Tuzo la Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) litatangaza juma lijalo washindi tano wa mwaka wa 2023 wa tuzo la Mabingwa wa Dunia, tuzo la Umoja wa Mataifa la ngazi ya juu zaidi linalotolewa kwa heshima ya mazingira.
Tuzo, ambalo kwa sasa limetimiza miaka 19, hutuzwa kwa viongozi waanzalishi kutoka kwa serikali, wanazuoni na sekta binafsi kwa kupelekea mabadiliko chanya kwa dunia asilia.
Tuzo la mwaka huu litatolewa kwa heshima ya wavumbuzi na miradi inayosaidia kukabiliana na uchafuzi wa plastiki, ambao Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa António Guterres hivi majuzi alitutahadharisha kuwa una “athari mbaya zaidi” kwa sayari.
Washindi watatangazwa tarehe 30 mwezi wa Oktoba mwaka wa 2023, kabla ya kikao cha tatu cha Kamati ya Majadiliano ya Serikali Mbalimbali, ambayo inaunda chombo cha kisheria cha kimataifa cha kukomesha uchafuzi wa plastiki.
Katika mwaka wa 2023, UNEP ilipokea mapendekezo 2,500 ya Tuzo la Mabingwa wa Dunia, na kuwa mwaka wa tatu mfululizo a kupokea mapendekezo mengi zaidi.
Masuluhisho bunifu
Plastiki imebadilisha maisha ya kila siku na kutoa manufaa mengi kwa jamii. Hata hivyo, binadamu hutengeneza takribani tani milioni 430 za bidhaa hizi kila mwaka, thuluthi mbili ni vitu ambavyo hufanywa taka baada ya muda mchache.
Kila mwaka, tani kati ya milioni 19 na milioni 23 za taka ya plastiki hujikuta kwenye mifumo ya ekolojia ya majini na kuchafua maziwa, mito na bahari. Utafiti unaonyesha kuwa, ikiwa mienendo ya sasa itaendelea, plastiki inaweza toa asilimia 19 ya uzalishaji wa gesi ya ukaa ulimwenguni inayoruhusiwa chini ya lengo kabambe zaidi la Mkataba wa Paris kufikia mwaka wa 2040. Kemikali ndani ya plastiki zimehusishwa na matatizo ya kiafya kwa binadamu.
Ili kukabiliana na janga, wataalamu wanasema lazima dunia ipunguze utengenezaji wa plastiki, kukomesha plastiki inayotumika kwa kipindi kifupi na inayotumika mara moja, kuimarisha mifumo ya kutumia tena, kuanza kutumia njia mbadala zinazojali mazingira, kuboresha uchakataji na kuzingatia mfumo mzima wa uchafuzi wa plastiki.
Mabingwa wa Dunia mwaka huu wanashughulikia mengi ya mambo hayo.
"Watu kote ulimwenguni wanajitokeza na mbinu bunifu za kukomesha uchafuzi wa plastiki na kuboresha sayari yetu. Mabingwa wa Dunia wako mstari mbele kwenye juhudi hizi," alisema Sheila Aggarwal-Khan, Mkurugenzi wa Idara ya Viwanda na Uchumi ya UNEP. "Wanatupa matumaini kuwa kuna masuluhisho kwa uchafuzi wa plastiki na kutukumbusha kuwa uendelevu wa mazingira ni muhimu katika kufikia maendeleo endelevu.
Kuleta mabadiliko
Tuzo la Mabingwa wa Dunia litatolewa kusherehekea watu wa kipekee katika makundi nne: Uongozi Unaozingatia Sera, Kujitolea na Kuchukua Hatua, Maono ya Ujasiriamali na Sayansi na Ubunifu.
Kufikia sasa washindi 111, ikijumuisha wakuu wa nchi, wanaharakati nyanjani, wajasiriamali wa ekolojia, vinara wa viwanda na wanasayansi waanzilishi, wametuzwa kama Mabingwa wa Dunia. Washindi wa mwaka jana wanajumuisha mwanauchumi Sir Partha Dasgupta kutoka Uingereza, mwanaharakati wa mazingira Cécile Bibiane Ndjebet kutoks Kameruni, mwanabayolojia Purnima Devi Barman kutoka India, mhifadhi mazingira Constantino Aucca Chutas kutoka Peru na arcenciel, shirika lisilo la biashara kutoka Lebanon.
UNEP huratibu na kuandaa tuzo la Mabingwa wa Dunia. Sifa za UNEP kama mamlaka ya kimataifa, isiyoegemea upande wowote kuhusiana na masuala ya mazingira inatokana na miaka 50 ya utafiti wa kisayansi wa kipekee unaochangia sera ya mazingira kimataifa.
Kuhusu Tuzo la UNEP la Mabingwa wa Dunia
Tuzo la UNEP la Mabingwa wa Dunia hutuza watu binafsi, makundi na mashirika ambayo huchukua hatua za kusababisha mabadiliko chanya kwa mazingira. Tuzo linalotolewa kila mwaka la Mabingwa wa Dunia ni tuzo la Umoja wa Mataifa la ngazi ya juu zaidi linalotolewa kwa heshima ya mazingira. #MabingwaWaDunia
Kuhusu kampeni ya #KomeshaUchafuzi
Ili kupambana na athari mbaya za uchafuzi kwa jamii, UNEP ilizindua #KomeshaUchafuzi, mkakati utakaopelekea hatua za dharura, za kiwango kikubwa na zilizoratibiwa dhidi ya uchafuzi wa hewa, ardhi na maji. Mkakati huu unaangazia athari za uchafuzi kwa mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa bayoanuai, na afya ya binadamu. Kupitia ujumbe unaotokana na sayansi, kampeni hii inaonyesha jinsi kuhamia sayari isiyo na uchafuzi ni muhimu kwa vizazi vijavyo.