Karakana ndogo ya Nzambi Matee mjini Nairobi nchini Kenya imejazwa mabomba ya chuma na vyuma kutoka kwa mashine.
Wasioelewa wanaweza kustaajabu ila kwa kwa Matee, mwenye umri wa miaka 29, mvumbuzi na mjasiriamali, vitu hivyo viko salama hapo. Hapa ndiko alikotengeneza kielelezo cha mashine kinachobadili plastiki iliyotupwa kuwa mawe ya kujengea njia ya wapitao kwa miguu - uvumbuzi mkuu wa kampuni yake, Gjenge Makers.
Kila siku, kampuni hiyo hutengeneza vibamba 1,500 vya plastiki, vinavyonunuliwa na shule na wamiliki wa majumba kwa sababu vinadumu na vinapatikana kwa bei nafuu. Kampuni ya Gjenge Makers inafanya chupa na vyombo vingine vya plastiki kuweza kutumika tena na kutoingia ardhini, au hata kusambaa kwenye barabara kuu mjini Nairobi.
"Ni jambo la kushangaza kuwa bado tunakumbwa na tatizo la kupata makazi mazuri - yanayohitajika mno kwa binadamu," alisema Matee. "Plastiki hutumiwa vibaya na wengi hawajaielewa. Ni muhimu mno, lakini ikishamaliza kutumika inaweza kuwa hatari mno kwa maisha.
Kampuni ya kutengeneza vibamba ya Gjenge imeithinishwa na Shirika la Kutathmini Ubora wa Bidhaa nchini Kenya. Huyeyuka kwa kiwango cha joto zaidi ya nyuzijoto 350, na ni dhabiti ikilinganishwa na matofali.
Kutokana na kazi yake, hivi karibuni Matee alitangazwa kuwa mshindi wa tuzo la Vijana Bingwa Duniani linalotolewa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP). Tuzo hilo hutoa ufadhili ili kupata hisa kwa kampuni na ushauri kwa vijana wanaharakati wa mazingira wanapoendelea kukabiliana na changamoto kuu zinazoikumba dunia.
"Ni sharti tutafakari jinsi tunavyozalisha viwandani na jinsi tunavyofanya bidhaa tunapomaliza kuzitumia," alisema Soraya Smaoun, mtalamu wa UNEP kuhusiana na mbinu za uzalishaji. "Uvumbuzi wa Nzambi Matee kwenye sekta ya ujenzi inaoyesha fursa zilizopo kwa uchumi na kwa mazingira tutakapoacha tu kutumia bidhaa mara moja na kuzitupa na kufanya bidhaa kuendelea kutumika kwa kipindi kirefu iwezekanavyo."
Maafa makubwa kutokana na plastiki
Plastiki inapatikana kote ulimwenguni. Kote ulimwenguni, chupa za maji ya kununuliwa milioni 1 hununuliwa kila dakikatrilioni 5 za mifuko ya plastiki inayotumiwa mara moja tu hutumika kwa mwaka.
Matee, aliyosomea taaluma kuu ya sayansi ya vifaa na aliyefanya kazi kama mhandisi katika sekta ya mafuta nchini Kenya, alishawishika kuzindua kampuni yake baada ya kukutana mara kwa mara na plastiki kwenye barabara kuu nchini Nairobi.
Katika mwaka wa 2017, Matee alijiuzulu kama mchanganuzi wa data na akafungua maabara ndogo nyumbani kwa mamake. Hapo, alianza kuunda na kufanyia majaribio vibamba vinavyotengenezwa kwa kuchanganya plastiki na mchanga. Majirani walilalamika kuhusu kelele kutoka kwa mashine alizokuwa anatumia, na kwa hivyo Matee akawaomba wavumilie kwa kipindi cha mwaka mmoja ili akaelewe kiiwango cha kuchanganya wakati wa kuchanganya matofali ya kujengea maeneo ya waotumia miguu.
"Sikutangamana na watu kwa kipindi cha mwaka mmoja, na nikatumia hela zote nilizokuwa nikiweka kufanya kazi hii," alisema. "Rafiki zangu waliingiwa na wasiwasi."
Kwa kujaribujaribu, yeye na wenzake waligundua kuwa baadhi ya plastiki ilishikana vizuri kuliko ingine. Mradi wake ulipigwa jeki wakati Matee alipopata ufadhili kushiriki programu inayotoa mafunzo kwa wajasiriamali katika jamii nchini Marekani. Huku akiwa amebeba baadhi ya vabamba vyake aliposaafiri, alitumia maabara ya vifaa katika Chuo Kikuu cha Colorado Boulder kufanyia majaribio zaidi na kuboresha viwango vya mchanganyiko wa mchanga na plastiki.
Matee pia alitumia fursa hii kuunda mashine ambayo angetumia kutengeneza matofali yale. "Pindi tunapofahamu kutengeneza kibamba kimoja, tunahitaji maarifa ya kutengeneza vibamba 1000," alieleza.
Kukamilisha kazi
Matee anakumbuka siku aliyofaulu kutengeneza kikamilifu vibamba kutoka kwa plastiki. "Ni siku ambayo sitawahi kuisahau!" alimaka. "Ni baada ya kujaribu kwa kipindi cha miaka mitatu. Niliacha kazi yangu. Nikatumia hela zote nilizokuwa nimehifadhi. Nilipungukiwa na pesa kiasi kwamba kila mtu alidhani kuwa nilikuwa nimepagawa na kwa hivyo wengi wao wakanishauri niachane na kazi hii."
Mojawapo ya shule zinazotumia vibamba ni Kituo cha Mafunzo ya Ufundi cha Mukuru (Mukuru Skills Training Centre) kinachopatikana kwenye kitongoji duni cha Mukuru Kyaba. Maeneo yake ya watoto kuchezea na njia zinazopatikana kati ya darasa moja na lingine yamewekwa vibamba maridadi vilivyotengenezwa na Matee. (Kabla ya kuwekwa vibamba, wanafunzi walitembea kwenye njia zilizokuwa na vumbi.)
"Tuna nia ya kuweka vibamba kila mahali shuleni," alisema mratibu wa programu, Anne Muthoni. "Si ghali na tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Nzambi. Vijana wanapaswa kutiwa motisha na kuhamasishwa kuhusu jinsi ya kutunza mazingira, huku wakijitengenezea pesa.
Matee huhimiza vijana kukabiliana na changamoto za mazingira kwenye maeneo wanayotoka. "Athari ghasi tunayosababisha kwa mazingira ni kubwa," alisema Matee. "Ni wajibu wetu kuboresha hali iliopo. Anza na suhuhu yoyote inayopatikana mahali ulipo na uendelee pasipo kuchoka. Utafurahia matunda yake."
Tuzo la Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa la Mabingwa wa Dunia na lile la Vijana Bingwa Duniani hutolewa kwa watu binafsi, makundi na mashirika ambayo juhudi zao zimesababisha mabadiliko chanya kwa mazingira.
Tuzo la Mabingwa wa Dunia linalotolewa na Umoja wa Mataifa ni tuzo la ngazi ya juu linalolenga kuwashirikisha vijana kwenye utatuzi wa changamoto kuu zinazokumba mazingira. Nzambi Matee ni mmoja wa washindi saba waliotangazwa mwezi wa Disemba mwaka wa 2020, tunapoelekea Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia, 2021-2030.
Kwa kuhamasisha kuhusu kazi muhimu inayofanywa na wanaharakati wa mazingira, tuzo la Mabingwa wa Dunia linatolewa ili kutoa motisha kwa watu zaidi na kuchombea watu zaidi kuchukua hatua za kushughulikia mazingira. Matuzo haya ni sehemu ya kampeni ya UNEP ya #ForNature (#TutunzeMazingira) kuongezea uzito Kongamano la Umoja wa Mataifa la Bayoanua (COP 15) ilitakalofanyika mjini Kunming mwezi wa Mei mwaka wa 2021, na kuimarisha juhudi za kushughulikia mazingira tunapoekea kongamano la Umoja wa Mataifa la Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) mjini Glasgow katika mwezi wa Novemba mwaka wa 2021.