Maji hufunika zaidi ya thuluthi mbili za sayari, ila maji yanayopatikana kwa urahisi – kutoka mitoni, maziwani, kwenye ardhioevu na chemichemi za maji – ni chini ya asilimia 1 ya maji yanayopatikana kote duniani.
Kadiri idadi ya watu duniani inavyoongezeka, ndivyo mahitaji ya maji yanavyoongezeka – kutumiwa kunywa na usafi wa mazingira, kwa kilimo na uzalishaji wa nishati na kwa matumizi mengineyo. Wakati uo huo, shughuli za binadamu na mabadiliko ya tabianchi yanavuruga mizunguko asilia ya maji, na kutoa shinikizo kwa vyanzo vya maji safi ambavyo ni mifumo yetu ya ekolojia ya maji safi. Uchafuzi, ukuzaji wa miundomsingi na uchimbaji wa malighafi huzidisha changamoto zilizopo.