- Tuzo la Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) la Mabingwa wa Dunia hutolewa kwa watu binafsi, makundi ya watu na mashirika ambayo matendo yao yameleta mabadiliko chanya kwa mazingira.
- Mapendekezo ya watakaowania mwaka huu yanakubaliwa tangu tarehe 28 Januari hadi tarehe 12 Februari 2021.
Nairobi, Januari 28, 2021 – Umoja wa Mataifa (UN) leo ulitoa wito wa kupendekeza majina ya watakaoshiriki katika tuzo lake la Mabingwa wa Dunia – tuzo la ngazi ya juu linalotolewa kwa watu binafsi na mashirika yanayotunza mazingira yetu na kuleta mabadiliko katika jamii.
Wito wa kupendekeza watakaoshiriki umetolewa mwezi mmoja baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kutoa onyo kuwa binadamu wametangaza vita dhidi ya mazingira kupitia uharibifu wa bayoanuai, kudidimia kwa mifumo ya ekolojia, uchafuzi wa hewa na maji, hali inayopelekea vifo vya mamilioni ya watu na hali ya mabadiliko ya tabianchi inayozidi kuwa mbaya kutokana na mioto na mafuriko.
Kwa kipindi cha miaka 15 iliyopita, tuzo la Mabingwa wa Dunia limekuwa likiangazia kazi inayofanywa na watu binafsi na mashirika ambayo yamejitolea kufanya kazi ili kuboresha sayari ili kutokuwa na ubaguzi na kuifanya kuwa endelevu. Washindi wameshirikisha wakuu wa nchi, wahamasishaji katika jamii, wakuu wa kampuni na wanasayansi waanzilishi.
Idadi kubwa ya watu ilipendekezwa katika mwaka wa 2020 kuliko mwaka mwingine wowote; hii ni idhibati ya kuongezeka kwa watu wanaojitolea kushughulikia mazingira. Washindi wa tuzo la Mabingwa wa Dunia 2020 ni:
- Waziri Mkuu Frank Bainimarama kutoka Fiji, aliyetuzwa katika kitengo cha Uongozi Unaozingatia Sera kwa juhudi zake za kimataifa za kushughulikia mazingira na kujitolea kwake kuweka mikakati ya kitaifa ya kushughulikia mazingira
- Dkt. Fabian Leendertz (Ujerumani), alituzwa katika kitengo cha Sayansi na Ubunifu kutokana na uvumbuzi wake kuhusiana na magonjwa kutoka kwa wanyama na kazi yake kwenye One Health
- Mindy Lubber (Marekani), alituzwa katika kitengo cha Maono ya Ujasiriamali kwa kujitolea kwake kuhimiza wawekezaji kuwekeza kwenye kampuni zisizochafua mazingira na kuwajibisha mashirika ya biashara kushughulikia mazingira na kuwa endelevu
- Nemonte Nenquimo (Ecuador), alituzwa katika kitengo cha Motisha na Kuchukua Hatua kwa kuwa mstari mbele kushirikiana na jamii za kiasili, hali iliyowezesha kusitisha uchimbaji wa visima kwenye misitu ya Amazon nchini Ecuador
- Yacouba Sawadogo (Burkina Faso), aliyetuzwa pia katika kitengo cha Motisha na Kuchukua Hatua kwa kuwafundisha wakulima njia zake za kiasili zinazojali mazingira za kuboresha mchanga wao na kuwezesha ardhi yao mbovu kutumika kwa kilimo na kupanda misitu barani Afrika
Washindi wa mwaka huu wanashirikisha Professor Robert D. Bullard (Marekani) aliyetuzwa tuzo la Mabingwa wa Dunia katika kitengo cha Mafanikio ya Kudumu kwa kujitolea kwake kuhakikisha kuwa mazingira yanafanyiwa haki.
Yeyote anaweza kupendekeza, awe mtu binafsi, taasisi za serikali, kampuni au mashirika. Makataa ya kupendekeza ni Februari 12, 2021.
Pendekeza Bingwa wa Dunia hapa.
MAKALA KWA WAHARIRI
Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa
UNEP ni mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira duniani. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.
Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:
Keishamaza Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, UNEP, +254717080753