Kongamano la Mazingira la Mawaziri wa Afrika (AMCEN) lilianzishwa katika mwaka wa 1985, kufuatia Kongamano la Mazingira la Mawaziri wa Afrika lililofanyika Cairo, nchini Misri. Kazi yake ni kuhamasisha kuhusu utunzaji wa mazingira barani Afrika; kuhakikisha kuwa mahitaji ya kimsingi ya binadamu yanapatikana ipasavyo na kwa njia endelevu; kuhakikisha kuwa maendeleo kwa jamii na kwa uchumi yanatekelezwa katika ngazi zote; na kuhakikisha kuwa shughuli na mazoea ya kilimo yanakidhi mahitaji ya utoshelezaji wa chakula katika ukanda huu.
Hatua zinazotumiwa na AMCEN kutafuta masuluhisho kwa masuala ya mazingira barani Afrika zimeendelea kuwa shirikishi na kupitia mashauriano tangu kuanzishwa kwake. Kuwepo kwa AMCEN kumekuwa na athari kwa namna masuala ya mazingira yanavyoshughulikiwa katika ukanda huu. AMCEN pia imechangia katika kuimarisha ushiriki na ushirikishwaji wa Afrika katika mazungumzo ya kimataifa na katika mikataba ya kimataifa kuhusu mazingira.
Wajibu wa AMCEN unajumuisha, miongoni mwa mambo mengine:
- Kutoa uongozi barani kote kwa kuhamasisha na kufikia maelewano kuhusu masuala ya mazingira ya kimataifa na ya kikanda;
- Kukuza misimamo ya pamoja ili kuwaongoza wawakilishi wa Afrika katika mazungumzo ya mikataba ya kimataifa inayowaunganisha kisheria;
- Kukuza kushiriki kwa Waafrika katika mazungumzo ya kimataifa kuhusu masuala ya kimataifa yalio na umuhimu kwa Afrika;
- Kupitia na kufuatilia programu za mazingira katika ngazi ya kikanda, katika eneo ndogo na katika ngazi ya kitaifa;
- Kutoa mwongozo wa kikanda wa kimkakati na kisera ili kukuza usimamizi mzuri wa mazingira wa kufikia maendeleo endelevu;
- Kukuza uidhinishaji na nchi za Kiafrika wa makubaliano ya kimataifa ya mazingira yanayohusiana na kanda hii;
- Kujengea Waafrika uwezo katika nyanja ya usimamizi wa mazingira.
Tangu kutokea kwa kikao cha kwanza cha AMCEN, kuna programu, mipango na shughuli kadhaa zilizoandaliwa ili kuwezesha utekelezaji mzuri wa kazi yake la kulinda mazingira barani Afrika. Imetekeleza hatua nyingi madhubuti kuhusiana na ukuzaji wa sera za kikanda, uhamasishaji, utetezi, uratibu, kushirikiana, usimamizi wa na usambazaji wa maarifa, na kutoa mafunzo. Kupitia mamlaka yake madhubuti ya kuitisha mikutano, imeleta pamoja Serikali za Afrika, taasisi na washirika wao wa maendeleo ili kujadiliana na kukuza misimamo ya pamoja kuhusu masuala muhimu ya kuzingatiwa kikanda, kimataifa na kote duniani.
Mipango ya kitaasisi
Katika mwaka wa 1997, AMCEN kwa kupitisha katiba yake ya kwanza kabisa, ilirasimisha kuwepo kwake kama mamlaka ya kudumu ya Mawaziri wa Afrika kuhusiana na mazingira na maendeleo endelevu. Kongamano hili ni chombo cha juu zaidi cha AMCEN cha kuunda sera. AMCEN ina Ofisi inayojumuisha Rais na makamu wa Rais wanne (kila mmoja akiwakilisha ukanda). Rais wa AMCEN huongoza vikao vya AMCEN, mikutano ya Ofisi na kuendesha shughuli za AMCEN wakati wa vikao vyake vya kawaida. Ofisi inawajibikia utekelezaji wa maamuzi ya Kongamano pamoja na uhusiano kati ya AMCEN na nchi wanachama na waangalizi wakati wa vikao. Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa kupitia Ofisi yake ya Afrika, imehudumu kama Sekretarieti ya AMCEN tangu kuanzishwa kwake. Sekretarieti inashirikiana na Rais wa AMCEN na Ofisi yake kuendesha shughuli za Kongamano.
AMCEN katika kikao chake cha 4, iliamua kuanzisha Dhamana ili kuhakikisha kuna chanzo endelevu cha fedha inayoolenga kufanya Kongamano kufana zaidi. Mfuko wa Dhamana ulianzishwa mwaka wa 1991, kutokana na michango inayotolewa kwa hiari. Lengo kuu la mfuko huu ni kutoa msaada wa kifedha, kikamilifu au kwa sehemu fulani, ili kuendesha taasisi za AMCEN na utekelezaji wa shughuli zake. Mfuko wa Dhamana unasimamiwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa ambalo ni Sekretarieti ya AMCEN.