Pixabay
07 Sep 2021 Toleo la habari Air quality

Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi ili kuwa na angaa za bluu inaonyesha uhusiano kati ya afya ya binadamu na ubora wa sayari

Nairobi, Septemba 7, 2021 – Leo, maadhimisho ya pili ya Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi ili kuwa na angaa za bluu yalitokea duniani chini ya kaulimbiu Hewa bora, Sayari Bora,inayoonesha uhusiano kati ya ubora wa hewa, afya ya binadamu na ubora wa sayari. Tisa kati ya watu kumi duniani hupumua hewa chafu, inayopelekea takribani vifo milioni saba kutokea mapema kila mwaka.

Katika mwaka wa 2019, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliteua Septemba 7 kama Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi ili kuwa na angaa za bluu. Siku – ambayo maadhimisho yake huandaliwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) – inasisitiza umuhimu wa hewa safi na hitaji la dharura la juhudi za kuboresha hali ya hewa ili kutunza afya ya binadamu.

Maadhimisho rasmi ya pili ya Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi ili kuwa na angaa za bluu yaliendela mijini Nairobi, New York na Bangkok. Viongozi wakuu wa ngazi ya juu kwenye hafla ya hii walijumuisha Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Inger Andersen, na Mwanasanyansi Mkuu wa UNEP, Andrea Hinwood, pamoja na wataalamu wengine na viongozi serikalini waliozungumzia juhudi za kimataifa zinazochukuliwa na kutochukuliwa kuhusiana na uchafuzi wa hewa.

Kwenye ujumbe kuhusu Siku hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, alisema: "Kama maovu mengi katika jamii, uchafuzi wa hewa ni kiashiria cha ubaguzi duniani. Umaskini unalazimisha watu kuishi karibu na vyanzo vya uchafuzi wa mazingira, kama vile viwanda na barabara kuu, na kuchoma fueli ya mango au kutumia mafuta ya taa kupika, kupasha moto, na kutoa mwangaza. Uchafuzi unaodhuru afya zetu pia unasababisha changamoto ya hali ya hewa. Natoa wito kwa nchi zote kuchukua hatua zaidi kuboresha hali ya hewa, kuwekeza kwenye nishati jadidifu badala ya fueli ya visukuku, kukomesha makaa ya mawe, na mabadiliko kwa kutumia magari yasiyozalisha gesi chafu."

Akizungumza katika hafla rasmi mjini Nairobi, Bi Andersen alisema:  "Kuboresha hali ya hewa hakutasaidia tu kuboresha afya zetu. Kutatusaidia kuiokoa sayari. Sisi sote tunapumua hewa ileile, na sisi sote tunawajibu wa kuilinda.  Ulimwengu unakuja pamoja, lakini tunahitaji kushughulikia ahadi na kuzifanya kuwa sera kupitia vitendo. Kwa afya ya binadamu na ubora wa sayari kwa vizazi vijavyo, 2021 utakuwa mwaka muhimu sana."

Hatua za kushughulikia uchafuzi wa hewa

Kuelekea Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi ili kuwa na angaa za bluu, UNEP ilijiunga na wabia kutangaza kukomeshwa kwa matumizi ya petroli iliyo na madini ya risasi, mafanikio makuu ambayo yatazuia vifo vya mapema zaidi ya milioni 1.2 na kuokoa Dola za Marekani trilioni 2.45 kwa mwaka .

Mwanzoni mwa Septemba, UNEP ilitoa tathmini ya kwanza kabisa ya sheria za uchafuzi wa hewa, iliyochunguza sheria za kitaifa za ubora wa hewa katika Mataifa 194 na Muungano wa Ulaya. Inaonyesha mielekeo ileile: nchi mbili kati ya tatu ulimwenguni zimeweka viwango vya kisheria vya ubora wa hewa nje ya majumba. Ila, pia inaonyesha jinsi ambavyo viwango vinatofautiana mno na haviingiani naMiongozo ya WHO. Inahitimika kwa kutoa wito wa mifumo dhabiti ya ufuatiliaji ili kutekeleza kikamilifi sheria za ubora wa hewa.

Tarehe 7 Septemba, ripoti ya pili kuhusu sera na programu za kimataifa za kupunguza uchafuzi wa hewa, Hatua kuhusu Ubora wa Hewa, inaonyesha kuwa nchi nyingi zimepitisha sera anuai za kupunguza uchafuzi wa hewa. Ila upungufu mkubwa katika utekelezaji, ufadhili, uwezo, pamoja na ufuatiliaji, inamaanisha kuwa viwango vya uchafuzi wa hewa vinasalia kuwa juu. Ripoti hiyo inakamilishanana mihtasari za ripoti sita za kikanda kutoka Afrika, Asia na Pasifiki, Ulaya, Amerika ya Kusini na Karibiani, Amerika ya Kaskazini, na Asia Magharibi.

Mbali na ripoti hizi, UNEP imeshikana mikono na IQAirkampuni ya teknolojia ya hali ya hewa ya Uswizi, kuzindua kifaa cha kupimia uchafuzi wa hewa duniani.  Chombo hicho,kilicho na uwezo wa kufikiri (artificial intelligence), kimejengwa kwenye jukwaa kubwa zaidi la data ulimwenguni, lililozinduliwa mwaka jana kukadiria idadi ya watu wanaokumbana na uchafuzi katika nchi yoyote, kila saa.

UNEP pia iliungana na Safaricom, kampuni ya mawasiliano nchini Kenya, na IQAir kupeperusha vipimo kamili vya uchafuzi wa hewa mjiji hadi kwenye bango kubwa la kidijitali.  Mradi huo wa majaribio ni wa kwanza wa aina yake barani na unajumuisha wadau kadhaa, pamoja na serikali za mitaa na watoaji wa matangazo. Unalenga kuimarisha ufahamu wa athari za uchafuzi wa hewa kati ya wakaazi milioni 4.7 mjini Nairobi, wanaoteseka mara kwa mara kutokana na viwango hatari vya chembechembe laini (PM2.5).

Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi ili kuwa anga za bluu, iliyoadhimishwa kwa mara ya kwanza katika mwaka wa 2020, inatoa wito wa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika ngazi za kimataifa, kikanda na mkoa. Ni jukwaa la kuimarisha mshikamano wa kimataifa pamoja na kuimarisha juhudi za kisiasa za kuchukua hatua dhidi ya uchafuzi wa hewa na mabadiliko ya tabianchi, ikijumuisha vitendo kama kuimarisha ukusanyaji wa data ya hali ya hewa, kushirikiana kufanya utafiti, kukuza teknolojia mpya na kushiriki njia bora.

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi ili kuwa na anga za bluu

Likisisitiza umuhimu wa kufanya juhudi zaidi za kuboresha ubora wa hewa, ikijumuisha kupunguza uchafuzi wa hewa, kutunza afya ya binadamu; kukiri kuwa kuboresha hali ya hewa kunaweza kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kwamba juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinaweza kuboresha hali ya hewa; Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliamua kuteua tarehe 7 Septemba kama Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi ili kuwa na anga za bluu. Maadhimisho ya kwanza yalitokea mwaka wa 2020, kwa kutoa wito kwa juhudi za kimataifa za kukomesha uchafuzi wa hewa.

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)

UNEP ni mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira ulimwenguni. UNEP  Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Keisha Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa.