pixabay
24 Oct 2024 Toleo la habari Kushughulikia Mazingira

Mataifa ni sharti yazibe pengo kubwa la uzalishaji wa hewa chafu katika ahadi mpya za kushughulikia tabianchi na kuchukua hatua haraka, au…

  • Bado inawezekana kiufundi kufikia lengo la nyuzijoto 1.5, lakini tu kupitia uhamasishaji mkubwa wa kimataifa unaoongozwa na G20 ili kupunguza uzalishaji wote wa gesi ya ukaa, kuanzia leo 
  • Kuendelea na sera za sasa kutasababisha ongezeko hatari la joto la hadi nyuzijoto 3.1 
  • Ahadi za sasa za kufikia mwaka wa 2030 hazijatimizwa; hata zikitimizwa, ongezeko la joto linaweza tu kudhibitiwa hadi kati ya nyuzijoto 2.6 na nyuzijoto 2.8 

 Cali/Nairobi, Octoba 24, 2024 – Mataifa ni sharti kwa pamoja yajitolee kupunguza uzalishaji wa gesi ya ukaa kwa asilimia 42 kufikia mwaka wa 2030 na asilimia 57 kufikia mwaka wa 2035 katika awamu ijayo ya Michango Inayoamuliwa na Taifa (NDCs) – na kuunga hali hii mkono kupitia hatua za haraka – au lengo la Mkataba wa Paris la kufikia nyuzijoto 1.5 litaangamia katika kipindi cha miaka michache, kwa mjibu wa Ripoti mpya ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa. 

NDC zilizosasishwa zinatarajiwa kuwasilishwa mapema ya mwaka ujao kabla ya COP30 nchini Brazili. Ripoti ya UNEP ya Pengo la Uzalishaji wa Gesi Chafu ya Mwaka wa 2024 Tusiendelee kuongeza joto angani … tafadhali! imegundua kwamba tusipoimarisha ahadi katika NDC mpya na kuanza kuzitekeleza haraka, dunia inaweza kuwekwa katika hali ya kushuhudia ongezeko la joto la nyuzijoto kati ya 2.6 na 3.1 katika kipindi cha karne hii. Hali hii inaweza kusababisha athari mbaya zaidi kwa watu, sayari na uchumi.

Kuweza kufikia nyuzi joto 2.6 itawezekana tu kutokana na utekelezaji kamili wa NDC za sasa zisizo na masharti na zile zilizo na masharti. Utekelezaji wa NDC za sasa zisizo na masharti pekee kunaweza kusababisha ongezeko la joto la nyuzijoto 2.8. Kuendelea na sera zilizopo tu kunaweza kusababisha ongezeko la joto la nyuzijoto 3.1. Chini ya hali hizi - ambazo zote zinazingatia uwezekano wa zaidi ya asilimia 66 - joto litaendelea kuongezeka hadi kwa karne ijayo. Kuongeza ahadi za ziada za kutozalisha hewa chafu na utekelezaji kamili wa NDC zisizo na masharti na zilizo na masharti kunaweza kupunguza ongezeko la joto duniani hadi nyuzijoto 1.9, lakini kwa sasa kuna imani ndogo kwa utekelezaji wa ahadi hizi za kutozalisha hewa chafu.

"Pengo la uzalishaji wa hewa chafu sio dhana ya kufikirika," alisema António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kupitia ujumbe wake wa video kuhusu ripoti hii. "Kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kuongezeka kwa uzalishaji wa hewa chafu na kuongezeka kwa majanga ya tabianchi ya mara kwa mara yalio na makali zaidi. Kote ulimwenguni, watu wanalipia vibaya zaidi. Uzalishaji wa kiwango cha juu wa hewa chafu unamaanisha kushuhudia viwango vya juu joto baharini vinavyozidisha vimbunga vibaya zaidi; kiwango cha juu joto kinamaanisha kugeuza misitu kuwa vifaa vya kuwaka haraka na kufanya miji kuwa sauna; kiwango cha juu cha mvua husababisha mafuriko kama ya nyakati za Biblia.

"Ripoti ya Leo ya Pengo la Uzalishaji wa hewa chafu iko wazi: tunacheza na moto; lakini hatuwezi kuendelea kucheza na wakati. Mda umeyoyoma. Kupunguza pengo la uzalishaji wa hewa chafu kunamaanisha kuziba pengo la ahadi zinazohitajika, kupunguza pengo la utekelezaji na pengo la kifedha. Kuanzia kwa COP29.”

“Wakati muhimu wa kushughulikia tabianchi umewadia. Tunahitaji uhamasishaji wa kimataifa kwa kiwango na kasi ambayo haijawahi kushuhudiwa hapo awali – kuanzia sasa, kabla ya awamu inayofuata ya ahadi za kushughulikia tabianchi – au lengo la kufikia nyuzij1.5 litaangamia hivi karibuni na lengo la kufikia nyuzijoto 2 linaelekea katika chumba cha wagonjwa mahututi," alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP. "Ninatoa wito kwa kila taifa: tusiendelee kuongeza joto angani, tafadhali. Tumieni mazungumzo yajayo ya COP29 mjini Baku, Azabajani, ili kuongeza hatua sasa, wekeni jukwaa la kuwa na NDC thabiti zaidi, na kisha mujitolee kuhakikisha lengo la nyuzijoto 1.5 linatimia.

"Hata dunia iikishindwa kufikia nyuzijoto 1.5 - na uwezekano wa hili kutokea unaongezeka kila siku – lazima tuendelee kujitahidi kutozalisha hewa chafu, na kuwa na dunia endelevu na inayostawi. Kila sehemu ya nyuzijoto inayoepukika ni muhimu kwa kuzingatia maisha yanayookolewa, uchumi unaolindwa, uharibifu unaoepukika, bayoanuai inayohifadhiwa na uwezo wa kupunguza kwa haraka kiwango chochote cha joto kinachoongezeka. 

Ripoti hiyo pia inaangazia kile ambacho kinahitajika ili kuweza kudhibiti ongezeko la joto duniani lisizidi nyuzijoto 2. Ili kuweza kufikia lengo hili, uzalishaji wa hewa chafu ni shati upungue kwa asilimia 28 kufikia mwaka wa 2030 na asilimia 37 kwa kuzingatia viwango vya mwaka wa 2019 kufikia mwaka wa 2035 – mwaka wa hatua mpya muhimu zinazohitaji kujumuishwa kwa NDC.

Matokeo ya kuchelewa kuchukua hatua pia yameangaziwa. Viwango vinavyohitaji kupunguzwa vinazingatia viwango vya mwaka wa 2019, lakini uzalishaji wa gesi ya ukaa umeongezeka hadi kufikia kiwango cha juu cha gigatoni 57.1 za kaboni dioksidi katika mwaka wa 2023. Ingawa hii itapunguza kiasi kidogo cha upunguzaji wa jumla unaohitajika kuanzia mwaka wa 2019 hadi mwaka wa 2030, kuchelewa kuchukua hatua kunamaanisha kwamba asilimia 7.5 ya uzalishaji wa hewa chafu unapaswa kupunguzwa kila mwaka hadi mwaka wa 2035 ili kufikia nyuzijoto 1.5 na asilimia 4 ili kufikia nyuzijoto 2. Kiwango kinachohitajika kupunguzwa kila mwaka kitaongezeka kila mwaka tunapochelewa kuchukua hatua.

Bado inawezekana kiufundi kuweza kufikia nyuzijoto 1.5, ila juhudi nyingi zinahitajika 

 Ripoti hii inaonesha kuwa bado inawezekana kiufundi kupunguza uzalishaji wa hewa chafu katika mwaka wa 2030 kwa kiwango cha juu cha hadi gigatoni 31 za CO2 – ambacho ni karibu asilimia 52 ya uzalishaji wa hewa chafu katika mwaka wa 2023 – na gigatoni 41 katika mwaka wa 2035. Hali hii inaweza kupunguza pengo hadi nyuzijoto 1.5 katika miaka yote, kwa gharama ya chini ya dola za Marekani 200 kwa kiwango cha tani ya CO2

Kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia ya nishati ya jua na nishati ya upepo kunaweza pelekea asilimia 27 ya jumla ya uwezo wa kupunguza uzalishaji wa hewa chafu katika mwaka wa 2030 na asilimia 38 katika mwaka wa 2035. Kushushughilikia misitu kunaweza kupelekea angalau asilimia 20 ya uwezo huu katika miaka hii yote. Mambo mengine thabiti ni pamoja na hatua mwafaka, uwekaji umeme na ubadilishaji wa nishati katika sekta za ujenzi, uchukuzi na viwanda.

Uwezo huu unaonyesha kuwa inawezekana kufikia malengo ya COP28 ya kuimarisha uwezo wa nishati jadidifu mara tatu kufikia mwaka 2030, na kuongeza maradufu kiwango cha wastani cha kimataifa cha matumizi bora ya nishati kufikia mwaka wa 2030, na kuachana na nishati ya visukuku, na kuhifadhi, kulinda na kuoresha mazingira na mifumo ya ekolojia.

Hata hivyo, kufikia hata sehumu ya uwezekano huu kutahitaji uhamasishaji wa kimataifa ambao haujawahi kushuhudiwa na mfumo unaozingatiwa na serikali nzima, unaozingatia hatua zinazoongeza manufaa ya kijamii na kiuchumi na kimazingira pamoja na kupunguza mwafaka.

Ongezeko la angalau mara sita la uwekezaji wa kukabiliana na hali unahitajika ili kutozalisha hewa chafu – unaoungwa mkono na mfumo wa ufadhili duniani na hatua thabiti za sekta binafsi na ushirikiano wa kimataifa. Hii ni kwa gharama nafuu: makadirio ya ongezeko la uwekezaji wa kutozalisha hewa chafu ni dola za Marekani kati ya trilioni 0.9 na trilioni 2.1 kwa mwaka kuanzia mwaka wa 2021 hadi mwaka wa 2050, uwekezaji ambao utakuwa na faida kutokana na gharama zilizoepukwa kutokana na athari mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa hewa, uharibifu wa mazingira na athari kwa afya ya binadamu. Kwa muktadha, uchumi duniani na masoko ya fedha yana thamani ya dola za Marekani trilioni 110 kwa mwaka.

Mataifa ya G20, haswa wanachama wanaozalisha hewa chafu zaidi, yanahitaji kufanya kazi nzito. Hata hivyo, kundi hili bado haliko karibu hata kufikia NDC za sasa. Nchi wanachama wanaozalisha hewa chafu nyingi zaidi zinahitaji kuwa mstari mbele wa kuimarisha hatua na kujitolea sasa na katika ahadi mpya.

Nchi wanachama wa G20, ukiondoa Umoja wa Afrika, zilichangia asilimia 77 ya uzalishaji wa hewa chafu katika mwaka wa 2023. Kuongezwa kwa Umoja wa Afrika kama mwanachama wa kudumu wa G20, hali ambayo inaongeza nchi zaidi ya maradufu kutoka nchi 44 hadi nchi 99, inaongeza kwa kiwango cha asilimia 5 tu hadi kufikia asilimia 82 - na kuangazia umuhimu wa kutofautisha majukumu kati ya mataifa. Usaidizi thabiti wa kimataifa na kuimarisha ufadhili wa kushughulikia tabianchi utakuwa muhimu ili kuhakikisha malengo ya kushughulikia mazingira na malengo ya maendeleo yanaweza kutimizwa kwa haki kwa nchi zote wanachama wa G20 na katika ngazi ya kimataifa. 

Muundo mzuri wa NDC ni muhimu 

 Ripoti hii pia inaonyesha jinsi ya kuhakikisha kuwa NDC zilizosasishwa zimeundwa vyema, ziwe mahususi na wazi ili kufikia malengo yoyote mapya yaliyowekwa. NDC ni sharti zijumuishe gesi zote zilizoorodheshwa katika Mkataba wa Kyoto, zijumuishe sekta zote, ziweke malengo mahususi kuhusiana na vipengele vilivyo na masharti na visivyo na masharti na zieleze kwa uwazi kuhusu jinsi wasilisho linavyoakisi sehemu kubwa ya juhudi na matarajio ya juu zaidi.

 Ni sharti pia zieleze kwa kina jinsi malengo ya kitaifa ya maendeleo endelevu yanavyoweza kufikiwa kwa wakati uo huo juhudi za kupunguza uzalishaji wa hewa chafu zinavyotekelezwa, na kujumuisha mpango wa utekelezaji wa kina na mfumo wa ukakuzi na uwajibikaji. Kwa soko linaloibuka na chumi zinazoendelea, NDC zinapaswa kujumuisha maelezo kuhusu usaidizi na ufadhili wa kimataifa unaohitajika.

 

MAKALA KWA WAHARIRI 

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)

UNEP ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira duniani. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano wa utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.     

 Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na: 

Kitengo cha Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa