilimia 78 ya wakazi barani Afrika husafiri kwa miguu na kutumia baiskeli kila siku, ila hali ngumu, hatari na zisizofaa huchangia kuongezeka kwa kasi kwa idadi ya magari katika miji na kuongezeka kwa idadi ya vifo barabarani. Hali iliyo na athari kubwa kwa afya ya watu na kwa mazingira: Watu wanaotembea 261 na waendeshaji wa baiskeli 18 huuawa kila siku barabarani, mbali na zaidi ya vifo 258,000 kila mwaka kutokana na uchafuzi wa hewa. Matokeo haya yanapatikana katika ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo, ambayo inapendekeza sera na uwekezaji wa kulinda na kusaidia Waafrika wanaosafiri kwa kutembea na kuendesha baiskeli – mara nyingi kwa kukosa njia mbadala.
Ripoti hiyo, Kutembea na Kuendesha Baiskeli barani Afrika - Ushahidi na Mazoea Bora ya Kuhamasisha Kuchukuliwa kwa Hatua, na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Makazi ya Binadamu (UN-Habitat), na Wakfu wa Walk21, ni ya kwanza kukusanya na kuchambua data kuhusu suala hili kwa kuzingatia mazingira mbalimbali katika nchi zote 54 barani Afrika. Utayarishaji wa ripoti hiyo ulifadhiliwa na Urban Pathways Project na Wakfu wa FIA. FIA ilishirikiana na UNEP kuzindua Programu ya Tumia Njia Pamoja na Wanaotembea na Kuendesha Baiskeli mwaka wa 2008.
Inaonyesha kuwa Mwafrika mmoja kati ya watano hutembea au kuendesha baiskeli kwa wastani dakika 56 kwa siku - mara 12 zaidi ya wastani ya kimataifa. Ijapokuwa watu hushauriwa kufanya mazoezi na Shirika la Afya Duniani, viwango vya juu vya mazoezi kupitia usafiri vinaweza pia kuashiria uhaba wa zana za usafiri wa umma na mpangilio mbaya wa matumizi ya ardhi.
Ripoti hiyo pia inachanganua data kuhusu ubora wa barabara zinazotumiwa na wanaotembea na kuendesha baiskeli na kiwango chao cha kuridhika na kufuraia sera zilizopo. Kwa upande wa usalama, takribani asilimia 95 ya barabara zilizotathminiwa zimekadiriwa kuwa duni kwa wanaotembea na wanaoendesha baiskeli na Mpango wa Kimataifa wa Kutathmini Barabara (iRAP) zilizofanyiwa utafiti kwa kuzingatia viwango vya usalama - na kufanya Afrika kuwa bara hatari zaidi duniani kwa watembeao na waendeshaji wa baiskeli. Kwa kuongeza, chini ya Mwafrika mmoja kati ya watatu huishi umbali wa kilomita 1 kutoka kwa usafiri wa umma – idadi ya chini zaidi duniani. Hii inasababisha kutoridhika kwa umma, kuongezeka kwa magari ya kibinafsi huku viwango vya mapato vikipanda na kuongezeka kwa viwango vya uchafuzi wa hewa - chanzo cha pili kikuu cha vifo barani.
Ili kunufaika kabisa kutokana na kutembea na kuendesha baiskeli, sera za serikali ni sharti zifanye kutembea na kuendesha baiskeli kuwa salama kwa wote. Ripoti hiyo inatoa wito kwa:
- Ulinzi zaidi kwa wanaotembea na kwa waendeshaji wa baiskeli, kwa kuzingatia mahitaji maalum ya wanawake, watoto na watu wenye ulemavu;
- Uwekezaji katika miundomsingi ya kutosha, ikijumuisha vivuko salama barabarani, njia pana zaidi za watembeaji na njia salama za baiskeli, kivuli, maeneo salama ya kuegesha baiskeli, mwangaza, na upatikanaji rahisi wa usafiri wa umma;
- Ukusanyaji bora wa data, ikiwa ni pamoja na kuchora ramani za vituo vya usafiri wa umma, data ya ajali na majeruhi, kushauriana na jamii kuhusu sera na michakato ya kuunda barabara kuu, na kukadiria kuridhika kwa umma.
"Ripoti hii inaangazia umuhimu wa uwekezaji endelevu ili kuboresha miundomsingi ya usafari kwa wanaotembea na kutumia baiskeli ili kukumbatia utofauti na ujumuishwaji, kuimarisha kuunganishwa na miifumo mingine ya usafiri, kuimarisha usalama barabarani na kuimarisha maisha kwa wakaazi wengi wa mijini kwa njia endelevu" alisema Prof. Manuel de Araújo, Meya wa Quelimane, Msumbiji - mji uliojumuishwa kwenye mradi wa Reclaiming Streets. "Hatua anuai zinaonyesha athari chanya za muda mfupi na mda mrefu na kufanya miji yetu na watu kuwa thabiti, wachangamfu, salama na wenye afya."
Ripoti hiyo inaonyesha hatua zilizopigwa mjini Addis Ababa na mipango ya zaidi ya kilomita 1000 za ardhi ya njia za wanaotembea na kuendesha baiskeli, mjini Yaoundé, na kuhitajika kwa kila jengo kuweza kufikiwa na wanaotembea kwa miguu, na jijini Nairobi, na ahadi zake za kutenga asilimia 20 bajeti yake ya uwekezaji katika miundomsingi ya wanaotembea na kuendesha baiskeli, na pia kwingineko nchini Ghana, Senegal, na Zambia.
"Kuweka mikakati ya miundomsingi kunaweza kuimarisha usalama, afya na kufarahisha zaidi ya watu bilioni moja barani, wakati uo huo kukidumisha kiwango cha chini cha gesi ya ukaa barani Afrika," alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP. "Mabadiliko ya kutumia usafiri salama na endelevu – yakiongozwa na viongozi wa miji barani Afrika - yanaweza kuunda miji bora zaidi, yenye usawa na inayostawi ustawi."
Tangu kuanza kwa janga la COVID-19, kumekuwa na ongezeko duniani la idadi ya watu wanaotembea na kuendesha baiskeli. Hii ni kutokana na mienendo ya miaka ya hivi karibuni katika miji ambayo imetoa kipao mbele kwa barabara za wanaotembea na kutumia baiskeli katika mikakati usafiri mijini. Kwa ujumla, licha ya hatua za kutia moyo katika bara zima, Afrika imebakia nyuma: ni nchi 19 tu (asilimia 35) ndizo zina sera kuhusu kutembea na kuendesha baiskeli na mikati kwa ujumla bado haizingatii wala kujumuisha watu wote.
“Kuna fursa ya kipekee ya kubadili jinsi tunavyoweka mikakati na kupanga miji yetu. Kwa kuzingatia maendeleo ya kimataifa wakati wa COVID-19 wakati miji ilipopanua maeneo ya kutembelea, ya kuendesha baiskeli na maeneo ya umma, ningependa kutoa wito kwa watoa maamuzi barani Afrika kukumbatia mafunzo kutoka kwa ripoti hii," Maimunah Mohd Sharif, Mkurugenzi Mtendaji wa UN Habitat alisema. “Uwekezaji katika kutembea na kuendesha baiskeli barani Afrika ni uwekezaji kwa watu. Hakuna suluhisho lingine kwa gharama nafuu zaidi la kufikia malengo ya usalama barabarani na hali ya hewa kwa wakati mmoja."
Na sera na rasilimali za kutosha, Afrika ambayo inapendelea kutembea na kuendesha baiskeli inaweza kupunguza gharama za msongamano, ajali na vifo barabarani, pamoja na kuboreshwa kwa hali ya hewa, afya na usalama wa umma. Haya yatapelekea kupiga hatua nyingi za Malengo ya Maendeleo Endelevu, ikijumuisha kupunguza vifo na kuboresha maisha (SDG 3: afya njema na ustawi), ukosefu wa usawa (SDG 10: kupunguza ukosefu usawa), uboreshaji wa hali ya hewa na kupunguza uzalishaji wa gesi chafu. (SDG 13: hatua za kushughulikia mazingira), na miundomsingi dhabiti zaidi (SDG 11: miji na jamii endelevu).
Kufuatia ripoti hii, UNEP inasimamia uundaji wa Ramani ya Barabara Barani Afrika kwa Usafiri Hai kwa nia ya kupata uungwaji mkono wa mawaziri kutoka nchi zote 54 za Afrika kufikaa mwishoni mwa mwaka wa 2023.
MAKALA KWA WAHARIRI
Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)
UNEP ni mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira ulimwenguni. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.
Huhusu Wakfu wa Walk21
Walk21 ni shirika la kimataifa la kutoa misaada linalojitolea kuhakikisha kuna haki ya kutembea na kufurahia kutembea huko. Walk21 hupigania ukuzaji wa jamii zenye afya, endelevu na fanisi ambapo watu huamua kutembea.
Kuhusu UN Habitat
UN-Habitat ni shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia makazi ya watu. Lina programu katika zaidi ya nchi 90 zinazosaidia watu katika miji na kutoa makazi kwa watu na lengo la kuwa na miji endelevu inayojali jamii na mazingira.
Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:
Keisha Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa,
Katerine Bezgachina, Mkuu wa Mawasiliano, UN-Habitat