Maswali yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu AMCEN

Kongamano la Mazingira la Mawaziri wa Afrika ni nini? 

Kongamano la Mazingira la Mawaziri wa Afrika (AMCEN) hukuza agenda ya mazingira barani Afrika. Kongamano lililoanzishwa mwaka wa 1985, huleta pamoja serikali za Afrika, taasisi na washirika wa maendeleo kuunda sera zinazolenga kushughulikia masuala muhimu zaidi ya mazingira barani.

Kongamano la Mazingira la Mawaziri wa Afrika hufanya vikao vyake vya kawaida mara moja kila baada ya miaka miwili na vikao maalum kati ya vikao hivyo vya kawaida inapohitajika. Ofisi ya Afrika ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) inahudumu kama sekretarieti ya Kongamano hili.

Uanachama

Nchi zote 54 za Afrika ni wanachama wa Kongamano hili.

Wajibu wa Ofisi ya Kongamano ni upi?

Ofisi ya Kongamano la Mazingira la Mawaziri wa Afrika ina wajibu wa kutekeleza maamuzi yanayofanywa na Kongamano hili na kudumisha uhusiano kati ya Kongamano hili na Nchi Wanachama wake na waangalizi kati ya vikao. Ofisi hufanya mkutana mara moja kwa mwaka na wakati mwingine wowote inapohitajika. Watakaohudumu Ofisini huchaguliwa na Kongamano katika kila kikao cha kawaida.

Kwa nini Kongamano hili ni muhimu?

Kama maeneo mengi duniani, Afrika inapambana na changamoto mbalimbali za mazingira. Ardhi inaharibiwa kwa kiwango cha kutisha, na kufanya kuwa vigumu kwa bara kujilisha. Uharibifu wa bayoanuai unaharibu utajiri asilia wa bara hili, na kuharibu mifumo ya ekolojia ambayo inashikilia kila kipengele cha maisha barani. Ongezeko la joto duniani tayari linatesa binadamu barani humu na mabadiliko ya tabianchi huathiri vibaya zaidi walio hatarini zaidi. Ni vigumu kwa sayari inayoshuhudia joto kali kutokomeza njaa na umaskini, au kufikia malengo mengine yaliyowekwa katika Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu na Ajenda ya 2063 ya Umoja wa Afrika. Kukabiliana na masuala haya ni jambo la dharura zaidi kwa sababu idadi ya watu barani Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara inatarajiwa kuongezeka maradufu kufikio mwaka wa 2050, jambo linaloweka shinikizo zaidi katika kanda hii.

Changamoto nyingi za kijamii na kiuchumi barani Afrika zinaweza kushughulikiwa kwa kukabiliana na changamoto zake za mazingira. Mifumo ya ekolojia inavuka mipaka ya kitaifa, mito huvuka mipaka na uharibifu unaofanywa kwa utajiri asilia wa nchi moja huathiri bara zima. Haya ndio yanayofanya Kongamano hili kuwa na uwezo wa kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kukuza sera za pamoja za mazingira muhimu sana kwa mapambano ya kuimarisha ustawi na kuimarisha maisha katika kanda. 

Kutokana na miongo kadhaa ya kujitahidi kufanya kazi ya kubainisha masuala, kukuza masuluhisho na kubuni sera bora, bara hili sasa lina mwongozo bora wa hatua za kushughulikia mazingira. Safari ya ukuzaji wa uchumi endelevu na Afrika ilio na ustawi zaidi imepamba moto.

Kongamano la Mazingira la Mawaziri wa Afrika lina uhusiano upi na Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa? 

Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa ni taasisi ya ngazi ya juu zaidi inayofanya uamuzi kuhusu mazingira duniani. Kongamano hili na Ofisi yake hushirikiana na UNEP ili kuhakikisha kuwa Kundi la wapatanishi Waafrika wanawasilisha mawazo yao kwa ufanisi na umoja katika Baraza. Maamuzi yaliyotolewa na Kongamano hili ni sehemu ya misimamo ya pamoja ya Afrika katika majadiliano wakati wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa.