Joyce Msuya ni Naibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa. Aliteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres mnamo Agosti mwaka wa 2018.
Kati ya Novemba 2018 na Juni 2019, Bi. Msuya alihudumu kwa mda kama Mkurugenzi Mtendaji. Alisimamia miradi ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa katika nchi 33 na kuwezesha kupitishwa kwa mikataba 9 ya kimataifa ya mazingira inayohusu changamoto za mazingira zinazopaswa kushughulikiwa kwa dharura.
Bi. Msuya ana tajriba ya zaidi ya miaka 20 katika uundaji wa mikakati ya kimataifa, masuala ya utenda kazi, ukuzaji wa maarifa na ubia katika maeneo ya Afrika, Asia na Latini ya Amerika.
Kabla ya kujiunga na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, Bi. Msuya alihudumu kama Mshauri wa Naibu wa Rais wa Benki ya Dunia wa eneo la Asia Mashariki na Pasifiki mjini Washington, D.C.
Tangu mwaka wa 2014 hadi mwaka wa 2017, Bi. Msuya alihudumu kama Mwakilishi Maalumu wa Benki ya Dunia na kama Msimamizi wa Ofisi ya Korea ya Benki ya Dunia. Alianzisha na kukuza mbinu za utenda kazi ofisini na kuimarisha ubia kati ya benki hiyo na nchi ya Korea.
Ameshikilia nyadhifa mbalimbali za ngazi ya juu katika Benki ya Dunia ikiwa ni pamoja na kuwa Mratibu wa Taasisi ya Eneo la Asia Mashariki na Pasifiki ya Benki ya Dunia nchini China, Afisa Mkuu wa Mikakati katika Shirika la Kimataifa la Fedha (Uzalishaji, Biashara itokanayo na mazao ya kilimo, na Utoaji wa Huduma). Pia alikuwa Msahauri Maalum wa Lord Nicholas Stern, Naibu Mkuu wa Rais wa Benki ya Dunia aliyehudumu pia kama Mtaamu Mkuu wa masuala ya uchumi. Bi. Msuya amefanya kazi na sekta za umma na sekta za kibinafsi wakati alipokuwa akifanya kazi na Benki ya Dunia.
Mwanamaikrobayolojia kutoka Tanzania, Bi. Msuya alianza kufanya kazi na Benki ya Dunia kama mtaalamu wa masuala ya afya barani Afrika mwaka wa 1998.
Bi. Msuya ana Shahada ya Uzamili katika Maikrobayolojia na Imunolojia kutoka Chuo Kikuu cha Ottawa, ncini Kanada. Pia ana Shahada ya Sayansi katika Bayokemia na Imunolojia kutoka Chuo Kikuu cha Strathclyde, nchini Scotland. Ana Astashahada katika Utendaji na Uendeshaji kwa Jumla (Executive General Management Certificate) kutoka Chuo Kikuu cha Johns Hopkins University (USA).
Bi. Msuya alitambuliwa kwa juhudi zake za kipekee kama alumna wa Chuo Kikuu cha Johns Hopkins mwaka wa 2019.
Ameolewa na ana watoto wawili.