Zaidi ya miaka miwili iliyopita, Christophe Hodder alichaguliwa kama Mshauri wa kwanza wa Umoja wa Mataifa wa Usalama wa Hali ya Hewa na Mazingira nchini Somalia. Tangu wakati huo, alianzisha juhudi za kimataifa za kuleta amani katika nchi iliyozama katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa kipindi cha miongo mitatu. Lengo lake kuu limekuwa kuisaidia Somalia kukabiliana na ukame uliodumu kwa muda mrefu na msururu wa changamoto nyinginezo za mazingira, ambazo zinaaminiwa kuchochea mzozo uliopo. Tuliketi chini na Hodder ili kuzungumzia kupungua kwa mvua nchini Somalia, jinsi mabadiliko ya tabianchi yanavyochangia kuongeza kwa ukosefu wa usalama, na jinsi nchi hiyo inavyoweza kujijenga upya.
Kuongezeka kwa joto (na) uharibifu wa mazingira vinaongeza ushindani unaopelekea mizozo.
Somalia inaendelea kushuhudia ukame tangu mwaka wa 2020, ukame ambao umepelekea zaidi ya watu milioni 7 kuathiriwa. Je, mabadiliko ya tabiachi ni chanzo cha ukosefu wa mvua?
Christophe Hodder (CH): Ingawa ni vigumu sana kufanya ulinganisho wa moja kwa moja kati ya mabadiliko ya tabianchi na kinachoshuhudiwa nchini Somalia kwa sasa, ni wazi kwamba matukio mabaya zaidi ya hali ya hewa, kama vile ukame na mafuriko, yanatokea mara kwa mara. Ukame ulikuwa ukishuhudiwa nchini Somalia kila baada ya miaka 10. Lakini ukame wa mwisho ulishuhudiwa mwaka wa 2018.
Je, mabadiliko ya tabianchi na uchimbaji wa malighafi huchangia vipi mizozo na ukosefu wa usalama nchini Somalia?
CH: Kuongezeka kwa joto (na) uharibifu wa mazingira vinaongeza ushindani unaopelekea mizozo. Nchini Somalia, wafugaji na wakulima mara nyingi huzozania ardhi ya kulisha mifugo au kufanyia kilimo. Utafiti wa Stefan Döring umeonyesha jinsi kupungua kwa viwango vya maji kwenye visima kulivyopelekea kuongezeka kwa ghasia katika jamii barani Afrika. Nchini Somalia, ghasia hizo katika jamii hupelekea mizozo kati ya wanajamii na kati yao na makabila mengine, hali inayohalalisha makundi ya wanamgambo.
Somalia imekuwa ikishuhudia vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka wa 1991. Je, kukuza amani kupitia mazingira kunawezaje kuchangia kudumisha amani?
CH: Juhudi zote za hapo awali hazikuzingatia mazingira endelevu kama kitu kinachoweza kuzalisha matokeo dhabiti ya kudumisha amani. Tunahitaji kushirikiana na wanajeshi, polisi na mamlaka za bahari ili kubadilisha mawazo yetu kwa hali ya hewa na mazingira ili kubuni masuluhisho ya muda mrefu yanayozingatia mazingira, mifumo ya ekolojia na usalama wa binadamu.
Unaweza kututolea mifano kadha kuhusiana na hali hiyo?
CH: Nchini Somalia, tunafanya majaribio ya upatanisho kupitia mazingira. Pia tunaangalia namna ya kupunguza uharibifu wa malighafi, kama vile kukata miti ili kupata makaa, jambo linalosababisha kuenea kwa jangwa, mizozo zaidi kuhusiana na malighafi na kupoteza makao. Vilevile, UNEP imeshirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo ili kuiga na kufanyia majaribio Masuluhisho kutokana na Mazingira.
Je, unaweza kutuambia zaidi kuhusu kazi ya UNEP ya upatanisho kupitia mazingira?
CH: Tunajaribu kutumia mbinu ambapo huwa tunaleta makabila mawili pamoja ili kuelewa mabadiliko ya tabianchi [na kuyaweka] kama mpinzani, badala ya wao kwa wao. Tunajaribu kuelewa ni wapi kuliko na ushindani au mzozo kuhusiana na rasilimali na jinsi Masuluhisho Kutokana na Mazingira yanavyoweza kusaidia kushughulikia hali hii.
[Kwa mfano], badala ya kuchimba tu kisima na kufikiria mambo yamekwisha, tunaangalia kina cha maji, hali ya udongo katika eneo hilo, na uwezekano wa kupanda mimea tena ili kupanua eneo la kulishia mifugo. Tunatumai kuwa Masuluhisho haya ya muda mfupi na muda mrefu yanayotokana na mazingira ni mambo yatakayoendelea kuangaziwa kati ya makabila na kupunguza mizozo.
Hakuna ulinzi rasmi chini ya sheria ya kimataifa kwa wakimbizi wa mazingira ijapokuwa kupoteza makao kutokana na hali ya mazingira ni suala nyeti nchini Somalia na Pembe ya Afrika. Tunawezaje kushughulikia hali hii?
CH: Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) na UNEP walifanya kazi nzuri na Samuel Hall kuhusu mazingira na ujirudiaji wa kupoteza makao kutokana na mizozo nchini Somalia. Inaonyesha kwamba ijapokuwa watu waliokimbia makwao kutokana na mizozo mara nyingi wanaweza kuhama na kurudi kwao na kurudia kazi zao, waliohama kutokana na mazingira mara nyingi hushindwa kurudi kwa sababu ardhi yao huharibiwa.
Wakati uo huo, waliohama kutokana na mazingira mara nyingi hukimbilia maeneo ya mijini, na kusababisha ukuaji wa miji kwa haraka bila mpangilio wowote na kuchangia matatizo mijini. UNEP kwa sasa inashirikiana na IOM huko Galmudug kwa mradi unaofadhiliwa na Muungano wa Ulaya ili kujenga jamii thabiti na kutafuta njia mbadala endelevu kwa upotezaji wa makazi.
Kutokana na ujuzi wako nchini Somalia, kuna umuhimu gani kwetu kuzingatia athari za mabadiliko ya tabianchi na jinsi ya kuyashughulikia kwa kuzingatia jinsia?
CH: Kuzingatia jinsia ni muhimu sana. Nchini Somalia, wanawake na watoto wengi kwa kuzingatia idadi ya watu waliopoteza makao. Wanawake waliopoteza makao wanabebeshwa mzigo wa kuhudumia familia zao katika mazingira yalio na changamoto nyingi Pia kuna kiwango kikubwa cha unyanyasaji wa kingono na kijinsia. Mbali na kukidhi mahitaji ya kulinda wanawake, kazi yetu inapaswa kukuza ushirikishwaji kamili na mzuri wa wanawake katika ujenzi wa amani. Imedhibitishwa kuwa wanawake wakishirikishwa katika upatanisho na michakato ya kujenga amani kutakuwa na amani ya kudumu zaidi.
Je, tunawezaje kuchochea hatua za kimataifa za kukabiliana na majanga yanayotokea polepole, kama vile mabadiliko ya tabianchi na ukame uliokithiri, nchini Somalia?
CH: Sidhani yanaendelea kutokea polepole. Ni wazi yapo kwa sasa. Tunahitaji kufanya ulinganisho kati ya mabadiliko ya tabianchi na yanayojiri nchini Somalia. Lakini sio tu Somalia. Tazama Sudan, Sahel, Mali, Afghanistan. Mabadiliko ya tabianchi yanavyopelekea ongezeko la mahitaji ya kibinadamu.
Tunahitaji kuangazia jinsi uchafuzi kutoka nchi zilizoendelea unavyochangia majanga haya ya kibinadamu. Tunahitaji kuharakisha Mkataba wa Paris na kuzingatia na kufadhili miradi inayojali mazingira. Tunahitaji kuimarisha ufadhili wa dharura ili kusaidia nchi, kama vile Somalia, ambazo zinatatizika kupata ufadhili wa mazingira.