Islamabad/Nairobi, 5 June 2021 – Watu binafsi, jamii, mashirika ya uraia, mashirika ya biashara, na serikali kote ulimwenguni waliadhimisha leo Siku ya Mazingira Duniani – huku maadhimisho rasmi yakiendeshwa mjini Islamabad – kwa kutoa ahadi na kutoa wito wa kuchukua hatua za kuboresha mifumo ya ekolojia ya mamilioni ya hekta kwa manufaa ya watu na mazingira.
Mwenyeji akiwa Pakistan kwa ushirikiano wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Mazingira Duniani yalishuhudia uzinduzi rasmi wa Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia 2021-2030. Wakiongozwa na Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan, wazungumzaji katika hafla hiyo - wakijumuisha Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, Rais wa China Xi Jinping, Katibu Mkuu wa UN António Guterres, wakuu wa mashirika ya UN na mawaziri wa serikali - walisisitiza umuhimu wa uboreshaji katika juhudi za kimataifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kukuza maendeleo endelevu.
"Uharibifu wa dunia asilia tayari umeathiri maisha ya watu wanaokadiriwa kuwa bilioni 3.2 - hiyo ni asilimia 40 ya jumla ya idadi ya watu ulimwenguni. Ila, dunia inaweza kustahimili. Ijapokuwa inahitaji msaada wetu. Bado tuna muda wa kukabiliana na uharibifu ambao tumesababisha, "Katibu Mkuu wa UN alisema. "Ndio maana, katika Siku hii ya Mazingira Duniani, tunazindua Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia. Vuguvugu hili la kimataifa litaleta pamoja serikali, mashirika ya biashara, mashirika ya uraia na wananchi kupitia juhudi za kipekee za kuimarisha Dunia. Kwa kuboresha mifumo ya ekolojia, tunaweza kuleta mabadiliko yatakayochangia kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu."
Muongo wa UN unakusudia kuhamasisha na kusaidia serikali, mashirika ya Umoja wa Mataifa, mashirika ya uraia, kampuni za sekta binafsi, vijana, vikundi vya wanawake, watu wa kiasili, wakulima, jamii za wenyeji na watu binafsi kote ulimwenguni, kushirikiana, kukuza na kuchochea miradi ya uboreshaji kote ulimwenguni. Muongo huo unakusudia kuhamasisha mamia ya mamilioni ya watu kuboresha mazingira na kukuza utamaduni wa kimataifa ambapo miradi ya uboreshaji itaimarishwa kote ulimwenguni.
"Hii ni fursa kwa ulimwengu - miaka 10 ijayo, ulimwengu lazima urekebishe mienendo yake. Ni mgongano kati ya tamaa zetu kwa upande mmoja na ubinadamu kwa upande mwingine; kuna haja ya kupima masuala haya kwa mizani," Waziri Mkuu Khan alisema. "Suala hili likipuuzwa na tamaa ya mali, matumizi na tamaa kufikia kiwango kama hicho, mara nyingi hali hii husababisha madhara mabaya mno kwa wanadamu."
"Tusipojali mazingira yetu, na mifumo yetu ya ekolojia, kutakuwa na madhara mabaya kwa binadamu na tutalazimika kulipia gharama ghali kutokana na hali hili," akaongeza.
Pakistan imeanza mipango kabambe ya kupanua na kuboresha misitu yake kama sehemu ya mradi wa miti bilioni 10, hivi majuzi ikipanda mti wake wa kufikisha bilioni moja ya miti; nchi hiyo pia imetoa ahadi za kupanda miti kwenye hekta bilioni moja kwa ardhi iliyoharibiwa kote nchini kufikia mwaka wa 2023 kama sehemu ya Bonn Challenge. Kwa kuongezea, hivi karibuni Pakistan ilizindua green bond yake ya kwanza, ikitafuta dola milioni 500 ya kufadhili miradi inajali mazingira na kuimarisha nishati isiyochafua mazingira katika sekta ya umeme nchini humo.
Uboreshaji wa mifumo ya ekolojia ni suhuhisho mwafaka. Unapunguza kasi ya mabadiliko ya tabianchi, inarejesha bayoanuai inayodidimia, inatoa ardhi yenye rutuba kwa kilimo, kutoa ajira na kuboresha uwezo wa mazingira kukabiliana na magonjwa yanayotokana na wanyama magonjwa tandavu," alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP.
"Tukifanya kazi kwa bidii kwa maeneo manne - kuwekeza kwenye mazingira; kulinda wale wanaosimamia ardhi; kuwa na miji isiyochafua mazingira; na kuboresha ekolojia ya bahari - tutaimarisha mazingira na kuboresha maisha ya kila mtu,” akaongezea.
Ahadi zingine kuu zilizotangazwa kuhusiana na Siku ya Mazingira Duniani na Muongo wa UN ni pamoja na ufadhili mpya wa zaidi ya pauni milioni 8 kutoka kwa Uingereza kutunza wanyamapori adimu na makazi yaliyo hatarini duniani kote; ahadi ya Yuro milioni 8.5 kutoka kwa shirika la kimataifa la Dove and Conservation za kutunza na kuboresha hekta 20,000 za misitu - sawa na miti milioni 3 - Kaskazini mwa Sumatra, Indonesia; ahadi ya E.ON, mwendeshaji mkubwa zaidi wa mitandao ya usambazaji wa nishati Ulaya, kuunda biotope kupitia kilomita 13,000 za laini za umeme ya voliteji ya juu katika maeneo ya misitu; Yuro Milioni 3 kutoka Uholanzi kusaidia katika uzinduzi wa Muongo wa UN, na kufadhili juhudi za kikanda katika nchi zinazoendelea chini ya Muongo mmoja wa UN, na tangazo la Ujerumani kwamba itakuwa nchi ya kwanza kutoa ufadhili - Yuro milioni 14 - kwa Mfuko wa Wabia Anuai wa Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia .
Mbali na Islamabad, hafla na miradi ya Siku ya Mazingira Duniani iliendeshwa kote ulimwenguni, ikijumuisha tamasha mtandaoni lililojumuisha Patti Smith, bendi ya Dave Matthews Band, Michael Stipe na wasanii wengine wa kimataifa; wimbo maarufu duniani Is It Too Much to Ask, ulioimbwa na DJ Don Diablo kwa ajili ya #GenerationRestoration; Darasa lililoendeshwa mtandaoni kuhusu Uboreshaji wa Mifumo ya Ekolojia, mradi mpya wa kupeleka vijana wa Afrika Kusini - na wengine - kwenye safari katika mandhari tatu za kipekee yanayotishiwa na maendeleo ya binadamu; mazungumzo ya kando na mashirika ya vijana na kadhalika.
Kwa kushirikiana na ByteDance, UNEP pia ilitoa wito kwa watumiaji wa mtandao wa kijamii wa TikTok kushiriki juhudi zao za kuboresha mifumo ya ekolojia, wakitumia hashtagi ya #GenerationRestoration. Video zilizo na hashtagi hiyo zimetazamwa zaidi ya mara milioni 40, na michango kutoka kwa washawishi wakiwemo Mabalozi wa Nia Njema wa UNEP Alex Rendell na Antoinette Taus.
Mabalozi wa UNEP wa Nia Njema Gisele Bündchen, dereva wa Formula E Lucas De Grassi na Dia Mirza pia walitoa msaada wao kwa Siku hiyo kwenye mitandao ya kijamii, wakati wasanii wa umri mdogo kama vile mshairi MmarekaniJordan Sanchez na msanii anayetumia mchanga wa India Sudarsan Pattnaik pia walibuni vitu vya kuonyesha umuhimu wa kufanya uboreshaji kwa dharura. Bonyeza hapa kupata orodha kamili ya hafla zinazofanyika kuhusiana na Siku ya Mazingira Duniani.
MAKALA KWA WAHARIRI
Kuhusu Siku ya Mazingira Duniani
Siku ya Mazingira Duniani ni chombo kikuu cha Umoja wa Mataifa cha kuhimiza uhamasishaji wa kimataifa na kuchukua hatua za kushughulikia mazingira. Siku inayoadhimishwa kila mwaka tangu mwaka wa 1974, Siku hiyo pia imekuwa jukwaa muhimu la kukuza maendeleo ya vipengele vya mazingira vya Malengo ya Maendeleo Endelevu. Wakiongozwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), zaidi ya nchi 150 hushiriki kila mwaka. Mashirika makubwa, mashirika yasiyokuwa ya serikali, jamii, serikali na watu mashuhuri kutoka pembe zote za dunia huhamasisha kuhusu mazingira wakati wa Siku ya Mazingira Duniani
Kuhusu Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia
Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia 2021-2030 unatoa wito wa kutunzwa na kuboreshwa kwa mifumo ya ekolojia kote ulimwenguni, kwa manufaa ya watu na mazingira. Unalenga kukomesha uharibifu wa mifumo ya ekolojia, na kuiboresha ili kufikia malengo ya kimataifa. Baraza la Umoja wa Mataifa lilitangazaMuongo wa Umoja wa Mataifa na unaongozwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa. Muongo wa Umoja wa Mataifa unaunda vuguvugu dhabiti lenye msingi mpana wa kimataifa ili kuimarisha uboreshaji na kuiwezesha dunia kuwa na hatima endelevu. Hiyo itajumuisha kuimarisha uwezo wa kisiasa wa uborejeshaji na maelfu ya miradi inayoendelea.
Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa
UNEP in mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira ulimwenguni. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.
Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:
Keishamaza Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, UNEP
Moses Osani, Habari na Vyombo vya Habari, UNEP
Pia unaweza kuwasiliana na ofisi zetu za kanda