- Ripoti ya hivi karibuni ya UNEP ya Pengo la Uzalishaji wa Gesi Chafu inaonyesha kuwa Ahadi Zinazowekwa na Taifa zitapunguza tu asilimia 7.5 ya uzalishaji wa gesi chafu uliokadiriwa kufikia mwaka wa 2030, huku asilimia 55 ikihitajika ili kufikia lengo la Paris la nyuzijoto 1.5
- Ahadi za mazingira za hivi karibuni za mwaka wa 2030 zinaonyesha ulimwengu unaenda kushuhudia ongezeko la joto la angalau nyuzijoto 2.7 katika karne hii
- Ahadi za kutozalisha gesi chafu zinaweza kupunguza nyuzijoto 0.5 zaidi, iwapo ahadi hizi zitaimarishwa na ikiwa ahadi za mwaka wa 2030 zitarandana na ahadi za kutozalisha gesi chafu
Nairobi, Oktoba 26, 2020 – Ahadi mpya na zilizosasishwa za mazingira bado hazitoshi kufikia malengo ya Mkataba wa Paris, zinafanya ulimwengu kuelekea kushuhudia ongezeka la joto la angalau nyuzijoto 2.7 katika karne hii, kwa mjibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) ya Uzalishaji wa Gesi Chafu Mwaka wa 2021: Joto Linazidi Kuongezeka.
Ripoti hiyo, ambayo sasa ni mwaka wake wa 12, inaonyesha kuwa Ahadi Zilizowekwa na Taifa (NDCs) – na ahadi zingine zilizotolewa kufikia mwaka wa 2030 lakini bado hazijawasilishwa katika NDC zilizosasishwa – hupunguza tu asilimia 7.5 ya makadirio ya uzalishaji wa gesi ya ukaa kufikia mwaka wa 2030, ikilinganishwa na msururu wa ahadi za awali. Upunguzaji wa asilimia 30 unahitajika kupunguza gharama za kufikia nyuzijoto 2 na asilimia 55 kufikia nyuzijoto 1.5.
Iliyotolewa kabla ya Kongamano la Umoja wa Mataifa la Mabadiliko ya Tabianchi (COP26), duru ya hivi karibuni ya mazungumzo kuhusu mazingira yanayofanyika mjini Glasgow, ripoti hiyo inatambua kuwa ahadi za kutozalisha gesi chafu zinaweza kuleta mabadiliko makubwa. Zikitekelezwa kikamilifu, ahadi hizi zinaweza kufanya makadirio yaliyofanywa ya ongezeko la joto ulimwenguni kufikia nyuzijoto 2.2, na kutoa matumaini kwamba hatua zaidi bado zinaweza kuondoa athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi. Walakini, ahadi za kutozalisha gesi chafu bado ni za kidhahania, hazijakamilika katika hali nyingi, na hazirandani na NDCs nyingi za mwaka wa 2030.
“Mabadiliko ya tabianchi sio tatizo la siku zijazo. Ni tatizo la sasa, alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP. "Ili kufaulu kudhibiti ongezeko la joto duniani lisizidi nyuzijoto 1.5, tuna miaka nane kuwa karibu kupunguza nusu ya uzalishaji wa gesi chafu: miaka nane ya kufanya mipango hiyo, kuweka sera, kuzitekeleza na mwishowe kupunguza. Mda unaendelea kuyoyoma.”
Kufikia tarehe 30 Septemba mwaka wa 2021, nchi 120, zinazowakilisha zaidi ya nusu ya uzalishaji wa gesi ya ukaa duniani, zilikuwa zimewasilisha NDCs mpya au zilizosasishwa. Kwa kuongezea, nchi tatu wanachama wa G20 zimetoa ahadi zingine mpya za kupunguza uzalishaji wa gesi chafu kufikia mwaka wa 2030.
Ili kufaulu kudhibiti ongezeko la joto duniani lisizidi nyuzijoto 1.5, dunia ina miaka nane kupunguza uzalishaji wa gesi chafu kwa gigatani 28 zaidi za CO2, sawa na (GtCO2e) kutoka kwa uzalishaji wa gesi chafu wa kila mwaka, kiwango zaidi ya kile kilichoahidiwa katika NDCs zilizosasishwa na ahadi zingine za mwaka wa 2030. Kwa kuzingatia kiwango hiki tu, uzalishaji wa kabonidioksidi pekee unatarajiwa kufikia gigatani 33 katika mwaka wa 2021. Tukizingatia gesi zingine zote za ukaa, uzalishaji wa gesi chafu kwa mwaka ni takribani GtCO2e 60. Kwa hivyo, kufaulu kufikia lengo la nyuzijoto 1.5, tunahitaji kupunguza karibu nusu ta uzalishaji wa gesi ya ukaa. Kufikia lengo la nyuzijoto 2, kiwango kinachohitajika kitapungua: uzalishaji wa gesi chafu utapungua kwa GtCO2e 13 kufikia mwaka wa 2030.
Alok Sharma, atakayekuwa Rais wa COP26, alisema ripoti hiyo ilisisitiza ni kwa nini nchi zinahitaji kuonyesha hatua kabambe za kushughulikia mazingira kwenye COP26: “Jinsi ripoti hii inavyoweka wazi, iwapo nchi zitatekeleza NDCs zake za mwaka wa 2030 na ahadi za kutozalisha gesi chafu ambazo zilitangazwa mwishoni mwa Septemba, tutashuhudia ongezeko la joto duniani la wastani ya zaidi ya nyuzijoto 2 tu kidogo. Uchanganuzi wa kukamilishana na huu unapendekeza kwamba ahadi zilizofanywa mjini Paris zingepunguza ongezeko la joto hadi chini ya nyuzijoto 4.
“Kwa hivyo hatua zimepigwa, lakini hazitoshi," aliongezea. Ndio sababu tunahitaji wazalishaji wakuu, mataifa ya G20, kutoa ahadi dhabiti zaidi za mwaka wa 2030 iwapo tunataka kufikia nyuzijoto 1.5 katika muongo huu muhimu."
Kuangazia kutozalisha gesi chafu
Ahadi za kutozalisha gesi chafu – na utekelezaji wake kikamilifu - kunaweza kuleta mabadiliko makubwa, waandishi wagundua, lakini mipango iliopo ni ya kidhahania na haijitokezi kwenye NDCs. Jumla ya nchi 49 ikijumuisha EU zimeahidi kutozalisha gesi chafu. Hii inashughulikia zaidi ya nusu ya uzalishaji wa gesi ya ukaa ndani ya nchi, zaidi ya nusu ya Pato la Taifa na theluthi moja ya idadi ya watu duniani. Malengo kumi na moja yamejumuishwa katika sheria, yanashughulikia asilimia 12 ya uzalishaji wa gesi chafu kote ulimwenguni.
Zikiimarishwa na kutekelezwa kikamilifu, malengo ya kutozalisha gesi chafu yanaweza kupunguza ongezeko la joto kwa nyuzijoto 0.5 zaidi, na kupunguza makadirio ya ongezeko la joto hadi nyuzijoto 2.2 Hata hivyo, nyingi ya mipango ya kitaifa itaanza kushughulikiwa baada ya mwaka wa 2030, hali inayoleta taswishi iwapo ahadi za kutozalisha gesi chafu zitafikiwa. Nchi kumi na mbili wanachama wa G20 zimetoa ahadi za kutozalisha gesi chafu, lakini bado zina utata. Hatua zinahitaji kuanza kuchulukiwa mapema ili kurandana na malengo ya mwaka wa 2030.
"Ni sharti ulimwengu uwe makini kwa janga linalotukumba kama spishi," Andersen aliongezea. “Mataifa yanahitaji kuweka sera ili kutimiza ahadi zake mpya, na kuanza kuzitekeleza kwa kipindi cha miezi. Yanahitaji kufanya ahadi za kutozalisha gesi chafu kuwa dhabiti zaidi, na kuhakikisha ahadi hizi zinajumuishwa katika NDCs, na hatua kuchukuliwa. Kisha yanahitaji kuwekaa sera za kuunga mkono azma hii kuu na, tena, yaanze kuzitekeleza kwa dharura.
“Ni muhimu pia kutoa msaada wa kifedha na kiteknolojia kwa mataifa yanayoendelea - ili kuyawezesha kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi yaliyopo na kuweka mikakati ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafu.”
Uwezo wa methani na mifumo ya masoko
Kila mwaka, Ripoti ya Pengo la Uzalishaji wa Gesi Chafu huangazia uwezo wa sekta maalum. Mwaka huu, inangazia methani na mifumo ya masoko. Kupunguza uzalishaji wa methani kutoka kwa mafuta ya visukuku, taka na sekta za kilimo kunaweza kuchangia kupunguza pengo la uzalishaji wa gesi chafu na kupunguza joto kwa kipindi kifupi.
Uzalishaji wa Methani ni mchangiaji wa pili kwa ukubwa wa ongezeko la joto duniani. Gesi hiyo ina uwezo wa kuongeza joto duniani zaidi ya mara 80 ikilinganishwa na kabonidioksidi kwa kipindi cha miaka 20; pia inadumu kwa kipindi kifupi angani ikilinganishwa na kabonidioksidi - miaka kumi na mbili tu, ikilinganishwa na hadi mamia ya miaka kwa CO2 - kwa hivyo kupunguzwa kwa methani kutapunguza ongezeko la joto haraka kuliko kupunguzwa kwa kabonidioksidi.
Hatua zilizopo za kiufundi kwa gharama ya chini au bila gharama yoyote pekee zinaweza kupunguza uzalishaji wa methani ya anthropogeniki kwa angalau asilimia 20 kwa mwaka. Utekelezaji wa hatua zote, pamoja na hatua pana za kimuundo na mienendo, kunaweza kupunguza uzalishaji wa methani ya anthropogeniki kwa angalau asilimia 45.
Masoko ya kaboni, wakati uo huo, yana uwezo wa kupunguza gharama na hivyo kuchombea ahadi kubwa zaidi za kupunguza uzalishaji wa gesi chafu, lakini tu iwapo sheria zitafafanuliwa wazi, na kuundwa ili kuhakikisha kuwa shughuli zinaonyesha kupunguzwa halisi kwa uzalishaji wa gesi chafu, na zinaungwa mkono na mipango ya kufuatilia maendeleo kwa njia ya uwazi.
Mapato yanayopatikana kupitia masoko haya yanaweza kufadhili shughuli za kupunguza na kutoa masuluhisho yanayoweza kutumika kutegemea nchi na katika mataifa yaliyo hatarini yanayoathiriwa mno na mabadiliko ya tabianchi.
Fursa ya kujiimarisha baada ya janga la korona imepotea mno
Mwishowe, ripoti inatambua kuwa fursa ya kutumia pesa kwenye bajeti kujinusuru na kujiimarisha baada ya COVID-19 ili kuimarisha uchumi huku tukiunga mkono hatua ya kushughulikia mazingira imepotea katika nchi nyingi.
Janga la COVID-19 lilipelekea kupungua kwa uzalishaji wa CO2 ulimwenguni kwa asilimia 5.4 katika mwaka wa 2020. Hata hivyo, uzalishaji wa gesi ya CO2 na zisizo za CO2 katika mwaka wa 2021 unatarajiwa kuongezeka tena kwa kiwango cha chini kiasi kuliko cha mwaka wa 2019.
Ni karibu asilimia 20 tu ya uwekezaji kwa jumla wa kujiimarisha baada ya janga kufikia Mei mwaka wa 2021 unaweza kupunguza uzalishaji wa gesi ya ukaa. Kati ya matumizi haya, angalau asilimia 90 ni kutoka kwa nchi sita wanachama wa G20 na mgeni mmoja wa kudumu.
Matumizi ya fedha ya kushughulikia COVID-19 yamekuwa chini sana katika uchumi wa kipato cha chini (dola za Marekani 60 kwa kila mtu) kuliko uchumi wa kipato cha juu (USD 11,800 kwa kila mtu). Mapengo kwenye ufadhili yanaweza kuzidisha mapengo katika mataifa yaliyo hatarini zaidi kuhusiana na uthabiti wa mazingira na hatua za kuyashughulikia.
MAKALA KWA WAHARIRI
Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)
UNEP ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira ulimwenguni. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.
Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:
Keisha Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, UNEP