Wakati mwingi katika mwezi uliopita Flipflopi, mashua iliyotengenezwa kutoka kwa plastiki iliyowahi kutumika, imekuwa ikizunguka ziwa kubwa zaidi barani Afrika, ikipambana na upepo mkali na mvua kubwa ili kuhamasisha kuhusu uchafuzi wa mazingira.
Wiki iliyopita, safari hiyo ilikamilika wakati meli hiyo yenye urefu wa mita 10 ilipoingia Mwanza, Tanzania, kituo cha mwisho katika safari yake kupitia nchi tatu ya kilometa 850 kwenye Ziwa Victoria.
Wakati wa safari hiyo, ambayo kwa kwa kiasi fulani ilifadhiliwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), kikosi cha Flipflopi kilikutana na wanasiasa, wanaharakati na maelfu ya watu wa kawaida ili kukuhamasisha kuhusu janga la plastiki kwenye Ziwa Victoria.
"Ninajivunia kuona jinsi ambavyo kampeni hii imeleta pamoja wadau na watoa maamuzi na kuimarisha mazungumzo ya kikanda kuhusu uchafuzi wa plastiki," alisema nahodha wa Flipflopi, Ali Skanda. “Sasa ni wakati wa kufanya mabadiliko yanayohitajika ili kuzuia wimbi la plastiki kabisa.
Jamii nyingi karibu na Ziwa Victoria, ambazo pwani zake ni makazi kwa watu milioni 40, kwa muda mrefu wamekuwa na tatizo la jinsi ya kutupa mifuko chupa na vyombo vya plastiki. Nyingi ya hizo plastiki zinazotumiwa tu mara moja, ikijumuisha ongezeko la barakoa na glavu, huishia katika Ziwa Victoria. Baada ya muda, takataka hizo zinaweza kuvunjikavunjika na kujipata katika mifumo ya chakula. Kiwango halisi cha uchafuzi wa plastiki bado hakijulikani, lakini utafiti mmoja uligundua kuwa asilimia 20 ya samaki katika Ziwa Victoria walikuwa na plastiki mwilini mwao.
“Kuna ushahidi dhahiri kwamba ekolojia ya Ziwa Victoria inashuhudia shinikizo kubwa mno. Ziwa hili lina jukumu kuu la kuwezesha maisha ya jamii katika ukanda wa Afrika Mashariki. Natoa wito kwa serikali za Kenya, Tanzania na Uganda kuimarisha ushirikiano wao ili kuimarisha uboreshaji wa malighafi hii muhimu. UNEP na wabia wake wako tayari kutoa msaada unaohitajika ili kufanikisha jambo hili," alisema Juliette Biao Koudenoukpo, Mkurugenzi wa UNEP na Mwakilishi wa Eneo la Afrika.
Flipflopi - iliyopata jina lake kutoka kwa ndara zilizo na rangi nyingi zilizowekwa kwenye sehemu yake ya nje na sakafuni- imeundwa ili kuonyesha jamii kile kinachoweza kufanywa na plastiki ambayo ingetupwa. Chombo chenye mizani tani saba, sehemu ya chini, na sehemu nyinginezo zimetengenezwa kutoka kwa mifuko za plastiki na chupa za plastiki kutoka fukwe za Lamu nchini Kenya, ambapo kilijengewa.
Mapema mwaka huu, Flipflopi ilifungwa kwenye lori na kusafirishwa kilometa 500 kwenda kupitia bara hadi mjini Kisumu nchini Kenya kwenye mwambao wa Ziwa Victoria. Kikosi chake, mchanganyiko wa mabaharia, wanasayansi na wanaharakati wa mazingira, walianza safiri yao tarehe 8 mwezi wa Machi, safari ambayo wakati mwingine ilikuwa hatari. Ziwa Victoria, ambalo ni kilomita 70,000 mraba, ni maarufu kwa hali mbaya ya hewa na hupelekea vifo vya hadi watu 5000 kwa mwaka, kwa mjibu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani. Wakati ilipookolewa kutokana na madhila yanayoweza kutokea kwenye ziwa hilo, Flipflopi ilikumbwa na upepo mkali na kufunikwa na mvua nzito, kikosi chake hakikuweza kuona mashua ya kuwasaidia iliyokuwa mita chache tu, alisema Dipesh Pabari, mwanzilishi mwenza wa mradi wa Flipflopi.
Ninajivunia kuona jinsi ambavyo kampeni hii imewaleta pamoja wadau na watoa maamuzi.
Bado, mashua ilipendeza, alisema Pabari, na kwa wiki nne zijazo, itasimama katika jamii nchini Kenya, Uganda na Tanzania, ikihubiri kuhusu umuhimu wa kutokomeza plastiki zinazotumiwa mara moja. Wakati wa safari hiyo, kaunti kadhaa za maeneo ya ziwa nchini Kenya zilijitolea kupiga marufuku matumizi ya plastiki zinazotumiwa mara moja. Pabari alisema kuwa Flipflopi pia ilikuwa mfano mzuri kwa jamii kuhusu kile kinachoweza kufanywa na plastiki iliyowahi kutumika.
"Ikiwa unaweza kujenga mashua kutoka kwenye mswaki wako, inaonyesha ni bidhaa muhimu mno." Lakini katika maeneo mengi mno, anasema, plastiki imetumiwa "vibaya."
Hali katika Ziwa Victoria ni sehemu ya janga la uchafuzi wa plastiki kwa jumla linaloikumba sayari, wataalam wanasema. Ulimwenguni kote, chupa za plastiki za maji ya kunywa milioni moja hununuliwa kila dakika na mifuko trilioni 5 ya plastiki inayotumiwa mara moja hutumika kila mwaka. Ni sehemu ndogo tu ya plastiki hiyo hutumika tena na tani milioni 8 za hiyo plastiki huishia kwenye bahari ulimwenguni kila mwaka.
Hakuna "njia ya pekee" ya kukomesha uchafuzi wa plastiki, alisema Heidi Savelli-Soderberg, ambaye anaongoza kikosi cha UNEP cha takataka ya baharini. Alisema nchi zinahitaji kushirikiana kushughulikia tatizo hili linalovuka mipaka.
"Hatuna uwezo wa kudhibiti taka za plastiki zilizopo. Hali itazidi kuwa mbaya iwapo hatutachukua hatua madhubuti kwa dharura. "
Usafiri wa Flipflopi ulifadhiliwa na serikali za Kenya, Uganda na Tanzania, Shirika la Maendeleo la Ufaransa, UN Live, mashirika ya sekta binafsi, ikijumuisha Waterbus, na Kampeni ya Bahari Safiya UNEP.
Kwa UNEP, mradi huo ni sehemu ya juhudi za kupunguza uchafuzi wa mazingira katika Ziwa Victoria, chanzo kikuu cha Mto Nile, maji ambayo hutumiwa na mamia ya mamilioni ya watu.
Baada ya kutia nanga mjini Mwanza nchini Tanzania, Flipflopi ilisafirishwa kwa lori kilomita 1,500 kwenda mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania, Dar Es Salaam, safari kupitia barabara mbaya ambayo Pabari alisema ilimpa "mvi kadhaa." Boti hiyo itakaa hapo kwa mfululizo wa hafla kabla ya safari yake ya mwisho kakupitia Bahari ya Hindi hadi bandari ya Lamu ambayo ni makazi yake.