Pixabay
27 Oct 2022 Toleo la habari Kushughulikia Mazingira

Hatua duni za kushughulikia mazingira zinapelekea hitaji la mabadiliko ya dharura katika jamii kuwa chaguo la pekee- UNEP

  • Ahadi za kushughulikia mazingira zitapelekea dunia kushuhudia ongezeko la joto la nyuzijoto kati ya 2.4 na 2.6 kufikia mwisho wa karne hii
  • Ahadi zilizosasishwa tangu kutokea kwa COP26 mjini Glasgow zinapunguza chini ya asilimia moja ya makadirio ya uzalishaji wa gesi ya ukaa kufikia mwaka wa 2030; asilimia 45 inahitajika ili kudhibiti ongezeko la joto duniani lisizidi nyuzijoto 1.5
  • Mabadiliko kwenye usambazaji wa umeme, viwandani, kwenye sekta ya uchukuzi na ujenzi na kwenye mifumo ya chakula na fedha yatasaidia kuleta mafanikio duniani.

Nairobi, Oktoba 27, 2022 - athari mbaya kwa hali ya hewa zinavyozidi kuongezeka kote duniani ujumbe ni kwamba uzalishaji wa gesi ya ukaa unapaswa kupungua kwa kasi, ripoti mpya ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) inadokeza kuwa jamii ya kimataifa bado iko mbali kufikia malengo ya Mkataba wa Paris, na inakosa mikakati ya kuaminika ya kufikia nyuzijoto 1.5.

Hata hivyo Ripoti ya Emissions Gap Mwaka wa 2022: Fursa inayodidimia – Changamoto za mazingira zinapaswa kushughulikiwa kwa dharura katika jamii inabaini kuwa ni mabadiliko ya dharura ya mfumo mzima- katika sekta ya usambazaji wa umeme, viwanda, uchukuzi na ujenzi, na katika mifumo ya chakula na ya kifedha - yanaweza kusaidia kuzuia maafa kwa mazingira. 

"Ripoti hii inatuambia kupitia njia ya kisayansi kile ambacho mazingira yamekuwa yakituambia, mwaka mzima, kupitia mafuriko mabaya, dhoruba na mioto mikali: tunapaswa kukoma kujaza gesi ya ukaa amgani, na kufanya hivyo haraka iwezekanavyo," alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP.  "Tulikuwa na fursa ya kufanya mabadiliko kwa haraka, lakini wakati huo umekwisha. Ni mabadiliko tu makubwa ya uchumi na jamii zetu yanayoweza kutuokoa kutokana na janga la mazingira linaloongezeka."

Mwaka ambao haukutumiwa vizuri

Ripoti inaonyesha kwamba licha ya uamuzi wa nchi zote katika mkutano wa kilele wa mazingira wa mwaka wa 2021 mjini Glasgow, Uingereza (COP26) wa kuimarisha Ahadi Zinazowekwa na Taifa zilizosasishwa na baadhi ya masaasisho kutoka kwa mataifa, hatua zilizopigwa bado ni duni zaidi. NDC zilizowasilishwa mwaka huu hupunguza tu kiwango cha gigatoni 0.5 cha uzalishaji wa gesi ya kaboniksidi (CO2), sawa na chini ya asilimia moja, kuzingatia makadirio ya uzalishaji wa gesi chafu duniani kufikia mwaka wa 2030.

Ukosefu huu wa kupiga hatua unafanya dunia kuendelea kushuhudia ongezeko la joto zaidi ya lengo la Mkataba wa Paris la chini ya nyuzijoto 2, na ikiwezekana nyuzijoto 1.5. NDC zinazotolewa kwa hiari zinakadiriwa kutoa fursa ya asilimia 66 ya kudhibiti ongezeko la joto duniani kuwa takriban nyuzijoto 2.6 kufikia mwishoni mwa karne hii. Kwa NDC zinazotolewa kwa masharti, zinazotegemea mambo mengine, kiwango hiki kitashuka hadi nyuzijoto 2.4. Sera zilizopo kwa sasa pekee zinaweza kupelekea ongezeko la nyuzijoto 2.8, hali inayoonyesha athari ya pengo kati ya ahadi na utekelezaji wake.

Ikiwezekana, utekelezaji wa NDC zote zinazotolewa kwa hiari pamoja na ahadi za kutozalisha hewa chafu vitawezesha tu ongezeko la nyuzijoto1.8, kwa hivyo kuna matumaini. Hata hivyo, hali hii haiwezekani kwa sasa kwa kuzingatia tofauti kati ya uzalishaji wa hewa chafu kwa sasa, malengo ya hivi karibuni ya NDC na malengo ya kudumu ya kutozalisha hewa chafu. 

Kiwango kikubwa kinahitaji kupunguzwa

Ili kufikia malengo ya Mkataba wa Paris, ulimwengu unapaswa kupunguza hewa ya ukaa kwa viwango vikubwa kwa kipindi cha miaka nane ijayo.

NDC zinazotolewa kwa hiari na zile zinazotolewa kwa masharti zinakadiriwa kupunguza uzalishaji wa hewa chafu duniani kufikia mwaka wa 2030 kwa asilimia 5 na 10 mtawalia, ikilinganishwa na uzalishaji wa gesi chafu kwa kuzingatia sera zilizopo kwa sasa. Ili kuwa na njia nafuu ya kudhibiti ongezeko la joto duniani lisizidi nyuzijoto 1.5, uzalishaji wa hewa chafu ni sharti upungue kwa asilimia 45 kwa kuzingatia sera zilizopo kwa sasa kufikia mwaka wa 2030. Kufia nyuzijoto 2 zinazolengwa, asilimia 30 inahitaji kupunguzwa.

Ili kupunguza viwango vikubwa namna hii tunahitaji  mabadiliko makubwa ya dharura ya mfumo mzima. Ripoti hii inaangazia jinsi ya kuleta baadhi ya mabadiliko haya katika sekta na mifumo muhimu.

"Ni suala nyeti, na wengine wanaweza kusema kuwa haiwezekani kubadilisha uchumi duniani na kuweza kupunguza maradufu karibu nusu ya uzalishaji wa gesi ukaa kufikaa mwaka wa 2030, lakini lazima tujaribu," Andersen alisema. Kila sehemu ya digrii ni muhimu: kwa jamii zilizo hatarini, kwa spishi na mifumo ya ekolojia, na kwa kila mmoja wetu." 

"Hata ikiwa hatutafikia malengo yetu ya mwaka wa 2030, lazima tujitahidi iwezekanavyo kukaribia nyuzijoto 1.5. Hii inamaanisha kuweka misingi ya mustakabali usizalisha hewa chafu: ule utakaotuwezesha kupunguza ongezeko la viwango vya joto na kutoa manufaa mengine mengi kwa jamii na mazingira, kama vile hewa safi, kazi zisizochafua mazingira na upatikanaji wa nishati kwa wote.”

Sekta ya umeme, viwanda, uchukuzi  na ujenzi

Ripoti hii inabaini kuwa Mabadiliko ya kuwezesha kutozalisha gesi ya ukaa katika usambazaji wa umeme, viwandani, kwenye sekta ya uchukuzi na ujenzi yanaendelea lakini yanahitaji kuimarishwa. Usambasaji wa umeme umeendelea zaidi, kwa sababu gharama za nishati jadidifu zimepungua mno. Lakini, kasi ya mabadiliko inapaswa kuimarishwa ikiwa ni pamoja na hatua za kuhakikisha mabadiliko ya haki na upatikanaji wa nishati kwa wote.

Kwa majengo, teknolojia bora zilizopo kwa sasa zinahitaji kutumika kikamilifu. Kwa viwanda na uchukuzi, teknolojia ya kutozalisha hewa ya ukaa inapaswa kuendelea kukuzwa na kutumiwa zaidi. Kuendeleza mabadiliko, sekta zote zinapaswa kuepuka kutumia miundomsingi mipya inayotumia mafuta mengi ya visukuku, kukuza na kutumia zaidi teknolojia isiyozalisha hewa ya ukaa, na kubadilisha mienendo. 

Mabadiliko ya mifumo ya chakula yanaweza kusababisha upunguzaji wa haraka na wa kudumu.

Kulenga mifumo ya chakula, ambayo hukadiria theluthi moja ya uzalishaji wote wa hewa chafu, inajumuisha kutunza mifumo asilia ya ekolojia, kutoa wito wa kubadilisha lishe, uboreshaji wa uzalishaji wa chakula shambani na uondoaji wa hewa ya ukaa kwenye mifumo ya usambazaji wa chakula.    Mabadiliko katika maeneo haya manne yanaweza kupunguza uzalishaji wa hewa chafu wa mifumo ya chakula kufikia mwaka wa 2050 kwa takribani theluthi moja ya viwango vya sasa; kinyume na uzalishaji wa hewa chafu unaoongezeka karibu maradufu iwapo hali ya sasa itasalia ilivyo. 

Serikali zinaweza kuleta mabadiliko kwa kufanyia marekebisho ruzuku na mifumo ya ushuru. Sekta ya kibinafsi inaweza kupunguza ubathirifu na uharibifu wa chakula, kutumia nishati jadidifu na kukuza vyakula vipya vinavyopunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa. Kila raia anaweza kubadilisha mtindo wake wa maisha ili kutumia chakula kinachopelekea mazingira endelevu na kupunguza hewa ya ukaa, hali itakayosababisha manufaa mengi ya kiafya.

Mfumo wa kifedha ni sharti uwezeshe mabadiliko

Mabadiliko ya kimataifa ya kuwa na uchumi wa kiwango cha chini cha hewa ya ukaa yanatarajiwa kuhitaji uwekezaji wa angalau Dola za Marekani kati ya trilioni 4 na 6 kwa mwaka. Hii ni sehemu ndogo tu (asilimia  kati ya 1.5 na 2) ya jumla ya mali ya sekta ya fedha inayosimaniwa, lakini ni muhimu (asilimia kati ya 20 na 28) kuzingatia rasilimali za ziada za kila mwaka zinazohitajika.

Mashirika mengi ya kifedha, licha ya ahadi zilizotolewa, yameonyesha kupiga hatua ndogo za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kutokana na manufaa ya maslahi ya muda mfupi, malengo yanayokingana na kutotambua hatari kwa hali ya hewa kikamilifu. 

Serikali na wadau wakuu wa kifedha watahitaji kushikilia mwelekeo uleule: mabadiliko ya mfumo wa fedha na miundo na taratibu zake, kushirikisha serikali, benki kuu, benki za biashara, wawekezaji wa taasisi na wahusika wengine wanaotoa ufadhili.

Ripoti inapendekeza mbinu sita za mabadiliko hanayohitajika kwenye sekta ya fedha, yanayohitaji kutokea kwa pamoja: 

  • Kuimarisha zaidi masoko ya fedha, ikiwa ni pamoja na kupitia kwa uainishaji na uwazi.
  • Kuanzisha kuwekea bei hewa ya ukaa, kama vile ushuru au mifumo ya biashara.
  • Kubadilisha matumizi ya fedha, kupitia kuhamasisha umma kuhusu sera, ushuru, matumizi na kanuni za kutumia fedha.
  • Kubuni masoko ya teknolojia ya kiwango cha chini cha hewa ya ukaa, kupitia kubadilisha mzunguko wa fedha, kuchochea uvumbuzi na kusaidia kuweka viwango.
  • Kuhamasisha benki kuu: benki kuu zinazidi kushughulikia changamoto za mazingira, ila hatua madhubuti zaidi kuhusu sheria zinahitajika kwa dharura.   
  • Kuanzisha "vilabu" vya mazingira katika nchi zitakazokubali, kuanzisha miradi ya kifedha katika nchi mbalimbali na ubia kupitia mabadiliko ya haki, ambayo yanaweza kubadilisha kanuni za sera na kubadilisha mkondo wa fedha kupitia vifaa vya kifedha vya kuaminika, kama vile dhamana huru.  

 

MAKALA KWA WAHARIRI



Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)

(UNEP) ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira duniani. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.  

Kwa mawasiliano zaidi, tafadhali wasiliana na:

Keisha Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa