"Ni sharti jamii za wenyeji zishirikishwe wakati wa kufanya maamuzi kuhusu misitu inayoathiri hali yao ya maisha," anasema Tecla Chumba, mama wa watoto wanne, mwanamke Mkenya kutoka kwa kabila la Lembus . Alianzisha muungano wa jamii za maeneo ya misitu na kutoa wito kwa Shirika la Misitu la Kenya kukabidhi kwa kila mwanachama shamba nusu ya heka na miche ya miti wanayoweza kupanda mbali na mimea yao wenyewe. Baadaye, wanachama hawa walitakiwa kurudisha mashamba haya baada ya miti kukua kwa miaka mitatu.
Mfumo huu hujulikana kama “shamba system” au "mradi wa mashamba ulioanzishwa ili kuboresha hali ya maisha." Ni mbinu inayotumiwa kupanda miti mahali ambapo miti ya kiasili imekatwa ili kupata mbao. Jamii hunufaika kwa kuweza kupanda mimea kama vile viazi, nyanya, maharagwe,mbaazi, mahindi na hata pia majani ya ng'ombe huku zikitakiwa kupanda miche na kutunza miti inayomea kwa kipindi cha miaka mitatu. Mbinu hii ya kilimo cha miti imewezesha wakulima wenyeji kutumia mbinu za kiasili kuua dudu bila kutumia dawa ya kuangamiza dudu. Wao hutumia samadi na jivu. Hatimaye Shirika la Misitu la Kenya hukabidhiwa kipande cha misitu kilicho na miti.
Kwa ushirikiano na Shirika la Misitu la Kenya, muungano wa jamii za maeneo ya misitu una mfumo wa usimamiaji wa misitu unaojumuisha wawakilishi 17 kutoka kwa muungano wa jamii za maeneo ya misitu. Wanachama pia wanaweza kutafuta kuni msituni, kufuga nyuki, kutafuta dawa, uyoga unaomea wenyewe na mboga zinginezo na matunda kutoka msituni. Pia wanaweza kupata maji, chakula cha mifugo, unyevu wa kukuzia miche yao nyumbani na kadhalika. Tangu mwaka wa 2010, mfumo wa "shamba system" umekuwa na kazi bora.
Lakini Shirika la Misitu la Kenya lilitangaza kukodisha shamba lake kwa kampuni inayonuia kupanda na kukata miti, na kupokonya muungano wa jamii za maeneo ya misitu haki ya kutumia shamba hilo, Chumba (kwa ushirikiano naMuungano wa Kitaifa Unaoleta Pamoja Miungano ya Jamii za Maeneo ya Misitu) walipeleka Shirika la Misitu la Kenya Mahakamani. Kwa sababu Miungano ya Jamii za Maeneo ya Misitu ilikuwa imetia sahihi mkataba wa usimamizi na Shirika la Misitu la Kenya, Muungano wa Kitaifa Unaoleta Pamoja Miungano ya Jamii za Maeneo ya Misitu ulishinda kesi hiyo. "Sheria ya Kenya ya mwaka wa 2016 ya kusimamia na kutunza misitu inaeleza kuwa Shirika la Misitu la Kenya ni sharti liheshimu na kushirikisha umma," alieleza Chumba.
Ushirikishaji wa umma umewekwa wazi na vyombo mbalimbali vya kuunda sheria nchini Kenya kama vile Katiba ya mwaka wa 2010, Sheria ya mwaka wa 2016 ya Usimamiaji na Utunzaji wa Misitu na ushirikishaji wa umma katika kanuni za mwaka wa 2009 za usimamizi wa misitu. Hata hivyo, kufikia mwaka wa 2015, sheria za kushirikisha wadau ikiwa ni pamoja na wenyeji hazikuwa wazi hasa kuhusu jinsi wanavyoweza kushiriki katika ufanyaji wa maamuzi kwenye sekta ya misitu.
“Utaratibu wa kushirikisha wadau na jinsi ya wao kuwa na elimu ya awali ya jinsi yakufanya uamuzi kwa hiari uliwekwa kwa ushirikiano kutoka kwa Wizara ya Mazingira na Misitu kama sehemu ya mradi wa UN-REDD uliolenga kusaidia Kenya kupitia Mradi wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP),” anasema Judy Ndichu, Mratibu wa Kiufundi wa Forest Carbon Partnership Facility nchini Kenya. "Unatoa fursa kwa jamii kushiriki katika mchakato wa kufanya uamuzi kuhusu miradi ya misitu ambayo maisha yao yanaitegemea."
Baada ya kushinda kesi katika mwaka wa 2013, Chumba aliendelea na 'shamba system' na anasema mfumo huo unaendelea kufaulu. Unapatikana katika maeneo yote nchini Kenya, lakini kuna maeneo ambayo hukumbwa na changamoto wakati ambapo mifugo huvamia mashamba yao, ijapokuwa hali hii inaendelea kuimarika. "Ng'ombe wakivamia shamba lako, unaweza kuita walinzi wa misitu watakaokamata ng'ombe hao," anasema. "Hatimaye, mmiliki wa ng'ombe hao atajitokeza kuwachukua na atalipia hasara iliyosababishwa na mifugo wake."
Anapongeza miungano ya jamii kutoka kwa maeneo ya misitu kwa kushiriki katika vuguvugu la REDD+ kwa sababu anaamini kuwa walifanya uamuzi mwafaka. "Miti ya kiasili ina umuhimu wake. Hufanya maji kurudi, huvutia nyuki na huzuia mchanga kubebwa na maji inapopandwa karibu na mito. Kwa hivyo sisi hupenda kuipanda na kuitunza, haswa pale tunapotuzwa pointi za kukabiliana na hewa ya ukaa maarufu kama carbon credits .
Mradi wa UN-REDD umekuwa mstari wa mbele kubuni sera zinazothamini na kutunza misitu na huduma zake za kijamii na za mifumo ya ikolojia inayotokana na misitu. Kujitolea kuzingatia mbinu zinazoheshimu haki za binadamu, kushirikisha makundi ya kijamii na wadau ni muhimu kwa malengo na kazi ya UN-REDD," asema Musonda Mumba, Msimamizi Mkuu wa Kitengo cha Mifumo ya Ekolojia ya Nchi Kavu na ambaye ni mwenyekiti wa kikosi kikuu kinachoandaa Karne ya Umoja wa Mataifa ya Kuboresha Mifumo ya Ekolojia Katika Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa.