Nairobi, Octoba 20, 2020 - Mamilioni ya magari yaliyowahi kutumika ikijumuisha motokaa, magari ya mizigo na basi ndogo yanayouzwa kutoka Ulaya, Marekani na Japan hadi kwa nchi zinazoendelea huwa ya kiwango duni na huchangia mno katika uchafuzi wa hewa na hivyo kuwa kizingitia cha kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kwa mjibu wa ripoti mpya kutoka kwa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP).
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa kati ya mwaka wa 2015 na mwaka wa 2018, magari milioni 14 yaliyowahi kutumika kwa mda yaliuzwa nje ya nchi kote duniani. Asilimia 80 yaliuzwa kwa nchi za kipato
Magari Yaliyowahi Kutumika na Mazingira - Maelezo ya Jumla kuhusu Magari Yaliyowahi Kutumika, Kiwango Chake na Sheria, ripoti ya kwanza ya aina yake, inatoa wito wa kuchukua hatua ya kutunga sera zinazokosekana kwa kuweka viwango vya chini vinavyohitajika ili kuhakikisha magari yaliyowahi kutumika hayachafui mazingira na ni salama kwa nchi yanayouzwa.
Ongezeko la mkusanyiko wa magari huchangia mno kwenye uchafuzi wa hewa na mabadiliko ya tabianchi; kote ulimwenguni, sekta ya uchukuzi huchangia takribani robo ya uzalishaji wa gesi chafu inayosiana na gesi ya ukaa. Hasa, uzalishaji wa gesi kutoka kwa magari ndicho chanzo kikuu cha chembechembe laini za (PM2.5) na nitrojeni oksidi (NOx) ambazo ni chanzo kikuu cha uchafuzi mijini..
"Kuhakikisha hakuna uchafuzi kutokana na mkusanyiko wa magari ni suala nyeti ili kukidhi kiwango cha hewa kinachohitajika na kufikia malengo ya hali ya hewa," alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP. "Miaka kadhaa iliyopita, idadi ya nchi zilizoendelea zinazouza magari yaliyowahi kutumiwa nje ya nchi imeongezeka; kwa sababu hali hii hutokea bila sheria na kupelekea kuuzwa kwa magari yanayochafua mazingira nje ya nchi."
"Kutokuwepo kwa sheria na kanuni za kufuatwa kunapelekea kuwepo na dampo la magari makuukuu, yanayochafua mazingira na yasiyo salama," aliongezea. "Nchi zilizoendelea ni sharti zisitishe kuuza magari yasiyojali mazingira nje ya nchi na kuyakagua iwapo ni salama na si eti hayaruhusiwi tena kwenye barabara zao. Nchi zinazopokea magari haya ni sharti zitunge sheria dhabiti ya kuhakisha zinapokea magari ya viwango vya juu.
Ripoti hiyo, kwa kuzingatia uchanganuzi uliofanywa kwa nchi 146 ilibaini kuwa theluthi mbili ya sera za kudhibiti magari kutoka nje ya nchi zilikuwa 'dhaifu' au 'dhaifu kabisa'. Hata hivyo, inaonyesha kuwa katika nchi ambazo zina sheria za kuongoza ununuzi wa magari kutoka nje ya nchi – hasa sheria kuhusiana na uchafuzi na miaka iliyopita tangu gari lilipotengenezwa – imewawezesha kupokea magari yaliyowahi kutumika ya viwango vya juu, ikijumuisha magari ya kisasa na yale yanayotumia umeme kwa gharama ya chini. Kwa mfano, nchi ya Moroko huruhusu tu ununuzi wa magari kutoka nje ya nchi yasiyozidi miaka mitano tangu yalipotengenezwa na yale yanayokidhi vigezo vya EURO4 Viwango vilivyowekwa na ulaya kuhusu uchafuzi; kwa hivyo, wao hupokea tu magari ya viwango vya juu na yasiyochafua mazingira kutoka Ulaya.
Ripoti hiyo ilibaini kuwa, nchi za Afrika zilinunua magari mengi mno yaliyowahi kutumika (asilimia 40) wakati wa utafiti uliofanywa, ikifuatiwa na nchi kutoka Uropa Mashariki (asilimia 24), Asia ya Pasifiki (asilimia 15), Mashariki ya Kati (asilimia 12) na Amerika ya Latini (asilimia 9)
Kupitia kwa bandari zake, Uholanzi ni mojawapo ya nchi barani Ulaya zinazouza magari nje ya nchi. Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Uholanzi kuhusu magari nchi hiyo huuza nje ya nchi ulibaisha kuwamengi ya magari hayo hayakuwa na cheti cha kuonyesha kuwa yalikuwa salama barabarani wakati yalipokuwa yanauzwa. Mengi ya magari hayo, tangu yalipotengenezwa yalikuwa yamemaliza kati ya miaka 16 na 20, na mengi hayakukidhi viwango vilivyowekwa na Ulaya kuhusu uchafuzi. Kwa mfano, wastani wa miaka ya magari yaliyowahi kutumika yaliyouzwa katika nchi ya Gambia ilikuwa miaka 19, huku robo ya magari yaliyouzwa nchini Nigeria ikiwa takribani wastani ya miaka 20.
"Matokeo haya ni idhibati kuwa hatua za dharura zinahitajika ili kuboresha ubora wa magari yanayouzwa nje ya Ulaya. Uholanzi pekee yake haiwezi kushughulikia suala hili. Kwa hivyo, ninatoa wito kwa Ulaya kuweka utaratibu utakaotumika, na kuwepo kwa ushirikiano wa karibu kati ya serikali za Ulaya na serikali za Afrika ili kuhakikisha kuwa EU inasafirisha tu nje ya nchi magari mazuri, yanayokidhi viwango vilivyowekwa na nchi magari hayo huuzwa kwazo" Stientje Van Veldhoven, Waziri wa Mazingira wa Uholanzi, alisema.
Magari mabovu yaliyowahi kutumika husabashi ajali nyingi za barabarani. Kwa mjibu wa ripoti hiyo, nyingi ya nchi zilizo na sheria 'dhaifu' au 'dhaifu kabisa' kuhusu magari yaliyowahi kutumika, ikijumuisha Nigeria, Zimbabwe, and Burundi, pia huwa na kiwango cha juu cha vifo vinavyotokana na ajali za barabarani. Nchi ambazo zimebuni sheria kuhusu magari yaliyowahi kutumika hupokea idadi kidogo ya magari na hushuhudia kiwango kidogo cha ajali.
UNEP, kwa ushirikiano na Mfuko wa UN Road Safety Trust na wadau wengineo, ni sehemu ya mradi mpya unaounga mkono kuwekwa kwa viwango vya wastani kwa magari yaliyowahi kutumika. Mradi huo kwanza utalenga nchi barani Afrika; nchi kadhaa barani Afrika tayari zimeweka viwango vya chini vya ubora; – ikijumuisha Moroko, Algeria, Côte d'Ivoire, Ghana na Mauritius – nchi zingine nyingi zimeonyesha nia ya kujiunga na mradi huu.
"Madhara yanayotokana na magari kuukuu yaliyowahi kutumika yako wazi. Data inayoonyesha ubora wa hewa mjini Accra inadhibitisha kuwa uchukuzi ndicho chanzo kikuu cha uchafuzi wa hewa mijini. Hii ndiyo sababu inayoifanya nchi ya Ghana kutoa kapaumbele kwa nishati isiyochafua mazingira, ikijumuisha fursa za kutumia mabasi yanayotumia umeme. Ghana ilikuwa nchi ya kwanza Afrika Magharibi kuanza kutumia fueli iliyo na kiwango cha chini cha Salfa na mwezi huu imeweka sheria zitakayoruhusu ununuzi wa magari kutoka nje yasiyozidi miaka 10 tangu yalipotengenezwa," alisema Prof. Kwabena Frimpong-Boateng, Waziri wa Mazingira, Sayansi, Teknolojia na Uvumbuzi wa Ghana.
Mwezi jana, Jumuiya ya Uchumi wa Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) zimeweka viwango vya magari na matumizi ya fueli isiyichafua mazingira vitakavyoanza kufanya kazi mwezi wa Januari mwaka wa 2021. Nchi wanachama wa ECOWAS zilihimiza pia kudhibiti miaka kwa magari yaliyowahi kutumika.
Ripoti hiyo inapendekeza utafiti zaidi kufanywa ili kuonyesha athari za magari yaliyowahi kutumika ikijumuisha magari makubwamakubwa.
MAKALA KWA WAHARIRI
Magari mepesi (LDVs) ni yepi ?
Kwa jumla magari aina ya LDVs hayazidi uzani wa tani 3.5, na yanajumuisha motokaa, SUVs na mabasi madogomadogo. Magari yanayozidi uzani wa tani 3.5 hurejelewa kama Magari Mazito (HDVs) na yanajumuisha malori mbalimbali na mabasi.
Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa
UNEP in mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.
Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:
Keisha Rukikaire,Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa rukikaire@un.org